|
Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-na maswahaba
wake-Allah awawiye radhi-wakakaa siku tatu walizo shurutiana na Makureishi.
Wakienda na kurudi katika pande zote za mji wa Makah kwa amani na salama.
Ndani ya siku tatu hizi, watu wa Makah waliona mandhari ya nguvu na mshikamno
baina ya waislamu. Na wakaona kila dalili za wema, mahaba na ukweli wa hali ya
juu baina ya waislamu na Mtume wa Allah. Kiasi cha kuwakodosha macho na
kuwatunduwaza na nyoyo zao zikijaa mshangao wa dini hii ambayo imeanza kupata
nguvu kubwa baada ya unyonge/udhalili wa kutupwa. Ikaanza kupendwa baada ya
kuchukukiwa upeo na ikatoka katika kukimbiwa na kupewa mgongo ikaingia katika
mshikamano na umoja. Na wakashangazwa mno na Mtume huyu asiyejua kusoma wala
kuandika kuweza kuunda umoja wenye nguvu kutokana na makundi tapanyika haya.
Nguzo za umoja huo zikiwa ni kuoneana huruma na kushikamana, lengo lake likiwa
ni kheri na kutengenea na msingi wake ni kumuabudu Allah asiye na mshirika.
Kutokana na yote haya, watu wa Makah wakachelea kufitinishwa dini yao na
waislamu, kabla kidogo ya kumalizika siku tatu za mkataba, akaja Suhail Ibn
Amrou na Huwaytwib Ibn Abdil-Izzaa, wakamwambia Mtume wa Allah-Rehema na Amani
zimshukie: “Muda wako umekwisha, tuondokee”. Mtume wa Allah akataka kuzizoesha
nyoyo za Makureishi na alikwishahisi kazi iliyofanywa na Uislamu ndani yao,
akawaambia wawili wale: “Mtakuwaje lau mtaniachia nikaingia kwa Bi. Harusi
hapa kwenu nasi tukakuandalieni chakula mkakila?” – Ikumbukwe kwamba Bwana
Mtume wakati akiwa Makah alikuwa amemposa Maimunah Bint Al-Haarith na alikuwa
bado hajaingia nyumbani – Watu wawili wale wakadiriki khatari inayowajongelea
wao na dini yao pindi wakiendelea kuzungumza na Muhammad. Na kwamba
watakapojumuika nae katika walima wa harusi na katika hali ya kuliwazika na
mkwe mpya anayetaka kuweka kigingi cha mafungamano. Basi hapana shaka kwamba
wao watashindwa nae na hapana wasiwasi juu ya uwezo wake katika kuwamiliki wao
kutokana na nguvu ya nafsi yake na utamu wa maneno yake. Na kwamba anaweza
kabisa kuvivunjilia mbali vizuizi vyote walivyo jiwekea na khususan ni baada
ya athari yake waliyoiona watu na baada ya watu wengi kuvutika na Uislamu.
Haya ndio mawazo yaliyokuwa yakijiri katika fikra za watu wawili hawa,
wakasema kwa upesi: “Sisi hatuna haja na chakula chako. Tuondokee, tunakuomba
kwa ahadi iliyo baina yetu utoke katika ardhi yetu, hizi siku tatu tayari
zimemalizika”. Ugumu na ukali huu wa maneno ulioonyeshwa na watu hawa,
ukaziamsha hasira za Sa’ad Ibn Ubaadah; kiongozi wa Answaar, akamuinukia
Suhail Ibn Amrou akiwa ameghadhibika na kumwambia: “Umesema uwongo wewe, huna
mama wewe! Hii sio ardhi yako wala ya baba yako. Wallah hataacha kuwa hapa ila
ataondoka kwa radhi yake”. Mtume wa Allah-Rehema na Amani
zimshukie-akatabasamu, kisha akasema: “Ewe Sa’ad! Usiwaudhi wageni
waliotutembelea kambini kwetu”. Halafu Mtume akaamrisha watu wajitayarishe kwa
msafara wa kurudi Madinah, watu wote wakaondoka kuelekea “Sarifa”. Hili ni
mojawapo ya maeneo ya vitongoji vya Makah, lililo karibu na “Tan-eem” kiasi
cha maili tisa kutoka Makah. Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alikuwa
amemposa Maimunah Bint Al-Haarith, aliyekuwa miongoni mwa wanawake watukufu wa
Kikureishi. Dada yake; Ummul-Fadhli Bint Al-Haarith alikuwa ni mke wa Al-Abbas
Ibn Abdul-Mutwalib. Kwa hivyo Sayyidina Al-Abbas ndiye aliyetawalia kumuoza
kwa Mtume, nae Bwana Mtume akaingia nyumbani hapo “Sarifa”.
iv.
Umrah hii ya Qadhaa
ilikuwa ni vita ya moyo kwa watu wa Makah:
Naam, hivi
ndivyo Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alivyoondoka Makah, akiacha
nyuma athari kubwa. Zikaifungukia dini yake nyoyo kukutavu, kundi miongoni
mwao likistaajabishwa na utekelezaji ahadi wa Mtume pamoja na kuwa na uwezo wa
kuvunja au kubadili. Na kundi jingine lilivutiwa na mtindo wa dini hii na
huruma ya Uislamu kwa wafuasi wake. Na utii na utulivu mzuri baina ya waislamu
na Mtume wao. Na kundi jingine likaona kuwa nyota njema inaelekea kuwa ni
fungu la Uislamu, kwa hivyo wakaonelea ni vema wakajiegemeza mapema kwenye
njia ya salama na amani. Ikutoshe kwamba Umrah hii ya Qadhaa imekuwa ndio
sababu ya kusilimu kwa Khalid Ibn Al-Waleed na Amrou Ibn Al-Aaswi.
|