|
i.
Msamaha wa Mtume wa
Allah wazifungua nyoyo za watu wa Makah kuuelekea Uislamu na kuzijaza mahaba
ya Mtume:
Kwa yakini
msamaha huu mtukufu uliteremsha baridi na salama ndani ya nyoyo zile
kukutavu ambazo muda mrefu ziliunguzwa na uadui kuielekea nafsi teule hii
(Mtume). Na ambazo kwa kipindi kirefu zilipofushwa na hasadi zikashindwa
kuuitika moyo – huruma huu (Mtume). Kwani Mtume wa Allah-Rehema na Amani
zimshukie-aliendelea kuwalingania kheri (Uislamu) watu hawa kwa zaidi ya
miaka ishirini. Na akijaribu kwa kila njia kuwaelekezea na kuwapondokeshea
kwenye kheri hiyo, lakini wao wakawa vipofu wasiione kheri hiyo na viziwi
wasiisikie: “NA WAKASEMA: NYOYO ZETU ZIMO KATIKA VIFUNIKO KWA HAYO MNAYO
TUITIA, NA MASIKIO YETU YANA UZIWI NA BAINA YETU NA WEWE LIPO PAZIA...”
[41:05] Na wakawa wakimbadilishia uadui kwa mapenzi na uovu kwa wema na
wakamkadhibisha, wakamkata pande na wakamfukuza Makah. Isitoshe wakampiga
vita na kumkusanyia washirika wa kumpiga na wakawa kipindi chote hicho
wakiingojea kwa hamu kuu fursa ya kumuangamiza. Sasa Allah alipo mpa ushindi
dhidi yao na akammakinisha shingo zao, Mtume wa Allah-Rehema na Amani
zimshukie-akayasahau yote yaliyo pita; yaani uovu na uadui walio mtendea. Na
si hivyo tu, akawazawadia msamaha mwema enevu, eeh ni nafsi tukufu iliyoje
hii, nafsi inayo lipa uovu kwa wema kwa adui mtenzwa nguvu! Hakika hiyo ni
nafsi ya Mtume mtukufu ambaye katu hakuweka nafsini mwake ila kheri na
hakuwa akitaka ila utengenevu tu. Na ambaye kamwe hakuwa jabari, dhalimu
wala mlipa kisasi na wala hakuwa katika ghadhabu na uradhi wake ila kama
asemavyo Allah Taala: “HAKIKA AMEKWISHA KUJIENI MTUME KUTOKANA NA NYINYI
WENYEWE (wanadamu), YANAMUHUZUNISHA YANAYO KUTAABISHENI ANAKUHANGAIKIENI
SANA. KWA WAUMINI NI MPOLE NA MWENYE HURUMA”. [9:128]
Kwa yakini msamaha huu ulikuwa ni ufunguzi (fat-hi) mwingine
ambao kupitia huo Allah alizifungua nyoyo kanushi hizi. Na kupitia ufunguzi
huo akakikunja kiwingu cha nafsi kibri hizi, kwa ajili hiyo basi zikawa
zinafurikwa na mahaba na ikhlasi. Na zikifuata twaa na zikijiunga chini ya
bendera ya Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-kwa khiari zikiwa
nyenyekevu. Na amesema kweli Allah Taala pale alipo sema: “MEMA NA MAOVU
HAYALINGANI. PINGA UOVU KWA LILILO JEMA ZAIDI. HAPO YULE AMBAYE BAINA YAKO
NAYE PANA UADUI ATAKUWA KAMA RAFIKI JAMAA WA KUKUONEA UCHUNGU. LAKINI
HAWAPEWI WEMA HUU ILA WANO SUBIRI, WALA HAWAPEWI ILA WENYE BAHATI KUBWA”.
[41:34-35] Hivi ndivyo Makah ilivyo ifungulia milango yake da’awah
(ulingano) na ikatupa dini-mapokeo yake na kumfuata Mtume wake aliye
muaminifu mwenye kuaminiwa. Kwa hatua/kitendo chao hicho, ngome ya shirki
ikawa imebomoka na kuanguka pwaa na kikaondoka kile kikwazo madhubuti
kilicho kuwa kikiizuia da’awah kwa zaidi ya miongo miwili. Na tangu siku
hiyo, Makah ikawa ndio Ka’abah ya Uislamu na Qiblah cha waislamu wa
mashariki na magharibi ya dunia. Na itaendelea kuwa hivyo mpaka hapo Allah
atakapo irithi ardhi na vilivyoko juu yake, inshallah.
ii.
Watu wa Makah wala
kiapo cha utii kwa Uislamu mbele ya Mtume:
Mtume wa
Allah-Rehema na Amani zimshukie-aliingia Makah mwezi 20-Ramadhani, mwaka wa
nane wa Hijrah (Januari 630 A.D.) Na akabakia humo kwa takriban siku
ishirini akipanga na kutengeneza mambo yake (Makah) na kuitoa katika anga la
shiriki kuileta katika anga la Uislamu na Tauhidi. Akamuamuru Bilali
kuadhini juu ya Al-Ka’abah akapanda juu yake na akaanza kuianikiza sauti
yake pande zote: “ALLAAHU AKBAR ALLAAHU AKBAR, ALLAAHU AKBAR ALLAAHU AKBAR.
