Makurayshi walipoona juhudi zao za kumuendea kiongozi wao Mzee Abu Twalib ili amzuie mwana
wa nduguye kuwatukania miungu wao zimegonga mwamba, hazikuzaa matunda yeyote. Na moto wa
Daawah ya dini mpya ndio unazidi kushika kasi na watu wanazidi kumfuata Nabii Muhammad.
Hapo ndipo wakaamua kujaribu kutumia mbinu ya kumfanyia kero na maudhi anuwai sambamba na
kumfanyia maskhara. Khasa khasa alipokuwa akienda kuswali. Katika jumla ya maudhi
aliyofanyiwa Bwana Mtume Rehema na Amani zimshukie ni ile hekaya
iliyopokelewa na Abdullah bin Masoud Allah amuwie Radhi amesema : Tulikuwa
msikitini pamoja na Mtume wa Allah akiswali. Akasema Abu Jahli : Hivi hapana mtu
akayaendea matumbo ya kinyesi cha ngamia wa Baniy Fulani akaja akamtupia huyu Muhammad
il-hali akiwa kasujudu? Akainuka Uqbah bin Abiy Muaytwi akaenda kuyachukua matumbo ya
kinyesi kile na kuja kumtupia Bwana Mtume il-hali akiwa kasujudu. Hakuweza wala kuthubutu
yeyote miongoni mwa waislamu waliokuwepo pale msikitini kumuondolea Bwana Mtume uchafu ule
kwa sababu ya unyonge na udhaifu waliokuwa nao wakati ule. Bwana Mtume Rehema na
Amani zimshukie akaendelea kusujudu na uchafu ule ukiwa juu yake mpaka alipokuja Bi
Fatmah binti yake, yeye ndiye aliyemuondolea uchafu ule na kuutupilia mbali. Bwana Mtume
alipoinuka alimuombea dua ya maangamivu mtu aliyefanya kitendo hiki kiovu akasema : Ewe
Mola wa haki liangamize kundi la Makurayshi, na akawataja watu kadhaa. Ibn Masoud anasema
: Nikawaona watu aliowataja Mtume wameuliwa katika vita vya Badri.
Abu Lahab ibn Abdul-Mutwalib, ami yake Mtume hakuwa nyuma katika kumfanyia maudhi Mtume
bali yeye ndiye aliyekuwa mbaya zaidi kuliko watu baki wasiokuwa jamaa zake Mtume. Huyu
alikuwa ni jirani yake. Alikuwa na zoezi la kukusanya takataka za kila aina na kuja
kuzitupia mlangoni kwa Bwana Mtume kila asubuhi. Mtume akiamka na kufungua mlango wake,
kitu cha mwanzo alichokutana nacho ni harufu mbaya iliyotokana na takataka zile. Bwana
Mtume akawa hana la kufanya bali kuuondosha uchafu ule na kwenda kuutupa panapostahiki
huku akisema : "Enyi wana wa Abdi Manaf ni ujirani gani huu ?! Ummu Jamiylah, mkewe
Abuu Lahab alikuwa bega kwa bega na mumewe akishirikiana katika nae katika matendo haya
maovu. Bibi huyu alikuwa akimtukana Bwana Mtume mara kwa mara na akieneza maneno ya fitina
na uchochezi dhidi ya Mtume, khasa khasa baada ya kushuka Suratil-Lahab, sura iliyotaja
kuangamia kwa Abi Lahab na mkewe huyu. Miongoni mwa matukio ya kero na maudhi dhidi ya
Bwana Mtume Rehema na Amani zimshukie ni lile tukio lililoripotiwa katika
sahihil-Bukhariy, Amesema Imaam Bukhariy Allah amrehemu Wakati ambapo Mtume
alipokuwa akiswali katika kikuta cha Al-Kaaba, alijiwa na Uqbah na Abi Muaytwi akaiweka
nguo yake shingoni mwa Mtume na kumtia kabari ya nguvu. Akaja Abu Bakri akamshika Uqbah
begani na kumsukumia mbali na Mtume, na akasema : "OH ! MTAMUUA MTU KWA SABABU
ANASEMA MOLA WANGU NI ALLAH ? NA KWA YAKINI AMEKUJIENI KWA DALILI ZA WAZI ZITOKAZO KWA
MOLA WENU ! (Muacheni msimuue)" [40:28]. Hizi ni kero na maudhi machache tu
aliyofanyiwa Bwana Mtume na Makurayshi ili yawe ni kichocheo cha kumfanya aache kulingania
dini aliyokuja nayo. Miongoni mwa watu waliokuwa mstari wa mbele kumfanyia maskhara na
kumcheza shere Bwana Mtume ni Al-Aaswi bin Waail. Huyu alikuwa ni adui mkubwa wa Bwana
Mtume na alikuwa akisema : Muhammad amewadanganya wafuasi wake eti watafufuliwa na kuwa
hai tena baada ya kufa, Wallah hakuna kinachotuangamiza ila ni upitaji wa masiku na miaka
tu. Mwenyezi Mungu Mtukufu akamrudi kwa madai yake haya kwa kusema : "NA WALISEMA
HAUKUWA (uhai) ILA NI UHAI WETU HUU WA DUNIA, (hakuna mwingine); TUNAKUFA NA TUNAISHI,
WALA HAKUNA KINACHOTUANGAMIZA ISIPOKUWA (huu huu) ULIMWENGU; (kwani ndiyo ada yake kufisha
na kuhuisha) LAKINI WAO HAWANA ELIMU YA HAYO (wanayoyasema) WANADHANI TU" [45:24].
