|
SOMO LA KWANZA.
i.
Majukumu ya uma wa
Kiislamu:
Fat-hi (ushindi) Makah ilikuwa ni tangazo la
kuingia kwa Peninsula ya Kiarabu katika wigo wa Uislamu na Waarabu wote kuwa
chini ya bendera yake. Baada ya Fat-hi Makah na kusilimu kwa Makureishi,
Waarabu wakatambua kwamba hawana njia ya kuhepa kuingia katika Uislamu sasa
au baadae. Hii ni kwamba Waarabu – kama anavyo sema Ibn Ishaq-Allah
amrehemu-: “Hakika si vinginevyo, walikuwa wakiungojelea Uislamu suala la
kitongoji hiki cha Makureishi ambao walikuwa ndio viongozi na watawala wa
watu. Wenyeji wa nyumba tukufu, kizazi cha Nabii Ismail Ibn Ibrahim-Amani
iwashukie. Walikuwa (hao Waarabu) hawaupingi Uislamu, ni Makureishi ndio
walio anzisha kumpinga na kumpiga vita Mtume wa Allah-Rehema na Amani
zimshukie. Makah ilipo funguliwa na Uislamu ukawatenza nguvu Makureishi,
Waarabu wakatambua kwamba hawana ubavu wa kupambana na Mtume wa Allah. Kwa
ajili hii, wakaingia katika dini ya Allah makundi kwa makundi kama alivyo
sema Allah Taala, wakitokea kila upande. Wakawa miongoni mwa muislamu aliye
ingia Uislamuni akawa muislamu, na mushrikina anaye jiandaa kuingia ndani ya
Uislamu ama leo au kesho. Haukupita ila mwaka mmoja tu, Peninsula ya Waarabu
ikawa ni kambi ya Uislamu na wenyeji wake wakawa ndio walinzi wake.
Kuanzia hapo, uma wa kiislamu ukaanza kujiunda ndani ya
Peninsula muundo wa dola na kuonekana ulimwenguni kama dola yenye nguvu za
kuilinda na kudhamini amani/usalama wake. Madhumuni ya uma huu hayakuwa kama
nyumati nyingine, bali muradi ni kuwa bora ya nyumati zote dhima yake ikiwa
ni kuondosha fisadi, kusawazisha kombo kombo, kuamrisha mema na kukataza
maovu. Ukisukumwa kuyaelekea haya na imani yake kwa Allah aliye pekee na
raghba yake ya kutaka maisha katika ardhi yawe juu ya msingi ambao Allah
amewawekea waja wake. Dola ya Kiislamu ilisimama juu ya msingi huu katika
Peninsula hii ya Waarabu. Na kwa lengo hili, ikaiwekea kanuni ambazo
zinadhamini usalama/amani ya jamii yake dhidi ya maafa yote. Kuilinda ardhi
yake dhidi ya kila adui na kuwaandaa watu wake kubeba majukumu ya uma
bora/teule. Na kustahamilia matokeo/natija zitakazo jitokeza kutokana na
mapambano dhidi ya dhulma na kusimamisha uadilifu. Na taklifu zinazo
ambatana na uondoshaji wa shari/uovu na kueneza kheri/wema na hii ni dhima
(kazi) nzito. Lakini ndio dhima ambayo Allah ameutwika uma wa Kiislamu na
akaufanya kuwa uma bora kwa ajili tu ya kuitekeleza kwao dhima hiyo.
Tunasoma: “NYINYI MMEKUWA BORA YA UMA WALIO TOLEWA WATU, KWA KUWA MNAAMRISHA
MEMA NA MNAKATAZA MAOVU, NA MNAMUAMINI ALLAH...” [3:110]
ii.
Kuundwa kwa dola ya
Kiislamu kulikuwa ni tishio kwa maslahi ya Urumi katika Rasi ya Kiarabu:
Wakati ambapo Mtume wa Allah-Rehema na Amani
zimshukie-alikuwa akiuandaa uma wake kwa ajili ya dhima (kazi) hii tukufu.
