Makala
Uislamu-Utangulizi
Fiqhi na Sheria 
Akhlaaq-Tabia
Sira ya Mtume
Nasaha za dini
Maswali na Majibu
Uliza Suala la dini
Jiunge na Mtandao !!!

 

SIRA YA MTUME (SAW)  

"BILA SHAKA MNAO MFANO MWEMA KWA MTUME WA MWENYEZI MUNGU…"Al-qur-an (33:21)

SOMO LA TANO - KHALID NA AMROU

 Faida

 

                       i.               Khalid na Amrou ndio waliokuwa mashujaa wa Makureishi na tegemeo lao vitani na walikuwa miongoni mwa maadui wakubwa wa Mtume:

             Huenda Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-hakupata kuwafurahikia watu waliosilimu baada ya Hijrah, kama alivyowafurahikia Khalid Ibn Al-Waleed na Amrou Ibn Al-Aaswi. Watu wawili hawa walisilimu baada ya Umrah ya Qadhaa, katika mwezi wa Safar (Mfunguo nne) wa mwaka wa nane. Furaha ya Mtume wa Allah kwa kusilimu kwa watu hawa ilikurubia kulingana na furaha yake wakati waliposilimu Umar Ibn Al-Khatwab na Hamzah Ibn Abdul-Mutwalib kabla ya Hijrah.

Watu wawili hawa; Khalid na Amrou walikuwa na daraja na utajo mkubwa kwa upande wa Makureishi, walikuwa ni miongoni mwa nguzo zao madhubuti. Ama huyu Amrou, yeye alikuwa ni katika kile kizazi bora cha Waarabu katika uelekevu na siasa na wepesi katika kushughulikia masuala tata. Khalid yeye alikuwa ni miongoni mwa weledi na mabingwa katika masuala ya vita nae ndiye aliyepewa dhima ya kuongoza kikosi cha farasi katika enzi za jahilia. Waliposilimu, nguvu ya Makureishi ikadhoofika kwa kiwango kikubwa mno kiasi cha kulitia ufa wa kutisha jengo lao. Jengo hili la Makureishi likaelekea kuanguka na hatimaye kuanguka kabisa baada ya miezi sita tu. Kama ambavyo kusilimu kwa mashujaa wawili hawa-Allah awawiye radhi-kulivyo idhoofisha janibu ya Makureishi, ndivyo kulivyoiimarisha janibu ya waislamu.

 

                     ii.               Kila mmoja; Khalid na Amrou alikuwa anafikiria kuhama Makah na kwenda kuishi ughaibuni:

            Tukirejea nyuma kila mmoja wa watu wawili hawa alikuwa amejawa na chuki kuu dhidi ya Mtume-Rehema na Amani zimshukie-kiasi cha kufikia kutamani kumtafuna akiwa hai. Walikuwa ni wapinzani wake wakuu, wakiipinga dini yake sana kuliko Makureishi wengine. Chuki na upinzani huu, ukamfikisha Khalid kushindwa kukaa Makah wakati Mtume akiwa humo akifanya Umrah ya Qadhaa. Akatoka Makah akiwa hana muelekeo maalumu ili muradi asiweze kuona wala kusikia khabari zo zote za Mtume. Tangu katika suluhu ya Hudaybiyah, yeye alianza kufikiria mahala pa kuhamia pale Makah itakapoingia mikononi mwa mtume. Kwani yeye kutokana na hali ya mambo ilivyokuwa ikijiri, alikuwa na yakini kabisa kwamba hatimaye ushindi utakuwa ni fungu la Mtume, Khalid mwenyewe anasimulia: “...(Mtume) alipofanya suluhu na Makureishi pale Hudaybiyah, nilijisemea nafsini mwangu: Kimebakia kitu gani? Niende wapi sasa? Je, niende kwa mfalme Najaashi, kwani huko Muhammad na maswahaba wake walipewa amani. Au niende kwa Hiraqli na huko niiache dini yangu na kuufuata unaswara au uyahudi? Au niende nje ya Bara Arabu au nijifungie nyumbani kwangu muda wa kusalikia uhai wangu?” Hakika huu ulikuwa ni mtosheo mkuu uliomkumba Khalid kiasi cha kumuhemeza asijue la kufanya wala pa kwenda.

Amrou nae kwa upande wake, alikuwa akifikiria kuhama kabisa Arabuni kwa sababu tu ya kumchukia Mtume. Na kuikimbiza nafsi yake, heshima na dini yake visije angukia chini ya utawala/mamlaka ya Muhammad. Amrou nae anasimulia, anasema: “...Ilipo fanyika suluhu ya Hudaybiyah na Mtume akaikubali na kuipitisha, nikawa najisemea: Mwaka ujao Muhammad anaingia Makah na maswahaba wake! Makah hapafai tena kukaa wala Twaif na wala hapana kitu bora kama kuondoka! Nami bado ni mbali na Uislamu na naona hata lau Makureishi wote watasilimu, mimi sitasilimu. Nikawakusanya watu wanaonikubali na kunisikiliza katika kaumu yangu na wakinitanguliza katika mambo yao, nikawauliza: Nyinyi mnajua kwamba mimi wallah kwa yakini naona jambo (dini) hili la Muhammad linaelekea kuyashinda mambo yote kwa kiasi cha kutisha. Basi mimi naonelea ni vema tukaungana na mfalme Najaashi, ikiwa Muhammad atashinda sisi tutabakia huko huko. Kwani kuwa chini ya mamlaka ya Najaashi ni bora kwetu kuliko kuwa chini ya Muhammad. Na iwapo itashinda kaumu yetu, sisi wanatujua kwa hivyo haitatujia kutoka kwao ila kheri. Wakasema: “Hiyo ndio fikra ya sawa sawa”.

Hivi ndivyo watu wawili hawa walivyokuwa wakifikiria kuhama kutoka katika ardhi ya Waarabu, pale ilipowabainikia kwamba nyota ya Muhammad inaelekea kunga’ara. Na kwamba nyota ya Makureishi inaendea kuzimika na kwamba hapana shaka wala nguvu ya kuizuia dini ya Muhammad kuishinda dini ya Makureishi. Lakini Allah ambaye funguo za nyoyo anazitamalaki yeye, alikwisha waandaalia sababu zilizofungua nyoyo zao kuuelekea Uislamu kwa namna wasiyoitazamia.

 



 | Tuandikie |