Makala
Uislamu-Utangulizi
Fiqhi na Sheria 
Akhlaaq-Tabia
Sira ya Mtume
Nasaha za dini
Maswali na Majibu
Uliza Suala la dini
Jiunge na Mtandao !!!

 

SIRA YA MTUME (SAW)  

"BILA SHAKA MNAO MFANO MWEMA KWA MTUME WA MWENYEZI MUNGU…"Al-qur-an (33:21)

II. VITA HIVI VIMEWASAJILIA WAISLAMU DARSA GANI ?

 Faida

 

  

      ii.          Vita hivi vimewasajilia waislamu darsa gani?

         Riwaya zinakhitilafiana katika kueleza khatima ya vita hivi: Je, vita hivi vilimalizika kwa waislamu kupata ushindi au kushindwa? Ibn Sa’ad-Allah-amrehemu-amepokea riwaya kutoka kwa Abu Aamir-Allah amuwiye radhi-ambaye alihudhuria kwa maana ya kushiriki vita hivyo: “Kwamba waislamu walisambaratishwa vibaya sana baada ya kuuawa kwa (kamanda wao) Ibn Rawaahah na wakatapanyika kiasi cha kutoonekana wawili wakiwa pamoja. Kisha akaitwaa bendera mmoja katika Maasnwaari akaisimika mbele ya watu, akaanza kuwapigia ukelele nao wakikusanyika. Hata walipo kuwa wengi akaenda na bendera mpaka kwa Khalid Ibn Al-Waleed akamkabidhi. Khalid alipo itwaa bendera aliwaendesha mbio watu wale (Warumi) vibaya mno kiasi cha kufikia waislamu kuziweka (kuwapiga) panga zao watakapo”.

Na al-Waaqidiy-Allah amrehemu-amepokea kutoka kwa    Al-Utwaaf Ibn Khalid-Allah amuwiye radhi: “Kwamba alipo uawa Ibn Rawaahah jioni, alilala Khalid Ibn Al-Waleed, kulipo pambazuka alidamka akiwa tayari amekipeleka mbele kikosi cha nyuma na kukirudisha nyuma kile cha mbele. Cha kulia akakipeleka kushoto na kile cha kushoto akakileta kulia, hapo ndipo makafiri walipo sema: Bila ya shaka umewajia msaada (nguvu mpya zaidi), wakaogofywa wakatapanyika hali ya kushindwa. (Waislamu) wakaua miongoni mwao idadi kubwa ambayo watu wale hawakupata kuua kwa waislamu”.

Na Musa Ibn Aqabah-Allah amrehemu-yeye anasema: “Waislamu waliridhiana baada ya (kuuawa kwa)  maamiri jeshi (walioteuliwa) na Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-kumteua Khalid Ibn Al-Waleed Al-Makhzuumiy (kuwa amiri jeshi wao). Hapo Allah akamtimua adui na kuwapa ushindi waislamu”.

Ibn Is-haaq-Allah amrehemu-anasema: “Thabit Ibn Aqram alichukua bendera akasema: Enyi kusanyiko la waislamu ridhianeni juu ya mtu miongoni mwenu (awe amiri wenu). Wakasema: Wewe (tumekuridhia), akasema: Mimi siliwezi jukumu hilo. Ndipo watu walipo ridhiana kumteua Khalid Ibn Al-Waleed, alipo itwaa bendera (ya uongozi) aliwarudisha nyuma watu wale (Warumi), kisha wakatawanyika hata akaweza kuondoka na watu (maswahaba)”.

