|
Baada ya Mtume Rehema na Amani zimshukie kuingia kambini katika boma
la Mzee Abu Twaalib, yeye na jamaa zake kufuatia vikwazo vya Makurayshi dhidi yao, Bwana
Mtume aliwaamrisha baadhi ya maswahaba wake kuhamia Uhabeshi kwa mara nyingine tena.
Wakahamia huko kufuatia agizo la Mtume wanamume themanini na tatu, wanawake wanane pamoja
na watoto kadhaa. Miongoni mwa waliokuwemo katika hijra hii ya pili ya Uhabeshi ni Uthmani
Ibn Affaan akiambatana na mkewe Bi. Rukia binti ya Mtume, mtoto wa ami yake Mtume Jaafar
Ibn Aby Twaalib akiwa na mkewe Bi. Asmaa bint Umays, Miqdaad Ibn Aswad, Abdullah Ibn
Masoud, Zubeyr Ibn al-awaam, Ummu Habiybah Bint Abiy sufyaan na wengineo wengi. Walipofika
Uhabeshi baada ya safari ndefu na yenye kuchosha, walipokelewa vizuri na Najaash Mfalme wa
nchi hii ya Uhabeshi. Wakapata amani, utulivu, salama na uhuru wa kuabudu bila ya
kubughudhiwa na yeyote.
Mwanachuoni wa sera Ibn Al-athiyr- Allah amrehemu anaelezea katika kitabu
chake AL-KAAMIL hali ilivyokuwa na hatua zilizochukuliwa na Makurayshi katika
kuidhibiti hali hiyo, anasema: Makurayshi walipoona kuwa wahamiaji/wakimbizi wa
Uhabeshi wamepata utulivu na amani katika nchi hiyo na kwamba Mfalme Najaash amewapokea
vizuri walipanga njama, wakamtuma Amri Ibn Al-aaswi na Abdullah Ibn Abiy Rabiah wampelekee
Najaash na mawaziri wake zawadi zenye thamani kubwa (hongo). Wakaenda mpaka wakafika
Uhabeshi, wakampelekea mfalme na mawaziri wake zawadi zao na wakamwambia mawaziri : Hakika
watu wapumbavu miongoni mwetu wameiacha dini ya jamaa zao na wala hawakuingia katika dini
ya Mfalme (wa nchi hii) na wamezua dini mpya tusiyoijua sisi wala nyinyi. Mabwana viongozi
wa jamaa zao wametutuma kwa mfalme warudishe kwao. Basi Mfalme atakapowataka ushauri
kuhusiana na watu hawa, mwambieni awarudishe kwetu na asizungumze nao chochote .
Makurayshi wawili wale walichelea Najaash akisikiliza maneno ya Waislamu hatowatoa.
Mawaziri wa Najaash baada ya kupokea hongo ile wakawaahidi kuwasaidia katika suala lao
hilo. Kisha wakapelekwa mbele ya mfalme wakamuelezea haja yao, mawaziri wake wakamshauri
awatoe waislamu. Mfalme akaghadhibika na kusema; Hapana, Wallah, sitowasalimisha
watu waliokimbilia kwangu, wakashukia katika nchi yangu na wakanichagua mimi na si
mwingine mpaka niwaite na kuwauliza juu ya wasemayo wajumbe hawa (kwa mkurayshi). Wakiwa
ni wakweli (katika wayasemayo wawili hawa) nitawasalimisha wakimbizi hawa. Kama hawako
kama wasemavyo(wajumbe hawa) sitawasalimisha (sitawatoa) na nitawafanyia ukimbizi mwema.
Najaash akawatumia mjumbe maswahaba wa mtume, awaite waje mbele yake. Wakahudhuria
barazani kwa mfalme wakiwa na azma ya kumwambia ukweli mtupu. Msemaji wao alikuwa ni Bwana
Jaafar Ibn Abiy Twaalib. Mfalme Najaash akawauliza; Ni dini gani hii ambayo
imekutenganisheni na jamaa zenu na wala hamkuingia katika dini yangu wala dini ya mila
yeyote ? Jaafar akajibu kwa niaba ya wenzake: Ewe mfalme, sisi tulikuwa ni
watu majahili, tukiabudu masanamu na kula mizoga, tukifanya mambo machafu na kukata udugu,
tukivunja haki ya ujirani, mwenye nguvu miongoni mwetu akimuonea mnyonge mpaka pale
Mwenyezi Mungu alipotuletea Mtume miongoni mwetu. Tunaijua vema nasabu yake, ukweli wake,
uaminifu wake na kujizuia kwake na machafu. (Mtume huyu) akatulingania kumpwkesha Mwenyezi
Mungu na tusimshirikishe na kitu/mtu yeyote. Tuache kuyaabudu masanamu na akatuamrisha
kusema ukweli, kutekeleza amana, kuunga udugu, kutekeleza haki za ujirani kuacha mambo ya
haramu na kumwaga damu. Akatukataza mambo machafu kusema uongo kula mali ya yatima na
akatuamrisha kuswali na kufunga na akaendelea kumtajia mambo kadhaa yaliyoletwa na Mtume
na Uislamu mpaka akafikia kusema: Basi tukamuamini (Mtume huyu) na kumsadiki,
tukayaharamisha aliyotuharamishia na tukayahalalisha aliyotuhalalishia. Hapo ndipo jamaa
na ndugu zetu walipoanza kutufanyia maadui, wakatuadhibu na kutufitinisha na dini yetu ili
turejee katika ibada ya masanamu. Basi walipotuzidi nguvu na kautufanyia dhulma na
kutuzuilia na dini yetu, ndipo tulipokuchagua wewe na sio mtu mwingine na tukatoka kwetu
kuja katika nchi yako na tunatarajia kutokudhulumiwa mbele yako ewe Mfalme" Baada ya
balozi wa kwanza wa Uislamu Jaafar Ibn Abiy Twaalib kwisha kusema maneno hayo, Najaash
akamuuliza tena: Je, unacho chochote alichokuja nacho Mtume wenu kutoka kwa Mwenyezi
Mungu? Jaafar akajibu: Naam, na akamsomea aya za mwanzo za Suurat
Mariam. Mfalme Najaash na Maaskofu wake wakalizwa na aya hizo, Najaash akasema :
Hakika maneno haya na yale aliyokuja nayo Issa yanatoka katika shubaka moja
(asili/chanzo kimoja)! Nendeni zenu (akawambia wajumbe wa Makurayshi) Wallah!
