Makala
Uislamu-Utangulizi
Fiqhi na Sheria 
Akhlaaq-Tabia
Sira ya Mtume
Nasaha za dini
Maswali na Majibu
Uliza Suala la dini
Jiunge na Mtandao !!!

 

SIRA YA MTUME (SAW)  

"BILA SHAKA MNAO MFANO MWEMA KWA MTUME WA MWENYEZI MUNGU…"Al-qur-an (33:21)

SOMO LA TATU-UMRAH YA QADHAA

 Faida

           Vita vya Khaybar vilichukua takriban mwezi mmoja na nusu, kwani Mtume-Rehema na Amani zimshukie-alikwenda huko mwanzoni mwa mwezi wa Muharram, mwaka wa saba. Na kurudi kutoka huko mwishoni mwa mwezi wa Safar, akakaa Madinah mwezi wa Rabiul-Awwal, Rabiut-thaaniy, Jumadaal-Uula, Jumaadal-Aakhirah, Rajab, Shaaban, Ramadhan na Shawwal, miezi minane. Na miezi yote hii minane ilipita katika hali ya utulivu na amani, hayakutokea ndani yake matukio yo yote makubwa yanayotishia amani au kuleta madhara kwa waislamu. Ila baadhi ya mapambano mepesi mepesi baina ya waislamu na makabila ya Kiarabu katika vitongoji vilivyouzunguka mji wa Madinah. Uchokozi wa watu hawa wachache, ulimlazimisha Bwana Mtume kutuma sariya (kikosi cha askari) kuyatia adabu makabila hayo madogo madogo. Pamoja na kuuawa kwa  baadhi ya askari hawa wa Bwana Mtume mapambanoni, hali ya mambo kwa ujumla wake ilikuwa ikitengenea siku hata siku. Na haiba (utisho) ya waislamu ikaendelea kukita katika nafsi za watu na wigo wake ukizidi kutanuka.

                    i.          Mtume wa Allah achukua hatua za tahadhari dhidi ya usaliti unaoweza kujitokeza upande wa Makurayshi:

           Ulipoandama mwezi wa Dhul-Qa’adah wa mwaka huu wa saba, Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akaanza kufanya maandalizi kwa ajili ya Umrah ya Qadhaa. Hii ndio ile Umrah waliyowafikiana na Makureishi katika suluhu ya Hudaybiyah, kwamba mwaka ule asiingie Makah na badala yake aje mwakani. Kwa hivyo Mtume akawaamuru maswahaba wake kujiaandaa kwenda kukidhi Umrah yao na kwamba asibakie hata mtu mmoja katika wale wote waliokuwepo Hudaybiyah mwaka jana. Kwa kauli hii ya Mtume, hakuna hata mtu mmoja aliyebakia nyuma asitoke na Mtume ila wale waliokufa au kuuliwa Khaybar. Pia walitoka pamoja na Mtume waislamu wengine ambao hawakuwa wamehudhuria Hudaybiyah. Idadi jumla ya waislamu katika msafara huu wa Umrah ya Qadhaa ilikuwa watu alfu mbili ukiachilia mbali watoto na wanawake. Mtume wa Allah akamtawadha ukaimu wa Madinah, swahaba wake Abu Dharri Al-Ghifaariy. Akaswaga ngamia sitini wakiwa ni wanyama wa sadaka na kuhirimia mlangoni mwa msikiti, kisha huyoo akashika njia akileta talbiyah na waislamu kuitikia nyuma yake.

Na katika jumla ya masharti waliyopewa ni kutokuchukua silaha yo yote zaidi ya panga zao zikiwa ndani ya ala zake. Lakini Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alichelea usaliti wa Makureishi, akachukua silaha, kofia za chuma, deraya na mikuki. Na akawaswaga farasi mia kwa ajili ya kuwasaidia iwapo vitazuka vita. Akamteua kuongoza suala la silaha Bashri Ibn Sa’ad na farasi akapewa Muhammad Ibn Maslamah. Walipofika Dhul-Hulayfah; kitongoji kilicho umbali wa kiasi cha maili nane kutoka Madinah, akazitanguliza mbele yake silaha na farasi. Muhammad Ibn Maslamah akaenda na farasi mpaka “Marid-dhwahraan”; mahala palipo umbali wa mwendo wa siku moja kutokea Makah. Hapo akalikuta kundi la Makureishi ambao walimuuliza sababu ya kuja na farasi, akawajibu: Huyoo Mtume wa Allah atapambazukiwa katika kambi hii kesho, inshallah. Tena hawa Makureishi wakamuona Bashir Ibn Sa’ad akiwa na silaha nyingi, wakatoka wangu wangu kuwaendea wenzao. Wakawapasha khabari ya silaha na farasi waliowaona, Makureishi wakafadhaika na kusema: “Wallah, sisi hatujapanga njama       zo zote dhidi yao nasi bado tuko katika mkataba na ahadi yetu. Basi ni kwa lipi Muhammad na maswahaba wake wanataka kutupiga?!’

                  ii.          Makureishi watishwa na uchukuzi wa silaha:

            Makureishi wakamtuma Mukriz Ibn Hafswi kuliongoza kundi la Makureishi kwenda kwa Mtume wa Allah, wakamwambia: “Ewe Muhammad! Hukupata kujulikana utotoni wala hivi ukubwani kuwa na sifa ya usaliti/khiana. Unathubutu kuingiza silaha kuwadhuru jamaa zako na ilhali mlishurutiziana kwamba usiingie na silaha ila silaha ya msafiri; panga zikiwa zimefutikwa alani?!” Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akawajibu: “Hakika mimi siingizi silaha kuwadhuru”. Mukriz Ibn Hafswi akasema: “Hivi ndivyo unavyojulikana kwa wema na utekelezaji wa ahadi”. Kisha akarejea Makah mbio akiwa na ujumbe wake, akawaambia wenzake: “Hakika Muhammad bado anaheshimu masharti mliyowekeana nae”. Makureishi waliposikia hivyo, wakashusha pumzi na kumpisha njia ili aweze kutekeleza Umrah yake kama walivyokubaliana.

                iii.          Makureishi wakinzana kwa kumuona Mtume na maswahaba wake wakifanya Umrah:

          Baadhi ya wapokezi wa Sira-Allah awarehemu-wanasema: Kwamba Makureishi walitoka mjini na kwenda majabalini na kumuachia Mtume mji wa Makah na wakasema: Hatutaki kumuona yeye wala maswahaba wake. Wengine wanasema: Kwamba walitoka kwenda kumuangalia vileleni mwa majabali ili muradi zimesemwa takriban kauli sita katika suala hili. Kwa ujumla ni kwamba wale watu watukufu/viongozi wa mushrikina walijificha wakichukia kumuona Mtume akiingia Makah kifua mbele. Kitendo ambacho walikihesabu kuwa ni kushindwa na hasimu yao huyu mkubwa. Wakati ambapo watu wa kawaida walikuwa na shauku kuu ya kumuona Mtume na maswahaba wake wakiingia Makah. Kwani khabari zilikwishatangaa baina yao kwamba Mtume na maswahaba wake wamedhoofishwa na homa ya Yathrib kiasi cha kushindwa hata kusimama. Kwa ajili hii, watu wakasukumwa kwenda kuwaona madhaifu, wakondefu hawa ili wawakejeli na kuwacheza shere. Lakini Mtume na maswahaba wake walipoingia, hali ya afya zao ilikuwa kinyume na uvumi ulioenea miongoni mwao, kwani walikuwa na afya njema na walionekana kuwa na nguvu.

 



 | Tuandikie |