|
i.
Mtume wa Allah ajiandaa
kwa Fat-hi Makkah na achukua hatua za makusudi kuepusha umwagikaji wa damu:
Mtume wa
Allah-Rehema na Amani zimshukie-akaanza kujiandaa na Fat-hi Makah,
akawatumia ujumbe watu wa vitongojini na mabedui walio mzunguka, waje
Madinah katika mwezi wa Ramadhani. Makabila yakauutika wito huo wa Mtume na
yakaanza kumiminika Madinah na kupiga kambi hapo. Mtume wa Allah akawa
makini mno, akawaficha watu makusudio yake, wasijue anaelekea wapi, hilo
lilikuwa ni sehemu ya hatua za makusudi kuepusha umwagikaji wa damu. Akaweka
walinzi katika njia zote ziingiazo na kutoka Madinah, wamrejeshe atokako
kila wanaye mtilia mashaka. Watu walipo kwisha kusanyika, ndipo alipo
wafahamisha kwamba anakusudia kwenda Makah na akawaamuru kujiandaa vema na
haraka kwa ajili ya safari hiyo. Na akamuomba Allah ajaalie Makureishi
wasijue lo lote katika kutoka kwake huku, ikawapelekea wao kujiandaa na vita
na hivyo kusababisha umwagikaji wa damu. Aende bila wao kujua wala kuhisi lo
lote ili awashtukize, kitendo kitakacho wafanya wasalimu amri.
ii.
Kosa la Haatwib Ibn
Abiy Bal-ta’ah:
Mtume wa
Allah-Rehema na Amani zimshukie-alipo kata shauri kwenda kwa Makureishi na
akawatangazia watu welekeya wake huo. Haatwib Ibn Abiy Bal-ta’ah
akawaandikia barua Makureishi, akiwaeleza juu ya azma hii ya Mtume wa Allah.
Akamkodi mwanamke mmoja kutoka katika kabila la Muzaynah, akampa barua ile
na akamuamuru afanye kila hila na kila aliwezalo kuifikisha barua hiyo Makah
kwa Makureishi. Mwanamke yule akaitwaa barua na kuificha tayari kwa msafara
wa Makah, huyoo akashika njia za panya (za uficho) hata akafanikiwa kutoka
nje ya Madinah na akawa sasa anashika njia iendayo Makah. Hapo ndipo ikamjia
Mtume-Rehema na Amani zimshukie-khabari kutoka mbinguni ikikielezea kitendo
alicho kifanya Haatwib. Bila kuchelewa Mtume akamtuma Sayyidina Ali Ibn Abiy
Twaalib na Zubeir Ibn Al-Awwaam kumfuata mwanamke yule, nao wakamdiriki
njiani kabla hajaingia Makah. Wakanyang’anya barua ile na kuiwasilisha mbele
ya Mtume wa Allah, Mtume akamuita Haatwib na kumuonyesha barua yake ile,
kisha akamuuliza: “Ni lipi lililo kupelekea hata ukaamua kufanya hivi?”
Haatwib akadhania kwamba tayari amesha hiliki na wala hana njia ya kuihepea
hilaki hiyo dhahiri. Kama kuna uokovu basi utatokana na yeye kumwambia
ukweli Mtume wa Allah, akasema: “Ewe Mtume wa Allah wee! Tafadhali
usinifanyie haraka, wallah mimi ninamuamini Allah na Mtume wake, bado
sijabadilisha wala kuiharibu imani yangu hiyo. Lakini mimi nilikuwa ni mtu
asiye na mtu wala jamaa kwa Makureishi na watoto na mke wangu wako huko, kwa
hivyo nikataka kuonekana mzuri kwao. Na Muhajirina walio pamoja nawe ambao
wana watoto na mali Makah, wao hawa wana ndugu watakao walinda watoto na
mali zao. Kwa hivyo nikapendelea, kwa kuwa sina nasabu kwa Makureishi, niwe
na mkono (wema) ambao kwa huo watawalinda watoto wangu. Na wala mimi
sikulifanya hili kwa kuwa nimetoka katika dini yangu na wala si kwa
kuuridhia ukafiri baada ya imani”.
iii.
