Makala
Uislamu-Utangulizi
Fiqhi na Sheria 
Akhlaaq-Tabia
Sira ya Mtume
Nasaha za dini
Maswali na Majibu
Uliza Suala la dini
Jiunge na Mtandao !!!

 

SIRA YA MTUME (SAW)  

"BILA SHAKA MNAO MFANO MWEMA KWA MTUME WA MWENYEZI MUNGU…"Al-qur-an (33:21)

WARUMI WAFANYA MAANDALIZI 

 Faida

 

           i.            Warumi wafanya maandalizi kabambe kuifyekelea mbali dola ya Kiislamu:

         Kutokana na maelezo yaliyo tangulia, itakubainikia kwamba Urumi haikuipuuzia hata kidogo da’awah ya Kiislamu. Allah alipo mfungulia Mtume wake Makah na da’awah ya Kiislamu ikaanza kutapanyika na kuenea pande zote za Peninsula ya Kiarabu. Warumi wakawa na yakini kwamba khatari inakaribia kuwagubika na kwa hivyo basi hapana budi zichukuliwe hatua za haraka ili kuiepusha khatari hiyo. Na ni vema ikakumbukwa kwamba dola ya Urumi wakati huo ilikuwa na nguvu kubwa na sauti katika ulimwengu ule kama ilivyo Marekani katika ulimwengu wetu huu wa leo. Na ni miaka michache tu ilikuwa imepita tangu itoke vitani na dola nyingine kubwa; Uajemi na kufanikiwa kuishinda. Urumi ilikuwa na nguvu kubwa ya kijeshi kuliko dola yo yote ya enzi hizo, nguvu iliyo ipa kiburi cha kuamini kuwa ina uwezo wa kuuponda ponda uma wa Kiislamu kama itakavyo. Kwa imani hiyo, Warumi wakaanza maandalizi kwa ajili ya kuufyeka uma huu mchanga unao anza kujiunda. Na pengine walikusudia kuushambulia ndani ya mipaka yake ili waukate kabisa mzizi wake na kuifutilia mbali dini yake. Wakakusanya majeshi wayatakayo na wakaandaa zana za vita wazitakazo na wakaanza maandalizi ya kuyakata masafa marefu ili kuwapiga waislamu kwao.

Khabari zikamfikia Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-kwamba Warumi wamekusanya chungu ya majeshi huko Shamu. Na kwamba mfalme Hiraqli amewapa watu wake chakula cha mwaka mzima. Na amekusanya washirika kutoka katika makabila ya Kiarabu ya Lakhum, Judhaam na Ghassaan na wametanguliza vikosi vyao vya mwanzo mahala paitwapo “Al-Balqaa”. Kwa khabari hizi, ikamlazimu Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-kufikiria namna ya kukabiliana na uadui huu. Na mbele yake zilikuwepo njia/hatua mbili za kukabiliana na uchokozi huu; ya kwanza ni kuwaacha Warumi wakitangatanga katika uwanda wa nchi yake, kisha akabiliane nao pale panapo mfalia. Na ya pili yeye aende kuwashambulia huko huko katika mipaka yao. Na njia ile ya kwanza ikawa ndio nyepesi zaidi, lakini inaweza kumpelekea yeye kuzikosa baadhi ya kabila ambazo ameingia nazo ushirika hivi karibuni. Kwa ajili hii basi, akachagua ile njia/hatua ya pili.

 

         ii.            Mtume wa Allah awaita maswahaba wake kupambana na Warumi na watu wanyoofu wa nia washindana katika kutoa gharama za vita:

         Na kikawaida, mzigo/jukumu la kuilinda Peninsula ya Kiarabu (wakati huo ilikwisha kuwa ngome ya dola ya Kiislamu) libebwe na wazalendo wa Peninsula hii, miongoni mwa walio silimu. Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akawatolea watu wito wa kutoka na akawatuma wajumbe kufikisha wito wake huo Makah na kwa makabila ya Kiarabu. Na akawafahamisha mapema anako kukusudia ili wapate kufanya maandalizi yanayo lingana na safari hiyo ndefu. Mtume wa Allah akawakhutubia watu, akawahimiza jihadi na akawaamrisha kutoa sadaka na akawaraghibisha matajiri kufanya kheri na wema. Na akawahimiza wenye uwezo kuwaandaa wasio na uwezo, hapo waislamu wakaangupiza kutoa katika mali zao, wakishindana katika kulitayarisha jeshi lao hilo.

Sayyidna Uthmaan Ibn Affaan-Allah amuwiye radhi-akatoa dinari alfu kumi, ngamia alfu tatu na farasi khamsini. Sayyidna Abu Bakri akaleta dirham alfu nne, zikiwa ndio mali yake yote na Sayyidna Umar Ibn Al-Khatwaab akaleta nusu ya mali yake. Sayyidna Abdur-Rahmaan Ibn Auf akaleta wakia mia mbili za fedha na Sayyidna Abbaas Ibn Abdul-Mutwalib akabeba mali inayo kisiwa kufikia dirham alfu tisini. Na Twalhah Ibn Ubeidillah, Sa’ad Ibn Ubaadah na Muhammad Ibn Maslamah, wakabeba mali nyingi na Aaswim Ibn Adiy akatoa sadaka makorobasi (aina ya makapu makubwa) tisini ya tende. Na wanawake wakachangia kila walicho kiweza katika mapambo yao, wakawa wakitupia katika nguo iliyo tandikwa mbele ya Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie. Mapambo yao waliyo vaa mikononi mwao, miongoni mwa bangili, pete na kadhalika. Na mapambo waliyo vaa miguuni mwao na yale ya masikioni mwao na shingoni mwao. Waislamu wakashindana kutoa, mpaka ikafikia mtu kumletea mtu mmoja au wawili ngamia, akiwaambia: “Ngamia huyu mtampanda kwa kupokezana”. Na mwingine akileta masurufu na kumpa baadhi yake mtu anaye toka kwenda katika jihadi.

Kama hivi ndivyo watakasifu wa nia walivyo kuwa wakifanya ukarimu kwa kutoa mali zao na wakishindana katika kuliandaa jeshi, kila mmoja kulingana na uwezo wake. Aliye weza kujigharamia yeye mwenyewe na mtu mwingine, alifanya hivyo kwa kadri alivyo weza. Na asiye weza alijigharamia yeye mwenyewe na ikatosha. Kundi la waislamu mafakiri likashindwa kujiandaa lenyewe, wakamuendea Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-wakimuomba awape vipando vya ziada alivyo navyo. Akawaondosha kwa kuwaambia: “...SINA KIPANDO CHA KUKUCHUKUENI (kwenda jihadini)...” [9:32] Wakaondoka na ilhali macho yao yakifurika machozi kwa huzuni ya heshima ya jihadi waliyo ikosa. Kwa sababu tu ya ufakiri wao na kushindwa kwao kujiandaa wao wenyewe kwa gharama zao.

 



 | Tuandikie |