|
SOMO LA SABA.
i.
Malezi matukufu:
Sa’ad akatoka akawakusanya Answaari katika uwanja
ule alioagizwa na Mtume, Mtume wa Allah-Rehema na Amani
zimshukie-akawaendea. Akamuhimidi Allah na kumsifia kwa sifa stahiki zake,
halafu akasema: “Enyi kusanyiko la Answaari! Ni maneno gani haya yaliyo
nifikia kutoka kwenu?! Na ghadhabu mliyo nayo juu yangu ndani ya nafsi
zenu?! Je, mimi sikukujilieni ilhali mu wapotofu, Allah akakuongozeni! Na
ilhali mkiwa mafakiri, Allah akakupeni ukwasi, na ilhali mkiwa maadui Allah
akaziunganisha nyoyo zenu?!” Wakasema: “Kwani ndivyo hivyo hivyo usemavyo,
Allah na Mtume wake wana fadhila na neema kuu juu yetu”. Halafu Mtume
akaendelea kusema: “Je, hamnijibu enyi kusanyiko la Answaari?, wakauliza:
“Tukujibu nini ewe Mtume wa Allah? Fadhila na neema ni zake Allah na Mtume
wake”. Mtume akasema: “Ama wallah, lau mngelitaka mngelisema na mngekuwa
mmesema kweli na mngesadikiwa (mngesema hivi): Ulitujilia ilhali ukiwa
mwenye kukadhibishwa, sisi tukakusadiki. Na ukiwa huna wa kukunusuru, sisi
tukakunusuru. Na ilhali ukiwa umefukuzwa, sisi tukakupa makazi na ukiwa
fakiri tukakukwasia kwa mali zetu. Hivi enyi kusanyiko la Answaari
mmeghadhibika nafsini mwenu kwa sababu tu ya kitu kidogo cha dunia nilicho
zitia nguvu kwacho nyoyo za watu ili wapate kusilimu na nyinyi nikakuachieni
Uislamu wenu? Hivi hamridhii enyi kusanyiko la Answaari, watu waondoke na
mbuzi na kondoo nanyi mkarejea na Mtume wa Allah kambini kwenu?! Naapa kwa
yule ambaye nafsi ya Muhammad i mkononi mwake, lau si Hijrah basi mimi
ningekuwa mtu miongoni mwa Answaari. Na lau watu wangelipita katika njia
moja na Answaari wakapita njia nyingine, basi mimi ningelipita njia ya
Answaari. Ewe Mola wa haki wee! Warehemu Answaari na watoto wa Answaari na
wajukuu wa Answaari”. Kwa maneno haya ya Mtume, watu wakalia kiasi cha
kuzilovya ndevu zao machozi na wakasema: “Tumeridhia Mtume wa Allah kuwa
ndiye mgao na fungu letu”.
Hili likawa ni somo la kina miongoni mwa masomo ya malezi
matukufu alilolitoa Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-kwa maswahaba
wake khususan na uma jamia. Tena limetolewa katika wakati munasibu kabisa na
unaofaa khasa kwa mtu kuweza kufaidika na kunufaika na somo. Somo hilo
likawainua na kuwaweka daraja ya juu katika daraja za utukufu wa kibinadamu.
Daraja iliyo wafanya kuwa juu ya mali, cheo na juu ya kila wanacho kigombea
watu miongoni mwa starehe na mapambo ya dunia.
ii.
Imani ndio silaha ya
kwanza ya muumini:
Kama ilivyo
kuwa ngawira katika vita vya Hunein ni somo miongoni mwa masomo ya malezi
matukufu kwa waislamu makhsusi. Ndivyo ambavyo kushindwa katika vita hivyo
kumekuwa ni katika jumla ya masomo ya malezi matukufu kwa waislamu wote.
Kwani waislamu walitoka kwenda katika vita hivi baada ya kuwa Allah
amewafungulia makomeo ya Makah. Na baada ya kuwadhalilishia wao kiburi na
jeuri ya Makureishi na baada ya kuwamilikisha suala la nyumba tukufu
(Al-Ka’abah). Na akawamakinishia tosi za Waarabu na Ghuba yote ikakurubia
kuifuata dini yao na kuwa chini ya mamlaka yao. Walitoka wakiwa katika
mlipuko wa ushindi kwa sababu ya yote haya na wakiwa katika majiono makubwa
kutokana na wingi wa idadi yao na nguvu ya zana za vita walizo kuwa nazo.
Wakauangalia wingi wao wakajiona na wakatulizana kwao na wakadhania kwamba
wingi wao huo ndio kila kitu. Basi Allah Taala akataka kuwafundisha kwamba
wakati mwingine wingi hughuri na kwamba nguvu mara nyingine hukhini. Na
kwamba nusra/ushindi u mikononi mwa Allah na kwamba njia na msingi wake,
hakika si vinginevyo ni imani ya kweli kwa Allah na wema wa kumtegemea yeye.
Na kwamba wingi, zana, maandalizi, mkakati wa vita na vinginevyo vyote
ambavyo waislamu wanatakiwa kuwa navyo kama sababu ya nguvu. Hakika vyote
hivyo vinasimama juu ya msingi huo na vinahitaji nguvu kutoka kwa msaidizi
huyu (Allah).
Katika vita hivi waislamu walifikilia wingi ambao haukuwahi
kufikiwa kabla, basi je wingi wao huo uliwasaidia kwa cho chote? Hawakuwa
wao pamoja na wingi wao huo ila washindwa, wakipaparika mbele ya adui yao
mpapariko wa mumbwi hadi kufikia kuchekwa na wachekao, akanena mneni wao:
“Ehee hivyo uchawi umebatilika leo, basi na ushindwa wao ukomelee baharini”.
Lakini kitu kimoja tu ndicho kilicho okoa hali hiyo, nacho ni hili kundi
dogo ambalo lilikamatana na imani yake na likamzunguka Mtume wa Allah-Rehema
na Amani zimshukie. Nae akaanza kukitia nguvu kwa ukweli na yakini yake na
akazielekeza nyoyo na nafsi zao kwa Allah aliye na nguvu ili zipate msaada
na nguvu kutoka kwake. Kundi dogo hili lilipo zitakasa nyoyo na nafsi zao
kwa Allah na zikawa na mafungamano mema nae, likajiwa na msaada kwa haraka
ya ajabu. Hapo ndipo udhaifu wake ukageuka kuwa nguvu na ushindwa wao ukawa
ni nusra/ushindi.
|