|
i) HALI YA KIDINI KATIKA BARA ARABU KABLA YA UISLAMU
Kabla ya kudhihiri kwa Uislamu Bara arabu halikuwa na dini moja
bali lilisheheni dini nyingi. Baadhi ya wakazi wake walikuwa wakifuata dini ya Nabii Musa
nao ni mayahudi na wengine waliifuata dini ya Nabii Isa, nao ni Manasara. Mbali na hawa
walikuwepo pia waliokuwa wakiyaabudia masanamu. Qur-ani Tukufu imeyataja baadhi ya
masanamu yaliyofanywa miungu kama vile Laata,Uzzah, Yaghuuth, Yauuqa na Nasrah. Kadhalika
lilikuwepo kundi dogo lililokuwa likifuata dini ya haki likimuabudu mola wa haki kupitia
mafundisho yaliyoletwa na Nabii Ibrahimu kutoka kwa Mwenyezi mungu.
Mwenyezi Mungu Mtukufu alipompa utume Muhammad na kumpa kazi nzito na jukumu kubwa la
kutangaza dini ya Kiislamu aliinuka na kuanza kuwalingania watu wamuabudu Mungu mmoja
asiye na mshirika na waache kuyaabudu masanamu waliyoyatengeneza wao wenyewe. Jawabu la
Maquraysh lilikuwa ni kumkadhibisha Mtume na kumpinga vikali sana. Isitoshe walimuadhibu
adhabu kali sana kila aliyemuamini na kumfuata Mtume ili iwe ni onyo kwa wengine.
Hawakukomea hapo tu bali waliwazuia watu kuonana na kumsikiliza Mtume lakini kwa sababu ya
subira, jihadi, imani yake na msaada wa Mwenyezi Mungu alifanikiwa kuwashinda maadui wa
Uislamu na kuieneza dini ya Mwenyezi Mungu miongoni mwa Waarabu na watu wa mataifa
mengine.
ii) IBADA YA MASANAMU
Kabla ya Uislamu waarabu walizama mno katika ibada ya masanamu
mpaka wakaijaza Al-Kaaba masanamu ambayo idadi yake ilifikia masanamu mia tatu na sitini
(360). Kila kabila lilikuwa na sanamu lake pekee na kila kaya/familia ilikuwa na sanamu
malum kwa ajili ya familia hiyo tu. Mtu alipotaka kusafiri, alilichukua safarini sanamu
moja ilikufanikiwa safarini na walikuwa wakiyatakasa na kuyatukuza masanamu haya kiasi cha
kuyatolea Qurubaani na dhabihu (sadaka za kuteketeza). Waarabu walipokuwa wakitaka ushauri
katika mambo yao mfano ndoa, biashara au safari basi uliendea "Hubal" sanamu
lililokuwa ndani ya Al-kaaba wakampa ngamia na dir-ham mia mshika kete ambazo moja ilikuwa
imeandikwa juu yake maneno"Mungu wangu amenikataza" na ya pili "Mungu wangu
ameniamrisha" ya tatu "Naam/Ndiyo" ya nne "Hapana". Jumla kete
zilikuwa ni saba, mshika kete huzizungusha na kuzichanganya kisha akaitoa moja na
kilichoandikwa juu yake ndio huwa amri iliyotoka kwa Mungu sanamu.
|