Na kulitwaharisha anga la uma huu kutokana na athari ya ufisadi na shirki na
kufuta katika ardhi yake nembo/alama za shirki na ibada za miungu sanamu. Na
akipeleka vikosi kwenye makabila ya Kiarabu yanayo mzunguka, kwenda
kuyavunjilia mbali masanamu na kuueneza Uislamu mahala pake. Warumi
kaskazini mwa Rasi hii, walikuwa wakiyaangalia matukio yote haya kwa jicho
la khofu. Mtazamo wao huo ulitokana na vitega uchumi mbali mbali vyao
walivyo kuwa wakivimiliki katika Rasi hii. Na hapana shaka kwamba maslahi
yao hayo yalikuwa yanaathiriwa na matukio haya yanayo jiri katika Rasi hii.
Warumi walikuwa na misafara ya biashara iliyo kuwa ikipita kusini na
kaskazini, mashariki na magharibi mwa Rasi hii ya Waarabu. Na walikuwa na
washirika miongoni mwa Waarabu walio kuwa wakiishi kaskazini mwa rasi hii,
hawa walikuwa wakipokea amri na kuunyenyekea utawala wa Kirumi. Na hali
kadhalika walikuwa na washirika katikati ya kisiwa hiki, Warumi
waliwategemea washirika wao hawa katika kuihami misafara yao ya biashara. Na
unaswara ambao ndio ulikuwa dini rasmi ya dola ya Kirumi, ulikuwa ndio dini
ya kabila la Ghassaani; washirika wa Warumi. Dini hii pia ilifuatwa na
Waarabu waungwana walio kuwa wakiishi kaskazini na kusini mwa Rasi hii.
Maslahi yote haya, Warumi waliwania kuyabakisha na miongoni
mwa vitendakazi ambavyo vilisaidia kusalikia kwa maslahi haya kwa Warumi. Ni
kwamba Waarabu kwa mazingira ya maisha yao, walikuwa ni makabila mtapanyiko
ambayo hayakuwa na umoja wala sauti moja. Na kila kabila lilikuwa
likishughulikia mambo yake lenyewe au mambo ya washirika wao tu basi.
Kutokana na mazingira haya, Waarabu waliishi katika mfarakano daima na ili
maslahi ya dola la Kirumi yaendelee kudumu hapana budi mfarakano huu baina
ya Waarabu uendelee. Uislamu ulipo dhihiri katika Rasi hii ya Waarabu na
ukaanza kuwaunganisha Waarabu na kuzikusanya safu zao chini ya bendera yake.
Na sauti yake ikaanza kupaaza na kupaaza mpaka ikagonga masikio ya wafalme
wa jirani yake na mzingo wake ukatanuka na kutanuka mpaka ukakurubia
kuzichanganya pande za Rasi hii ya Waarabu. Hapo Warumi wakaanza kuitanabahi
khatari itokanayo na tukio jipya hili linalo jiri katika mkondo wa historia.
Na huenda cha mwanzo kilicho wazindua ni ule mlingano (da’awah) – jasiri
ulio elekezwa na Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-kwa mfalme
Qayswari wa Urumi. Akimlingania kumuamini Allah pekee na kumfuata katika
anacho kilingania na awalinganie wafuasi wake miongoni mwa Warumi na wasio
Warumi kuingia katika Uislamu. Na akimbebesha jukumu la kuzembea kuutangaza
na kuufikisha mlingano huu kwa wafuasi na washirika wake.
Tarekh (historia) inatuonyesha kwamba Qayswari hakuipuuzia
khatari ya mlingano huu, bali yeye ndiye wa mwanzo aliye itangaza khatari
hiyo kwa masultani na wafalme wenzake. Hiraqli alipo fikiwa na ujumbe wa
Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akaanza kuulizia juu ya Muarabu
anaye tokana na kaumu ya Mtume huyu ili apate kumuuliza khabari zake.
Akauliza mpaka akakwaana na Abu Sufyaan Ibn Harb, akaanza kumuuliza maswali
ya mtu mjuzi mpelelezi kuhusiana na kila alilo taka kujua juu ya mtume huyu
mpya. Hata alipo tosheka na kujua hakika yake, akamwambia Abu Sufyaan:
“Ikiwa uyasemayo ni kweli, basi atamiliki mahala hapa ilipo kanyaga miguu
yangu hii”.
|