|
Baada ya jitihada na juhudi kubwa aliyoifanya Bwana Mtume-Rehema na
Amani zimshukie- kugonga mwamba na kushindwa kuwakomboa makurayshi walio wengi kutoka
katika viza vya ushirikina kuja katika nuru ya Uislamu Bwana Mtume akayakinisha kuwa
makurayshi wataendelea kubakia katika lindi la kufru na upinzani kwa kipindi kiruefu na
kwamba hawatamuabudu Allah pekee asiye na mshirika mpaka awaletee adhabu kutoka kwake au
kupitia mikono (nguvu) ya waumini. Hapo ndipo Mtume alipowapa mgongo na kungojea
adhabu/hukumu ya Mwenyezi Mungu. Akaazimia sasa kuzielekeza, nguvu zake kwa watu wa
makabila mengine. Watu wa mwanzo aliowafikiria Bwana Mtume baada ya makarayshi ni watu wa
kabila la Thaqiyfy waliokuwa wakiishi Twaif. Twaif huu ni mji uliopo kusini mashariki ya
mji wa Makkah. Sababu iliyompelekea Mutme kuwapa watu wa Twayfu umuhimu wa pili baada ya
Makurayshi, kuhodhi nafasi ya kwanza ambayo hawakuienzi ni ule udugu uliokuwepo baina yake
na wao. Hapa ni vema ikakumbukwa kwamba Bwana Mtume alinyonyeshwa na Bi Halimah mkazi na
mwenyeji wa kitongoji cha Baniy Saad ambacho ni miongoni mwa vitongoji vinavyounda
mji huu wa Twayf. Kwa hivyo utaona watu wa Twaif kwa kigezo hiki cha Mtume kunyonya kwao
wanazingatiwa kwa mujibu wa sheria kuwa ni wajomba zake Mtume ujomba wa kunyonya, basi wao
ndio ndugu zake wa karibu zaidi baada ya makurayshi.
Tukizipekua kurasa za historia tutaona ni namna gani
mzungumzaji/msemaji wa watu wa Twaif alivyoutumia undugu huu kumlainisha Mutme na
kumshinikiza awaonee huruma na kuwaachia huru mateka wa vita vya Hunayn. Miongoni mwa
aliyoyasema ilikuwa
Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, hakika miongoni mwa mateka
hawa wamo shangazi, na wajomba zako waliokulea. Tumekulea na kukunyonyesha kwa hivyo sisi
pamoja na yote haya yaliyotokea ni wazee na jamaa zako,
Kwa hiyo maumbile ya undugu huu yakamsukuma Bwana Mtume kwenda Twaif
kuwalingania ndugu zake hawa dini ya haki na wampe hifadhi na wamsaidie katika kuufikisha
ujumbe huu wa Mola wake baada ya makurayshi kuukataa na si kuukataa tu bali kumpiga vita
vikali kabisa. Hivyo ndivyo alivyofanya Mtume akatoka katika mwezi wa Shanwal (Mfunguo
Mosi) wa mwaka wa kumi wa utume yaani tangu kupewa utume kuelekea Twaif kutafuta hifadhi
na msaada kwa watu wa huko. Kuna umbali wa zaidi ya maili mia moja na ishirini (120
miles). Mwendo wa miguu wakati huo ni kiasi cha siku nne mchana na usiku kutoka Makkah
mpaka kufika Twaif, baina ya milima na mabonde. Bwana mtume aliongozana katika safari yake
hii yenye kuchosha na mtumishi wake Zayd Ibn Haarithah. Tukirejea nyuma kidogo kuuangalia
mji wa Twaif katika uwanja wa dini/itikadi tutaukuta hauko mbali sana na hali ya mji wa
Makkah. Wakati ule Twaif ndio yalikuwa makao makuu ya ibada kongwe ya "Laata.
Laata hili ni sanamu lililkuwwa likiabudiwa, kuadhimishwa na kuchukuliwa kama mungu muweza
mwenye nguvu. Watu wa kabila la thaqiyfa walilijengea sanamu hili nyumba maalumu ya ibada,
wakienda kuliabudia humo na kuifananisha nyumba yao hiyo na Al-Kaabah tukufu na kulifanya
eneo lililoizunguka nyumba hiyo kuwa na eneo takatifu kama lile linaloizunguka Al-Kaabah.
