|
HIJRA YA KWANZA YA UHABESHI (ERITREA)
Bwana Mtume Rehema na Amani zimshukie alipoona kwamba Makurayshi
wanazidi kuendeleza sera yao ya mateso na ukatili dhidi ya maswahaba kwa ajili tu ya
kulinda hadhi na heshima ya miungu yao na nafasi yao baina ya Waarabu isichukuliwe na
Uislamu. Kadhalika Mtume alipoona kuwa yeye hana ubavu wa kukabiliana na kupambana na
Makurayshi ili kuiondosha dhulma hii kwa maswahaba wake na akaiona hatari na fitna
inayowanyemelea kutokana na ukali na uchungu wa adhabu na mateso hayo. Mtume alitambua
fika kwamba maswahaba ni wanadamu kama wanadamu wengine, wanaathirika na adhabu na mateso
kama watu wengine, adhabu isije ikawafikisha mahala wakajiuliza, hivi ni kwa nini
tunaadhibiwa, bila shaka ni kwa ajili ya Uislamu tu, Uislamu ambao unashindwa kututetea na
kutuhami, basi ni vema kama tutauacha Uislamu na kurejea katika dini ya mababa zetu ili
tusalimike na adhabu na mateso haya tuyapatayo. Hii ndiyo fitna na hatari aliyoichelea
Bwana Mtume kama kiongozi mwenye kuwajibika kwa watu wake alijiona ana wajibu na jukumu la
kulitafutia ufumbuzi tatizo hili. Akakaa chini na kutafakari, baada ya kutafakari kwa
makini akaona hakuna suluhisho jingine zaidi ya kuwakimbia makurayshi kwa kuhamia
Uhabeshi. Akawashauri maswahaba: "Mnaonaje lau mtatoka mkaelekea Uhabeshi, kwani huko
kuna mfalme ambaye mtu hadhulumiwi mbele yake, hiyo ni ardhi (nchi) ya ukweli, mpaka hapo
Mwenyezi Mungu atakapokupeni faraja na matokeo kutokana na hali hii (ya adhabu na mateso)
mliyo nayo." Nchi hii ya Uhabeshi ilikuwa ikifuata dini ya unaswara, dini ya Nabii
Isa Ibn Mariamu Rehema na amani zimshuie Mfalme wa nchi hii Najaash alikuwa
ni mfuasi mkweli wa dini hii. Wakahamia Uhabeshi kutokana na ushauri huu wa Bwana Mtume,
wanamume kumi na mbili (12) na wanawake watano (5). Miongoni mwa wakimbizi na wahamiaji
hawa walikuwemo Uthman Ibn Affaan na mkewe Ruqayah binti ya Mtume, Zuberi Ibn al-Awwaam
mtoto wa Ami yake bi Khadijah mkewe Bwana Mtume, Uthmaan Ibn Madh-uun, Utbah Ibn Rabia na
Mkewe Sahlah Bint suhayl. Hili ndilo kundi la mwanzo la Waislamu kuhamia Uhabeshi, na hii
ndio hijra ya kwanza katika Uislamu. Hijra hii ilikuwa katika mwezi wa Rajab, mwaka wa
tano wa utume, yaani tangu Bwana Mtume Rehema na Amani zimshukie
alipokabidhiwa rasmi na Mola wake jukumu la kuuongoza umah.
Waanga na wathirika hawa wa mateso ya makurayshi walipofika Uhabeshi, walipokelewa vema na
mfalme Najaash, wakapata tena amani na utulivu walioukosa katika nchi yao wenyewe.
Ukarimu, amani na utulivu huu ukawashajiisha kuwatumia ujumbe ndugu zao wengine
wanaoadhibiwa Makkah waje kujiunga nao huko. Hivi ndivyo mfalme huyu muadilifu
alivyowatendea wakimbizi hawa waislamu kwa kuyafuata mafundisho sahihi ya Nabii Issa
amani ya Allah imshukie
(II) KUSILIMU KWA HAMZAH NA UMAR
Kwa upande mwingine adhabu, mateso, maudhi na makero ya Makurayshi kwa waislamu
yaliwaletea faraja waislamu.
Mateso na makero haya ndiyo yaliyokuwa sababu na changamoto kubwa ya kusilimu mtu mkubwa,
mwenye sauti na nguvu katika mji wa Makkah. Mtu aliyekubaliwa na kutambuliwa na Makurayshi
kama shujaa. Mtu huyu si mwingine bali ni ami yake Mtume Hamzah Ibn Abdul-Mutwalib, mtu
aliyekuwa nguzo kuwa kwa upande wa Makurayshi.
