|
Makurayshi
walipoona na kutambua kuwa njia, mbinu na hila zote walizozitumia ili kupambana, kuzuia na
hatimaye kuliua kabisa wimbi la harakati za dawah ya Bwana Mtume zimegonga ukuta,
hazikuzaa matunda yoyote bali ndio zilizidi kulichochea wimbi hilo. Wakaona uislamu
unazidi kudhihiri na kuenea kwa kasi kubwa isiyoweza kuzuilika. Wakaona wanazidi
kuwapoteza watu muhimu na mihimili kwa upande wao na watu hao hao kuwa ni sababu ya
uislamu kuzidi kupata nguvu na himaya. Walipoona kukua kwa nguvu ya waislamu, waislamu
ambao walikuwa wakiziswali swala zao kwa uficho mkubwa sasa wanathubutu na kujasiri
kuswali hadharani mbele ya macho yao katika haram (eneo takatifu) ya Alkaaba.
Wakaweza kusoma Qur-ani mbele ya kadamnasi ya makurayashi, jambo ambalo halikupata
kufanywa huko nyuma. Hapa sasa ndipo makurayshi walipohemewa wasijue la kufanya hasa
walipokuwa hawawezi kukabiliana na Bwana Mtume kwa hoja. Baada ya kutafakari na kuumiza
vichwa kwa muda mrefu wakaibuka na kile walichoamini kuwa ndio silaha kali itakayoua na
kuangamiza kabisa harakati za Nabii Muhammad. Silaha hii haikuwa nyingine bali ni ile
silaha ya kuwekewa vikwazo vya kiuchumi na kijamii, silaha ambayo imekuwa ndio mtindo wa
mabeberu na madhalimu wa leo. Mwanasira mkubwa Is-haaq - Allah amerehemu
anatusimulia hali ilivyokuwa, anasema; Makurayshi walipoona kwamba maswahaba wa
Mtume wa Mwenyezi Mungu - Rehema na Amani zimshukie wamefikia katika nchi ambayo
wamepata amani na kwamba (mfalme) Najaash amewazuia (amekataa kuwatoa) wale waliokimbilia
kwake. Na (waliopoona) kwamba Umar amesilimu, yeye na Hamzah Ibn AbdilMutwalib
wamekuwa pamoja na Mtume wa mwenyezi Mungu na maswahaba wake na Uislamu ukaanza kuenea
katika makabila (mbali mbali ya Waarabu). Walikutana na kula njama za pamoja katika kuweka
azimio la pamoja dhidi ya Baniy Haashim na Baniy Mutwalib (koo za Mtume). Wakaweka azimio
la kutokuwaolea wala kuwaoza, kutokuwauzia chochote wala kununua kutoka kwao.
Wakakongamana kwa hilo na kuandika azimio la mkataba, kisha wakalibandika azimio hilo
ndani ya al-Kaaba ili kuzitia nguvu nafsi zao. Makurayshi walipofikia uamuzi huo, Baniy
Hashim na baniy Mutwalib wakaungana pamoja na Mzee Abu Twaalib wakaingia katika ngome /
boma lake. Alitoka katika baniy Haashim Abu Lahab AbdulUzzah Ibn
abdul-Mutwalib akaungana na Makurayshi dhidi ya jamaa zake.
Kwa mujibu wa wanazuoni wa sira na taarikh (Historia) tukio hili la vikwazo
lilikuwa katika mwaka wa saba wa Utume. Hivyo ndivyo Baniy Haashim na Baniy Mutwalib
walivyozuiliwa katika boma la Abu Twaalib pamoja na wanawake na watoto wao, wakiwa hawana
mawasiliano yoyote na yeyote. Hawapati chakula, maji wala kitu chochote. Makurayshi
wakazidisha ukatili wao mpaka ikafikia mfanyabiashara yeyote anayekuja mjini makkah kuleta
bidhaa za mazao ya chakula wao (makurayshi) humuwahi akiwa bado nje ya mji wakainunua
bidhaa yote aliyokuwa nayo kwa maradufu ya thamani. Walifanya hivyo ili kuhakikisha kuwa
hakuna chakula kinachowafikia Waislamu mpaka wasalimu amri na waache harakati zao. Abu
Lahab na Abu Jahli ndio waliokuwa viongozi wa kusimamia harakati hizi za vikwazo dhidi ya
Waislamu. Abu Lahab, yeye alikuwa akiwachochea wafanya biashara wawapandishie bei ya
bidhaa Waislamu ili washindwe kununua. Nao wafanya biashara, kwa upande wao walikuwa
wakuitikia wito huu wa Abu Lahab wakiwapandishia bei waislamu mara dufu ya mara dufu.
