Makala
Uislamu-Utangulizi
Fiqhi na Sheria 
Akhlaaq-Tabia
Sira ya Mtume
Nasaha za dini
Maswali na Majibu
Uliza Suala la dini
Jiunge na Mtandao !!!

 

SIRA YA MTUME (SAW)  

"BILA SHAKA MNAO MFANO MWEMA KWA MTUME WA MWENYEZI MUNGU…"Al-qur-an (33:21)

SOMO LA TATU.

 Faida

             i.          Abu Sufyaan asilimu:

(Anasema Sayyidina Al-Abbas-Allah amuwiye radhi): Nikaenda nae khemani kwangu, akalala kwangu. Kulipo pambazuka nikadamkia nae kwa Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie. Mtume alipo muona akasema: “Ole wako ewe Abu Sufyaan! Hivi bado haujafika wakati wewe kujua kwamba hapana Mola apasaye kuabudiwa kwa haki ila Allah?” Akajibu (Abu Sufyaan): “Nakuapia kwa baba na mama yangu. Wallah kwa yakini nimeyakinisha lau kungekuwa na mungu mwingine pamoja na Allah, basi hakika angelinitosheleza kwa cho chote”. Mtume akasema: “Ole wako ewe Abu Sufyaan! Hivi bado tu haujafika wakati wewe kutambua kwamba mimi ni Mtume wa Allah?” Akajibu (Abu Sufyaan): “Ama hili, wallah mpaka sasa bado kuna kitu ndani ya nafsi yangu”. Al-Abbas akasema: “Ole wako! Silimu na ushuhudie kwamba hapana Mola apasaye kuabudiwa kwa haki ila Allah na kwamba Muhammad ni Mtume wa Allah, kabla hujapigwa shingo yako”. (Anasema Al-Abbas): Basi akatoa shahada ya haki. Nikasema: “Ewe Mtume wa Allah! Hakika Abu Sufyaan ni mtu apendaye fakhri, basi mpe kitu cho chote”. Akasema (Mtume): “Naam, atakaye ingia nyumbani kwa Abu Sufyaan, huyo yuko katika amani na atakaye jifungia mlango wake huyo (pia) yuko katika amani na atakaye ingia msikitini huyo nae yuko katika amani”.

Alipo kwenda ili aondoke, Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akasema: “Ewe Abbas, mzuie kwenye njia panda nyembamba ya bondeni, mpaka yampitie majeshi ya Allah apate kuyaona”. (Anasema): Nikatoka nae mpaka nikamzuilia pale alipo niamrisha Mtume wa Allah kumzuilia. Yakapita makabila na bendera zao, basi halikupita kabila lo lote ila aliniuliza kuhusiana nalo. Mpaka akapita Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-pamoja na kikosi chake cha kijani kikiwa na Muhajirina na Answaari-Allah awawiye radhi. Akasema (Abu Sufyaan): “Sub-haanallah ewe Abbas! Hawa ni kina nani?” nikamjibu: “Huyo ni Mtume wa Allah pamoja na Muhajirina na Answaari”. Akasema: “Hapana ye yote mwenye ubavu wa kusimama na hawa! Wallah ewe Abal-Fadhli, kwa yakini asubuhi ya leo ufalme wa mwana wa nduguyo umekuwa mkubwa!” Nikasema: “Ole wako! Hakika huo ni utume (na wala sio ufalme)”. Akasema: “Haya na iwe hivyo, halafu...”. nikasema: “Uokovu kwa watu wako”.

 

           ii.          Abu Sufyaan awatahadharisha Makureishi na awatolea wito wa kujisalimisha:

         Akaenda mpaka alipo wafikia akapiga ukelele kwa sauti ya juu: “Enyi kusanyiko la Makureishi! Huyoo Muhammad amekujilieni na jeshi msilo na ubavu nalo. Basi ye yote ataye ingia nyumba ya Abu Sufyaan, huyo yuko katika amani”. Hind Bint Utbah akamuinukia akamshika ndevu zake na kusema: “Muueni mzee huyu mpumbavu”. Akasema (Abu Sufyaan): “Ole wenu! Huyu (mwanamke) asikughurini, kwani ni kweli kabisa amekujieni Muhammad na nguvu msiyo iweza. Basi ye yote atakaye ingia nyumba ya Abu Sufyaan, huyo yuko katika amani”. Wakasema” Allah akuhilikishe! Nyumba yako itatusaidia nini sisi?” Akaendelea kusema: “Na atakaye jifungia mlango wake, huyo (pia) yuko katika amani na atakaye ingia msikitini naye yuko katika amani”. Basi watu wakatapanyikia majumbani mwao na msikitini.

Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alipo fika “Dhiy Twuwaa” na akawa karibu kuingia Makah. Akalitawanya jeshi kwenye njia zote zitokazo na kuingia Makah na akawa ameifunga kwa pande zake zote. Akamuamuru Zubeir Ibn Al-Awwaam aingie na kikosi chake upande mmoja na Sa’ad Ibn Ubaadah aingie na kikosi chake kwa upande mwingine. Na akamuamuru Khalid Ibn Al-Waleed kuingia na kikosi chake kwa upande mwingine na akamtanguliza mbele yake yeye (Mtume) Abu Ubaidah Ibn         Al-Jarraah. Na Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akaingia kwa upande wa “Adhaakhira” mpaka akashukia nyanda za juu za Makah, hapo akapiga khema.

 

         iii.          Mtume wa Allah alipupia mno kutokumwagika damu kusiko kwa lazima:

         Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie alikuwa na pupa mno kuhakikisha kuwa damu haimwagiki Makah, akakataza vita. Pupa yake hii ikamfikisha kumng’oa Sa’ad Ibn Ubaadah madarakani na kumpa madaraka hayo mwanawe; Qays Ibn Sa’ad. Alichukua khatua hiyo pale ilipomfikia khabari kwamba Sa’ad amesema akiwakamia Makureishi alipo kuwa akielekea kuingia Makah: “Leo ni siku ya malanyama! Leo itahalalishwa haramu!” Lakini Allah Taala zitukukie hekima zake, alitaka katika siku hii ya “ufunguzi – mweupe” kumwagika baadhi ya matone ya damu. Kwani Khalid Ibn Al-Waleed alipata upinzani upande wake kutoka kwa baadhi ya Makureishi, akalazimika kukabiliana na nguvu kwa kutumia nguvu. Hapo wakauawa waislamu wawili na Makureishi ishirini na kitu. Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alipo liona tukio hilo alighadhika na kusema: “Mimi sikukataza vita?”, akaambiwa: Ewe Mtume wa Allah, hakika Khalid alipigwa naye akapigana. Akasema (Mtume): “Hukumu ya Allah ni kheri”.  

 



 | Tuandikie |