Sababu ya kusilimu kwa simba wa Allah Hamzah, jina alipewa kutokana na mchango wake mkubwa
alioutoa katika kupigania dini ya Mwenyezi Mungu Mtukufu. Siku moja, Hamzah alitoka
asubuhi akiwa amevaa nguo nadhifu za kifakhari, akiwa na upanga wake, akitembea kwa
maringo, kifua mbele. Katika matembezi yake hayo alimpitia mjakazi mmoja aliyekuwa njiani,
mjakazi yule akamwambia " Lau Baba Amaarah (Hamzah) angeliyasikia maneno mabaya
aliyoyasema Abu Jahli kumwambia mwana wa nduguye Muhammad, basi asingelitembea kwa maringo
kiasi hiki". Hamzah akamuuliza yule mjakazi "Kwani amesema nini?"
Akamwambia "Hakika Abu Jahli amemtukana Muhammad matusi machafu ya kufedhehesha
sana". Hamzah akaondoka pale akiwa amepandwa na mori wa hasira, amekuwa mwekundu
kutokana na hasira, akamuendea mbaya wake Abu Jahli. Akamkuta akiwa amekaa barazani na
viongozi wa Makurayshi, bila hata ya kuwaslimia kama ilivyokuwa ada na desturi yao,
akamuwasha kibao cha nguvu cha uso na kumwambia kwa sauti ya ukali iliyojaa hasira zote.
"Vipi unathubutu kumtukana Muhammad na ilhali mimi nimekwishaingia katika dini
yake?" Baada ya kusema maneno hayo, Hamzah akaondoka akenda kwa Mtume na kuutangaza
Uislamu wake, akasilimu. Kusilimu kwake ikawa ni sababu ya Uislamu na Waislamu kupata
nguvu na utukufu. Makurayshi wakatambua kwamba sasa Muhammad amepata ngome kuu na Hamzah
hatakuwa tayari kuona mwana wa nduguye akidhulumiwa na kuonewa. Hamzah baada ya kusilimu
aliulekeza ushujaa na nguvu zake zote katika kuitetea na kuuipigania dini ya Mwenyezi
Mungu, ni kwa sababu hii ndiyo Bwana mtume akamuita "Simba wa Allah"
Allah amuwiye radhi yeye na maswahaba wote wa Bwana Mtume. Anga la Mji wa Makkah lilitanda
khofu na fazaa kubwa kutokana na waislamu kuhama Uhabeshi na kusilimu kwa shujaa Hamzah.
Mambo mawili haya yaliacha pengo kubwa sana kwa upande wa Makurayshi. Watu wenye hisia na
muono wa mbali waliliona pengo hili na hatari yake ya baadaye. Miongoni mwa watu hao
alikuwa ni Umar Ibn Khatwaab, jambo hili lilimkosesha usingizi Umar, ambaye alikuwa ni
kijana shujaa, bingwa wa vita na fakhari ya Makurayshi. Alikuwa adui mkubwa wa Mtume na
waislamu. Umar akaona balaa hili la jamaa zake kuhamia Uhabeshi, kutukaniwa dini yao na
Makurayshi kugombana na kuzozana wao kwa wao, yote haya yamesababishwa na huyu Muhammad.
Umar akaona suluhisho na ufumbuzi pekee kwa tatizo hili ni kuukata mzizi wa fitina hiii,
kwa hivyo akaazimia kumuua Mtume kwa mkono wake mwenyewe ili watu wapumzike na hicho
walichokiita wao shari lake. Ndipo siku moja akatoka nyumbani kwake akiwa na upanga wake
kibindoni, anamuendea Bwana Mtume ili amkate kichwa. Mwanasira mkubwa Ibn Ishaaq
Allah amrehemu analisimulia tukio hili, anasema :- "Nuaim Ibn Abdillah
akakutana nae (Umar) njiani, akamuuliza : Unakwenda wapi ewe Umar ? (Umar) akamjibu
"Ninamkusudia huyu Muhammad ambeye amewatenganisha Makurayshi, ameikosoa dini yao na
kuwatukania miungu wao, naenda kumuua !" Nuaim akamwambia wallah, nafsi yako
inakudanganya ewe Umar ! Hivi unafikiri Baniy Abdi Manaaf watakuachia utembee juu ya ardhi
utakapomuua Muhammad? Kwa nini basi usianze kutengeneza na kushughulikia masuala ya ndugu
zako kwanza?" (Umar) akamuuliuza (Nuaim): Ndugu zangu gani hao? Akamjibu : Shemeji
yako na mwana wa ami yako Said Ibn Zayd na dada yako Fatmah Bint Khatwaab, Wallah
wamekwisha silimu na kumfuata Muhammad katika dini yake, basi anza na hawa kwanza. Ibn
Ishaaq anaendelea kusema pale pale Umar akabadili njia, akamuendea dada na shemeji yake
nyumbani kwao. Akawakuta pamoja na Khabaah Ibn Arat akiwasomea Surat Twaaha katika
karatasi aliyoishika. Walipomsikia Umar, Khabaab akakimbia na kwenda kujificha, Fatmah
akaificha ile karatasi. Umar alipoingia akawauliza: Ni sauti gani hii niliyoisikia ?
