|
iv.
Mtume wa Allah
awafuatilia maadui mpaka Twaif baada ya kuwasambaratisha Hunein:
Mtume wa
Allah-Rehema na Amani zimshukie-akaamuru mateka na mali zikusanywe na
kupelekwa katika bonde la “Ji’iraanah”. Halafu Mtume na maswahaba wake
wakaenda Twaif, ambako Maalik Ibn Auf na baadhi ya watu wake na wale wa
Thaqiyf walio ponyoka walikimbilia huko. Thaqiyf walikuwa wamejihifadhi
ngomeni mwao na kufunga milango yake na wakawa wamechukua chakula na silaha
za kutosha muda mrefu. Hayo yakiwa ni maandalizi ya botari (mzingiro) ndefu,
iwapo Mtume ataamua hivyo. Na Thaqiyf walikuwa na umahiri mpevu kwa mapigano
ya ndani ya ngome, wakakongamana kuzilinda ngome zao kwa nguvu zao zote. Na
kuzuia kila jaribio litakalo fanywa na waislamu kwa lengo la kuzifikia na
hatimaye kuzifungua ngome zao.
Mtume-Rehema na Amani
zimshukie-alipo fika Twaif na akaona watu wake wamejitia ngomeni, akataka
kuwangojelea kidogo akitumai huenda wakajisalimisha wenyewe bila ya vita.
Lakini alipo karibia tu ngome za Twaif, ikamnyeshea mvua ya mishale,
likauawa kundi la waislamu na lingine kujeruhiwa. Mtume na naswahaba wake
wakarudi nyuma umbali ambao mishale haiwezi kufika, hapo akapiga kambi
kuzizunguka ngome zile. Akawapiga botari kwa takriban siku sihirini na moja.
SOMO LA SITA.
i.
Waislamu watumia njia
zote kuwatoa maadui ngomeni mwao bila mafanikio:
Ndani ya
kipindi chote hicho, waislamu wakawa wanatumia njia/mbinu mbali mbali
kuwatoa maadui ngomeni mwao bila mafanikio. Wakawataka watoke baadhi yao
kuja katika mapambano ya wawili wawili (mubaarazah), wakakataa, wakawaibisha
kwa uoga na kutimua mbio, hilo pia lisiwatoe. Wakafunga kombeo kubwa na
kuwarushia mawe makubwa ili kubomoa maingilio ya ngome, mawe hayo
hayakufikia lengo. Baadhi ya waislamu wakaingia katika kifaru (tank) cha
mbao, wakasonga mbele ili kwenda kuutoboa ukuta wa ngome. Thaqiyf
wakawarushia vipande vya chuma vilivyo tiwa motoni vikawa vyekunduu, hivi
vikawaunguza na kuwalazimisha waislamu kutoka ndani ya kifaru chao cha mbao.
Hapo wakarushiwa mawe na kuuawa baadhi yao, baada ya jaribio hilo la kubomoa
ukuta kukwama waislamu wakaanza kukata mizabibu yao. Thaqiyf wakamtumia
ujumbe Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-wakimuomba asiikate, aiache
kwa ajili ya Allah na ndugu, Mtume akawakataza waislamu wasiendelee kuikata.
Naam, hivi ndivyo
waislamu walivyo jaribu kwa kila njia/mbinu zao kuwatoa mushrikina ndani ya
ngome zao au kuwaingilia humo, wasiweze. Mtume wa Allah akaamrisha upigwe
munada kwa watumwa wa Thaqiyf ya kwamba: “Ye yote atakaye toka kuja kwetu,
basi huyo yuko huru”. Watumwa wale walipo usikia munada huo, wakapenya
miongoni mwao kiasi cha watu kumi na kitu, Mtume akawaacha huru kama alivyo
ahidi.
ii.
Mtume wa Allah asitisha
mzingiro wa adui:
Mtume wa
Allah-Rehema na Amani zimshukie-akajua kupitia kwa wale watumwa alio waacha
huru, kwamba Thaqiyf wamejitia ngomeni na chakula cha kutosha mwaka mzima.
Na kwamba wao wameazimia kubakia ngomeni mwao humo mpaka hapo chakula chao
kitakapo malizika, hapo ndipo watatoka na kupigana hadi mtu wa mwisho. Mtume
akaona kwa taarifa hii aliyo ipata, hakuna faida ya kuendelea na botari na
kwamba hivi sasa nguvu ya adui imekatika hatoweza kuleta madhara tena. Na
kwamba katika maficho yake hayo amekuwa mithili ya kicheche ndani ya shimo
lake; akimngojelea atamkamata na akimuacha hatamdhuru. Na miezi mitukufu
ambayo vita vimeharimishwa ndani yake ilikuwa inakaribia, Mtume akaonelea
afunge msafara na maswahaba wake wamuache adui huyu kwa muda. Huenda Allah
akawaongoa, wakamjia ilhali wakiwa waislamu watiifu na hivyo ndivyo ilivyo
kuwa. Yakamthibitikia Mtume wa Allah yale aliyo yatamani, kwani haikupita
ila miezi michache tu, Thaqiyf wakaukubali Uislamu na wakaingia katika dini
ya Allah kwa uradhi wa nafsi zao, wakiwa wanyenyekevu.
|