Mtume wa Allah
alisawazisha kosa la Haatwib:
Mtume wa
Allah-Rehema na Amani zimshukie-akaona ukweli wa maneno ya Haatwib na nia
yake njema iliyo mpelekea kufanya kosa hilo, akawaambia watu walio mzunguka:
“Ama hakika yeye amekuelezeni kweli katika aliyo waambia”. Mtume wa Allah
akarudi nyuma kimawazo na kuangalia namna mtu huyu alivyo kuwa katika jihadi
huko nyuma na alivyo tumia upeo wa nguvu na ushujaa wake katika kuuhami
Uislamu. Kwa kuyaangalia mazuri haya ya nyuma, Mtume akapondokea katika
kumsamehe swahaba wake huyu juu ya kosa lake hili. Ama Sayyidina Umar-Allah
amuwiye radhi-suala la khiana hii lilikuwa kubwa mno kwake khasa kutokana na
kwamba mpika khiana mwenyewe ni mmoja kati yao. Akamuangalia Haatwib,
akamwambia: “Allah akuangamize! Unamuona Mtume wa Allah anapita njia za
panya (ili watu wasijue), halafu wewe unawaandikia Makureishi (kuwajulisha)?
Ewe Mtume wa Allah, hebu niachie niikate shingo ya mnafiki huyu”.
Mtume-Rehema na Amani zimshukie-akatabasamu kutokana na hamasa za Umar na
akasema: “Na lipi litakalo kujulisha ewe Umar, huenda Allah aliwacho mozea
watu wa Badri (walio pigana vita hivi) akawaambia: Tendeni mlitakalo, kwa
yakini mimi nimekwisha wasameheni”.
Kufuatia tukio hili, Allah Taala akashusha aya za mwanzo za
Suratil-Mumtahinah akiwatahadharisha waislamu kumfanya adui yao rafiki. Au
kumpa baadhi ya siri zao hata kama kuna sababu gani ipelekeayo hivyo, kwani
adui ni adui tu vyo vyote atakavyo kuwa. Na kumfanya adui kuwa ndio kipenzi,
hiyo ni khiana isiyo na kiasi, akasema Taala: “ENYI MLIO AMINI! MSIWAFANYE
ADUI ZANGU NA ADUI ZENU KUWA MARAFIKI MKIWAPA MAPENZI, NA HALI WAO
WAMEKWISHA IKATAA HAKI ILIYO KUJIENI, WAKAMFUKUZA MTUME NA NYINYI KWA SABABU
MNAMUAMINI ALLAH, MOLA MLEZI WENU. MNAPO TOKA KWA AJILI YA JIHADI KATIKA
NJIA YANGU NA KUTAFUTA RADHI YANGU, MNAFANYA URAFIKI NAO KWA SIRI, NA MIMI
NAYAJUA MNAYO YAFICHA NA MNAYO DHIHIRISHA. NA MWENYE KUFANYA HAYO KATI YENU
BASI AMEIPOTEA NJIA YA SAWA. WAKIKUWEZENI WANAKUWA MAADUI ZENU, MA
WANAKUKUNJULIENI MIKONO YAO NA NDIMI ZAO KWA UOVU. NA WANAPENDA MUWE
MAKAFIRI. HAWATAKUFAENI JAMAA ZENU, WALA WATOTO WENU SIKU YA KIYAMA, ALLAH
ATAPAMBANUA BAINA YENU, NA ALLAH ANAONA MNAYO YATENDA”. [60:1-3]
iv.
Jeshi la Fat-hi Makah:
Mtume wa
Allah-Rehema na Amani zimshukie-akampa ukaimu wa Madinah, Abu Dharri
Al-Ghifaariy-Allah amuwiye radhi. Akatoka Madinah akiwa na maswahaba wapatao
alfu kumi, katika Muhajirina na Answaari na ujumbe wa makabilia ya Kiarabu
ulio itikia wito wake. Likaondoka jeshi hili kubwa likilikata jangwa pana
kuelekea Makah, si kwa lengo la kwenda kumwaga damu huko na kuwaua watu
wasio na hatia, la hasha. Wala si kwa dhamira ya kupora mali na kukalia haki
za watu kimabavu, lakini ilikuwa ni kwa ajili ya kufungua makufuli ya mji
mtakatifu. Na kuuondoshea mji huu vizuizi na vipingamizi na kuufanya kama
alivyo ufanya Allah: “NA KUMBUKENI TULIPO IFANYA ILE NYUMBA (ya Alkaaba) IWE
PAHALA PA KUKUSANYIKIA WATU NA PAHALA PA AMANI...” [2:125] Na aineze hapo
dini ya haki ambayo kwayo Allah amewaleta mitume wote ili wawatoe watu
kutoka katika viza (shirki) kuwatia katika nuru (Uislamu).
|