ASH-HADU AN LAA ILAAHA ILLAL-LAAH, ASH-HADU AN LAA ILAAHA ILLAL-LAAH.
ASH-HADU ANNA MUHAMMADAN RASUULULLAAH, ASH-HADU ANNA MUHAMMADAN
RASUULULLAAH. HAYYA ‘ALAS-SWALAAH, HAYYA ‘ALAS-SWALAAH. HAYYA ‘ALAL-FALAAH,
HAYYA ‘ALAL-FALAAH. ALLAAHU AKBAR ALLAAHU AKBAR. LAA ILAAHA ILLAL-LAAH”.
Halafu swala ikakimiwa, akainuka Mtume wa Allah-Rehema na Amani
zimshukie-kuwaswalisha watu katika “Haram” ya nyumba tukufu ya Allah. Na
watu nao wakasimama pamoja nae katika safu zao, wakirukuu kwa rukuu yake na
wakisujudu kwa sijida yake na wakiinuka kila alipo inuka na wakikaa kila
alipo kaa.
Mandhari nzuri hii ikawa na athari yake tendaji ndani ya
nafsi za mushrikina miongoni mwa wazalendo wa Makah. Wakaupokea Uislamu kwa
khiari zao na wakamkusanyikia Mmtume wa Allah-Rehema na Amani
zimshukie-wakila kiapo cha utii kwa Uislamu. Mtume akakaa kuwangojelea
katika kilima Swafaa, Sayyidina Umar-Allah amuwiye radhi-akasimama kwenye
majlisi ya Mtume akipokea kiapo cha watu kwa niaba ya Mtume. Akawa anachukua
kiapo kwao juu ya usikivu na utii kwa Allah na Mtume wake katika yale
wayawezayo. Alipo maliza kuchukua kiapo cha wanaume, wakaja wanawake wakila
kiapo juu ya kutomshirikisha Allah na cho chote, wala hawataiba, hawatazini.
Na wala hawatawaua watoto wao, hawatazua uzushi wanao uzua tu wenyewe baina
ya mikono yao na miguu yao na wala hawatamuasi katika jambo jema. Mtume
akawapokelea kiapo chao hicho cha utii na akawaombea maghufira kwa Allah.
Kwa ajili hiyo basi, Makah ikaingia katika kundi la Uislamu na ikawaenea
watu wote roho mpya ya uhuru, udugu na usawa. Na ikawa miongoni mwa mambo
yaliyo wasukuma watu wa Makah kuingia katika Uislamu, ni kwamba Mtume wa
Allah-Rehema na Amani zimshukie-hakumtenza nguvu ye yote kuukubali Uislamu.
Pamoja na ukweli kwamba alikuwa na nguvu na mamlaka ya kufanya hivyo, lakini
katu hakutumia nguvu yake hiyo kumlazimishia mtu Uislamu. Bali aliwaacha
huru kuchagua dini waitakayo; atakaye kuwa muislamu na asilimu na atakaye
kubakia na dini yake na abakie. Kiasi kwamba hata Swafwaan Ibn Umayyah alipo
kuja kutaka kusilimu, alimwambia Mtume wa Allah: “Nipe khiari miezi miwili”,
Mtume-Rehema na Amani zimshukie-akamwambia: “Wewe una khiari miezi minne”.
Pamoja na kwamba huyu Swafwaan alikuwa miongoni mwa wale ambao Mtume wa
Allah aliruhusu wauawe, kwa sababu ya uadui wao mkubwa na maudhi yao kwa
waislamu. Lakini bado alipewa uhuru wa kuchagua na kuamua, msamaha huu wa
Mtume kwa watu alio kwisha toa ruhusa ya kuuawa siku ya Fat-hi Makah
ukiuachilia mbali msamaha wake enevu kwa watu wa Makah. Ulikuwa ni miongoni
mwa vishawishi na vichocheo vya kukubalika kwa Uislamu Makah, basi haukupita
muda mrefu ila wazalendo wote wa Makah walisilimu. Wakaridhia Allah kuwa
ndiye Bwana Mlezi wao badala ya masanamu, Uislamu ndio dini yao badala ya
ushirikina na Muhammad ndiye mtume wao.
Watu hawa ambao Mtume wa Allah-Rehema na Amani
zimshukie-aliruhusu kumwagika patupu damu yao, walikuwa kiasi cha watu kumi
na watano hivi; wanaume na wanawake. Miongoni mwao akiwemo huyu Swafwaan Ibn
Umayyah, Ikrimah Ibn Abu Jahli, Wahshiy Ibn Harb; muuaji wa Sayyidina Hamzah
na Hind Bint Utbah; mlaji wa ini la Hamzah. Walikuwa ni adui dhahiri aliye
fikilia upeo wa uadui na maudhi kwa waislamu. Mtume wa Allah aliwasamehe
wengi miongoni mwao, hakuua miongoni mwao ila wanaume watatu na mwanamke
mmoja.
|