Ibn Kathir-Allah amrehemu-amenukuu katika kitabu chake [AL-BIDAAYATU WAN-NIHAAYAH] maneno ya Ibn Ishaaq, Al-Waaqidiy na Musa Ibn Uqbah, halafu akasema: “Kunamkinika kujumuisha baina ya kauli ya Ibn Is-haaq na wengineo na mjumuisho huo ni kwamba zama Khalid alipo itwaa bendera aliwanasua waislamu mpaka akawaokoa kutoka mikononi mwa makafiri wale wa Kirumi. Kulipo pambazuka na akabadilisha mpango wa jeshi (katika medani ya vita), kulia na kushoto, mbele na nyuma-kama alivyo litaja hilo Al-Waaqidiy. Warumi wakadhania kwamba hilo linatokana na nguvu mpya iliyo wajia waislamu, Khalid alipo warudisha nyuma, wakawashinda kwa idhini ya Allah”...Ibn Kathir-Allah amrehemu-akaitilia nguvu rai yake kwa kauli ya Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-iliyomo katika hadithi iliyo pokelewa na Imamu Bukhaariy-Allah amrehemu-kutoka kwa Anas Ibn Maalik-Allah amuwiye radhi: “Halafu ukaitwaa bendera upanga miongoni mwa panga za Allah, Allah akaleta ushindi kupitia mikono yake”. Kama alivyo toa ushahidi kwa kauli iliyo tajwa na Al-Waaqidiy na Musa Ibn Uqbah na alivyo taja Ibn Is-haaq ya kwamba Qutwbah Ibn Qataadah – nae ndiye aliyekuwa kiongozi wa kikosi cha kulia cha waislamu. Alimrudisha nyuma Ibn Rawaahah – nae ndiye (aliye kuwa) amiri – jeshi wa (kundi la) Waarabu wa Kinaswara, akamuua.

    iii.          Ushindi na ushindwa katika medani ya vita hupimwa na malengo yaliyo fikiwa:

         Ni mamoja kuwa yaliyo tokea ni yale yalipokewa na Ibn Is-haaq au na wengineo, hakika si hali ya kawaida watu alfu tatu kuwashinda watu laki mbili na kufanikiwa kuchukua mateka. Au kuwaua hadi kuwafagia kabisa, inatosha tu kwamba wao pamoja na uchache wao kuweza kusimama mbele ya idadi hii ya kutisha kwa siku moja au zaidi katika mapambano makali kabisa. Kisha wakaweza kutoka ilhali hawakuuawa miongoni mwao ila watu kumi na mbili tu. Lau kama waislamu wangelitoka kwenye vita hivi bila ya kumuua adui hata mmoja, bado huo ungekuwa ni ushindi kwao. Basi ni hali gani na kwa yakini imepokewa katika baadhi ya riwaya kwamba wao waliua miongoni mwao (hao Warumi) idadi ambayo wao (Warumi) hawakuua kwao (Waislamu)?! Na kwamba mushrikina walisambaratika mbele yao kiasi cha waislamu kuwafyeka kwa panga watakavyo?!

Na huenda pakasemwa: Hakika maneno haya yametiwa chimvi. Lakini sura zilizo onyeshwa na waislamu katika vita hivi dhidi ya Warumi, zinaya thibitisha madai haya kwa kiwango kikubwa kabisa. Kwani waliuawa mfululizo maamiri jeshi wote watatu (walio teuliwa na Mtume) katika siku ya kwanza tu ya vita. Na hili lilitosha kuwapelekea waislamu kukimbia au kusambaratika, kwani ada/desturi ya zama hizo ilikuwa ni jeshi kutimua mbio pale anapo uawa amiri jeshi wao. Na huenda hili ndilo lililo mfanya adu kuzielekeza hujuma zake kwa maamiri, lakini pamoja na yote hayo bado waislamu hawakutimua mbio. Bali walithibiti na kuendelea kusimama kidete mbele ya adui yao mpaka ukaingia usiku ambapo kila kundi lilirejea kambini kwake kujiandaa na mpambano wa kesho. Na lilikuwa ni jambo mumkini kwa waislamu kukimbia wakaenda zao salama chini ya pazia la usiku huu, lakini katu hawakufanya hivyo. Bali walidamka mapema kwenda mpambanoni katika namna/mtindo ulio waogofya na kuwatetemesha Warumi mpaka wakakosa kujiamini, wakashindwa kuwashambulia waislamu. Hapo waislamu wakafurahi kwa kurudi kwao nyuma, basi hii ni taswira miongoni mwa taswira jumla za vita zilizo onyeshwa na waislamu katika vita hivi. Ama taswira binafsi, aliyo ionyesha kila mtu miongoni mwao. Hii hapa iliyo onyeshwa na Ja’afar Ibn Abi Twalib-Allah amuwiye radhi-pale alipo shuka kitatangeni akiwa juu ya farasi wake akiwachoma panga adui. Mpambano ulipo muhemea akashuka juu ya farasi wake, akamchinja kwa upanga wake, kisha akaanza kupigana akitembea na ilhali kaishika bendera kwa mkono wake wa kulia. Ulipo katwa mkono huu wa kulia, akaibeba bendera kwa mkono wa kushoto, nao ulipo katwa akaikumbatia kwa vifupa panya vyake hadi akauawa.

