|
iii.
Amrou abadilika kutoka
katika dhamira ya usaliti na kuukumbatia Uislamu:
Ama Amrou, yeye alihajiri kwenda kwa mfalme
Najjaashi wa Uhabeshi akiwa na kundi la wenzake walio ambatana nae. Kufika
kwake huko kukasadifiana na kufika kwa Amrou Ibn Umayyah; mjumbe maalumu wa
Mtume kwa Najaashi. Mjumbe huyu alikuwa ameleta barua ya Mtume aliyo muandikia
Najaashi, hapo ndipo Amrou Ibn Al-Aaswi akadhania kwamba hiyo ndio fursa
adhimu ya kumshambulia mjumbe wa Mtume. Kwa mashambulizi hayo, atakuwa
ameiponya chuki/ghadhabu ya moyo wake na atakuwa ametoa msaada usio sahaulika
milele kwa Makureishi. Amrou mwenyewe anahadithia: “Basi nikawaambia wenzangu:
Huyoo ni Amrou Ibn Umayyah! Lau ningeingia kwa Najaashi nae akanipaye, basi
ningeliipiga shingo yake, kwa yakini Makureishi wangeliona kuwa mimi
nimewatoshea kwa kumuua mjumbe wa Muhammad. Basi nikaingia na kumsujudia kama
nilivyokuwa nikifanya (hapo kabla), akasema: Karibu rafiki yangu! Je,
umeniletea hadiya (zawadi) yo yote kutoka nchini mwako? Nikamjibu: Naam,
nyingi mno. Nikampa zikamstaajabisha na akazipenda, nilipoona uzuri wa nafsi
yake, nikasema: Ewe mfalme wee! Hakika mimi nimemuona mtu mmoja akitoka kwako
nae ni mjumbe wa adui yetu aliye tudhulumu. Akaua watukufu wetu, basi naomba
unipe mtu huyo ili nipate kumuua. Akaghadhibika, akaunyanyua mkono wake na
kuipiga pua yangu pigo ambalo nilidhania kuwa kaivunja. Mionzi/tundu za pua
yangu zikachuruzika damu, basi nikawa naifuta damu hiyo kwa nguo yangu. Basi
ukanipata udhalili ambao lau ardhi ingenipasukia ningeliingia ndani yake kwa
kumchelea, halafu nikasema: Ewe mfalme wee! Wallah, lau ningeliyakinisha kuwa
wewe unalichukia hili, basi nisingeliomba. Akasema: Hivi wewe unaniomba nikupe
mjumbe wa mtu ambaye anajiwa na malaika mleta wahyi ambaye alikuwa akimjia
Musa-Amani iwashukie-ili umuue?”
Amrou anaendelea kusimulia: “Basi Allah akaubadilisha moyo
wangu kutoka katika dhamira mbaya niliyo kuwa nayo na nikajisemea: Huyu
ameitambua haki na Waarabu na wasio waarabu nawe unaikhalifu? Kisha nkauliza:
Ewe mfalme unalishuhudia hilo? Akajibu: Naam, ninalishuhudia hilo mbele ya
Allah ewe Amrou,basi nakuomba unitii na umfuate. Wallah, kwa yakini yeye yuko
katika haki na bila ya shaka atawashinda wapinzani wake wote kama Musa alivyo
mshinda Firauni na jeshi lake. Nikamuuliza: Je, unanipa kiapo cha utii kwake
juu ya Uislamu? Akajibu: Naam, akaukunjua mkono wake na akanipa ahadi ya utii
kwa Uislamu, kisha akaagiza tasa la maji, akanisafisha damu na kunivika nguo
nyingine. Halafu tena nikatoka nikimkusudia Mtume wa Allah-Rehema na Amani
zimshukie-basi nikakutana na Khalid Ibn Al-Waleed. Na hiyo ilikuwa ni kabla ya
Fat-hi Makah, nikasuhubiana nae mpaka tukafika Madinah”.
iv.
Khalid abadili azma ya
kuukimbia Uislamu na badala yake aukimbilia:
Ama Khalid, yeye aliendelea kubakia katika hali ya
kutoshewa na kuhemewa, akifikiria upande wa kuelekea. Alibakia katika hali
hiyo mpaka Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akaingia Makah katika
Umrah ya Qadhaa, akatoka nje ya Makah asishuhudie kuingia kwa Mtume wa Allah,
Khalid anahadithia: “Na ndugu yangu Al-Waleed alikuwa amengia pamoja nae
(Mtume), akanitafuta asinipate, akaamua kuniandikia ujumbe, tahamaki
kumeandikwa: Kwa jina la Allah Mwingi wa Rehema Mwenye kurehemu. Ama baad,
hakika mimi sijapatapo kuona ajabu zaidi kuliko kuukataa kwako Uislamu na
ilhali wewe una akili kubwa. Na mithili ya Uislamu hajingikiwi nao mtu ye yote
na Mtume wa Allah ameniuliza kuhusu wewe, akasema: Yu wapi Khalid”, nikamjibu:
Allah atamleta, akasema: Mtu kama yeye si wa kujingikiwa na Uislamu, lau
angeli ziunganisha nguvu zake pamoja na waislamu dhidi ya mushrikina,
ingelikuwa ni kheri kwake, nasi tungelimtanguliza mbele. Basi nakusihi ewe
ndugu yangu uzidiriki kheri zilizo kufutu (pita). Uliponifikia ujumbe wake
huo, nikapata nguvu ya kutoka na ukanizidishia raghba ya Uislamu na
yakanifurahisha mno maneno ya Mtume wa Allah. Basi nikaota usingizini kama
kwamba niko kwenye mji finyu wenye ukame, nikatoka kwenda kwenye mji wenye
neema na wasaa”.
v.