sitawasalimisha kwenu watu hawa katu! Amri Ibn Al-aaswi akamwambia Najaash (Maneno
ya uchochezi): Hakika watu hawa wanamsema vibaya Nabii Issa (wewe huwajui tu)"
Najaash akawauliza maswahaba wanasema nini kuhusiana na Nabii Issa Masibu Jaafar akajibu :
Tunasema juu yake yale aliyotuletea Mtume wetu kwamba : Yeye (Issa) ni mja na Mtume
wa Mwenyezi Mungu na ni Roho itokanayo naye (Mwenyezi Mungu kama roho nyingine) na (ni
kiumbe aliyeumbwa kwa) tamko lake (tu Mwenyezi Mungu ) alilolitia kwa bikira Mariam.
Najaash akasema baada ya kusikia maneno hayo: Nabii Masihi Issa yuko hivyo hivyo,
kama ulivyosema. Akawageukia waislamu na kuwaambia: Enendeni katika amani,
sipendi nipate jabali la dhahabu na nikawa nimemuudhi hata mtu mmoja tu katika
nyinyi, na akazirudisha zawadi zote alizoletewa na Makurayshi kama hongo ili
awafukuze waislamu katika nchi yake na kuwarudisha kwao Makkhah. Hivi ndivyo jaribio hili
la Makurayshi kutaka kuwarejesha waislamu adhabuni na matesoni lilivyoshindwa vibaya
kutokana na msimamo wa waislamu kusema kweli mbele ya Mfalme Muadilifu, Mpenda haki Mfuasi
wa kweli wa dini yake. Waislamu wakaishi raha Mustarehe kwa amani na salama katika nchi ya
Mfalme huyu. Mfalme huyu kama vitabu vya sera na tarekh vinavyosema alisilimu yeye pamoja
na makasisi na mapadri waliokuwa wakimzunguka mbele ya kiongozi wa wakimbizi wa haki Bwana
Jaafar Ibna Abiy Twaalib. Inasemekana hakuishi muda mrefu baada ya kusilimu kwake, akafa.
Bwana Mtume Rehema na amani zimshukie akapelekewa khabari za kifo cha Mfalme
huyu na Malaika Jibrilu amani ya Allah imshukie kwa amri ya Mwenyezi Mungu
Mtukufu. Baada ya kupata khabari hizi, Bwana Mtume aliwakusanya maswahaba na kumswalia
marehemu mfalme huyu swala ya maiti ghaibu na huo ulikuwa ni mwaka wa saba wa utume.
Ama tukirejea nyuma kuwaangalia maswahaba wa Mtume, wakimbizi waliopata amani,
utulivu, ulinzi na usalama pia haki na uhuru wa kuabudu katika nchi hii ya ughaibuni,
waliendela kuishi katika nchi hii baada ya kupata baraka zote za mfalme na hasa pale
alipowarejesha maadui zake Makkah mikono mitupu. Hakuna hata mtu mmoja kati yao aliyerejea
Makkah ila Bwana Uthman Ibn Affaan, kwani yeye baada ya kuhakikisha kuwa waislamu wako
katika hali ya amani na salama alirejea Makkah pamoja na mkewe Rukia binti aya Mtume ili
kwenda kusaidiana na Mtume katika kuieneza daawah ya Uislamu. Ama wahamiaji wengine
wote waliendela kuishi ugenini uhabeshi kwa kipindi cha muongo mmoja (takriban miaka kumi
na moja). Hii ni kwa mujibu wa watalamu wa sera na tarekh. Hawakurudi mpaka Bwna Mtume
alipohamia Madinah na kurudi kwao ilikuwa ni baada ya mkataba wa suluhu ya Hudaibiyah
baina ya Makurayshi na Bwana Mtume
|