|
i) UPINZANI WA MAKURAYSHI DHIDI YA MTUME
Uislamu ukazidi kusambaa katika mji wa makkah na khabari zake kuenea pande zote za
mji huo, na watu wakaingia katika uislamu makundi kwa makundi. Hapa ndipo Mtume-Rehema na
Amani zimshukie akaitumia fursa hii kwanza kuikosoa miungu sanamu ya Makurayshi kwa
nini mnayaobudia masanamu yasiyodhuru wala kukunufaisheni? Miungu wasiyoweza kujisaidia
wao wenyewe, vipi watakusaideni nyinyi? Miungu wasioweza kujilinda wao wenyewe vipi
watakulindeni nyinyi? Kwa ujumla Bwana Mtume Rehema na Amani zimshukie akawa
anawaonyesha Makurayshi ubaya na upotofu wa itikadi yao na dini wanayoifuata. Hapa ndipo
makurayshi walipozinduka na kuiona khatari inayowakabili kutokana na dini hii mpya
aliyokuja nayo Bwana Mtume. Ili kukabiliana na mawimbi makubwa ya dini hii, Makurayshi
wakaanza kumfanyia Mtume namna mbalimbali za kero na maudhi kiasi walichoweza. Isitoshe
wakawa wanamcheza shere khasa khasa anapotoka kwenda kuswali- Wakamzulia kwamba Mtume ni
mwendawazimu asiye na akili na wakati mwingine wakisema ni mchawi na mara nyingine
wakimwambia kuwa ni kuhani na muimba mashairi. Mwenyezi Mungu Mtukufu akiyakanusha madai
yao hayo na kusisitiza kwamba Mtume wake Muhammad hana hata sifa moja miongoni mwa sifa
hizo walizomzulia. Mwenyezi Mungu aliapia hilo na kusema
"BASI NAAPA KWA MNAVYOVIONA NA MSIVYOVIONA KWA HAKIKA HII NI KAULI ILIYOLETWA NA
MJUMBE (WA ALLAH) MWENYE HISHIMA (Kubwa). WALA SI KAULI YA MTUNGA MASHAIRI (Kama
mnavyosema). NI MACHACHE SANA MNYOYAAMINI. WALA SI KAULI YA MCHAWI (kama mnavyodai). NI
KIDOGO KABISA KUWAIDHIKA KWENU. NI UTEREMSHO UTOKAO KWA MOLA WA VIUMBE VYOTE"
[69:38-43].
Pamoja na ukweli huu juu ya Nabii Muhammad bado Makurayshi hawakumuamini bali ulikuwa kama
ndio kichocheo cha upinzani. Makurayshi wakaanza kuwatahadharisha na kuwazuia watu
wasikutane na mtume na wala wasimsikilize kabisa. Hatua zote hizi hazikusaidia kitu wala
kuwaletea Makurayshi nafuu yeyote. Kwa hivyo wakaamua kukutana katika mkutano wa dharura
ili kujadili juu ya hii dini mpya ya Nabii Muhammad. Dini ambayo imekuwa ni hatari kubwa
inayokaribia kuimeza na kuiua kabisa dini yao ya ushirikina. Wakabadilishana mawazo na rai
jinsi ya kufagilia mbali dini hii mpya inayowataka waache ibada ya miungu wengi kuja
kwenye ibada ya Mungu Mmoja wa Pekee asiye na mshirika.
Vijana wa Kikurayshi ambao mara nyingi ni watu wenye hamasa, jazba na mori. Hawa waliona
njia bora ya kuimalizia mbali dini hii ni kuukata kabisa mzizi wa fitna. Na hili
halipatikani ila ni kwa kuuwawa Nabii Muhammad haraka iwezekanavyo kabla sumu yake
haijatapakaa na kuathiri zaidi. Ama wazee, ambao hawa mara nyingi uzoefu umeonyesha ni
watu wanaotawaliwa na hekima na busara. Hawa waliona ni vema wakaketi chini pamoja na
Nabii Muhammad ili kulitafutia ufumbuzi tatizo hili la mgogoro wa dini kwa njia ya salama
na amani. Rai hii ya wazee ikapita na kukubaliwa. Japo teule la wazee likaenda kukutana na
Mtume na kijaribu kumshawishi aachane na hii dini mpya aliyokuja nayo ambayo inaigawa
jamii ya Kikurayshi. Aache kuikosoa miungu yao na arudi katika dini ya wahenga. Bwana
Mtume- Rehema na Amani zimshukie- hakuwafikiana nao na akawaambia kama alivyofundishwa na
mola wake :-
"SEMA ENYI MAKAFIRI! SIABUDU MNACHOABUDU WALA NYINYI HAMUMUABUDU NINAYEMUABUDU. WALA
SITAABUDU MNACHOABUDU. WALA NYINYI HAMTAMUABUDU NINAYEMUABUDU. NYINYI MNA DINI YENU NA
MIMI NINA DINI YANGU" [109:1-6]
Makurayshi walipoona kwamba jitihada zao hizi hazizai matunda na Bwana Mtume anazidi kuwa
mkaidi, hataki kuwasikiliza, wakamkemea vikali aache mara moja kuitukana miungu na aache
