|
SOMO
LA KWANZA.
i.
Vita vya Mu'utah vilikuwa
ni matokeo ya barua za da'awah zilizo pelekwa kwa wafalme:
Vita hii ilikuwa katika mwezi wa Jumaadal-Uula
(Mfungo Nane) mwaka wa nane wa Hijrah sawa na mwezi Septemba/629 A.D., kiasi
cha miezi mitano tu baada Umrah ya Qadhaa. Imamu Bukhaariy na Ibn
Is-haaq-Allah awarehemu-wameviita vita hivi kwa jina la "vita (ghazwah) vya
Mu'utah" badala ya "sariyah ya Mu'utah" kutokana na wingi wa jeshi la waislamu
katika vita hivi. Hata kama Mtume wa Allah-Rehema na Amani
zimshukie-hakushiriki na "Mu'utah" ni kimojawapo ya vijiji/vitongoji
vya "Al-Bulqaa" katika mipaka ya Shamu kwa upande wa Hijaaz. Kiasi
cha umbali wa mwendo wa makambi mawili kutokea Baytul-Maqdis (Jerusalem),
mashariki mwa bahari iliyo kufa (dead sea).
Sariyah hii ilikuwa ni natija ya da'awah (ujumbe wa Uislamu)
ulio elekezwa na Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-kwa wafalme wa
Peninsula ya Kiarabu na maeneo ya pembezoni mwake. Wajumbe wa Mtume
waliwapelekea barua zake wafalme hao, basi wako miongoni mwao walio upokea
vema ujumbe huo wa Mtume na wakasilimu. Wengine walizuiwa na mazingira yaliyo
wazunguka kuuitikia ujumbe huo, lakini hilo halikuwa pelekea kutokuwapokea
vema wajumbe walio tumwa kwao. Wako pia walio upokea ujumbe kwa ugumu na
ukukutavu wa moyo lakini bila ya kumdhuru mjumbe, hilo lilitokana na
mazoea/kanuni ya kisiasa baina ya mataifa. Kanuni inayo hukumu kuheshimiwa
mjumbe kwa hali yo yote, kwani dhima ya mjumbe ni kufikisha tu ujumbe
aliotumwa kwa mlengwa. Kwa msingi huu basi, hakumuelei mlengwa kumdhuru vyo
vyote utakavyo kuwa ujumbe aliompelekea. Hii ilikuwa na bado inaendelea kuwa
ndio kanuni ya msingi katika mahusiano ya kidplomasia baina ya mataifa. Na kwa
msingi huo ndipo Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-aliwapelekea ujumbe
wafalme na viongozi walio mzunguka. Nao kwa kuuheshimu msingi huo huo,
wakawapokea vema wajumbe walio tumwa kwao bila ya kuwadhuru au kuwadhalilisha.
Isipokuwa mtu mmoja tu; Shurahbiyla Ibn Amrou Al-Ghasaaniy-mmojawapo wa
magavana wa Urumi walio tawala Shamu. Huyu hakui heshimu kanuni hii,
akaivunja, yeye alikutana na Al-Harith Ibn Umeir mjumbe wa Mtume kwa gavana wa
Basrah, akamuuliza anaelekea wapi. Alipo tambua kwamba yeye ni mmojawapo wa
wajumbe wa Mtume, akaamuru afungwe na aletwe mbele yake, akamkata kichwa.
ii.
