Makala
Uislamu-Utangulizi
Fiqhi na Sheria 
Akhlaaq-Tabia
Sira ya Mtume
Nasaha za dini
Maswali na Majibu
Uliza Suala la dini
Jiunge na Mtandao !!!

 

SIRA YA MTUME (SAW)  

"BILA SHAKA MNAO MFANO MWEMA KWA MTUME WA MWENYEZI MUNGU…"Al-qur-an (33:21)

KA'B AMUELEZA UKWELI MTUME

 Faida

 

 III.       Ka’ab amueleza ukweli Mtume wa Allah:

         Ka’ab Ibn Maalik-Allah amuwiye radhi-anaendelea kusimulia khabari yake, anasema: “Nilipo msalimia Mtume, akatabasamu tabasamu la mtu aliye ghadhibika, halafu akasema: Njoo. Nikaenda mpaka nikakaa mbele yake, akaniuliza: “Ni lipi lililo kubakisha nyuma? Hivi wewe hukuwa umeshanunua kipando chako?” Nikajibu: “Kwani wallah, na hakika mimi wallah ewe Mtume wa Allah, lau ningelikuwa mbele ya asiye kuwa wewe miongoni mwa watu wa dunia. Najiona ningeliokoka na ghadhabu yake kwa udhuru, kwani mimi nimepewa ufundi wa kuzungumza. Lakini mimi wallah, ninajua leo nikikuongopea ukaniridhia, ninachelea Allah kukufanya unighadhibikie. Na nikikueleza ukweli utanighadhibikia, hakika mimi ninatarajia ndani ya ukweli huo kupata msamaha wa Allah hapo baadae. Wallah, hapana mimi sikuwa na udhuru wo wote! Wallah, katu sikuwa mwenye nguvu zaidi na mwepesi mno kuliko wakati nilio bakia nyuma nisitoke pamoja nawe”. Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akasema: “Ama huyu, hakika amesema kweli, basi nenda zako mpaka Allah akuhukumu”.

Basi nikainuka nikaondoka, wakanifuata haraka watu katika Baniy Salamah, wakaniambia: “Wallah, hatukujua kuwa umefanya kosa kabla ya leo, umeshindwa kutoa udhuru kwa Mtume wa Allah kama walivyo fanya walio bakia nyuma! Hakika ilikuwa inakutoshea dhambi yako hiyo (ya kusema uwongo), istighfaari ya Mtume wa Allah”. Basi wallah, hawakucha kunikaripia na kunikemea mpaka nikataka kurejea kwa Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-nikaikadhibishe nafsi yangu. Halafu nikawauliza: Je, yamemkuta haya pamoja nami mtu mwingine au ni miye tu? Wakajibu: “Naam, watu wawili wamesema kama ulivyo sema wewe na wao wakaambiwa kama ulivyo ambiwa wewe”. Nikauliza: Ni kina nani hao? Wakasema: “Muraarah Ibn Rabee Al-Amriy na Hilaal Ibn Umayyah Al-Waaqifiy”. Wakanitajia watu wawili wema walio shiriki katika vita vya Badri, ambao mimi nina kigezo chema kwao. Basi nikashikilia msimamo wangu pale walipo nitajia watu hao.

 

