Makala
Uislamu-Utangulizi
Fiqhi na Sheria 
Akhlaaq-Tabia
Sira ya Mtume
Nasaha za dini
Maswali na Majibu
Uliza Suala la dini
Jiunge na Mtandao !!!

 

SIRA YA MTUME (SAW)  

"BILA SHAKA MNAO MFANO MWEMA KWA MTUME WA MWENYEZI MUNGU…"Al-qur-an (33:21)

III. HILA/MBINU YA KAMANDA KHALID YALIOKOA JESHI LA WAISLAMU

 Faida

 

                 iii.          Hila/mbinu ya kamanda Khalid yaliokoa jeshi la waislamu:

         Baada ya kuuawa kwa kamanda Ibn Rawaahah, waislamu wakawafikiana kumteua Khalid Ibn Al-Waleed kuwa kamanda wao mpya atakaye waongoza katika mapambano yao dhidi ya jeshi kubwa la Warumi. Alipoitwaa bendera ya vita, akaongoza mapambano ya kumrudisha nyuma adui na kumzungusha mpaka giza likaingia na kila kundi kurudi kambini kwake kujiandaa na mpambano wa siku ifuatayo. Ni chini ya pazia la usiku huu, ndipo kamanda huyu shujaa alipo ibuka na mbinu ya kubadilisha mpango mzima wa jeshi katika medani ya vita. Kikosi kilicho kuwa kikipigana upande wa kulia akakipeleka kushoto na kile cha kushoto akakihamishia kulia. Cha mbele akakihamishia nyuma na kile cha nyuma akakileta mbele na akaandaa kundi maalumu nyuma ya jeshi kutimua vumbi na kupiga makelele wakati wa maawio. Majeshi mawili haya yalipo kutana asubuhi, kila kikosi cha adui kikaziona nyuso ngeni tofauti na zile ilizo ziona jana yake na wakaona bendera nyingine sio zile walizo ziona. Hili likawadhanishia kwamba waislamu wamepata nguvu mpya, wakaogopa kuingia mpambanoni, kwani bado walikuwa na fikra za mpambano mkali wa jana yake. Ambapo waislamu walikuwa wachache lakini waliwapeleka mchakamchaka na kuua idadi isiyo kidogo, haya leo tayari wameongezeka hali itakuwaje?! Hila/mbinu hii ya kamanda mahiri Khalid-Allah amuwiye radhi-ikafanikiwa kumukhadaa adui. Nae akaitumia vema khofu yao hiyo, akawa anawazungusha askari wake na kurejea nyuma kwa umahiri makini. Mpaka Warumi wakadhania kuwa hiyo ni mbinu ya kuwavutia jangwani ili wakawasagesage huko, kwa hivyo hawakuwafuata. Khalid nae akaendeleza mapambano mepesi dhidi ya makundi makubwa ya adui mpaka akafanikiwa kuliponyosha jeshi lake mikononi mwa adui mwenye uchu wa kuangamiza. Kwa mbinu yake hii akawa amefanya kinacho paswa kufanywa na kamanda mahiri mwenye uoni wa mbali katika hali/mazingira kama hayo. Na bora ya kinacho fanywa katika hali kama ile ni kurejea nyuma kwa amani, kitu ambacho pengine ni kigumu zaidi kuliko kupata ushindi. Hii ni kwa sababu kupata ushindi ni jambo linalo wezekana kwa nyenzo ya wingi wa zana, watu na kustahamili. Lakini kurudi nyuma kwa salama mbele ya adui mwenye zana na watu si suala liwezwalo na kila mtu ila awe mtu huyo na ujuzi wa masuala ya uongozi katika medani ya vita.

 

         iv.          Mtume atangaza kuuawa kwa maamiri jeshi na kuusifia ushujaa wa Khalid:

         Hivi ndivyo Khalid alivyo weza kuliokoa jeshi lake dhidi ya hilaki dhahiri na kurudi nalo bila ya kupoteza ila roho kumi na mbili tu. Kabla jeshi halijakanyaga ardhi ya Mu’utah, Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akawatangazia maswahaba wake Madinah khabari za kuuawa kwa maamiri jeshi wake. Alitoa tangazo hilo ilhali macho yake yakifurika machozi kwa kuwahuzunikia. Imamu Bukhaariy-Allah amrehemu-amepokea kwa Isnadi ya Anas Ibn Maalik-Allah amuwiye radhi-kwamba Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-aliwatangazia watu kuuawa kwa Zayd, Ja’afar na Ibn Rawaahah kabla ya ujio wa khabari hiyo, akasema (mithili ya mtangazaji wa redio): “Bendera imetwaliwa na Zayd, ameuawa, kisha akaichukua Ja’afar nae akauawa, ikachukuliwa na Ibn Rawaahah nae akauawa – (na macho yake yakibubujika machozi) – mpaka ukaichukua bendera upanga miongoni mwa panga za Allah, hadi Allah akaleta ushindi juu yake”.