Katika kuzidi kumfanyia maskhara Bwana Mtume, Al-Aaswi huyu alikuwa anadaiwa na Khabbaab
bin Al-Arratta mojawapo wa wafuasi wa Bwana Mtume, ulipofika wakati walioagana wa kulipa
deni, muislamu huyu alimuendea Al-Aaswi ili amlipe deni lake. Al-Aaswi akamwambia : Si
anadai huyo Muhammad ambaye wewe umeingia katika dini yake kwamba watu wa peponi watapata
chochote wakitakacho ? Khabbaab akamjibu : Ndiyo. Al-aaswi akasema : Basi nisubirie mpaka
siku hiyo nitakapopewa mali na watoto ndipo nitakulipa deni lako. Hapo ndipo iliposhuka
kauli yake Mola Mtukufu : "JE UMEMUONA YULE ALIYEZIKANUSHA AYA ZETU NA AKASEMA KWA
HAKIKA NITAPEWA (huko akhera) MALI NA WATOTO (kama nilivyopewa hapa) JE AMEPATA KHABARI ZA
GHAIBU AU AMECHUKUA AHADI KWA (Allah) MWINGI WA REHEMA (juu ya haya) ? SIYO! HAKIKA
TUNAANDIKA ANAYOSEMA NA TUTAMZIDISHIA MUDA (mkubwa) KATIKA ADHABU [19:77-79].
Hiki ni kisa kimojawapo miongoni mwa visa vya kumcheza shere alivyofanyiwa Bwana Mtume.
Lengo na madhumuni ikiwa ni kumkatisha tamaa ili aache kuendelea kuutangaza Uislamu, dini
ambayo iko dhidi ya mfumo wa maisha waliojichagulia na ambao wameuzoea kwa miongo ya
miaka. Kuucheza kwao shere na kumfanyia maskhara hakukumfanya Mtume arudi nyuma, bali
aliwapuuza na kuendelea na jukumu alilopewa na Mola wake na Mwenyezi Mungu Mtukufu akazidi
kumtia nguvu kwa kuwaangamiza wote waliokuwa wakimcheza shere kama tunavyosoma :
"HAKIKA SISI TUNAKUTOSHA KUKUKINGIA (shari ya) WANAOFANYA DHIHAKA" [15:95].
Miongoni mwao wako waliouliwa vitani na wengine walipatwa na maradhi makubwa, wakafa
kutokana na maradhi hayo. Hila na mbinu hizi za maudhi na dhihaka ziliposhindwa, wakabuni
mbinu mpya. Mbinu hii haikuwa nyingine bali ilikuwa ni ile mbinu ya kulichafua jina na
sifa ya Mtume kwa kumpaka matope ya sifa mbaya ili kufuta kule kukubalika kwake na jamii.
Kwa hiyo wakaanza kumsingizia na kutangaza kuwa Bwana Mtume Rehema na Amani
zimshukie ni mwendawazimu, asiyejua wala kulitambua alisemalo bali huropoka tu
kutokana na wazimu wake. Mara nyingine walidai eti ni mchawi na wakati mwingine walimuita
kuwa ni kuhani na mtunga mashairi. Kwa sababu hizo wakawa wanawatahadharisha watu
wasikutane nae, wasizungumze nae na wala kumsikiliza asije akawaroga na kuwafanya waache
dini ya mababa zao na kumfuata yeye. Mwenyezi Mungu Mtukufu anamtakasa Mtume wake na
tuhuma hizo za maadui wake, tusome : "BASI ENDELEA KUWAKUMBUSHA. NA WEWE KWA NEEMA ZA
MOLA SI MCHAWI WALA SI MWENDAWAZIMU (kama wanavyosema). NDIYO WANASEMA KUWA HUYU
(Muhammad) NI MTUNGA MASHAIRI, TUNAMTAZAMIA KUPATIKANA NA MAUTI (kama walivyokufa washairi
wengine)" [52:29-30].
Hizi ni baadhi tu ya hila na mbinu walizotumia Makurayshi katika kujaribu kulizima wimbi
la mageuzi ya kiitikadi yaliyokuwa yakiongozwa na Bwana Mtume Rehema na Amani
zimshukie -
|
| |
TUJIFUNZE NA TUKUBALI : kuwa maadui wa
Uislamu hutumia hila na mbinu mbalimbali chafu ili kuzorotesha na hatimaye kuzuia harakati
za Uislamu katika ardhi hii. Mojawapo wa mbinu kongwe watumiazo ni kuwapa majina na sifa
mbaya Waislamu safi/wakweli ili wapate fursa ya kuwahujumu bila ya kulaumiwa na Ulimwengu.
|