Wakamjibu: Hukusikia cho chote. Akawaambia : hapana. Wallah nimesikia kitu na
nimekwishaambiwa kwamba nyinyi mmekwisha mfuata Muhammad katika dini yake! Umar kwisha
kusema maneno hayo, akamtia kabali shemeji yake. Dada yake kuona hivyo, akamuendea Umar
ili amnasue mumewe, Umar akampiga dada yake kibao cha nguvu kilichomtoa damu. Hapo ndipo
ile nguvu ya imani ilipowajia dada na shemeji yake, wakamwambia : Naam, sisi tumekwisha
silimu na tumemuamini Allah na Mtume wake, sasa wewe fanya utakalo ! ama kweli damu si
maji. Umar alipoiona damu ya dada yake ikichuruzika, moyo wake ukajawa na huruma na
akajuta kwa nini amefanya kitendo hicho, akamwambia dada yake Hebu nipe hiyo karatasi
ambayo nimekusikieni mkiisoma hivi punde, ili nipate kuona alichokuja nacho Muhammad. Umar
alikuwa ni mtu anyejua kusoma na kuandika. Dada yake akamjibu bila ya khofu wala woga; Ewe
kaka yangu, hakika wewe ni najisi kutokana/kwa sababu ya ushirikina wako na karatasi
(kitabu) hii haigusi/haishiki ila aliye twahara, Umar kwa kuwa alikuwa na shauku ya kutaka
kujua kilichoandikwa ndani ya ile karatasi, akainuka akaenda kukoga. Hapo ndipo dada yake
alipompa ile karatasi na ilikuwa imeandikwa Suurat twaha (sura ya 20), akaisoma.
Alipoisoma mwanzo mwanzo tu wa sura akasema : Maneno mazuri na mtukufu yaliyoje ! Khabbaab
alipoisikia kauli hiyo akatoka mafichoni alipokuwa, akamwambia Umar: Ewe Umar, Wallah mimi
ninatarajia kwamba Allah ameikubali dua ya Mtume wake kwako, kwani mimi nimemsikia jana
akisema: "Ewe Mola wa haki upe nguvu (usaidie)Uislamu kwa (kusilimu) Amr Ibn Hishaam
(jahl) au Umar Ibn Khatwaab" Khabab akaendelea : Ala ! ala! Ewe Umar, Umar akamwambia
Hebu nifahamishe alipo Muhammad, nikasilimu. Khabbaab akamwambia : Yuko katika nyumba
moja, jirani na kilima Swafaa pamoja na kundi la maswahaba wake. Umar akamweka upanga wake
katika ala kibindoni, akatoka na kumuendea Bwana Mtume. Alipofika akagonga mlango,
walipoisikia sauti yake, akainuka mtu mmoja na kwenda kuchungulia, akamuona Umar akiwa na
upanga wake mkononi. Akarejea kwa Mtume akiwa amefadhaika na kumwambia : Umar huyo, yuko
mlangoni na upanga wake. Hapo ndipo (simba wa Allah) Hamzah Ibn Abdul- Mutwalib akasema
kwa ushujaa: Muacheni apite, ukiwa amekuja kwa kheri ameipata na iwapo amekusudia shari,
tutamuua kwa upanga wake mwenyewe. Bwana Mtume Rehema na Amani zimshukie - akasema
"Muacheni apite". Alipoingia Mtume akamuuliza : "Umejia nini? Ewe mwana wa
Khatwaab? Umar akamjibu: Ewe Mtume wa Allah, nimekuja ili nimuamini Allah na Mtume wake.
Ibn Is-haaq anasema : Mtume wa Allah akapiga takbira iliyowatambulisha maswahaba kwamba
Umar amesilimu. Ama kweli baada ya dhiki faraja, hivyo ndivyo Mwenyezi Mungu
alivyowafariji waislamu wanyonge kwa kuwaleta katika Uislamu watu hawa mashuhuri. Kusilimu
kwa Hamzah na Umar ilikuwa ni katika mwaka wa tano wa utume
|