|
ii.
Mkakati wa adui ulikuwa
ni kuwashambulia waislamu kwa ghafla kutokea kila upande wakati wa alfajiri:
Hawaazin na
Thaqiyf na washirika wao miongoni mwa makabila ya Kiarabu walikuwa tayari
wamesha toka na watu wao kuelekea bonde la Hunein. Hili ni mojawapo ya
mabonde ya Tihaamah, bonde lenye mteremko mkali, lililo tandawaa katika njia
nyembamba za majabalini. Maalik Ibn Auf akaonelea apige kambi katika
maingilio ya bonde hili na aitumie hali – maumbile ya mahala hapo katika
kuzivunja nguvu za waislamu. Akakipanga kimoja cha vikosi vyake juu ya zile
njia finyu za majabalini na vikosi vilivyo salia akavipanga pembeni mwa
jangwa na fichifichi zake. Na akawapa amri warusha mishale wake
kukishambulia kwa nguvu zote kikosi cha mwanzo cha waislamu mara tu kitakapo
tokezea. Wawamwagie mvua ya mishale kutokea pande zote mpaka waingiwe na
kiwewe, mashambulizi haya makali na ya kushtukiza yatauharibu mpango wao
mzima wa vita. Hapo ndipo jeshi litawavaa nao wakiwa katika hamkani na kutoa
pigo takatifu litakalo wamaliza kabisa na kuwafanya wasalimu amri.
Hivi ndivyo Maalik Ibn
Auf alivyo upanga mkakati wake wa vita, kama kwamba alitambua mkakati wa
adui yake nae akaanzia hapo hapo. Riwaya mbali mbali zimetaja kwamba Mtume
wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alifika Hunein jioni ya siku ya Jumatatu,
mwezi 10-Shawwal. Ulipo ingia usiku, Maalik Ibn Auf akawaendea watu wake na
kuwapanga katika medani ya vita; bonde la Hunein. Akawapa amri ya
kumshambulia Mtume na maswahaba wake mashambulizi ya mtu mmoja. Mtume kwa
upande wake, akawapanga maswahaba wake kivita wakati wa maladaku (karibu na
alfajiri). Akawapanga safu safu na kuwapa bendera za vita wanao stahiki
miongoni mwa Muhajirina na Answari na kabila za Waarabu. Akamuweka Khalid
Ibn Al-Waleed mbele ya kikosi cha farasi, kama kwamba mkakati wa Mtume wa
Allah-Rehema na Amani zimshukie-ulikuwa ni kumshtukiza adui wakati wa kabla
ya alfajiri. Wakati ambao watu huwa wamelala fofofo na si Mtume wala
maswahaba wake aliye kuwa anajua kuwa tayari adui yao kesha watangulia.
Wakiwa wamejificha kuwangojelea katika vichochoro na finyu za majabalini.
iii.
Adui awashtukiza
waislamu na kuwafanya kutapanyika hovyo:
Katika kiza
cha alfajiri, waislamu wakasonga mbele, kikaenda kikosi chao cha mbele cha
wapanda farasi chini ya uamiri wa Khalid Ibn Al-Waleed. Nyuma yake
vikifuatia vikosi vingine vya jeshi na nyuma ya jeshi hili akafuata Mtume wa
Allah akiwa amempanda nyumbu wake mweupe. Akiwa amevaa vazi rasmi la vita,
akizungukwa na maswahaba kadhaa mongoni mwao akiwemo ami yake Abbas Ibn
Abdul-Mutwalib. Kikosi cha mbele kilipo kanyaga tu maingilio ya bonde,
kikashtukizwa na mvua ya mishale inayo washukia katika kiza kutokea kila
upande. Kiasi cha kutotambua mvua hiyo inatokea mbinguni au ardhini, ardhi
pamoja na ukunjufu wake ikawawia finyu na hawakuwa na budi ila kurejea
nyuma. Urejeaji nyuma wao huu ulikuwa ni wa ghafla na usio na mpangilio,
adui akaitumia vema fursa hiyo, akashambulia kwa farasi na miguu. Akieneza
kwa waislamu michomo ya mishale na mapigo ya panga hata yakafumuka mauaji
katika kabila la Baniy Naswri Ibn Muaawiyah kisha yakapindukia kwa Baniy
Ruaab. Kizaizai na kimuhemuhe kikalienea jeshi la waislamu, safu zake
zikatambaliwa na khofu ya ushindwa, watu wakaanza kurudi nyuma hovyo bila ya
kujielewa.
iv.
Mtume wa Allah athibiti
mbele ya adui na awaita watu kurejea katika medani ya vita:
Mtume wa
Allah-Rehema na Amani zimshukie-alipo kiona kitimtim na fazaa hii na
akawaona maswahaba wake wakikimbia hovyo hovyo. Akaanza kuwapigia ukelele:
“Mnaenda wapi watu nyie! Njooni kwangu, mimi ni Mtume wa Allah! Mimi ndiye
Muhammad mwana wa Abdul-Mutwalib!...”
Mimi ndiye Mtume wala
si uongo *** mimi ndiye kijana wa Abdul-Mutwalib!
Maswahab wakiwa katika
kizaizai chao, hawasikii wala hawafahamu, wala hawatambui cho chote katika
vilivyo wazunguka. Mpaka wakachangukana na Mtume wa Allah-Rehema na Amani
zimshukie-wakimuacha na watu wachache katika Muhajirina na Answaari na watu
wake wa nyumbani (jamaa/ndugu zake). Abbas Ibn Abdul-Mutwalib; ami yake
Mtume, alikuwa ni mtu mwenye sauti kali, Mtume akampa amri awakhofishe
Muhajirina na Answaari warejee. Abbas akaanza kupiga mayowe: “Enyi kusanyiko
la Answaari ambao mlitoa makazi na mkamnusuru Mtume nyiee! Enyi kusanyiko la
Muhajirina ambao mlikula kiapo cha utii chini ya mti ule nyiee! Njooni kwa
Mtume wa Allah nyieee!” Ukelele ule ulipo gonga tu ngoma za masikio yao,
ukawa kama ni dawa iliyo warejeshea fahamu zao wakageuka wakichupiana kwa
Mtume wa Allah ilhali wakisema: “Labbayka Labbayka!” Kiasi cha kufikia mmoja
wao kushuka juu ya ngamia wake na kukimbia kwa miguu kutokana na kuzuiwa na
msongamano wa watu. Akiharakia kwa Mtume, akiwa na upanga na ngao yake,
likakusanyika kumzunguka Mtume kundi la watu wakweli katika azma na imani
yao. Likasimama kidete mbele ya adui mpaka likafanikiwa kuyazuia
mashambulizi yake, halafu tena waislamu wakakamatana barabara. Na wakati huo
tayari kulikuwa kumesha pambazuka, wakaweza kuona maficho ya adui,
wakamshushia mashambulizi ya mtu mmoja. Makundi ya adui yakatapanywa kama
kundi la nzi walio kurupushwa, waislamu wakawa wanawafukuza, wakauawa walio
uawa, wakatekwa walio tekwa na wakakimbia walio ponyoka. Ama kiongozi wao;
Maalik Ibn Auf, yeye alikimbilia kwenye ngome za Twaif akapata hifadhi humo,
huku akiacha nyuma yake kila alicho kiswaga; mali, wanyama, wanawake na
watoto. Waislamu wakapata ngawira nono mno ambayo ni dhiki mno kuihesabu
ukaisha.
|