Makala
Uislamu-Utangulizi
Fiqhi na Sheria 
Akhlaaq-Tabia
Sira ya Mtume
Nasaha za dini
Maswali na Majibu
Uliza Suala la dini
Jiunge na Mtandao !!!

 

SIRA YA MTUME (SAW)  

"BILA SHAKA MNAO MFANO MWEMA KWA MTUME WA MWENYEZI MUNGU…"Al-qur-an (33:21)

SOMO LA TATU 

 Faida

             I.      Safari hii iliyo sheheni kila aina ya taabu ilikuwa ni mtihani ulio wapambanua waumini na wanafiki:

         Kwa yakini kabisa, taabu hii iliyo wafika waislamu katika safari yao hii ya kwenda Tabuuk, ilikuwa ni mtihani/jaribio kwao kutoka kwa Allah Mola Muumba wao. Alitaka kupitia mithani huo kuwapambanua waumini, kuwatakasa na kuwaandaa kustahamilia taabu ya kuipigania dini yake. Na ili apate kuona kiwango cha subira ya wasubiriao na ukweli wa wakweli katika njia ya kuihami dini yao. Ikawa hawawezi kuistahamilia tabu hii ila wale walio na imani ya kweli na itikadi iliyo kita mizizi. Ama wanafiki na wale walio jionyesha kuwa na imani, hawa walisukwasukwa na kudhoofu azma zao, wakawa wakipenya nyuma ya safu wakirejea walikotoka.

Ibn Is-haaq-Allah amrehemu-anasema: “Kisha Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akaendelea kwenda, ikawa mtu mmoja mmoja anabakia nyuma asende nae. Maswahaba wakimwambia: Ewe Mtume wa Allah wee! Fulani amebakia nyuma, nae huwajibu: “Muacheni, ikiwa kuna kheri kwake, Allah atakukutanisheni nae na akitokuwa hivyo, basi Allah amekupumzisheni nae”. Abu Dhari akabakia nyuma na ngamia wake, alipo ona anamchelewesha akachukua mzigo wake akaubeba mgongoni kwake, kisha akatoka akizifuatia nyayo za Mtume wa Allah kwa miguu. Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akashuka katika baadhi ya mashukio yake, mmoja katika waislamu akaona kitu kwa mbali, akasema: Ewe Mtume wa Allah wee! Hakika huyo (ajaye) ni mtu anatembea njiani peke yake. Mtume wa Allah akasema: “Kuwa (ewe ujaye ni) Abu Dhari!” Watu walipo mtia machoni, wakasema: Ewe Mtume wa Allah wee! Wallah, ni Abu Dhari kweli! Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akasema: “Allah amrehemu Abu Dhari! Anatembea peke yake kwa miguu, atakufa peke yake na atafufuliwa peke yake”.

 

          II.      Abu Khaythamah:

         Kuna kundi la waislamu lililo kawizwa na kutokuwepo mjini mpaka likabakia nyuma lisitoke pamoja na Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-bila ya kuwa na shaka. Miongoni mwao alikuwemo Ka’ab Ibn Maalik, Muraarah Ibn Rabeea, Hilaal Ibn Umayyah na Abu Khaythamah. Hawa walikuwa ni watu wakweli, usio tiliwa shaka Uislamu wao. Ama hawa watatu tulio wataja mwanzo, hawa walikawizwa na azma zao na wakatambaliwa na unyongevu na kikawaghuri wao kivuli (cha miti yao) na maji hata wakakaa wasende vitani. Nao walikuwa na jambo pamoja na Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-Allah akateremsha Qur-ani katika jambo hilo. Ama Abu Khaythamah, yeye alijidiriki kabla muda haujapita, akaungana na Mtume wa Allah.

