Makala
Uislamu-Utangulizi
Fiqhi na Sheria 
Akhlaaq-Tabia
Sira ya Mtume
Nasaha za dini
Maswali na Majibu
Uliza Suala la dini
Jiunge na Mtandao !!!

 

SIRA YA MTUME (SAW)  

"BILA SHAKA MNAO MFANO MWEMA KWA MTUME WA MWENYEZI MUNGU…"Al-qur-an (33:21)

AYA ZILIZOSHUKA KATIKA VITA HIVI

 Faida

 

        IV.      Aya zilizo shuka katika vita hivi ndizo zilizo kuwa ndefu kuliko zote kuwahi kushuka katika vita vingine vyote:

         Wakati wa kurejea kwake Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-Madinah, zilimshukia aya katika Surat Tawbah [9] zikizungumzia suala la wale walio bakia nyuma wasende vitani; miongoni mwa wanafiki na wale walio zembea bila ya kuwa na udhuru wo wote. “Na aya hizi ambazo Allah alimshushia Mtume wake kuhusiana na suala zima la vita hivi, ndizo aya ndefu kuliko zote kuwahi kushushwa katika kuelezea mapambano baina ya waislamu na mahasimu wao. Kuanzia aya ya 38 ya Surat Tawbah mpaka mwisho wa sura; aya ya 129, utaona ni jumla ya aya 91 zinavizungumzia vita hivi. Aya zimeanza na kuamsha hima ya waislamu ili kujibu hujuma za Kimasihia dhidi ya Uislamu na kuwafahamisha matokeo mabaya ya kuzembea kwao katika kuitekeleza fardhi hii. Na kuwapa hisia kwamba Allah hakubali hata upunje wa kupindukia mipaka katika kuihami na kuinusuru dini yake. Na kwamba kurejea nyuma mbele ya magumu yanayo zuia kupigana na Warumi, kunahesabiwa kuwa ni mtelezo kuelekea uritadi na unafiki: “ENYI MLIO AMINI! MNA NINI MNAPO AMBIWA: NENDENI KATIKA NJIA YA ALLAH, MNAJITIA UZITO KATIKA ARDHI? JE, MMERIDHIA MAISHA YA DUNIA KULIKO YA AKHERA? LAKINI STAREHE ZA MAISHA YA DUNIA KULINGANISHA NA YA AKHERA NI CHACHE. KAMA HAMWENDI ATAKUADHIBUNI ADHABU CHUNGU, NA ATAWALETA WATU WENGINE, WALA NYINYI HAMTAMDHURU CHO CHOTE. NA ALLAH NI MUWEZA WA KILA KITU”. [9:38-39]” – Nukuu kutoka kitabu {FIQ-HUS-SEERAH}

Aya zikaendelea kueleza kwa uwazi na ukali, zikawafedhehesha wanafiki, zikawafichua wenye kuzinga zinga na zikawatweza watafuta ubwete na raha. Ambao walipendelea zaidi kukaa vivulini majumbani mwao na mashambani mwao kuliko joto la jangwani na uchovu wa safari: “WALIFURAHI WALIO ACHWA NYUMA KWA KULE KUBAKIA KWAO NYUMA NA KUMUACHA MTUME WA ALLAH. NA WALICHUKIA KUPIGANA JIHADI KWA MALI ZAO NA NAFSI ZAO, NA WAKASEMA: MSITOKE NJE KATIKA JOTO! SEMA: MOTO WA JAHANNAMU UNA JOTO ZAIDI, LAITI WANGELIFAHAMU! BASI NA WACHEKE KIDOGO; WATALIA SANA. HAYO NI MALIPO YA YALE WALIYO KUWA WAKIYACHUMA. BASI ALLAH AKIKURUDISHA KWENYE KIKUNDI KIMOJA MIONGONI MWAO – NA WAKAKUTAKA IDHINI YA KUTOKA – SEMA: NYINYI HAMTATOKA PAMOJA NAMI KABISA, WALA HAMTAPIGANA NA ADUI PAMOJA NAMI. NYINYI MLIRIDHIA KUKAA NYUMA MARA YA KWANZA, BASI KAENI PAMOJA NA HAO WATAKAO BAKIA NYUMA. WALA USIMSWALIE YE YOTE KATIKA WAO AKIFA, WALA USISIMAME KABURINI KWAKE. HAKIKA HAO WAMEMKATAA ALLAH NA MTUME WAKE, NA WAKAFA NA HALI NI WAPOTOFU. WALA ZISIKUSHITUE MALI ZAO NA WATOTO WAO. ALLAH ANATAKA KUWAADHIBU KWA HAYO KATIKA DUNIA; NA ZITOKE ROHO ZAO NA HALI WAO NI MAKAFIRI”. [9:81-85]

