|
v.
Al-Abbas afanya
jitihada za makusudi kuwapa amani Makureishi:
Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alipo fika
katikati ya safari yake, alikutana na Al-Abbas Ibn Abdil-Mutwalib akihajiri
Makah kuja Madinah na familia yake. Kukutana huku kukawa ni sadfa yenye
baraka, kwa kukutana huku Allah Taala alizihifadhi damu zisimwagike na
akayawepesisha mambo. Na kwao, Allah akaisakhirisha njia ya Fat-hi Makah kwa
namna aliyo kuwa akiitazamia Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie. Kwani
Al-Abbas alimtuma mtu kuipeleka Madinah familia yake na yeye akarejea Makah
na jeshi la Mtume. Jeshi lilipo kuwa umbali wa mwendo wa siku moja tu
kuingia Makah, Mtume na maswahaba wake wakapiga kambi na wakati huo ulikuwa
ni usiku. Mtume wa Allah akaamrisha iwashwe mioto eneo lote kuzunguka kambi,
wakawasha mienge alfu kumi ya moto. Mwangaza wake ukaanza kuzagaza katika
giza la jangwani mpaka ukaufanya usiku ule mithili ya mchana kutokana na
mwangaza wake. Hili likamuogofya mno Al-Abbas na akawachelea watu wa Makah
kufikwa na matokeo ya mshtukizo huu khatari, na akakadiria mpambano wa
Makureishi na jeshi hili kubwa. Na khasara ya mali na nafsi itakayo patikana
kutokana na mpambano huo, kwa kuyakadiria yote haya akaanza kufikiria
mbinu/njia itakayo wapatia amani Makureishi na kuwaokoa dhidi ya hilaki hii
inayo karibia kuwashukia.
Al-Abbas mwenyewe anahadithia: “Mtume wa Allah-Rehema na
Amani zimshukie-alipo piga kambi (Mar-radhwahraan), nafsi yangu
iliwaonea sikitiko watu wa Makah na nikajiambia: Eeh asubuhi mbaya iliyoje
kwa Makureishi! Wallah lau Mtume wa Allah ataingia Makah kwa nguvu kabla
hawajamjia na kumtaka amani, hakika hapana shaka hiyo ni hilaki ya
Makureishi mpaka mwisho wa dunia! (Anaendela kusimulia): Basi nikakaa juu ya
nyumbu wa Mtume wa Allah, nikatoka nae mpaka sehemu iitwayo (Al-Araak),
nikajiambia: Huenda nitawapata baadhi ya watafuta kuni au wauza maziwa
au mtu mwenye haja anaye kwenda Makah. Ili awape khabari watu wake juu ya
mahala alipo Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-wapate kuja kumtaka
amani kabla hajaingia kwa nguvu. Na ikawa katika qadari na hukumu ya Allah
ni kutokea kwa Abu Sufyaan Ibn Harbi, Hakim Ibn Huzaam na Budeil Ibn Warqaa
wakiwa katika harakati za kupekua khabari. Wakitafuta kupata au kusikia
khabari, basi wallah nami nikienda juu ya nyumbu wa Mtume wa Allah
nikilitafuta nililo litokea. Mara tahamaki nikasikia mazungumzo ya Al-Abbas
na Budeil nao wakijibizana, Abu Sufyaan akisema: “Sijapatapo katu kuona
mioto wala kambi kama hii ya usiku wa leo!”, hapo Budeil akamwambia: “Wallah
hao ni Khuzaah (kabila) wameunguzwa na moto wa vita (wamepandwa na mori wa
vita)”. Abu Sufyaan akamjibu: “Khuzaah ni madhaifu na wachache mno hii
kuweza kuwa kambi na mioto yao”.
(Al-Abbas anaendelea): Basi nikaitambua sauti yake, nikaita:
“Ewe babie Handhwalah”, akaitambua sauti yangu akasema: “Babie Al-Fadhli
(wewe)!” Nikaitika: “Naam”, akauliza: “Una nini wewe, nakufidia baba na mama
yangu (uniambiae)”, nikamwambia: “Ole wako ewe Abu Sufyaan! Huyo ni Mtume wa
Allah-Rehema na Amani zimshukie-akiambatana na maswahaba wake. Wallah
asubuhi mbaya iliyoje kwa Makureishi! Akauliza: “Basi itumiwe hila gani,
nakufidia baba na mama yangu?” Nikajibu: Wallah iwapo atakushinda ataipiga
shingo yako! Basi panda nyuma ya nyumbu huyu nikupeleke kwa Mtume wa Allah
nikakuombee amani”. (Anasema Al-Abbas): Akapanda nyuma yangu na wale wenzake
wakarejea, nikaja nae. Kila nilipo upitia moto miongoni mwa mioto iliyo
washwa na waislamu, waliuliza: Nani huyo? Wanapo muona nyumbu wa Mtume wa
Allah nami nikiwa nimempanda, husema: Huyo ni ami wa Mtume wa Allah
amempanda nyumbu wake (Mtume). Mpaka nilipo upitia moto wa Umar Ibn
Al-Khatwaab-Allah amuwiye radhi-akauliza: “Nani huyo?” na akaniinukia. Alipo
muona Abu Sufyaan nyuma ya mnyama, akasema: “Abu Sufyaan adui wa Allah! Kila
himda njema zinamstahikia Allah ambaye amekumakinisha kwetu bila ya mkataba
wala ahadi”. Kisha huyoo akatoka wangu wangu kuelekea aliko Mtume wa
Allah-Rehema na Amani zimshukie-nami nikampeleka shoti nyumbu nikamtangulia
kufika. Nikachupa kutoka juu ya nyumbu na nikaingia kwa Mtume nikifuatiwa na
Umar, akasema: “Ewe Mtume wa Allah! Huyoo Abu Sufyaan, adui wa Allah, Allah
amemmakinisha kwetu bila ya ahadi wala mkataba. Basi niachie niipige shingo
yake nimuulie mbali”. Mimi nikasema: “Ewe Mtume wa Allah! Hakika mimi
nimekwisha mpa hifadhi”. Halafu nikakaa kwa Mtume wa Allah nikamshika kichwa
chake nikasema: “Wallah usiku wa leo (Abu Sufyaan) asizungumze na mtu ye
yote ila mimi tu”.
Al-Abbas na Umar wakaendelea kujibizana mbele ya Mtume wa
Allah-Rehema na Amani zimshukie-kwa suala la Abu Sufyaan, mpaka Mtume
akasema: “Ewe Abbas nenda nae katika khema lako na uje nae kutakapo
pambazuka”.
|