Sadfa yenye kunadi saada:
“Nilipo azimia kutoka kwenda Madinah, nikakutana
na Swafwaan Ibn Umayyah, nikamwambia: Ewe babie Wahbi, hivyo wewe huoni kuwa
Muhammad amewashinda Waarabu na wasio waarabu? Basi lau tungelimuendea na
tukamfuata, kwani heshima yake ndio heshima yetu! Akanikatalia vikali kabisa
na akasema: Hata kama watu wote watamfuata mimi sitamfuata abadan.
Nikajisemea: Huyu ni mtu aliye changanyikiwa, baba na kaka yake waliuliwa
katika vita vya Badri. Na nikakutana na Ikrimah Ibn Abu Jahli, nae nikamwambia
maneno kama niliyo mwambia Swafwaan. Nae akanijibu kama nilivyojibiwa na
Swafwaan, nikajisemea: Yafiche niliyo kwambia, akasema: Sitayataja. Halafu
nikakutana na Uthman Ibn Twal-hah, nikajisemea: Huyu kwangu mimi ni rafiki;
basi nikapenda nimwambie. Kisha nikakumbuka kuuawa kwa baba yake; Twal-hah na
ami yake Uthman na nduguze wanne, kwani wote hao waliuliwa katika vita vya
Uhud. Kwa ajili hiyo, nikaona vibaya kumwambia, kisha nikamwambia hali halisi
ilivyo: Hakika si vinginevyo, sisi hivi sasa ni mithili ya mbweha aliye
shimoni, lau atamwagiwa ndoo ya maji basi bila ya shaka atatoka nje. Halafu
tena ndipo nilipomwambia yale niliyo waambia akina Swafwaan na Ikrimah.
Akaniitika haraka kinyume na matarajio yangu, basi haikuchomoza alfajiri mpaka
tukakutana “Baiajaj”, tukadamka mpaka “Al-Haddah”. Hapo tukamkuta Amrou Ibn
Al-Aaswi, akasema: Karibuni watu nyie! Tukamjibu: Nawe karibu! Akatuuliza:
Mnakwenda wapi? Tukamjibu: Tunakwenda kuingia katika Uislamu, akasema: Nami
hilo ndilo lililo nileta. Tukaambatana sote mpaka tukaingia Madinah”.
vi.
Mtume wa Allah
afurahishwa mno na kusilimu kwa mashujaa wawili hawa:
Walipowasili Madinah, wakashukia nje ya mji, Mtume
akapashwa khabari yao, akafurahi mno na akawaambia maswahaba wake: “Makah
imekupeni bora ya watoto wake”. Khalid anasema: “Basi tukavaa nguo zetu zilizo
nzuri kabisa, kisha tukatoka kwenda kwa Mtume wa Allah-Rehema na Amani
zimshukie. Nikakutana na ndugu yangu; Al-Waleed, akaniambia: Harakisha, kwani
Mtume wa Allah amefurahishwa na ujaji wenu na anakungojeeni. Tukachapusha
mwendo, nikamchomozea Mtume, basi aliendelea kutabasamu mpaka tukasimama mbele
yake. Nikamwamkua kwa maamkuzi ya utume, nae akaiitikia salamu yangu kwa uso
mkunjufu. Nikasema: Hakika mimi ninashuhudia kwamba hapana afaaye kuabudiwa
kwa haki ila Allah na kwamba wewe ni Mtume wa Allah. Akasema (Mtume): “Himda
zote njema zinamstahikia Allah aliye kuongoa”. Mimi nilikuwa naona kuwa una
akili kubwa sana, nikataraji haita kusalimisha ila kwenye kheri”. Nikasema:
Ewe Mtume wa Allah wee! Niombee Mungu anisamehe mapambano niliyo yaendesha
dhidi yako! Mtume-Rehema na Amani zimshukie-akasema: “Uislamu unayakata yote
yalio kuwa kabla yake”. Amrou na Uthman nao wakaenda mbele na kula kiapo cha
utii kwa Mtume wa Allah”.
Amrou Ibn Al-Aaswi nae anasema: “Wallah, Mtume wa Allah-Rehema
na Amani zimshukie-hakutulinganisha mimi na Khalid katika masuala muhimu na ye
yote miongoni mwa maswahaba wake tangu tuliposilimu. Na tulikuwa na daraja
hiyo hiyo katika ukhalifa wa Abu Bakri. Na nilikuwa katika hali hiyo zama za
Umar na Umar kwa Khalid alikuwa kama ni mtu mwenye kulaumu”.
Kwa yakini Uislamu ulijipatia nguzo kuu mbili na mashujaa
wawili kutokana na kusilimu kwa Khalid na Amrou. Mashujaa hawa walitoa mchango
mkubwa sana katika historia nzima ya ushindi wa Uislamu. Na Mtume wa
Allah-Rehema na Amani zimshukie-aliendelea kumtawalisha Khalid kikosi cha
farasi kama alivyo kuwa akitawalia katika zama za jahilia. Na akamuita: “panga
la Uislamu”, nae akawa ni upanga uliotolewa na Allah kuwafyeka makafiri-Allah
amuwiye radhi na maswahaba wote pia.
|