Kuuawa kwa mjumbe wa
Mtume aliye mtuma kwa mtawala wa Basrah ulikuwa ni uchokozi wa wazi na uadui
wa moja kwa moja kwa Uislamu:
Kuvunjwa kwa kanuni za Kidplomasia na kuuawa kwa
mjumbe wake, kulimkasirisha mno Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie. Na
akalichukulia hilo kuwa ni uchokozi wa wazi na ni suala ambalo si vema
kulinyamazia na kuliacha kupita hivi hivi tu. Khususan ikizingatiwa kwamba
Uislamu bado ulikuwa ukiendelea kusimika nguzo zake katika Peninsula ya
Kiarabu. Kwa hivyo bado kulikuwa na haja kubwa ya kuhifadhi na kulinda haiba
yake na fikra iliyo kuwemo ndani ya nafsi za watu wakati huo ni kwamba Uislamu
ni nguvu isiyo shindika. Na kwamba unapata msaada kutoka kwa Allah Taala na
chini ya taathira ya itikadi hii walisilimu watu wengi kwa kupenda au kwa
khofu, khusasan mabedui. Wengi wao walikuwa wakisilimu chini ya nyenzo ya
khofu ya nguvu ya Uislamu au chini ya msukumo wa tamaa ya kupata ngawira. Na
wala kuingia kwao Uislamuni hakukutokana na kusadiki na kuamini itikadi ifaayo
na adabu tukufu zilizomo ndani ya Uislamu. Hakika si vinginevyo, kusilimu kwao
kulikuwa ni kwa mtu mwenye pupa ambaye anavizia fursa na kuangalia mazingira.
Na wakawa kama anavyo sema Allah Taala: "MABEDUI WAMESEMA: TUMEAMINI. SEMA:
HAMJAAMINI, LAKINI SEMENI: TUMESILIMU. KWANI IMANI HAIJAINGIA KATIKA NYOYO
ZENU..." [49:14] Na kama asemavyo: "NA KATIKA MABEDUI HAO WAKO WANAO FIKIRI
KUWA WANAYO YATOA NI GHARAMA YA BURE, NA WANAKUNGOJEENI MAMBO YAKUGEUKIENI.
MAGEUKO MAOVU YATAKUWA JUU YAO! NA ALLAH NI MWENYE KUSIKIA MWENYE KUJUA".
[9:98]
Kwa ajili hii, Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akawa
na pupa mno ya kuhakikisha kuwa haiba ya Uislamu haipungui upande wo wote. Ili
hilo lisipelekee kuteteresha itikadi iliyomo mioyoni mwa watu kuuelekea
Uislamu kwa hali yo yote. Na kuyanyamazia mauaji ya Al-Haarith Ibn Umeir
lilikuwa ni jambo linalo pomosha utukufu/heshima ya Uislamu na kupunguza haiba
yake. Kwa hivyo basi, ikawa hapana budi kufanya kitendo ambacho kitailinda
haiba ya Uislamu. Na kuwahisisha watu ndani ya Peninsula ya Kiarabu na nje
yake kwamba Uislamu sio nguvu ya kuchezewa na kudharauliwa. Ni kutokana na
kuyazingatia yote haya kwa kina, ndipo Mtume wa Allah-Rehema na Amani
zimshukie-alipofikia uamuzi wa kutuma kikosi cha askari huko Shamu. Mahala
ambapo aliuliwa kwa dhulma mjumbe wake; Al-Haarith Ibn Umeir ili kuwatia adabu
wachokozi wale. Na kuuondoshea Uislamu jeuri na udhalili ulio fanyiwa.
iii.
Uandazi wa jeshi na
upangaji wa mikakati:
Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akapiga
mbiu, watu wakatoka mbio mbio kuitika wito wake. Wakaja wakapiga kambi mahala
paitwapo "Al-Jurfu" mpaka idadi yao ikafikia watu alfu tatu. Mtume alipo
kwisha waandaa na kuwaweka tayari kwa vita, akawaambia: "Amiri-Jeshi wenu
ni Zayd Ibn Haarith, akiuawa atashika uamiri Ja'afar Ibn Abu Twaalib, nae
akiuawa atashika Abdullah Ibn Rawaahah. Huyu nae akiuawa, basi waislamu
waridhiane baina yao mtu watakayempa uamiri". Na akawaamuru waende mahala
alipouliwa Al-Haarith Ibn Umeir, wawalinganie Uislamu watu wa huko, wakiitika
wawakubalie na wawachie. Na kama hawakuitika, basi takeni msaada kwa Allah juu
yao na piganeni nao na akawausia kutofanya usaliti wala wasimuue mtoto wala
mwanamke. Wala wasimuue mzee kikongwe, wala mtu aliye jihifadhi katika nyumba
yake ya ibada, wala wasikate mti wala kubomoa nyumba.
|