Makala
Uislamu-Utangulizi
Fiqhi na Sheria 
Akhlaaq-Tabia
Sira ya Mtume
Nasaha za dini
Maswali na Majibu
Uliza Suala la dini
Jiunge na Mtandao !!!

 

SIRA YA MTUME (SAW)  

"BILA SHAKA MNAO MFANO MWEMA KWA MTUME WA MWENYEZI MUNGU…"Al-qur-an (33:21)

IV. DORIA SINDIKIZI YA MTUME YAINGIA MAKKAH

 Faida

           Ukweli ni kwamba kuingia kwa Mtume na maswahaba wake Makah, kulikuwa ni mandhari inayo lazimisha kutafakari na kustaajabu pamoja. Kwani Mtume-Rehema na Amani zimshukie-aliingia Makah akiwa na doria inayokodosha macho na kuziroga akili. Yeye alikuwa amempanda ngamia wake; Al-Qaswaa na waislamu wakiwa wamevaa mapanga yao wamemzunguka kila upande wakimlinda dhidi ya lo lote linaloweza kufanywa na Makureishi. Wakipaaza sauti za talbiyah: “LABBAYKAL-LAAHUMMA LABBAYKA!”, na Abdullah Ibn Rawaahah akishika hatamu za ngamia wa Mtume akiimba beti za mashairi. Hata walipofika “Haram” ya Makah, Mtume akamwambia: “Eeh ewe Ibn Rawaahah! Sema: LAA ILAAHA ILLAL-LAAHU WAHDAU, SWADAQA WA’ADAU WA NASWARA ‘ABDAU WA A’AZZA JUNDAU WAHAZAMAL-AHZAABU WAHDAU (badala ya kuimba mashairi)”. Ibn Rawaahah akaanza kusema maneno hayo aliyofundishwa na Mtume na watu wakimuitika nyuma yake kwa hamasa na mori mkuu. Na mwangwi ukizianikiza sauti zao hizo pande zote za mji wa Makah na zikigonga ngoma za masikio ya wale waliotoka ili wasizikie wala kuuona msafara wa Mtume ukiingia Makah.

 

SOMO LA NNE.

                    i.          Mtume wa Allah na maswahaba wake wadhihirisha nguvu yao kwa maadui zao:

            Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alikuwa akiujua uvumi ulioenezwa dhidi yake na maswahaba wake. Kwa ajili hii, akawausia maswahaba wake ya kwamba isionekane kwao dalili yo yote ya uchovu/unyonge. Na akawaamrisha kuvaa rubega na kwenda matiti (mbiombio) katika twawafu ili mushrikina wauone ukakamavu na nguvu yao. Mtume wa Allah akaingia Masjidil-Haraam akiwa kavaa rubega na waislamu wakivaa kama yeye, akaenda mpaka akaligusa “Hajarul-Aswad” kwa fimbo yake ndogo na kusema: “Allah amrehemu mtu ambaye amewaonyesha (makafiri) leo nguvu”. Kisha akaondoka akienda mbiombio kuizunguka nyumba tukufu ya Allah na maswahaba wakimfuatia mpaka zikamalizika mara tatu za mwanzo. Halafu ndipo alipowatembeza mwendo wa kawaida katika mara nne zilizobakia ili kukamilisha mizunguko saba ya Twawafu. Mushrikina wakapatwa na mshangao mkubwa walipoiona nguvu, ukakamavu na uchangamfu wa waislamu. Wakapigana vikumbo wanaume, wanawake na watoto kuzunguka msikiti mtukufu wakigombea kuwaona waislamu wakitufu huku wakiambizana: “Ni hawa ndio mlidai kwamba homa imewadhoofisha?! Hakika wao wanachapusha mwendo kama anavyochapua swala”.

Walipomaliza kutufu, Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alikwenda na maswahaba wake katika eneo la ibada ya Sa’ayi (kwenda baina ya vilima Swafaa na Marwaa). Akafanya sa’ayi akiwa amempanda ngamia wake mpaka akamaliza mara saba. Alipoikamilishia Marwaa ile mara ya saba, Mtume alisimama akasema: “Hapa ndio mahala pa kuchinjia wanyama wa sadaka na njia zote za Makah ni mahala pa kuchinjia”. Kisha ndipo alipomchinja hapo Marwaa mnyama wake wa sadaka na wakashirikiana nae katika mnyama huyo waislamu waliohudhuria Hudaybiyah. Aliyempata ngamia alichinja ngamia na asiyepata alicihinja ng’ombe kutokana na uadimu wa ngamia wakati huo. Halafu tena ndipo Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-aliponyoa akifuatiwa na maswahaba wake na kwa tendo hili la kunyoa, wakawa wamefungukana na Umrah yao.

Na ikumbukwe kwamba farasi na silaha zilikuwa zimeachwa katika eneo la karibu liitwalo “Ya’ajaj” umbali wa maili nane kutokea Makah. Na wakaachwa watu mia mbili kulinda, waislamu walipokamilisha Umrah yao, Mtume akawatuma maswahaba mia mbili kwenda huko ili kulinda silaha na farasi. Ili kutoa nafasi kwa walinzi wa mwanzo kuja kutekeleza ibada ya Umrah.

                  ii.          Bilali aadhini juu ya Al-Ka’abah:

           Kisha Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akaingia ndani ya              Al-Ka’abah na kukaa humo mpaka ukaingia wakati wa swala ya Adhuhuri. Akamuamuru Sayyidina Bilali-Allah amuwiye radhi-kuadhini juu ya Al-Ka’abah. Kitendo cha Bilali, mtu mweusi tena mtumwa kupanda juu ya Al-Ka’abah tukufu na kutoa wito mtukufu (adhana) kiliwaudhi na kuwaghadhibisha upeo Makureishi. Kiasi cha kufikia Suhail Ibn Amrou na wenziwe aliokuwa nao kufunika nyuso zao pale waliposikia adhana. Ikrimah Ibn Abu Jahli yeye akashindwa kabisa kuvumilia, akasema: “Kwa yakini Allah amemkrimu Abul-Hakam (baba yangu) kwa kumfisha mapema, hakufika kumsikia mtumwa huyu akiyasema haya ayasemayo!” Na Swafwaan Ibn Umayyah akasema: “Kila himda njema zinamstahikia Allah aliyemfisha baba yangu kabla ya kuyaona haya!” Na Khalid Ibn Useid yeye akasema: “Kila himda njema ni milki yake Allah aliyemfisha baba yangu kabla ya kuiona siku hii (ya aibu), mpaka (mtumwa) Ibn Ummu Bilali anapiga ukelele wa punda juu ya Al-Ka’abah!”

 



 | Tuandikie |