|
iii.
Ukweli halisi wa kudumu
unao pasa kujulikana na waislamu wa leo:
Naam, namna
hivi waislamu walizitegemea nafsi zao kwa kipindi cha mchana na Allah
akawatupa mkono. Hapo ndipo ukapatikana ushindwa pamoja na wingi wa idadi na
zana za kivita. Walipo tanabahi wakarejea kwa Bwana Mlezi wao na kumtaka
msaada, ukawajia msaada huo, kuungwa mkono na kutiwa nguvu. Hapo ndipo
ikapatikana nusra na ushindi mtukufu: “HAKIKA ALLAH AMEKUNUSURUNI KATIKA
MAPIGANO MENGI, NA SIKU YA HUNAYNI AMBAPO WINGI WENU ULIKUPANDISHENI KICHWA,
LAKINI HAUKUKUFAENI KITU. NA ARDHI IKWA DHIKI KWENU JUU YA UPANA WAKE. KISHA
MKAGEUKA MKARUDI NYUMA. KISHA ALLAH AKATEREMSHA UTULIVU WAKE JUU YA MTUME
WAKE NA JUU YA WAUMINI. NA AKATEREMSHA MAJESHI AMBAYO HAMKUYAONA, NA
AKAWAADHIBU WALE WALIO KUFURU. NA HAYO NDIO MALIPO YA MAKAFIRI”. [9:25-26]
Hivi ndivyo Allah anavyo ielezea hali ya waumini ilivyo kuwa katika vita vya
Hunein ambamo aliwapa somo la kiamalia, nao wakawaidhika nalo na kujifunza
kutokana nalo. Basi je, waislamu leo wanajua uhalisia wa hali yao? Na je,
wanakihisi kiwango cha udhaifu wao mbele ya adui yao? Na je, wanaijua siri
ya udhaifu walio nao pamoja na wingi wao kiidadi ukiwalinganisha na adui
yao? Hakika siri hii, iko wazi uwazi wa jua kwa kila aonaye, lakini waislamu
wa leo wanaifumbia macho. Na wanavizika vichwa vyao mchangani mithili ya
mbuni ili wasiione, kwani ni kweli kabisa kwamba leo waislamu wameigura dini
yao. Wamemsahau Allah wakayatupa mafundisho ya Mtume wake, naye
akawasahaulisha nafsi zao hata wakashindwa kujitambua. Wakawa mithili ya
mmea ulio kauka maji yake, kikakosekana chakula chake, ukawa bua linalo
peperushwa na upepo. Kwa yakini waislamu leo ni wengi mno duniani
ukiwalinganisha na wale wa wakati wa Mtume na baada yake kidogo. Lakini
wingi wao hauwasaidii kwa cho chote ila kuzidi udhalili na unyonge na
kukhasimiana wao kwa wao. Po pote unapo waona utakuta na kugundua kuwa
wanatawaliwa na maadui wa dini yao ama moja kwa moja au kwa mkono wa siri.
Hao ndio waendeshaji wa mambo yao yote kiasi hata cha kufikia kuingilia dini
yao, hao ndio wezi na wafaidika wa rasilimali za nchi zao. Udhalimu na
ukandamizaji wao huo huupangia mikakati ya wazi na kuipitishia maazimio na
mikataba katika makongamano na mikutano yao. Namna hivi ndivyo inavyo
thibitika kauli ya Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-kwa waislamu wa
leo: “Mataifa yanakurubia kuitana dhidi yenu kama walaji wanavyo itania
sahani (ya chakula)…” Maswahaba wakauliza: Je, huko ni kutokana na
uchache wetu zama hizo, ewe mtume wa Allah? Akajibu: “Hapana, bali nyinyi
zama hizo mtakuwa wengi, lakini mtakuwa takataka mithili ya povu la bahari”.
Hakika hali ya waislamu
leo pamoja na wingi wao, inashabihiana na hali waliyo kuwa nayo waislamu wa
mwanzo katika vita vya Hunein. Wingi wao ulipo wavimbisha kichwa, halafu
usiwasaidie kwa lo lote. Tofauti pekee iliyopo baina ya waislamu sisi wa leo
na wale wenzetu walio tutangulia katika kuiweka misingi ya dini hii. Ni
kwamba waislamu wa Hunein walitanabahi na kuzinduka, haraka wakarejea kwa
Bwana Mlezi wao nae akawaletea haraka nusra na msaada wake. Ama waislamu wa
leo, bado wanaendelea kukoroma usingizini na wanajitenga mbali na njia ya
sawa itakayo waondosha katika udhalili na unyonge ulio wagubika gubigubi.
Je, bado haujafika wakati kwa waislamu kuamka usingizini mwao na wakazinduka
kutokana na mghafala ulio wapata?! Na wakaiunga hali yao hii na ya wakale
wao watukufu na masiku yao yale ya mng’aro?! “JE, WAKATI HAUJAFIKA BADO KWA
WALIO AMINI ZIKANYENYEKEA NYOYO ZAO KWA KUMKUMBUKA ALLAH NA HAKI ILIYO
TEREMKA? WALA WASIWE KAMA WALIO PEWA KITABU KABLA YAO, MUDA WAO UKAWA MREFU,
KWA HIVYO NYOYO ZAO ZIKAWA NGUMU NA WENGI WAO WAKAWA WAPOTOVU”. [57:16]
Huenda
wakati sasa ndio umefikia, na pengine wimbi hili la mwamko lililo anza
kusambaa katika ulimwengu wa Kiislamu ni bishara ya mapambazuko mapya kwa
uma huu. Na ni miongoni mwa chomozi za nuru njema kwa uma huu ulio hemewa,
nuru itakayo utoa kutoka vizani kuuongozea kwenye njia ya sawa. Na kuuweka
juu ya khazina ya nguvu na utukufu alio utia Allah ndani ya dini yao. Hapo
uma ukapata nguvu baada ya udhaifu/unyonge, utukufu baada ya udhalili na
kunadi saada baada ya dhiki.
iv.
