|
iii.
Mtume wa Allah
azifutilia mbali athari za shirki katika mji wa Makah na vitongoji jirani:
Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akaanza
kuzifuta athari za shirki katika mji wa Makah. Akatoa amri ya kuvunjwa
masanamu yote yaliyo kuwa yamewekwa kuizunguka Al-Ka'abah. Kama wasemavyo
wapokezi wa Sira, yalikuwepo masanamu mia tatu na sitini katika mzingo wa
Al-Ka'abah. Kila kitongoji miongoni mwa vitongoji vya Waarabu kilikuwa na
sanamu lake maalumu, basi masanamu yote hayo yakavunjwa kwa amri ya Mtume.
Kwa kitendo hicho, athari ya ibada ya miungu sanamu ikawa imefutwa kabisa
kwenye Al-Ka'abah tukufu. Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alipo
maliza kuitwaharisha Al-Ka'abah kutokana na athari ya kuabudiwa asiye
Allah. Alimuamrisha mlinganiaji kuwalingania watu wa Makah ya kwamba: "Ye
yote mwenye kumuamini Allah na siku ya mwisho, basi asiliache nyumbani kwake
sanamu ila amelivunja". Na haikuwepo nyumba yo yote Makah ila ndani yake
kulikuwa na sanamu ambalo hutabaruku nalo watu wa nyumba hiyo na
wakijipangusa nalo wanapo ingia au kutoka nyumbani. Watu wa Makah wakaupokea
munada wa Mtume kwa utii ulio tukuka, wakayaendea masanamu waliyo kuwa
wakiyaabudu na kuyavunja vunja. Hind Bint Utbah akawa analipiga shoka sanamu
lake hata akalivunja vipande vipande ilhali akisema: "Tulikuwa ghururini
kwako".
Halafu Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akavituma
vikosi kwenda kwa makabila ya Waarabu yaliyo izunguka Makah. Waende huko
kuyavunjilia mbali masanamu ya huko, akamtuma Khalid Ibn Al-Waleed
kukiongoza kikosi cha watu thelathini kwenda "Batwn Nakhlah" kulivunja
"Uzzah". Hili ndilo lililo kuwa kubwa la masanamu ya Makureishi, akalivunja
kama alivyo amrishwa. Akamtuma Amrou Ibn Al-Aaswi na kundi la waislamu
kwenda kwa kabila la Hudheil ili kulivunja sanamu lao "Swuwa'a", akalivunja.
Akamtuma Sa'ad Ibn Zayd kwenda Mushallal katika mwambao wa pwani na watu
ishirini kulivunja "Manaata"; sanamu la kabila la Kalbi na Khuzaah,
akalivunja. Namna hivi ndivyo Mtume wa Allah-Rehema na Amani
zimshukie-alivyo kuwa akizifuta sura/alama na athari za shirki katika mji wa
Makah na vitongoji vyake. Hadi athari zake ziondoke kabisa ndani ya nafsi na
mpaka akili zihajiri mawazo/fikra za mapokeo na ada na nyoyo zitakate na
kila kinacho zizuia kufungamana na Allah Mola pekee asiye na mshirika.
SOMO LA TANO – VITA VYA HUNEIN
i.