kuwatenganisha, la haachi basi hatua kali zitachukuliwa dhidi yake. Likateuliwa jopo
kwenda kuonana na Ami yake Mtume Mzee Abu Twalib ambaye alionekana kuwa ndio
ngome na himaya ya Mtume. Wajumbe wa jopo hili walikuwa pamoja na Utbah bin Rabiah,
Shaybah bin Rabiah, Abu Sufyan bin Harb, Al-aaswi bin Hisham, Al-waliid bin Mughiyrah na
wengineo. Wakamwambia Mzee Abu Twalib : Ewe Abu Twalib, hakika mwana wa nduguyo
amewatukana miungu wetu na kuikosoa dini yetu na kusema kuwa wahenga wetu walikuwa katika
upotofu. Sasa, tunakutaka umzuie aachane na sisi tupambane nae wenyewe" Abu Twalib
akawajibu kwa maneno mazuri, wakaenda zao. Mtume akaendelea na kazi yake, akiidhihirisha
na kuitangaza dini ya haki. Makurayshi kuona hivyo wakamuendea tena Mzee Abu Twalib na
kumwambia : Ewe Abu Twalib, wewe kwetu ni mtu mwenye heshima, cheo na utukufu. Sisi
tulikuomba umzuie mwana wa nduguyo nawe hukutaka kumzuia. Nasi Wallahi sasa
hatuna tena subira juu ya suala hili. Hatutokubali kutukaniwa wahenga wetu na miungu wetu.
Sasa, ima umzuie au nyinyi na sisi tupambane mpaka apatikane mshindi. Kisha wakashika njia
na kwenda zao. Mzee Abu Twalib akaachwa njia panda akiwa hajui afanye nini. Kutengana na
jamii yake, hili lilikuwa jambo zito sana kwake na kumuacha mwana wa nduguye aadhibiwe na
Makurayshi, hili pia lilikuwa jambo zito kabisa. Afanyeje sasa katika kipindi hiki kigumu
ambamo Makurayshi hawana tena mzaha na wako tayari kufanya lolote kuilinda hadhi na
heshima ya dini yao. Akamuita mwanawe na kumwambia : Ewe mwana wa ndugu yangu, jamaa zako
wamenijia na kuniambia jambo kadha wa kadha. Basi nakuomba unionee huruma mimi na ujionee
huruma wewe kutokana na hasira za jamaa zako, na wala usinitwishe mzigo nisioweza kuubeba.
Mtume akadhania Ami yake sasa anamtupa mkono na kuwaachia nafasi wapambane naye, kutokana
na kauli yake hiyo. Bwana Mtume Rehema na Amani zimshukie akamjibu Ami yake
na kumwambia : "Wallah! Lau wataliweka jua katika mkono wangu wa kulia na mwezi
katika mkono wangu wa kushoto ili kunishinikiza niache jambo hili, nisingeliacha katu
mpaka Mwenyezi Mungu aipe ushindi dini yake au mimi niangamie!". Kisha Mtume akampa
mgongo Ami yake kutaka kuondoka huku analia. Ami yake akamuita : Njoo ewe mwana wa ndugu
yangu !. Mtume akaja, akamwambia : Nenda ewe mwana wa ndugu yangu, na sema utakalo. Wallah
sitokusalimisha kwa jambo baya, kamwe.
Makurayshi walipoona kwamba Mzee Abu Twalib hataki kumkataza mwanawe wakamuendea na
Ammaarah bin Waliid bin Mughira, wakamwambia : Ewe Abu Twalib, huyu hapa Ammaarah bin
Waliid kijana mzuri kuliko wote wa Makurayshi, mtwae awe mwanao na umsalimishe kwetu huyu
mwana wa nduguyo ambaye ameikhalifu dini yako na dini ya baba zako na amewafarikisha jamaa
zako, tuachie tumuue. Mzee Abu Twalib akawajibu : Wallah ni kibaya mno kitendo
mnachonitaka nikifanye! Mnanipa mwanenu nikuleleeni kisha nikupeni mwanangu mumuue ? Hili
Wallah kamwe halitakuwa !. Msimamo huu wa Ami yake Mtume haukuwafurahisha Makurayshi hata
kidogo bali ulizidi kuamsha na kuchochea hasira na ghadhabu za Makurayshi dhidi ya Mtume.
Mzee Abu Twalib akaona kadhia hii imekuwa kubwa, hawezi kuikabili peke yake. Akaamua
kuwakusanya jamaa zake Banii Hashim na kuwaeleza yote yaliyojiri baina yake na Makurayshi
tangu mwanzo mpaka mwisho. Wakaanza kushauriana cha kufanya, hatimaye wakaafikiana kwa
kauli moja kulinda hadhi na heshima yao. Wasimame imara safu moja kumlinda na kumtetea
Mtume hata kama hayuko pamoja nao kiitikadi pamoja na kwamba hili litawagharimu sana
|