Mtume wa Allah
awarudishia Hawaazin mali na watu wao:
Mtume wa
Allah-Rehema na Amani zimshukie-alipo maliza kugawa mateka na mali, ukamjia
ujumbe wa waislamu wa Hawaazin, wakitarajia kurudishiwa mali na watoto wao.
Mtume akawakhiarisha kuchagua baina ya mateka na mali, nao wakakhitari
watoto na wake zao. Mtume akawaambia maswahaba wake: “Hakika watu hawa
wamekuja ilhali wakiwa ni waislamu, nami nilikuwa nimechelewesha ugawaji wa
mateka wao. Nikawapa khiari kuchagua, hawakuchagua mali juu ya wake na
watoto, basi ye yote mwenye cho chote cha mateka wao na nafsi yake ikawa
njema kukirudisha, basi njia i wazi. Na atakaye kataa, basi awarudishie tu
na huo uwe ni mkopo ametukopesha sisi, nae atapata mafungu sita kwa kila
mmoja wetu katika mali atakayo tupa Allah”. Maswahaba wakasema: “Tumeridhia
na tumesalimu amri”. Wakawarudishia wake na watoto wao na wala hakuna aliye
sita kufanya hivyo ila Uyainah Ibn Hiswn. Yeye huyu alikataa kumrejesha
kikongwe aliye angukia mikononi mwake kama mgao na fungu lake kutokana na
ushiriki wake vitani, halafu baadae akamtoa. Kisha Mtume wa Allah-Rehema na
Amani zimshukie-akauuliza ujumbe wa Hawaazin khabari za aliye kuwa kiongozi
wao; Maalik Ibn Auf. Akaelezwa kuwa bado yuko Twaif pamoja na kabila la
Thaqiyf , akawataka wamfikishie khabari kwamba iwapo atamjia ilhali yu
muislamu, atamrejeshea mali na watu wake. Na ziada ya hivyo, atampa na
ngamia mia, Maalik alipo fikiwa na ahadi hiyo ya Mtume wa Allah, akawatoroka
Thaqiyf na kumuendea Mtume wa Allah ilhali akiwa tayari ni muislamu. Mtume
akamtekelezea ahadi yake na akamsimika kuwa amiri wa watu wake walio silimu,
akawa anawaongoza kupigana na Thaqiyf na kuishambulia mifugo yao mpaka
wakasongeka.
v.
Mtume arejea Madinah:
Mtume wa
Allah-Rehema na Amani zimshukie-alipo maliza suala la ngawira, akaondoka
hapo Ji’iraanah kwenda kufanya Umrah. Na huo ulikuwa ni usiku wa Jumatano,
mwezi kumi na mbili, Dhul-Qa’adah (Mfunguo Pili). Akahirimia umrah, akaingia
Makah akatufu, akafanya Sa’ayi na akanyoa, halafu akarejea Ji’iraanah usiku
ule ule.
Mtume wa
Allah alimuachia ukhalifa wa Makah Attaab Ibn Usayd na akamuacha pamoja nae
Muaadh Ibn Jabal awafundishe watu dini pamoja na kuwasomesha Qur-ani. Attaab
huyu alikuwa kijana mbichi wa umri upatao miaka ishirini hivi, lakini
alikuwa mcha-Mungu mno, sifa iliyo mstahikisha kuwa amiri wa Makah pamoja na
umri wake huo mdogo. Mtume wa Allah akamuandikia kupata dirham moja kila
siku, Attaab akawa anasema: “Allah asilishibishe ini la mwenye kusikia njaa
pamoja na kupata dirham moja! Kwa yakini Mtume wa Allah ameniruzuku dirham
moja kila siku, kwa hivyo mimi sina haja kwa ye yote”.
Halafu
Mtume wa Allah-Rehema na amani zimshukie-akaondoka kurejea Madinah,
akawasili huko mwishoni mwa Dhul-Qa’adah au mwanzoni mwa Dhul-Hijjah
(Mfunguo Tatu), mnamo mwaka wa nane Hijriah. Hivi ndivyo mwaka wa nane
ulivyo tamatia kwa fat-hi (ushindi) Makah na kuondosha kikwazo kikuu kilicho
kuwa kimeziba njia ya da’awah. Kwa kuondoka kwake, chemchem ya Uislamu
ikachimbuka katika ardhi ya Ghuba na kuzifunika janibu zake zote. Ukaingia
mwaka wa tisa, zikaja jumbe za Waarabu kutokea pande zote za Ghuba, zikaja
Madinah kwa khiari zao. Ili kuutangaza Uislamu na utiifu wao kwa Mtume na
wakaingia katika dini ya Allah kwa radhi ya nafsi zao bila kutenzwa nguvu.
|