Kabila za Hawaazin na
Thaqiyf zajiandaa kumshambulia Mtume, lakini Mtume awawahi:
Makabila mawili; Hawaazin na Thaqiyf yalichelea
kunyolewa na wembe ulio wanyoa Makureishi, wakavunjiwa masanamu yao na
kubadilishiwa dini yao ya tangu na tangu. Ukaondoshwa utukufu na fakhri yao
na wakawa chini ya mamlaka ya kijana mdogo; Muhammad, wakachelea kufikwa na
haya yaliyo wafika Makureishi. Kabila la Thaqiyf lilikuwa na makazi yake
Twaif, likijiranikiana na Hawaazin walio ishi kwenye majabali yanayo
kizunguka kitongoji cha Twaif. Twaif ndicho kilicho kuwa kitongoji chenye
ardhi yenye rutuba kuliko vitongoji vyote vya rasi ya Waarabu. Na ndio iliyo
kuwa makao ya "Laata"; sanamu kubwa la Waarabu baada ya "Hubal". Wazalendo
wa Twaif wakadhania kwamba Muhammad akisha wamaliza Makureishi, lazima
atakuja kwao. Watu wenye busara na sauti kutoka katika makabila mawili haya;
Hawaazin na Thaqiyf wakakutana na kushauriana. Baada ya mashauriano yao
hayo, wakawafikiana kwa kauli moja kumshambulia Mtume kabla hajawashambulia
wao. Yakajiunga nao makabila ya Naswru, Jusham, Sa'ad Ibn Bakri na baadhi ya
watu wa kabila la Baniy Hilaal. Wakapata watu wengi, washirika hawa walipo
kusanyika wakampa uongozi Maalik Ibn Auf; mtu wa kabila la Naswru awaongoze
katika mapambano yao dhidi ya Muhammad.
Huyu Maalik Ibn Auf alikuwa ni kijana mbichi, mwingi wa
jazba, akaona asiwapeleke watu wake katika medani ya vita ila kwa
hamasa/jazba na mori mkubwa. Akawatoa watu wake kwenda medanini wakiwa
pamoja na mali, wake na watoto wao ili kuwatia hamasa na kuwafanya kuwa
tayari kufa kwa ajili ya kuilinda heshima yao. Miongoni mwa watu wake
alikuwemo Duraid Ibn Swimah ambaye alikuwa mzee aliye komazwa na uzoefu na
vita, akawa na uoni wa mbali. Lakini wakati huo alikuwa ni mtu mzima sana,
kwa hivyo hakuwa tena na uwezo wa kuongoza jeshi. Alipo sikia juu ya mpango
huu wa kamanda kijana; Maalik Ibn Auf, akamuuliza sababu ya kufanya hivyo,
Maalik akamjibu: "Hakika si vinginevyo, nimetaka niweke nyuma ya kila mtu
mke na wanawe na mali yake ili awapiganie". Duraid akamuuliza: "Je, mtu
aliye shindwa ana matashi? Hakika kama ushindi ni wako, basi hatokunufaisha
ila mtu na upanga na mkuki wake basi. Na fungu lako likiwa ni ushindwa
utakuwa umefedheheshwa kwa ahali zako na mali yako". Lakini Maalik akawa
mkaidi asimsikilize mtu mzima huyu mwenye busara, uoni na uzoefu wa kutosha.
Akaishikilia rai yake, akatoka na watu wake kwenda kwenye medani ya vita,
wakiwa na familia zao na mali yao.
Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akasikia juu ya
maandalizi kabambe yaliyo fanywa na Hawaazin na Thaqiyf dhidi yake. akamtuma
jasusi miongoni mwa majasusi wake akampelelezee ukweli wa khabari hii iliyo
mfikia. Ulipo mbainikia ukweli wa azma yao juu yake, Mtume akapanga
kuwashambulia kwa kuwashtukiza kabla wao hawajamuwahi. Akatoka Makah siku ya
Jumamosi, mwezi 6-Shawaal {28/January/630 A.D.} akiwakusudia Hawaazin na
Thaqiyf akiwa na watu alfu kumi na mbili; watu alfu kumi alio kuja nao Makah
na alfu mbili katika watu wa Makah. Watu wa Makah walishiriki katika vita na
wakampa Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-msaada wa mali na silaha
alio utaka. Swafwaan Ibn Umayyah alimwazima Mtume nguo mia moja za vita
(dir-u) na baadhi ya watu watukufu wa Makah walimkopesha mali zao ili
kumuwezesha kufanikisha vita. Na wakatoka pamoja naye watu wengi katika
mushrikina, jeshi likatoka katika mandhari ya nguvu kubwa likiwa na alama
zote za ushindi. Kiasi cha kuwafanya waislamu kudhania kwamba katu
hawatoshindwa kwa wingi wao huo mpaka yasemekana kwamba wanawake na watoto
wa Makah walitoka nyuma ya jeshi hili kwa tamaa ya kupata ngawira.
|