Ibn Is-haaq-Allah amrehemu-anasema: “Halafu tena Abu Khaythamah akarejea mjini – (baada ya Mtume kuondoka kwa siku kadhaa) – kwa ahali zake katika siku ya joto kali. Akawakuta wake zake wawili katika vibanda vyao ndani ya bustani yake ya mitende. Na kila mmoja akiwa amekinyunyizia maji kibanda chake na kumuwekea maji baridi na kumuandalia chakula. Alipo fika akasimama mlangoni mwa kibanda, akawaangalia wake zake na vile walivyo muandalia, akasema: Mtume wa Allah yuko katika unguzo la jua, upepo na joto na Abu Khaythamah akiwa katika kivuli baridi, chakula kilicho andaliwa, mwanamke mzuri, akikaa kwenye mali yake?! Hii sio insafu wala uadilifu! Halafu akasema: Wallah, sitaingia kibandani kwa mmoja wenu mpaka niungane na Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie! Haya niandalieni pamba (chakula cha njiani). Wakamuandalia, kisha akamleta ngamia wake akapakia mizigo yake tayari kwa safari. Kisha huyoo akatoka kumfuatia Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-hata akamdiriki pale alipo piga kambi Tabuuk.

 

       III.      Mtume wa Allah hakumkuta hata Mrumi mmoja Tabuuk na aamua kutokusonga mbele:

         Wakati Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alipo fika Tabuuk na akawa kwenye mipaka ya dola ya Kirumi, hakumkuta ye yote katika maadui. Na yawezekana kwamba Warumi walipendelea kuwa ndani ya nchi ya Urumi ili wapate kujihifadhi na ngome zake pale ilipo wafikia khabari ya jeshi hili la waislamu na nguvu zake, kama anavyo sema Daktari Haikal. Na pia inawezekana waislamu waliacha kusonga mbele pale walipo tambua kinyume na walivyo kuwa wakifikiria, kwamba Hiraqli hajaandaa jeshi kushambulia Madinah. Mwandishi wa kitabu “Al-imtaau”, anapita mapito haya, anaona kwamba alivyo khabarishwa Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie. Kwamba Hiraqli na watu wake wako karibu na Shamu wanakuja kushambulia Madinah, zilikuwa ni khabari batili na wala Hiraqli hakulikusudia hilo.

Vyo vyote ulivyo kuwa uhakika wa suala hili, ni kwamba Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alisimama hapo Tabuuk na wala hakuvuka kwenda mbele. Akavituma vikosi vyake kwa washirika wa Urumi miongoni mwa manaswara wa Kiarabu waishio katika mzonge wa Tabuuk. Watu wa Aylah, Adhruhu, Jarbaa, Maqnaa na Duumatul-Jandal wakafanya nae suluhu juu ya kutoa kodi na waingie katika dhima na amani ya Uislamu. Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akakaa hapo Tabuuk kiasi cha siku kumi hivi. Halafu akawataka maswahaba wake ushauri juu ya kuvuka mpaka na kuingia ndani ya miji ya Shamu. Sayyidna Umar-Allah amuwiye radhi-akamwambia: “Ewe Mtume wa Allah! Ikiwa umeamrishwa kwenda basi nenda”. Mtume akasema: “Lau ningelikuwa nimeamrishwa, basi nisingelitaka ushauri”. Umar akasema: “Ewe Mtume wa Allah! Hakika Warumi wana majeshi shirika mengi na huko Shamu hakuna muislamu hata mmoja. Nawe umewakurubia na ujio wako tayari umesha wafadhaisha, basi lau mwaka huu ungelirejea uone au Allah alete amri yake”.

Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akaufuata ushauri wa Umar na akaamuru kurejea. Basi jeshi likarejea Madinah baada ya Mtume kuiweka katika hali ya amani mipaka ya kaskazini ya dola ya Kiislamu. Kutokana na mikataba aliyo andikiana na Manaswara wa Kiarabu walio jiranikiana na dola ya Urumi. Na kurejea kwake Mtume, Madinah kulikuwa ndani ya mwezi wa Ramadhani [Desemba – 630 A.D.]. Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alipo karibia kuingia Madinah, watu walitoka kumlaki. Pamoja nao walitoka watoto, wanawake na vijakazi. Na wanawake wa tabaka la juu wakapanda juu ya majumba yao wakiimba na kughani kwa ajili ya kufurahikia kurudi kwa Mtume wa Allah.

 



 | Tuandikie |