Makala
Uislamu-Utangulizi
Fiqhi na Sheria 
Akhlaaq-Tabia
Sira ya Mtume
Nasaha za dini
Maswali na Majibu
Uliza Suala la dini
Jiunge na Mtandao !!!

 

SIRA YA MTUME (SAW)  

"BILA SHAKA MNAO MFANO MWEMA KWA MTUME WA MWENYEZI MUNGU…"Al-qur-an (33:21)

SURA YA KUMI NA MBILI -
FAT-HU MAKKAH

 Faida

SOMO LA KWANZA.

      i.        Makah ndio ilikuwa kitovu cha vitongoji vyote vya Hijaazi na ngome kuu ya dini ya masanamu:

         Hivyo ndivyo ilivyo kuwa Makah katika Peninsula nzima ya Kiarabu na Al-Ka'abah ndio iliyo kuwa makao makuu ya miungu-masanamu na welekeya wa macho ya watu wote. Na ndio iliyo kuwa dango la matumaini ya makabila yote, yale ya karibu na yale ya mbali. Na Makureishi ndio walio kuwa walinzi na waangalizi wa Al-Ka'abah na ndio walio kuwa wameshikilia hatamu za uongozi wa kidini na kisiasa. Na daraja/hadhi ya makabila mengine kwa Makureishi ilikuwa ni hadhi ya bwana na mtwana au kiongozi na muongozwa. Kwa mtazamo huu, ndio makabila ya Kiarabu kwa tofauti zao yalikuwa yakifuatilia kwa makini na karibu kabisa mpambano ulio kuwa ukiendelea baina ya Muhammad na Makureishi. Na wakifuatilia harakati na hatua zake mfuatilio – makini, na harakati na hatua zote hizi zilikuwa zikiacha athari za wazi katika mielekeo ya makabila haya. Mielekeo kwa upande wa ama kuukubali Uislamu au kuukataa na ama kuunga mkono au kuupinga.

Na pamoja na vita na matukio yaliyo duru baina ya waislamu na Makureishi kwa upande mmoja, na baina ya waislamu na mayahudi kwa upande wa pili. Na kwa upande mwingine baina ya waislamu na warumi na makabila ya Kiarabu ya pande za Peninsula. Yalikuwa na athari katika kudhihiri na kuenea kwa Uislamu miongoni mwa makabila mengi, hakika Makah kuendelea kubakia katika ushirikina wake nayo ikiwa ndio kitovu cha vitongoji vyote na ngome kuu ya dini – sanamu. Ilikuwa ni kizuizi na kikwazo dhidi ya kutawala kwa Uislamu katika Peninsula nzima ya Kiarabu. Na ili Peninsula iufuate Uislamu na makabila yauridhie kuwa dini na itikadi yao, ilikuwa hapana budi Makureishi wauamini kwanza Uislamu na ukumbatiwe na Makah iliyo kitovu cha vitongoji.

    ii.        Suluhu ya Hudaybiyah ilikuwa ndio mwanzo wa kuanguka kwa ngome hii kongwe:

         Suluhu (mkataba) ya Hudaybiyah baina ya Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-na Makureishi mnamo mwaka wa sita Hijiria, ilikuwa ndio ufunguo wa kwanza wa ngome hii kongwe. Katika suluhu hiyo, Makureishi walikiri kwamba Muhammad ni kiongozi wa itikadi mpya na kwamba hapana ubaya kuandikiana nae mkataba utakao zihakikishia amani pande mbili hizi hasimu. Wakalazimika kufikia azimio/uamuzi huo baada ya jitihada zao za kuutokomeza Uislamu kugonga mwamba. Makureishi walibakia kwa takriban miongo miwili wakiwa hawamtambui mtume, wala dini hii anayo itangaza ambayo inaikhalifu dini na itikadi yao. Wakashikilia utukufu na ukubwa wao huku wakimzulia mtume uongo mbali mbali na kumvika sifa mbaya mbaya kwa lengo la kumchafulia jina lake na kuubomoa mlingano wake miongoni mwa Waarabu. Zama walipo shindwa kwa njia na mbinu zao zote kuutokomeza Uislamu na kumuua kiongozi wake, ndipo walipo lazimika kuamiliana nae muamala wa mpinzani kwa mpinzani. Na kufanya suluhu japo kwa muda mchache ili kujikinga na hatari yake na kupata amani upande wake. Na suluhu hii ikawa ndio ufunguo wa mwanzo ambao Allah aliutumia kufungulia milango na makomeo ya Makah.

  iii.        Umrah ya Qadhaa ikawa ndio ufunguo wa pili wa ngome hii:

