Makala
Uislamu-Utangulizi
Fiqhi na Sheria 
Akhlaaq-Tabia
Sira ya Mtume
Nasaha za dini
Maswali na Majibu
Uliza Suala la dini
Jiunge na Mtandao !!!

 

SIRA YA MTUME (SAW)  

"BILA SHAKA MNAO MFANO MWEMA KWA MTUME WA MWENYEZI MUNGU…"Al-qur-an (33:21)

IV. WARUMI WALIPOKEA JESHI LA WAISLAMU KWA MAANDALIZI YA KUTISHA :

 Faida

          Jeshi la waislamu likatoka likiwa na zawadi ya wasia wa Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie. Likisindikizwa na kila aina ya dua za waislamu, Bwana Mtume akalisindikiza mpaka katika jangwa la Wadaa, hapo akaagana nalo na kurejea Madinah. Na mkakati ulio kuwa umepangwa na jeshi ni kumshambulia adui kwa kumshtukiza kabla hajajiandaa. Lakini khabari za kutoka kwa jeshi hili zikavuja na kumfikia adui, akaanza kujiandaa. Maandalizi yao yakawa ya kutisha kwa idadi ya askari na zana za vita kwa kiwango kinacho tunduwaza na kuduwaisha. Kiwango kinacho onyesha nguvu, utajiri, fahkri na mamlaka kiasi cha kuwastaajabisha waislamu.

Amepokea Al-Waaqidiy-Allah amrehemu-kwa isnadi ya Abu Hurayrah-Allah amuwiye radhi-amesema: Nilihudhuria Mu'utah, mushrikina walipo tukaribia tuliona maandalizi ya silaha na watu yasiyo weza kukabiliwa na ye yote. Macho yakakodoka, Thabit Ibn Arqam akaniambia: Ewe Abu Hurayrah, kama wewe unaona makusanyo kathiri. Nikamjibu: Naam, akasema: Hakika wewe hukuhudhuria (vita vya) Badri pamoja nasi, kwa yakini sisi hatunusuriwi (kwa sababu ya) wingi (wa watu/zana)!

Riwaya zinakurubia kujumuika kwamba Warumi waliwapokea waislamu kwa askari laki mbili; laki moja ikiundwa na Warumi wenyewe na nyingine ikiundwa na manasara wa Kiarabu. Waislamu kupokewa na idadi hii ya kutisha, hakika inahisisha kwamba Warumi walifadhaika mno pale walipo tambua kwamba waislamu wamewatokea. Na kwamba walikuwa wakijaribu kuufikiria upeo wa nguvu ya waislamu isiyo ya kawaida. Nguvu iliyo eneza khofu pande zote za Peninsula ya Kiarabu, nguvu ambayo majeshi shirika yameshindwa mbele yake. Nguvu ambayo ngome madhubuti za Mayahudi pamoja na nguvu yao kubwa, havikuweza kuthibiti mbele yake. Nguvu ambayo ilimpa Muhammad ujasiri wa kumlingania Uislamu Hiraqli pamoja na mamlaka na nguvu zake alizo kuwa nazo. Naam, hapana budi kwamba wao walianza kuusawirisha upeo wa nguvu hii na kuiona kuwa ni kitu kisicho wezwa. Ndipo walipo anza kuiandalia nguvu zote waziwezazo na kama huu si ukweli, basi je ni jambo la kawaida watu laki mbili kujikusanya kwa ajili ya kupigana na watu alfu tatu?!

 

 

SOMO LA PILI.

 

         i.        Ibn Rawaahah awashajiisha waislamu kupambana na warumi:

