|
Hivi ndivyo majeshi ya waislamu yalivyo ingia Makah
bila ya mapambano na ukatimia ufunguzi wa mji wenye amani bila ya mapigano
makubwa. Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akaingia Makah akiwa
amempanda ngamia wake. Na hakuingia kama wanavyo ingia washindi kwa mbwembwe
na jeuri kuu, bali yeye aliingia katika hali ya unyenyekevu mkubwa akiwa
ameinamia chini. Kichwa chake kikirubia kumgusa ngamia wake, hiyo ikiwa ni
alama ya shukrani kwa Allah kwa neema hii ya ufunguzi mkubwa aliyo mpa.
Mtume akaendelea kuisoma Suratil-Fat-hi [48] mpaka akafika kwenye Al-Ka’abah
akiwa pamoja na waislamu. Akaigusa nguzo ya Al-Ka’abah kwa kifimbo chake
kidogo, akapiga takbira na waislamu nao wakaiitikia takbira yake. Takbira
zao hizi zikautikisa mji mzima wa Makah mpaka Mtume akawaashiria wanyamaze.
Halafu Mtume akatufu Al-Ka’abah mbio mbio akiwa amempanda ngamia wake na
katika kila mzunguko akiligusa “Hajarul-Aswad” kwa kifimbo chake mpaka
akaikamilisha Twawaafu yake.
Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alipo maliza Twaafu
yake akashuka juu ya ngamia wake akaenda “Maqaamu Ibraahim”, hapo akaswali
rakaa mbili. Kisha akaenda kwenye maji ya Zamzam akayanywa na kutawadha huku
waislamu wakiwa wamemzunguka wakigombea maji yake ya udhu wakijimwagia
nyusoni mwao. Mushrikina wakiyaangalia yote hayo kwa mshangao mkubwa
wakisema: “Hatujapatapo kamwe kuuona wala kuusikia ufalme kama huu!”
iii.
Mtume wa Allah atoa
msamaha mwa maadui zake, msamaha usio na kifani katika Historia:
Kisha Mtume wa Allah-Rehema na Amani
zimshukie-akakaa kwenye pembe ya msikiti mtakatifu na Sayyidina Abu Bakri
akiwa amesimama nyuma yake na upanga mkononi. Halafu Mtume akamuita Uthman
Ibn Twalhah, akaja akamfungulia Al-Ka’abah, akaingia ndani na akaswali humo
rakaa mbili. Alipo maliza akasimama mlangoni mwa Al-Ka’abah akasema:
“Hapana mola afaaye kuabudiwa kwa haki ila Allah pekee, ameisadikisha ahadi
yake, amemnusuru mja wake na ameyashinda makundi peke yake”. Halafu
akatoa khutba ndefu, akataja ndani yake jumla ya hukumu za sheria, kisha
akasema: “Enyi kusanyiko la Makureishi! Hakika Allah amekuondosheeni
ushupavu wa kijahili na kujitukuza kwa mababa. Watu wote wanatokana na Adamu
na huyo Adamu anatokana na udongo”. Halafu akaisoma aya hii: “ENYI
WATU! HAKIKA SISI TUMEKUUMBENI KUTOKANA NA MWANAMUME NA MWANAMKE. NA
TUMEKUJAALIENI KUWA MATAIFA NA MAKABILA ILI MJUANE. HAKIKA ALIYE MTUKUFU
ZAIDI KATI YENU KWA ALLAH NI HUYO ALIYE MCHAMNGU ZAIDI KATIKA NYINYI. HAKIKA
ALLAH NI MWENYE KUJUA MWENYE KHABARI”. [49:13] Kisha akasema: “Enyi
kusanyiko la Makureishi! Mnasemaje na mnadhania mimi nitakufanyeni nini?”.
Wakajibu: “Kheri, wewe ni ndugu mwema mwana wa ndugu mwema!”, Mtume akasema:
“Ninasema kama alivyo sema ndugu yangu Yusuf: Leo hapana lawama juu yenu.
Allah atakusameheni, naye ni Mwingi wa kurehemu kuliko wote wanao rehemu.
Enendeni zenuni ilhali mkiwa huru!”
Unaonaje, hivi watu wa
Makah walitarajia msamaha huu lau kama mfunguzi wa Makah angelikuwa ni mmoja
wapo wa makamanda au wafalme? Naamini kwamba lau tutapekua kurasa za
Historia tangu mwanzo wake hadi mwishgo wake, tusingelimpata hata mtu mmoja
aliye chukua msimamo huu mtukufu kwa adui zake. Naam, ni ukweli ulio dhahiri
kwamba hakuna katika Historia yote msamaha ulio fikia msamaha huu walio
upata watu wa Makah. Hii ni kwa sababu hakuna katika watu wote, mwanadamu
aliye fikilia ukamilifu wa kiutu kiasi alicho fikia Muhammad; Mtume wa
Allah-Rehema na Amani zimshukie. Kwa ukweli huu basi, sio ajabu kwa Mtume wa
Allah kuchukua msimamo huu wa pekee katika Historia nzima kwa adui zake.
Mtume wa Allah hakuwa mmojawapo wa makamanda au wafalme, wala hakuwa
akiyalenga yale wayalengayo wafalme; yaani kushibisha matamanio ya nafsi
zao. Hakika si vinginevyo, hiyo ilikuwa ni rehema kutoka kwa Allah Taala
aliyo ipeleka kwa waja wake na hapo ndipo unapo dhihirika ukweli wa kauli
yake Taala: “NASI HATUKUKUTUMA ILA UWE NI REHEMA KWA WALIMWENGU WOTE”.
[21:107] Kwa hivyo basi, po pote anapo kuwepo Mtume na rehema ya Allah
huwepo pamoja naye, ikamuenea rafiki na adui, muumini na kafiri. Kila mmoja
akapata fungu lake katika rehema hiyo, kama vitongoji vya ardhi vinavyo
chukua baraka ya mvua, basi ikatoa matunda rutuba yake au ikapoa hewa yake.
|