         Baada ya mwaka huo, Umrah ya Qadhaa ikawa ndio ufunguo wa pili wa ngome hii. Kwani mdhihiriko wa waislamu katika Umrah hii nao wakiwa katika hali ya kupendana na kuhurumiana kwao, kuzoeana na kushikamana kwao. Nidhamu yao ya hali ya juu kabisa katika kumtii kiongozi na mapenzi ya kweli na ikhlasi yao kwa Mtume wao. Na hamasa yao kubwa kuielekea dini yao na kushikamana kwao kidhati na adabu zake, na kuitakafutiza kwao upeo nyumba tukufu ya Allah na kuyaadhimisha matukufu yake. na yote waliyo kuwa wakiyatekeleza katika Umrah hii, wakiwa ndani ya hamasa hii, mshikamno huu, nidhamu hii na kujiweka kwao mbali na kila linalo tia dosari tabia za mtu. Mdhihiriko wa waislamu katika yote haya, ulidhihirisha na kutusha mtikisiko adhimu ndani ya nafsi za watu wa Makah. Na ukagusa tao la imani ndani ya nyoyo zao na kulitikisa mtikisiko mkubwa, basi wakawa wanawaangalia waislamu mtazamo wa kushangazwa nao na ukubwa. Na wakauangalia Uislamu mtazamo wa tafakari – mazingatio na wakawa wanajaribu kufanya mlinganyo baina ya dini hii mpya na itikadi waliyo nayo wao. Na baina ya mapokeo yasiyo kubaliwa na akili na yasiyo thibitishwa na mantiki na wakiweka katika mizani matukufu haya yatekelezwayo na waislamu kwa unyenyekevu mkubwa na moyo mmoja na puo na mchezo waufanyao wao katika ibada zao, kama tunavyo soma: "NA HAIKUWA IBADA YAO KWENYE HIYO NYUMBA (Al-Ka'abah) ILA KUPIGA MIUNZI NA MAKOFI..." [8:35]

Naam, wakaanza kuchunguza na kutafakari na wakagundua tofauti kubwa na ya mbali baina ya itikadi yao na ile itangazwayo na Muhammad. Hapo nyoyo zao zikaulainikia Uislamu na vifua vyao kuusikiliza, kwa ajili hii wakasilimu miongoni mwao walio weza kuudhihirisha Uislamu wao. Na wakausirisha Uislamu wale wasio weza kuutangaza kwa sababu ya unyonge wao. Na wengi miongoni mwao wakajiandaa kwa nyoyo na nafsi zao kusilimu, lau kama si pingamizi – mazingira na manufaa ya muda yaliyo wazuia kwa kitambo tu. Mtikisiko huu ulio ipata itikadi ya watu wa Makah katika Umrah ya Qadhaa, ukawa ni ufunguo mwingine ambao Allah aliutumia kufungulia makomeo ya Makah.

  iv.        Hatimaye Makureishi wauvunja mkataba wa amani wa Hudaybiyah;

         Kisha baada ya hapo, Allah Taala akataka kufungua makomeo yote yaliyo bakia ya ngome hii, yakatokea yaliyo tokea katika mwaka wa nane; yaani Makureishi kuvunja mkataba ule wa Hudaybiyah. Ilivyo kuwa ni kwamba yalikuwepo machafuko ya umwagaji wa damu baina ya kabila la Bakri na Khuzaah katika zama za Jahilia. Ilipo fikiwa suluhu ya Hudaybiyah na kabila la Khuzaah likaingia katika ushirika na Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie. Na lile la Bakri likawa mshirika wa Makureishi, vita vikasita baina ya makabila mawili haya na kila moja likapata amani upande wa adui yake. Kisha ikatokezea kwamba siku moja mtu mmoja wa kabila la Bakri kusimama na kuanza kumfanyia istihizai na kebehi Mtume wa Allah mbele ya usikivu wa mtu wa kabila la Khuzaah; washirika wa Mtume. Yule Mkhuzaai akashindwa kustahamili, akainuka na kumpiga mchokozi yule, kitendo hicho kikauamsha na kuuchochea uadui wa tangu ulio kuwepo baina ya makabila mawili hayo. Kabila la Bakri ambalo mtu wao kapigwa, likaanza kujiandaa kulipa kisasi kwa kabila la Khuzaah na wakasadiwa juu ya hili na watu katika Makureishi. Usiku mmoja watu kadhaa wa kabila la Khuzaah walikuwa katika eneo lao lenye maji likiitwa "Al-Watiyr", wakavamiwa na watu wa kabila la Bakri na washirika wao Makureishi. Khuzaah kuona hivyo, wakakimbilia katika "haram" – eneo takatifu la Al-Ka'abah ili kupata hifadhi hapo, lakini hilo halikuwazuia Wabakri kuwafuata, wakawashambulia na kuua miongoni mwao kiasi cha watu ishirini. Hapo ndipo Wakhuzaah walipo muomba msaada Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-wakatuma ujumbe wa watu Madinah. Wakamkhabarisha Bwana Mtume khiana waliyo fanyiwa na Wabakri na namna walivyo saidiwa na Makureishi. Mtume akamwambia kiongozi wao baada ya kuwasilisha malalamiko yao kwa njia ya ushairi: "Umenusuriwa ewe Amrou Ibn Salim". Kwa hili Mtume akaona ndio fursa muafaka ya kuifungua Makah, akaanza kujiandaa kwa ajili ya ufunguzi huu.

 



 | Tuandikie |