Makala
Uislamu-Utangulizi
Fiqhi na Sheria 
Akhlaaq-Tabia
Sira ya Mtume
Nasaha za dini
Maswali na Majibu
Uliza Suala la dini
Jiunge na Mtandao !!!

 

SIRA YA MTUME (SAW)  

"BILA SHAKA MNAO MFANO MWEMA KWA MTUME WA MWENYEZI MUNGU…"Al-qur-an (33:21)

V. ABU SUFYAN AJARIBU UPEO WA UWEZA WAKE KUSAHIHISHA MAKOSA YALIYOFANYWA NA MAKUREISHI

 Faida

          Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akakadiria kwamba Makureishi watadiriki ubaya wa kitendo walicho kitenda. Na kwamba hapana budi watamtumia ujumbe ili kutengeneza hali/uhusiano ulio haribiwa na khiana yao, ndipo Mtume akawaambia maswahaba wake: "Kama kwamba Abu Sufyaan amekujilieni ili kuutia nguvu mkataba na kuongeza muda". Yote aliyo yakadiria na kuyatazamia Mtume, yakatokea kama alivyofikiria, kwani Makureishi walihisi mwisho mbaya utakao ifuatia khiana yao. Wakamtuma Madinah kiongozi wao Abu Sufyaan Ibn Harb ili pengine yeye anaweza kuyadiriki na kuyasahihisha matokeo ya kosa hili baya. Na Abu Sufyaan alikuwa anauhisi uzito wa suala hili analo liendea, kwa hivyo hakupendelea kwenda moja kwa moja kuonana na Mtume, mpaka kwanza aandae njia na mazingira ya kukutana nae. Akaanzia kwa binti yake Ummu Habibah; mke wa Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-ili apate kumuombea kwa Mtume. Alipo taka kukalia tandiko la Mtume, Ummu Habibah akalikunja, Abu Sufyaan akastaajabishwa na kitendo hiki alicho fanyiwa na binti yake mwenyewe. Akamuuliza: "Ewe kijibinti changu wee! Umechukizwa mimi kulikalia tandiko hili?", binti akamjibu wazi usoni akisema: "Lakini hilo ni tandiko la Mtume wa Allah na wewe mtu mshirikina ni najisi, kwa ajili hiyo sikupenda ulikalie tandiko la Mtume wa Allah". Jawabu hilo likawa ni pigo lenye mshindo mkuu moyoni mwa Abu Sufyaan ambalo hakulitazamia tena kutoka kwa mtu wake wa karibu mno kama binti yake. Akajikuta hawezi kujimudu, akamwambia binti yake akimueleza fedheha na udhalili ulio mpata: "Wallah ewe binti yangu imekupata shari baada yangu".

