|
Ilipita miaka mitatu il-hali Mtume wa Mwenyezi Mungu akiulingania Uislamu kwa siri.
Maswahaba wa Mtume Allah awawie -Allah amuwie radhi wote pia hawakubakia
nyuma bali walikuwa bega kwa bega na Bwana Mtume wakiwalingania watu Uislamu. Wakawa
wanautikia wito huu wa kuingia huu wa kuingia katika Uislamu watu ambao Mwenyezi Mungu
alikwisha waandikia uongofu miongoni mwa wanaume na wanawake wa Makkah. Kwa hiyo idadi ya
waislamu ikawa inazidi kidogo kidogo siku hata siku, hii ni kwa sababu watu waliogopa
kusilimu kwa kuchelea shari na nguvu ya makurayshi. Ikawa wanaosilimu, husilimu kwa
tahadhari kubwa, kwa kuchelea wasijulikane.
Ili kuepuka kugongana na kukwaruzana na jamaa zake Bwana Mtume -Rehema na Amani
zimshukie- alitafuta mahala pa faragha, palipo mbali na watu ili pawe ndio kito chake cha
kukutana na maswahaba wake. Mahala hapa pateule hapakuwa pengine ila ni nyumba ya Bwana
Arqam bin Abil-Arqam, iliyoko jirani na Jabali Swafaa. Bwana Arqam alikuwa ni miongoni mwa
viongozi wa makurayshi waliosilimu mwanzo kabisa. Historia ya Uislamu haiandikiki bila ya
kuitaja nyumba hii. Ndani ya nyumba hii ndimo Mtume alikuwa akikutana na maswahaba wake
akiwawaidhi, akiwaswalisha, akiwasomea wahyi/ufunuo wa Qur-ani uliomshukia na kuwafundisha
jinsi ya kuishi na mafundisho hayo ya Qur-ani. Kwa hivyo nyumba hii ikawa ndio msikiti wao
wa kwanza wakifanya ibada zao humo, ikawa ndio chuo cha mafunzo na malezi na ikawa ndio
klabu yao ya ushauri nasaha na upangaji na upangaji wa mikakati na mipango ya
baadaye. Pamoja na upinzani mkubwa wa makurayshi Bwana Mtume akaendelea kulingania kwa
siri mpaka ilipomshukia kauli yake Mwenyezi Mwenyezi Mungu Mtukufu : "BASI YATANGAZE
ULIYOAMRISHWA (wala usijali upinzani wao) NA UJITENGE MBALI NA (vitendo vya) HAO
WASHIRIKINA" [15:94].
Baada ya amri na tangazo hili, hapa sasa ndipo Bwana Mtume akabadilisha mtindo wa
ulinganiaji. Akaanza kuulingania Uislamu kwa dhahiri bila ya khofu wala uficho. Akapanda
juu ya jabali Swafaa na akaanza kuwaita watu kwa sauti ya juu : "Enyi jamaa
zangu!" Akawaita jamaa/watu wake kwa namna na mtindo uliokuwa umezoeleka miongoni
mwao walipokuwa na jambo muhimu. Zikamuitikia na kumjia koo zote kumi na mbili za
makurayshi, walipokusanyika ndipo akawaeleza alilowaitia, akaanza kwa kusema :
"Mnaonaje, lau nitakwambieni kwamba nyuma ya jabali hili (Swafaa) kuna jeshi linakuja
kukushambulieni, Je mtanisadiki ?" Wote wakajibu kwa sauti moja : Ndio, wewe kwetu
hutuhumiwi kwa baya lolote, na kamwe hujapata kutuongopea. (Mtume) akawaambia : "Basi
(ikiwa ni kweli hayo muyasemayo) mimi ni muonyaji kwenu nyinyi mbele ya adhabu kali ! Enyi
wana wa Abdul Mutwalib! Enyi wana wa Abdi-Manaaf! Enyi wana wa Taym! Enyi wana wa
Makhzuum! Enyi wana wa Asad!