 

           V.      Ni jukumu la kila mtu katika uma wa Kiislamu kutekeleza wajibu wake katika kuuhami umma wakati wa hatari:

         Na atakaye zitupia jicho la uchunguzi aya alizo teremshiwa Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-katika vita vya Tabuuk. Atazikuta ndizo kali kuliko zote zilizo pata kushushwa kuhusiana na kadhia ya wabakiao nyuma wasende vitani. Pamoja na ukweli kwamba hayakutuka mapambano katika vita hivi na wala waislamu hawakukutana na adui yao. Kinacho dhihirika ni kwamba kadhia iliyopo katika suala la jihadi si jambo la kutuka au kutokutuka kwa mapambano, la hasha. Hakika si vinginevyo, ni suala la wajibu wa waislamu kuulinda uma wao dhidi ya kila adui anaye taka kuwachokoza/kuwashambulia, ni mamoja hilo limekuwa kiamalia au kinia. Ni wajibu wa kila mmoja katika uma wa Kiislamu kuitekeleza sehemu yake katika kuuhami uma, ila awe na udhuru – hemezi unao mzuia kuutekeleza wajibu wake huo: “HAPANA LAWAMA KWA WANYONGE, WAGONJWA NA WASIO PATA CHA KUTUMIA, MAADAMU WANAMSAFIA NIYA ALLAH NA MTUME WAKE. HAPANA NJIA YA KUWALAUMU WANAO FANYA WEMA. NA ALLAH NI MWENYE KUSAMEHE MWENYE KUREHEMU. WALA WALE WALIO KUJIA ILI UWACHUKUE UKASEMA: SINA KIPANDO CHA KUKUCHUKUENI. TENA WAKARUDI NA MACHO YAO YANAMIMINIKA MACHOZI KWA HUZUNI YA KUKOSA CHA KUTOA. IPO NJIA YA KUWALAUMU WALE WANAO KUOMBA RUHUSA WASENDE VITANI NA HALI WAO NI MATAJIRI. WAMERIDHIA KUWA PAMOJA NA WANAO BAKIA NYUMA. NA ALLAH AMEWAPIGA MUHURI JUU YA NYOYO ZAO, KWA HIVYO HAWAJUI”. [9:91-93]

Kutoka na mtiririko wa maelezo ya aya hizi, kubakia nyuma kwa walio bakia nyuma katika vita vya Tabuuk, wasende vitani bila ya udhuru. Kumekuwa ni ukataaji wa kutekeleza wajibu ulio faradhishwa kwa kila muweza katika uma wa Kiislamu na ni kuacha kuinusuru jamii wanayo jinasibisha nayo. Na ni udhaifu katika kipindi kibaya na kigumu, ikawa hapana budi suala lao hili liwekwe wazi kwa jamii ili wasije vunjwa tena moyo na watu kama hao hapo baadae. Na ikawa hapana budi watiwe adabu kali itakayo kuwa onyo kali kwao na kwa wengine ili waogope. Sasa basi ama watubie na kurejea katika safu za jamaa wakiwa wana usuluhivu wa kubakia. Au jamaa iachane kabisa na watu hao, wao wasiwe miongoni mwa kundi hili lililo pamoja na Mtume na wala kundi hili lisiwe pamoja nao.

 



 | Tuandikie |