|
iii.
Mtume wa Allah atumia
zawadi nono kuwashawishi viongozi wa Makureishi kusilimu:
Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-na
maswahaba wake-Allah awawiye radhi-wakaondoka kurejea “Ji’iraanah; mahala
ambapo ngawira ya Hunein ilihifadhiwa. Huko Mtume akaamuru ngawira hiyo
ihesabiwe, wakakutikana ngamia ishirini na nne alfu, mbuzi/kondoo arobaini
alfu. Wakia alfu nne za madini ya fedha, na wanawake na watoto alfu sita.
Mtume wa Allah akawaweka kando mateka wale (wanawake na watoto), akaanza
kugawa mali baina ya maswahaba wake. Fungu la mpiganaji wa miguu likawa ni
ngamia wanne na mbuzi/kondoo arobaini na fungu la mpanda farasi likawa ni
mara tatu ya hivyo.
Na zilivyo kuwa nafsi kwa mujibu wa maumbile yake ni zenye
kuchomozea mali na kukawa kutoa ni ufunguo miongoni mwa funguo za nyoyo na
mlango miongoni mwa milango ya nafsi. Mtume wa Allah-Rehema na Amani
zimshukie-akazidisha mgao kwa kundi la watukufu katika Makureishi, viongozi
na maamiri wa Waarabu. Akikusudia kwa yote hayo, kuzivutia nyoyo zao kwenye
Uislamu. Mtume alitambua kwamba wengi miongoni mwa walio silimu katika kundi
hili la viongozi, bado wana pepeso za jahilia. Na kwamba wengi miongoni mwa
ambao hawajasilimu, walitoka katika vita hivi kwa tamaa tu ya kupata
ngawira. Kwa ajili hii basi, Mtume akaona ni vema azitie nguvu nyoyo zao kwa
kuwamegea fungu nono la mali. Hili likapelekea kusilimu kwa wale ambao
walikuwa si waislamu na kuzidi imani ya Uislamu kwa wale walio kwisha
silimu.
Imeandikwa katika kitabu [IMTAA’UL-ASMAA] kwamba Abu Sufyaan
Ibn Harb alikuja mbele ya Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-na ilhali
fedha ikiwa mbele yake, akasema: “Ewe Mtume wa Allah wee! Umekuwa mwingi wa
Makureishi kwa mali!” Mtume akatabasamu, Abu Sufyaan akasema: “Nipe katika
mali hii ewe Mtume wa Allah, Mtume akasema: “Ewe Bilaali, mpimie Abu Sufyaan
wakia arobaini za fedha na mpe ngamia mia moja”. Abu Sufyaan akasema: “Na
mwanangu Yazid je?”, Mtume akasema: “Mpimie Yazid wakia arobaini na mpeni
ngamia mia moja”. Abu Sufyaan akasema: “Na mwanangu Muaawiyah, ewe Mtume wa
Allah”. Mtume akasema: “Ewe Bilali mpimie wakia arobaini na umpe ngamia mia
moja”. Abu Sufyaan baada ya kupewa vyote hivyo akasema: “Hakika kwa yakini
wewe ni karimu, nakufidia baba na mama yangu. Wallah nilikupiga vita, basi
neema/bora ya mpigwa vita ni wewe! Kisha nikakupa amani, basi bora ya mpewa
amani ni wewe! Allah akujaze kheri!”
Na imepokewa kwamba Mtume wa Allah-Rehema na Amani
zimshukie-siku hiyo alimpa Swafwaan Ibn Umayah ngamia mia moja, kisha mia
wengine na mia tena. Halafu akamuona akilikodolea macho bonde lililojaa
mifugo, akamuuliza: “Limekupendeza bonde hili ewe Abu Wahab?”, akajibu:
“Naam”. Mtume akamwambia: “Hilo ni lako na vyote vilivyomo humo”. Swafwaan
akasema: “Hakika wafalme hawawi na nafsi njema kiasi hiki, nafsi ya ye yote
haikuwa njema kiasi hiki ila mtu huyo ni mtume. Nashuhudia kwamba hapana
afaaye kuabudiwa kwa haki ila Allah na kwamba wewe ni Mtume wa Allah.
iv.
Baadhi ya maswahaba
walishindwa kuiona falsafa ya Mtume katika hili na kuanza kumdhania dhana
mbaya:
Ilifichikana
kwa wengi miongoni mwa maswahaba hekima ya Mtume wa Allah-Rehema na Amani
zimshukie-katika upaji na utoaji huu kwa makundi fulani ya watu. Mpaka
baadhi ya watu wakafikia kusema: “Hakika wallah mgao huu si wa uadilifu na
wala haukukusudiwa kwao dhati ya Allah”. Mtume wa Allah alipo yasikia maneno
hayo, alighadhibika mno akasema: “Ni nani basi atakaye fanya uadilifu ikiwa
Mtume wa Allah hakufanya uadilifu? Allah amrehemu Musa aliudhiwa kwa maudhi
makubwa kuliko haya, akasubiri”. Na hata ikafikia mabedui kuchelea mali zote
kuchukuliwa na watukufu/viongozi hao, wakamfuata Mtume wa Allah wakisema:
“Ewe Mtume wa Allah, tugawie fungu letu”. Wakamshikilia na kumng’ang’ania
hadi wakamshurutisha kukaa penye mti, wakampokonya shuka lake la kujitandia.
Mtume akasema: “Enyi watu nyie, nirejesheeni shuka langu, wallah lau mimi
ningelikuwa na mifugo kwa idadi ya miti ya Tihaamah, kwa yakini
ningelikugawieni wote. Kisha msinikute mimi kuwa ni bakhili, wala muoga wala
muongo”. Halafu akaung’oa unywele kutoka katika nundu ya ngamia, akauinua
baina ya vidole vyake akasema: “Wallah mimi sina katika mgao wenu hata
unywele huu ila khumsi (1/5) na hiyo khumsi yenyewe imerejeshwa kwenu”.
Hekima/falsafa hii
ilifichikana hata kwa Answaari, kiasi cha kufikia kunong’ona baina yao.
Imepokewa kutoka kwa Abu Said Al-Khudriy-Allah amuwiye radhi-amesema: “Zama
Mtume wa Allah alipo wapa kile alicho wapa Makureishi na kabila za Waarabu
katika mali ile. Na Answaari hawakupata cho chote katika mali hiyo, kikundi
hiki cha Answaari kikatokota kwa ghadhabu nafsini mwao, mpaka akafikia
kusema mmoja wao: “”Wallah Mtume wa Allah amekutana na jamaa zake”. Sa’ad
Ibn Ubaadah akaingia kwa Mtume wa Allah akasema: “Ewe Mtume wa Allah, hakika
kikundi hiki cha Answaari kinaunguzwa na ghadhabu juu yako ndani ya nafsi
zao kwa ajili ya vile ulivyo fanya katika mali hii uliyo ipata. Ukawagawia
jamaa zako na ukatoa mali adhimu kwa makabila ya Waarabu na kikundi hiki cha
Answaari hakikupata cho chote katika mali hiyo”. Mtume wa Allah-Rehema na
Amani zimshukie-akauliza: “Wewe uko upande gani katika hilo ewe Sa’ad?”,
akajibu: “Ewe Mtume wa Allah, mimi siko ila pamoja na jamaa zangu”. Mtume
akasema: “Haya nikusanyie jamaa zako hao katika uwanja huu”.
|