Hakika Mwenyezi Mungu ameniamrisha kuwaonya jamaa
zangu wa karibu na mimi similiki manufaa yenu ya duniani na wala similiki fungu lenu la
akhera ila mtakaposema : Hapana Mola afaaye kuabudiwa kwa haki ila ALLAH pekee. Enyi
kusanyiko la Makurayshi, ziokoeni nafsi zenu kutokana na adhabu ya moto, kwani mimi
sitakufaeni chochote mbele ya Mwenyezi Mungu. Hakika mfano wangu nanyi ni mfano wa mtu
aliyemuona adui, akakimbia haraka kuwaambia jamaa zake wamuwahi adui, akawa apiga ukelele
: Eeh! Eeh! Mmevamiwa, mmevamiwa!
Kabla Mtume hajamaliza kusema, Abuu Lahab {Ami yake} akamkata kauli na kumwambia :
"Umeangamia ewe mwana kuangamia!
. Hivi hili ndilo ulilotukusanyia?" Abu
Lahab ndiye aliyekuwa mtu wa kwanza kumjibu, kumuudhi na kumkadhibisha Bwana Mtume na
kumfukuzia watu. Hapo ndipo Mwenyezi Mungu Mtukufu akaishusha kauli yake : "PANA
KUANGAMIA MIKONO MIWILI YA ABU LAHAB! NAYE AMEKWISHAANGAMIA. HAYATAMFAA MALI YAKE WALA
ALIVYOCHUMA. (Atakapokufa) ATAUINGIA MOTO WENYE MWAKO (mkubwa kabisa). NA MKEWE, MCHUKUZI
WA KUNI (za fitna). (Kama kwamba) SHINGONI MWAKE IKO KAMBA ILIYOSOKOTWA (anayochukulia
kuni za fitna hizo)" [111:1-5]
Mkewe Abu Lahab, Ummu Jamiyl alikuwa akimchukia sana Bwana Mtume na alikuwa akifanya
zoezi la kumfitinisha Mtume na jamaa zake kwa kueneza maneno ya uzushi na uongo mpaka
Mwenyezi Mungu akamsifia kwa sifa mbaya kabisa, akamuita MCHUKUZI WA KUNI. Hii ni sifa ya
ufitina na uchochezi. Kwa ujumla mama huyu mbaya na mumewe walikuwa ni maadui wakubwa wa
Bwana Mtume.
Ukelele wa Bwana Mtume Rehema na Amani zimshukie katika jabali Swafaa
haukupotea bure bali ulileta taathira fulani katika jamii ya Makurayshi mjini Makkah.
Tangu siku ile khabari za dawah zikaenea mji mzima wa Makkah, zikawa ndizo khabari
zilizoyatawala mabaraza na vilabu vya Makkah. Watu wakawa wanaulizana kwa shauku ya kuaka
kujua : Ni dini gani hii anayolingania Muhammad ? "BASI WAKO MIONGONI MWAO AMBAO
ALLAH AMEWAONGOA, NA WAKO MIONGONI MWAO AMBAO UPOTOFU UMETHUBUTU JUU YAO" [16:36].
Wale ambao Mwenyezi Mungu Mtukufu alikwishawaandikia kuongoka wakawa wakimuendea Mtume kwa
uficho kumtaka awape ufafanuzi wa maelezo ya kina kuhusiana na dini mpya anayoilingania.
Naye Nabii Muhammad akawa anawakinaisha kimaelezo, walipotosheka wakatangaza kusilimu. Ama
wale ambao walioandikiwa uovu tangu azali, hawa waliipa mgongo dawah ya Mtume,
wakashindwa kuiona haki kuwa ni haki na kuifuata. Hawa waligawika makundi mawili; kundi
moja lilikuwa na msimamo wa kumkataa Bwana Mtume na dini yake bila ya kumfanyia uadui.