Muislamu akifikishwa hapo, hushindwa kununua chochote na kuamua kurudi kambini mikono
mitupu na kuwaona watoto wakilizana kwa njaa. Ama Abu Jahli, yeye daima alikuwa macho
kuhakikisha kuwa vikwazo vinatekelezwa ipasavyo na hakuna mtu yeyote anayekwenda kinyume
na maazimio ya vikwazo dhidi ya Waislamu. Abu Jahli alifanya hivyo ili kuhakikisha kuwa
vikwazo vinafikia lengo lake ambalo lilikuwa ni kuwalazimisha Baniy Haashim na Baniy
Mutwalib waache kumkingia kifua Bwana Mtume na na wamsalimishe mikononi mwa makurayshi
wamuue. Au Bwana Mtume aache na kuzitupilia mbali harakati zake za Daawah na kwa hali hiyo
watakuwa wameukatilia mbali mzizi wa fitna Uislamu kama walivyoliona hilo kwa
maono na mtazamo wao. Vikwazo hivi vikaendelea kwa kipindi kisichopungua miaka mitatu
ilhali Baniy Haashim na Baniy Mutwalib (Waumini na wasio waumini) wote kwa pamoja wakiwa
kambini katika boma la Mzee Abu Twaalib. Hali ikawawia ngumu mpaka wakalazimika kula
majani na mizizi ili kujinusuru maisha yao kutokana na janga hili la njaa ambalo
lilisababishwa na vikwazo vya makurayshi dhidi yao. Habari na vilio vilivyotokana na
vikwazo hivi zikawafikia watu na Waarabu waliokuwa wakija Makkah katika musimu wa Hijjah.
Watu hawa wakawa wakiulizana juu ya Daawah hii iliyowapelekea Makurayshi kutokuwa na
huruma hata chembe na kuwawekea ndugu zao wenyewe vikwazo hivi vibaya ambavyo havijapata
kutokea katika historia ya Waarabu. Baada ya kujiuliza huku, Waarabu wakatambua kuwa ni
lazima Daawah hii itakuwa ni kitu hatari sana, kwa hivyo wakataka kujua hakika na ukweli
wake. Wakaanza kuwatuma vijana wao kwenda kule kambini kupeleleza habari za Daawah hii ya
Nabii Muhammad na madhumuni/malengo yake. Hii ikawa ndio sababu ya kuenea kwa habari za
Uislamu baina ya Waarabu. Mambo yakawa kinyume na matarajio ya Makurayshi, kwani lile
walilotaka kulificha na kulizuia lisienee sasa ndilo linafichuka na kuenea kwa kasi. Tena
sasa Mtume hapati taabu ya kulingania Uislamu bali watu wenyewe sasa ndio wanazitafuta
habari za Uislamu. Habari za Uislamu zikafika mjini na vitongojini (Vijijini). Hapa sasa,
Makurayshi wakatambua kwamba vikwazo vyao vimepita bure, havikutimiza lengo lake. Wakahisi
kuwa Waarabu hawakupendezwa wala kufurahishwa na kitendo chao hiki kibaya na wakachelea
kupoteza heshima na utukufu wao baina ya Waarabu kutokana na ukatili wao huu. Hapa sasa,
Makurayshi wakaanza kugawanyika na kutofautiana katika swala zima la vikwazo. Baadhi yao
wakajiwa na hisia za utu na kuona ubaya wa kitendo walichokifanya dhidi ya ndugu zao
wenyewe. Wakaanza kulidiriki swala hili kwa njia za uficho, wakaanza kutoa misaada ya
chakula kwa ndugu zao hawa waliowekewa vikwazo na kuishi kambini. Miongoni mwa watu hawa
waliwathiriwa na hisia hizi za utu, alikuwa ni Bwana Hishaam Ibn Amri. Huyu alikuwa
akimchukua ngamia wake na kumbebesha shehena ya chakula, kisha hutoka nae usiku katika
hali ya uficho na kwenda nae mpaka katika kambi ya wahanga/waathirika wa vikwazo vile.
Akifika huko, humfungua na kushusha shehena yote ya chakula kwa wahanga bila ya kuchukua
chochote kutoka kwao kama malipo. Bwana yuyu aliendelea na zoezi lake hili mpaka pale
Makurayshi walipongamua na kumtolea maneno ya ukali kiasi cha kutaka kumuua. Abu Sufyaan
Ibn Harb akawambia nduguze Makurayshi Mwacheni! Mtu anawaunga nduguze. Ama mimi
ninaapa kwa jina la Allah, lau sisi sote tungelifanya kama afanyavyo yeye ingelikuwa ni
jambo bora kabisa
Miongoni mwa waliokuwa wakipeleka chakula alikuwemo pia Bwana Hakimu Ibn Hizaam.
Siku moja akiwa katika harakati zake za kupeleka chakula kama alivyojipangia akiwa na
mtumishi wake amebeba ngano, akakutana njiani na mtu muovu Abu Jahli. Bwana Hakiim
alikusudia kumpelekea chakula kile shangazi yake Bi Khadijah mkewe Bwana Mtume ambaye
alikuwa ni miongoni mwa wahanga wa vikwazo kule kambini. Abu Jahli akamwambia hakim
"Unawapelekea chakula Baniy Haashim? Wallah huendi wewe wala chakula chako mpaka
nikufedheheshe mjini Makkah! Wakiwa katika mzozo huo, akawatokea Abul-bakhtary Ibn
Hishaam, akamuuliza Ab Jahli: Una nini wewe na yeye ? chakula chake, anampelekea
shangazi yake, hivi unamzuia asimpelekee? Muachie aende zake Abu Jahli akagoma
katakata, mpaka wakaanza kutukanana. Abul-bakhtariry akachukua mfupa wa ngamia akampiga
nao Abu Jahli na kumtoa ngeu, hapa ndipo Bw. Hakim akapata penyo akashika njia na kwenda
zake
|