Taswira nyingine pia inaonyeshwa na Khalid Ibn Al-Waleed-Allah amuwiye radhi-pale aliposema kama ilivyo pokewa na Imamu Bukhaariy-Allah amrehemu: “Ulipogongwa mkono wangu mapanga tisa siku ya vita vya Mu’utah, basi haukubakia mkononi mwangu ila ubapa wa kulia”. Haya wewe unaonaje, Khalid aliua watu wangapi hata akasibiwa na panga hizi zote?! Na wenzake miongoni mwa mashujaa walio hifadhi Qur-ani waliua watu wangapi katika kundi kubwa la adui?! Na tunainyaka kwa haraka sura nyingine miongoni mwa sura za kusonga mbele na kuyavaa mauti bila ya kujali. Sura hii tunaiona kupitia idadi hii ya chomo za panga zilizo elekezwa kwa Sayyidina Ja’afar-Allah amuwiye radhi-mpaka ikasemwa kuwa ilikuwa michomo zaidi ya tisini. Hakika ikiwa michomo hii inafahamisha kitu, basi inafahamisha juu ya upeo wa muislamu katika kuifia dini yake na upeo wa kujitoma kwake ndani ya safu za adui bila ya kujali wingi na nguvu ya adui huyo.

    iv.          Vita vya Mu’utah vilibakisha athari gani katika nafsi za Warumi?

         Hakika sura hizi na nyinginezo tunazo farijika nazo katika vita hivi, zinatujengea taswira-jumla iliyo achwa na waislamu ndani ya nafsi za adui yao siku ya Mu’utah. Kwa hivyo basi ni israfu ya maneno na sisi kutia chumvi kuwakalifisha waislamu kutenda zaidi ya hayo waliyo yatenda. Na tunasema kuwa kwa hayo waliyo yatenda, wao waliwashinda mushrikina katika vita hivi. Na iwapo mambo huzingatiwa kutokana na natija (matokeo) zake na matendo huzingatiwa kwa khatima yake. Ikiwa hivyo ndivyo, basi inatosha kuwa ni ushindi kwa waislamu kwamba wao waliacha athari ya khofu ndani ya nafsi za adui yao. Khofu iliyo wafanya kuacha mapambano na kuogopa kuwafuata pale waislamu walipo kuwa wakirudi nyuma kwa umahiri mkubwa. Na kwamba athari hii ilitosha kabisa kuipa amani mipaka ya dola ya Kiislamu kwa upande wa Shamu. Si Warumi wala washirika wao miongoni mwa Waarabu walio jasiri kuwashambulia waislamu baada ya vita hivi. Na athari hii iliendelea mpaka siku ya vita vya “Tabuuk”, pale Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alipo waongoza maswahaba wake kwenda kupambana na Warumi baada ya mwaka. Siku hiyo Warumi hawakuweza kusimama na waislamu na badala yake wakakhiari amani kuliko kupambana na hasimu huyu ambaye ameitoa nafsi yake katika kuilinda na kuitetea dini yake. Adui asiye jali mauti wala kuogopa vita hata kama adui ana nguvu kubwa zilizoje.

Vita hivi si tu viliacha athari kwa Warumi na washirika wao peke yao, la hasha, bali athari hii ilivuka mipaka na kupindukia katika nafsi za makabila. Makabila yaliyo kuwa yakiishi nchani nchani mwa Shamu na Iraq, yalibakia na athari kubwa ya kushangazwa na waislamu. Athari iliyo wapelekea wengi miongoni mwa makabila ya Baniy Suleim, Ash-jaa, Ghatwfaan, Absi, Dhubyaan na Fazaarah kuingia katika Uislamu kwa khiari zao wenyewe.

 



 | Tuandikie |