Khabari za tukio hili zilileta mshindo mkuu ndani ya nafsi za waislamu mpaka watu wa Madinah wakubwa kwa wadogo wakatoka kwenda kulilaki jeshi. Watoto wadogo nao hawakubakia nyuma, wakatoka wakikaza mwendo mpaka Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akiwaonea huruma kutokana na umbali mrefu walio kimbia, akasema: “Watwaeni watoto, muwabebe na mimi mnipe mtoto wa Ja’afar”. Mtume akamtwaa Abdullah Ibn Ja’afar akambeba mbele yake juu ya mnyama wake mpaka wakakutana na jeshi mahala paitwapo “Al-Jurfu”. Watu wakadhania kwamba jeshi limeshindwa, wakaanza kuwamwagia mchanga wa uso huku wakisema: “Enyi watimua mabio nyie! Hivi mmekimbia katika njia ya Allah?!”, Mtume-Rehema na Amani zimshukie-akiwaambia: “Wao si watimua mabio, lakini wao ni wenye kuswaga, insha-Allah”.

 

SOMO LA TATU

             i.          Msimamo wa Ibn Rawaahah:

         Riwaya/mapokezi yanatofautiana katika kutaja msimamo wa Ibn Rawaahah pale alipotwaa bendera ya uongozi wa jeshi baada ya kuuawa kwa kamanda Ja’afar. Ibn Is-haaq-Allah amrehemu-yeye amepokea kwamba zama Abdullah Ibn Rawaahah alipo itwaa bendera alisonga nayo mbele akiwa juu ya farasi wake. Akawa anajitoma medanini na huku anasita kidogo, kisha ndipo akajitoma mzima mzima, akapigana hata akauawa. Na Al-Waaqidiy-Allah amrehemu-anasema: Ibn Rawaahah alipigana na adui kwa muda kidogo kisha tim akatimua mbio. Akailaumu nafsi yake kwa nini amekimbia, akashuka kutoka katika farasi wake akapigana na adui mpaka akauawa shahidi kama mtangulizi wake. Na wala Imamu   Al-Baihaqiy na Musa Ibn Uqbah-Allah awarehemu-hawakutaja cho chote kuhusiana na msito huu kama walivyo nukuliwa na Ibn Kathir-Allah amrehemu. Kadhalika Al-Muqriziy-Allah amrehemu-hakulitaja hilo katika kitabu chake [IMTAAUL-ASMAAU], wala Ibn Sa’ad katika [ATTWABAQATIL-KUBRAA].

Na Abdullah Ibn Rawaahah-Allah amuwiye radhi-kama anavyo sema Ibn Is-haaq mwenyewe na Wanasira wengine, ndiye aliye washajiisha na kuwahamasisha waislamu kupigana na Warumi pale waliposita kufanya hivyo. Nae ndiye aliye tajwa na Ibn Is-haaq katika riwaya yake kwamba alikitema kipande cha nyama kilicho kuwa kinywani mwake wakati alipoona vita vinauma. Na akaona vibaya kubakia duniani hata kwa kipindi kidogo nae akiwa  mbali na medani ya vita. Hivi haiwi kuwa kuna mgongano kwa mtu mwenye ari na yakini kama hii kuingia katika medani ya vita akiwa anasita na kukhofu?! Kisha haiwi ni kukinzana yeye kuwashajiisha wenzake kupigana na Warumi, halafu yeye mwenyewe akawa muoga?! Basi ni wapi alikuwa Ibn Rawaahah wakati vilipo anza vita baina ya waislamu na Warumi?! Hivi yeye hakuwa akipigana katika vita hivyo kama mmojawapo wa jeshi la waislamu?! Na je, kweli inaingia akilini kuwa shujaa mstari wa mbele kama askari, halafu awe mwenye kusita na khofu akiwa kamanda?!!!

 



 | Tuandikie |