  IV.       Kuadabisha na kunyoosha:

         Akazidi kusema: “Na Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akakataza watu kuongea nasi, sisi watu watatu miongoni mwa walio bakia nyuma wasende pamoja naye vitani. Basi watu wakatuepuka na kutubadilikia mpaka nikaoina mbaya ardhi ile ikawa kama si ile ardhi niijuayo, tukakaa katika hali hiyo ya mtengo kiasi cha siku khamsini. Ama wale wenzangu wawili, wao wakajisalimisha wakakaa majumbani mwao, hawakutoka kabisa. Ama mimi ndiye niliye kuwa kijana kati yao na mwenye moyo thabiti, basi nikawa natoka nahudhuria swala ya jamaa pamoja na waislamu. Na nikizunguka masokoni, basi hapana mtu ye yote anaye nisemesha. Na nikimuendea Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-ninamsalimia naye akiwa katika kitako chake baada ya swala. Nikijiambia moyoni: Je, ameitukutisha midomo yake kuitikia salamu yangu au la. Kisha huswali Sunnah karibu naye huku nikimtazama kwa wizi, ninapoa anza kuswali huniangalia na nikigeukia upande wake hukengeuka nami. Hata kilipo repa kitambo cha kukatwa pande na watu, nikaenda nikauparamia ukuta wa nyumba ya Abu Qataadah. Huyu ni binamu yangu na aliye kipenzi mno kwangu, nikamtolea salamu, basi wallah hakunijibu, nikamwambia: Ewe Abu Qataadah, ninakuapia kwa Allah, hivi unajua kwamba mimi ninampenda Allah na Mtume wake? Akanyamaza kimya asinijibu kitu, nikarudia tena nikamuapia, akanyamaza kimya. Nikamuapia na kurudia mara ya tatu, ndipo akasema: “Allah na Mtume wake ndio wajuao zaidi (ukweli wa hayo uyasemayao)”. Macho yangu yakafurika machozi furi furi, nikarudi nyuma nikaparamia ukuta nikaondoka zangu”.

 

     V.       Warumi wajaribu kuitumia fursa hii kumfarakanisha Mtume na maswahaba wake:

         Anasema Ka’ab: “Basi wakati mmoja nikiwa natembea sokoni Madinah, tahamaki huyo ni Mnabati miongoni mwa Manabati wa Shamu walio kuja kuuza chakula Madinah, akiuliza: “Ni nani atakaye nifahamisha Ka’ab Ibn Maalik?”, watu wakaniashiria mimi. Hata alipo nijia akanipa waraka kutoka kwa mfalme wa Ghassaan, nikausoma na ndani yake mliandikwa: “Ama baad, hakika imetufikia khabari kwamba mtu wako (Muhammad) amekukata pande. Na wala Allah hakukuweka kwenye nchi ya udhalili wala mapuuzo, basi njoo kwetu tutakuliwaza”. Nikajisemea nilipo kwisha isoma: Na hili tena ni balaa jingine! Nikaenda nikaitia kwenye tanuri la moto nikaichoma. Hata zilipo pita siku arobaini katika zile siku khamsini, tahamaki huyoo ni mjumbe wa Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-ananijia. Alipo fika akasema: “Hakika Mtume wa Allah anakuamuru ujitenge na mkeo”. Nikauliza: Nimtaliki au nifanyeje? Akajibu: “Hapana (usimtaliki), bali jitenge naye usimkurubie”. Na akawatumia ujumbe kama huo wale wenzangu wawili. Nikamwambia mke wangu: Nenda kwenu, ukae huko mpaka Allah alihukumu suala hili”.

Ka’ab anasema: “Mke wa Hilaal Ibn Umayyah akamuendea Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akasema: “Ewe Mtume wa Allah! Hakika Hilaal Ibn Umayyah ni mtu mzima asiye weza kujihudumia mwenyewe na wala hana khadimu (mtumishi). Basi je, unaona vibaya mimi kumuhudumia yeye?” Mtume akajibu: “Hapana (sioni vibaya), lakini asikukurubie (kimwili)”. Akasema: “Wallah, hakika yeye hana nguvu ya lo lote. Wallah, amekuwa akilia tangu lilivyo kuwa suala lake hili hadi hii leo”. Mmoja wa watu wangu akaniambia: “Lau ungeli mtaka idhini Mtume wa Allah kwa mkeo, kwani amempa idhini mke wa Hilaal Ibn Umayyah amtumikie”. Nikasema: Wallah, simtaki idhini Mtume wa Allah kwa mke wangu, ninajuaje ataniambia nini nitakapo mtaka idhini na ilhali mimi ni kijana?”

 



 | Tuandikie |