Makurayshi na waarabu wote walikuwa wakilitukuza na kuliadhimisha sana sanamu hili
Laata kama walivyokuwa wakiliabudia na kuliadhimisha Hubali sanamu
kubwa kuliko yote yaliyokuwamo ndani ya al-Kaaba. Mwenyezi Mungu anayataja masanamu haya
ndani ya Qur-ani. JE MUMEWAONA LAATA NA UZZAH NA MANATA (Mungu wenu) MWINGINE WA
TATU (Kuwa ndio waungu hao badala ya Allah)? (53: 19 20)
Thaqifu na Makurayshi walijuwa na mafungamano na mahusiano mazuri ya
kidipomasia ya muda mrefu. Thaqiyfu walifanya kila njia ili kuudumisha na kuuimarisha
uhusiano wao huu na walikuwa wakifuatilia kwa makini suala la daawah ya Mtume kwa
makurayshi na namna Makurayshi walivyoipokea daawah hii. Alikuwa wakijua kuwa
Makurayshi wanaihami miungu yao kwa nguvu zao zote ili kulinda heshima, hadhi na maslahi
yao mbele ya waarabu wenziwao kadhalika Thaqiyfu walikuwa wanachelea kuanguka kwa hadhi na
uungu wa Mungu wao sanamu. Laata ikiwa wataukubali uislamu walioletewa na
mwana wao wa kunyonyoa Nabii Muhammad na zaidi ya hayo walikuwa wakichunga uhusiano wao na
Makurayshi usivunjike kwa kukikubali kile kisichotakiwa na jirani zao makurayshi kwa
sababu yo yote ile iwayo Thaqiyfu hawakuubali ujumbe wa Mtume na wala hawakumpa mapokezi
mazuri ya kidugu. Bwana Mtume Rehema na Amani zimshukie alikaa Twaifu kwa kipindi
kisichopungua siku kumi katika kipindi hiki hakumsaza yeyote miongi mwa viongozi na
watukufu wa kabila hili la Thaqiyfu ila alimuelezea habari za uislamu na kumtaka ampe
hifadhi na msaada ili aweze kuufikisha ujumbe aliokuja nao kutoka kwa Mola wake. Lakini
kwa masikitiko makubwa hapana hata mtu mmoja wa Twaifu aliyemuitika na kumuamini Bwana
Mtume, si mwanamume wala mwanamke, na si muungwana wala mtumwa, na si mtukufu wala
mnyonge, kama kwamba wote hawa walikongamana juu ya hili. Mtume akaamua kurejea kule kule
Makkah kutoka Twaifu akiwa amehuzinishwa sana na kuvunjwa moyo na watu wa Twaifu
aliowategemea na kuwapa umuhimu na nafasi ya pila baada ya makurayshi. Watu wa Twaifu
hawakukomelea kuukataa ujumbe wa Mutme tu bali walimfanyia mzaha na masikhara na zaidi ya
yote hayo walimpopoa kwa mawe. Katika kukaa kwake Twaif, Bwana Mtume aliwaendea watoto wa
Amri Ibn Umayr Ibn Auf ambao ni Abdu Yaa Layl na nduguze Mosoud na Habiyb, hawa walikuwa
ni miongoni mwa mabwana wakubwa wa kabila la Thaqiyfu. Mtume akawaelezea juu ya ujumbe
aliotumwa na Mwenyezi Mungu kuwafikishia na akawaomba wampe hifadhi ili aweze kuitekeleza
kazi yake hiyo. Mtume hakuambulia cho chote kutoka kwa mabwana hawa zaidi ya dhihaka na
maskhara, aliambiwa na mmoja wao. Hivi huyo Mungu hakupata mtu wa kumtuma ila wewe
tu!". Maneno haya na mengine mabaya zaidi kuliko haya yaliikata kabisa tamaa ya Mtume
alivyokuwa nayo juu ya watu wa Twaif kuwa huenda wakamkubali na kumuamini Mtume akafukuzwa
na Thaqiyfu kutoka Twaif, akaambiwa. Ewe Muhammad, ondoka katika mji wetu na nenda