Kundi jingine lilimpinga vikali na kumpiga vita kwa hali na mali na kupanga mikakati ya
kuwazuia watu wasimfuate Mtume. Wengi miongoni mwa watu wa kundi hili la pili walikuwa ni
viongozi na matajiri, hawa waliiona dini hii mpya ni hatari kwa maslahi na nyadhifa zao
katika jamii. Muhammad akikubalika na jamii na kushika hatamu za uongozi, atakuwa na sauti
na hili litapelekea kuanguka kwa nyadhifa na maslahi yao. Miongoni mwa maadui wakubwa
katika kundi hili, walikuwa ni Abu Jahl bin Hisham, Abu Lahab bin Abdul-Mutwalib na Uqbah
bin Abi Muayt. Hawa wawili Abu Jah na Uqbah walikuwa ni jirani zake Mtume,
wakimuudhi upeo wa kumuudhi. Katika hili Mtume Rehema na Amani zimshukie
anasema katika riwaya iliyopokelewa na Bi Aysha Allah amwie radhi
"Nilikuwa ninaishi na majirani wawili wabaya; baina ya Abi Lahab na Uqbah bin Abi
Muayt, walikuwa wakichukua utumbo wa mbuzi na kuja kuutupia mlangoni kwangu mpaka takataka
zao wakizitupia mlangoni kwangu!" Naye Bwana Mtume akiziondosha taka zile na kusema :
"Enyi wana wa Abdi Manaf, ni ujirani gani huu ?". Watu wanyonge yaani watumwa,
wajakazi, masikini na mafakiri wa Makkah wakawa wanamfuata na kumsikiliza Mtume kila
alipokuwa akiulingania Uislamu. Hawa walikuwa wamechoshwa na mfumo wa uonevu na
ukandamizaji wa dini ya Makurayshi. Kwa hivyo walikuwa na matumaini kwamba Uislamu ndio
mfumo wa maisha utakaowakomboa kutoka katika udhalimu, uonevu na unyanyasaji. Uislamu ndio
utakaowapa matumaini ya maisha bora, haki na usawa na kuwatoa katika tabaka la chini
ambako walionekana kuwa ni sawa na wanyama au duni kuliko wanyama. Na kweli Uislamu
uliwawekea misingi madhubuti ya maisha na ukawafungulia mlango wa matumaini ya amani,
salama na utulivu. Bwana Mtume alikuwa akiwaambia kwamba gharama na thamani pekee
wanayotakiwa kuitoa kama kiingilio na tiketi ya mfumo huu mpya uliosheheni haki, uadilifu
na usawa ni kwa wao kuijaza mioyo yao imani ya Allah, Mungu Mwenyezi asiye na mshirika na
maisha yao yote yapambwe na amali/matendo mema. Mwenyezi Mungu akawaongoza masikini hawa,
wakawa wanaingia katika dini yake makundi kwa makundi. Naye Bwana Mtume akiwapokea kwa
wema na ukarimu mkubwa na akiwafanya sawa na wale waumini ambao walikuwa ni viongozi na
watu watukufu. Hakumbagua baina ya tajiri na masikini, mnyonge na mwenye nguvu wala baina
ya Mwungwana na Mtumwa. Bwana Mtume akajiweka baina yao daraja ya ndugu mwenye huruma na
mzazi rahimu "
ANAWAAMRISHA MEMA NA ANAWAKATAZA MABAYA NA KUWAHALALISHIA VIZURI
NA KUWAHARIMISHIA VIBAYA NA KUWAONDOLEA MIZIGO YAO NA MINYORORO ILIYOKUWA JUU YAO (yaani
sheria ngumu za zamani na mila za kikafiri)." [7:157].
Mtume aliwaonyesha mfano mwema wa tabia nao wakimfuata na kumuiga na wakizifuata nyayo
zake katika matendo na kauli. Wakimtii twaa ya kweli na upendo tunamwomba Mola wetu
Mtukufu awaridhie maswahaba wa Mtume wake wote- Amin.
|