Kisha huyoo akatoka nyumbani kwa Mtume akiwa mvunjifu wa moyo na majeruhi wa kifua, mpaka akaingia msikitini aliko kuwepo Mtume wa Allah. Akamsemeza, Mtume hakumjibu kitu, kutojibiwa na Mtume lilikuwa ni pigo kubwa zaidi kuliko lile la kwanza alilo lipata kwa binti yake. Akatoka msikitini akiwa mnyonge mno na mwenye uso wa kukata tamaa, akaenda kutaka msaada na uombezi kutoka kwa maswahaba wa Mtume. Basi hakupata hata mtu mmoja aliye tayari kuipokea haja yake na kuiwasilisha kwa Mtume. Alimuendea Sayyidina Abu Bakri-Allah amuwiye radhi-yeye akamtaka udhuru wa kutoliweza hilo kwa lugha ya upole. Akatoka, huyoo mpaka kwa Sayyidina Umar-Allah amuwiye radhi-huko akakaripiwa na kutolewa maneno makali, akaambiwa: "Mimi ndio nikuombeeni nyinyi kwa Mtume wa Allah, mimi?! Wallah, lau nisingelipata ila chembe ndogo tu basi ningepigana nanyi kwayo". Baada ya kugonga mwamba kwa Umar akamuendea Sayyidina Aliy Ibn Abiy Twaalib-Allah amuwiye radhi-akamwambia: "Ewe Aliy, hakika wewe ndiye mtu mwenye udugu wa karibu zaidi nami na kwa yakini nimeletwa na haja fulani. Basi nisirejee patupu kama nilivyo kuja, basi nakuomba uniombee". Aliy akamwambia: "Ole wako ewe Abu Sufyaan! Wallah, Mtume wa Allah amekwisha azimia jambo, ambalo sisi hatuwezi kumzungumza katika hilo". Na yasemekana kwamba Abu Sufayaan alikwenda pia kwa Sayyidina Uthman Ibn Affaan, Sa'ad Ibn Ubaadah na wengineo miongoni mwa maswahaba wakubwa katika Muhajrina na Answaari, na kila mmoja wao akimwambia: "Dhima/amani yangu iko katika dhima ya Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-na wala hapana ye yote achukuaye dhima juu yake". Alipo kata tamaa kupata alilo litaka kwa wote hawa, ndipo alipofikia uamuzi wa kwenda kwa Bi. Fatimah; binti ya Mtume. Nae akiwa na mwanawe; Al-Hassan akiwa anatambaa tambaa mbele yake, akamwambia: "Ewe binti Muhammad! Je, kunakuelea kuchukua dhima baina ya watu hawa?", akamjibu: "Hakika si lo lote, mimi ni mwanamke", Abu Sufyaan akamwambia: "Muamrishe mwanao huyu achukue dhima baina ya watu, nae atakuwa bwana wa Waarabu hadi mwisho wa ulimwengu". Bi. Faatimah akamwambia: "Wallah mwanangu huyu bado hajafikilia kuchukua dhima baina ya watu, na hapana ye yote awezaye kuchukua dhima juu ya Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie".

Baada ya jitihada zake hizo kushindwa, ndipo alipo rejea kwa Sayyidina Aliy, akamwambia: "Ewe babie Hassan, hakika mimi nayaona mambo yananiwia ugumu sana, hebu basi nipe nasaha zako". Aliy akamwambai: "Wallah sijui cho chote kitakacho kusaidia, lakini jambo moja wewe ni bwana wa Kinaanah. Basi cha kufanya, wewe inuka uchukue dhima mwenyewe baina ya watu, kisha ushike njia uondoke kwenu". Abu Sufyaana akauliza: "Hivi wewe unaona hilo litanisaidia cho chote?", Aliy akamjibu: "Wallah, hapana sidhanii hivyo, lakini mimi sina ushauri mwingine zaidi ya huo". Abu Sufyaan akainuka msikitini mle akasema: "Enyi watu nyie! Hakika mimi nimechukua dhima baina ya watu". Halafu akampanda ngamia wake, huyoo akaondoka kurejea Makah, huku akimeza machungu ya kurejea patupu na unyonge. Alipo fika kwa Makureishi wakamuuliza: "Kuna nini huko utokako?", akajibu: "Nimemuendea Muhammad nikamsemsha, basi wallah hakunijibu cho chote! Kisha nikamuendea Ibn Abu Quhaafah (Abu Bakri) na kwake sikupata kheri yo yote. Halafu tena nikamuendea Ibn Al-Khatwaab, huyo nikamkuta adui mkubwa kuliko wote. Kisha nikamuendea Aliy, huyu akawa laini kuliko wote na akaniashiria jambo nililo lifanya. Basi wallah sijui litasaidia cho chote au la". Wakamuuliza: "Haya ni jambo gani hilo? Akajibu: "Aliniamuru kuchukua dhima baina ya watu, nami nikafanya hivyo". Wakauliza: "Je, Muhammad amelipitisha hilo? Akajibu: "Hapana", wakamwambia: "Ole wako! Wallah mtu huyo hakuzidi ila kukuchezea tu".

 



 | Tuandikie |