         Waislamu hawakuwa wakiifikiria nguvu na maandalizi ya adui yao, walipo fika "Maan"; hii ni ngome kubwa katika nchi ya Palestina umbali wa mwendo wa siku tano kwa ngamia kutokea Damascus (Syria). Hapo ndipo walipojua maandalizi ya idadi na zana yanayo wangojea, wakapiga kambi hapo siku mbili wakishauriana juu ya suala hili. Kisha wakapata wazo la kumuandikia barua Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-wamueleze hali halisi waliyo ikuta huko. Ili ama awaongezee nguvu au awape shauri la kufanya walitekeleze, lakini Abdullah Ibn Rawaahah akazidiwa na mori wa imani, akainuka akiwashajiisha wenzake akiwaambia: "Enyi kaumu yangu! Hakika kile mnacho kichukia, kwa yakini ni kufa shahidi ambako mmetoka mkikutafuta. Wallah sisi hatukuwa tukipigana na watu kwa wingi wa idadi wala silaha wala wingi wa farasi. Hatupigani nao ila ni kwa sababu ya dini hii ambayo Allah ametutukuza kwayo. Enendeni, wallah mmeona siku ya (vita vya) Badri hatukuwa ila na farasi wawili na siku ya Uhud hatukuwa ila na farasi mmoja tu! Enendeni, hakika si vinginevyo, hilo ni mojawapo ya mazuri mawili; ama kuwashinda na hilo ndilo alilo tuahidi Allah na Mtume wake na miadi ya Allah haina kukhalifiwa. Au kufa shahidi, basi tukutane na ndugu zetu (katika imani) tuambatane nao peponi".

Maneno haya ya Ibn Rawaahah yakatenda ndani ya nafsi za watu kile kitendwacho na uchawi, wakasonga mbele kukutana na adui wakiwa hawajali cho chote. Wakaenda mpaka wakafika baada ya mwendo wa siku mbili "Al-Balqaa" katika nchi ya Shamu. Hapo wakayakuta makundi makubwa ya adui yakiwa yamejikusanya katika kijiji kinacho itwa "Mashaarif". Vikosi vya adui vikaanza kuwajongelea, waislamu wakajikusanya katika kijiji cha Mu'utah ili wapate ngome hapo. Lakini Warumi wakawashukia mithili ya mumbwi wa maji, wakasonga mbele na farasi wao katika mandhari inayo kodosha macho na kudumaza akili. Waislamu wakaikabili hali hiyo ya kutisha kwa kuzikusanya pamoja nguvu zao na wakapigana katika utaratibu wa "shinikizo mkusanyiko kwa katikati". Wakaweka pande zote mbili nguvu inayo zuia kuzungukwa na adui, upande wa kulia akawepo Qutwbah Ibn Qataadah na ule wa kushoto alikuwepo Ubaadah Ibn Maalik. Majeshi haya mawili yakapambana katika mpambano mkali kabisa kuwahi kutokea katika historia ya mapambano ya waislamu dhidi ya makafiri.

 

 

       ii.        Mpambano ulikuwa ni mkali mno:

         Zayd Ibn Haarithah akaongoza mapambano chini ya bendera ya Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie. Waislamu nao wakapigana pamoja nae wakiwa wamekamatana barabara katika safu zao mpaka damu ya Zayd ikachuruzika mithili ya maji na viungo vyake vikatapanyika. Zayd alipouawa, bendera ya waislamu ikashikwa na Ja'afar Ibn Abu Twaalib kama alivyo agiza Mtume wa Allah. Akaongoza mapambano ya kufa na kupona chini ya bendera hiyo, hata mpambano ulipo mmaliza nguvu kabisa na akazungukwa na adui. Alimrukia farasi wake na kumchinja kwa upanga wake, kisha akajitosa katikati ya maadui akipigana nao akienda kwa miguu na bendera akishika kwa mkono wake wa kulia. Ukapigwa upanga mkono wake wa kulia ukakatwa, akaishika bendera kwa mkono wake wa kushoto, nao pia ukakatwa. Akaikumbatia bendera kwa vifupa panya vyake mpaka akauwa, mwili wake ukakutwa na michomo ya mikuki kiasi cha tisini. Baada ya kuuawa Ja'afar, bendera ikatwaliwa na Abdullah Ibn Rawaahah. Kinacho dhihirika hapa ni kwamba mpambano katika vita hivi ulikuwa ni mkali mno kiasi cha kuwafanya waislamu kujisahau, wasikumbuke hata kula na kunywa. Ibn    Is-haaq-Allah amrehemu-amepokea riwaya kwamba Abdullah Ibn Rawaahah alipo shuka mpambanoni, binamu yake alimletea mfupa wa nyama, akamwambia: "Hebu utie nguvu uti wa mgongo wako kwa kula mfupa huu, kwani hakika wewe umekutana na hali nzito katika siku zako hizi". Akautwaa mfupa ule na kung'ata pande, halafu akasikia mzongo upande wa mahasimu wao, akasema: "Na wewe uko duniani?, akautupa mfupa ule, akautwaa upanga wake akasonga mbele akipigana mpaka akauawa.

 



 | Tuandikie |