mji mwingine uutakao usije ukawasumu na kuwalaghai vijana wetu wakufuate katika dini yako
hiyo. Baada ya kuambiwa hivyo, Bwana Mtume akawa hana uchaguzi wala uamuzi ila
kuondoka mjini kwa watu. Kama ambavyo Thaqiyfu hawakumpa Mtume mapokezi mazuri alipowasili
kwao ndivyo hivyo walivymsindikiza wakati alipokuwa akitoka mjini kwao. Kwani walimsakizia
na kumtomezea watumwa wao, watoto na wendawazimu wamtukanae na kumzomea. Watu
wakamjongelea njiani, wakajipanga safu mbili, huku na huku, Mtume alipopita wakaanza
kumpopoa kwa mawe. Ikawa Mutme hainui hatua ila alipigwa na jiwe, mpaka miguu yake ikawa
inavuja damu na viatu vyake vikarowa damu chapa chapa. Mvua ya mawe ilipomzidia alikaa
chini, wakamfuata na kumuinua, akianza kutembea wanampopoa tena huku wakicheka. Hakukuwepo
na ye yote wa kumsaidia katika wakati huu mgumu zaidi ya mtumishi wake Zayd Ibn Haarithah
Allah amuwiye radhi. Lakini atafanya nini Zaydi mmoja, peke yake mbele ya kundi la
majahili hawa? Alichochofanya Zaydi ni kujigeuza yeye mwenyewe kuwa ni ngao ya kumkinga
Bwana na Mtume wake, lakini wapi akimkinga huku, anapigwa kule na yeye mwenyewe akipigwa
vile vile mpaka akapasuliwa ngeu nyingi za kichwa. Mtume akaenda hivyo hivyo na mtumishi
wake mpaka alipoufikilia ukuta/uzio wa bustani ya wawili Utbah na Shaybah, Ibn Rabiah,
akajibanza hapo na wale maadui wakashika njia kurudi Twaif baada ya kuitosheleza kiu yao.
Mtume akakaa chini ya mzabibu mmoja bustanini mle kuvuta pumzi kisha Mtume aliinuka na
kuswali kama ilivyokuwa ada yake anapopatwa na jambo kubwa kama hilo alipomaliza kuswali
ndipo alipoinua mikono yake na kuielekeza mbinbuni na kuomba ile dua yake ijulikanayo kama
Dua ya Twaifu: akasema: Ewe Mola wa haki wee! Ninaushitakia kwako udhaifu wa
nguvu zangu, na uchache wa mbinu zangu na unyonge wangu kwa watu, ewe Mwenye kurehemu
zaidi kuliko wenye kurehemu wote! Wewe ndiye Bwana Mlezi wa wanyonge wote na wewe ndiwe
Bwana Mlezi wangu pia. Unaniweka mikononi mwa nani, kwa mtu wa mbali anayenichukia au kwa
adui uliyemmilikisha suala langu? Ikiwa hukinighadhibikia, basi mimi sijali (haya
yayonipata) lakini kuniepusha kwako na mabalaa/maafa kuwe na ukunjufu zaidi kwangu.
Ninajilinda kwa nuru ya dhati yako ambayo imeviangazia viza na kutengenea kwayo masuala ya
kidunia na akhera (ninajilinda) na kunishukia ghadhabu yako. Radhi ni zako mpaka uridhie
na hapana hila wala nguvu ila kwako tu!! Mandhari na hali hii aliyokuwa nayo Mtume
iliziathiri nyoyo za wamiliki wa bustani hii, ndugu wawili Utbah na Shaybah watoto wa
Rabiah, wakamuonea huruma. Wakamtuma mtumishi wao aliyekuwa akiitwa Adaasi
kumpelekea zabibu. Adaasi alimpelekea zabibu, Adaasi alipompa Mtume Zabibu alizopewa na
mabwana wake, Mtume alipokea na kumshukru, kisha akasema.Bismillahir Rahmaanir
Rahiym na kuanza kula Adaaasi akashangazwa sana na jambo hili akamtazama Mtume na
kumwambia. Wallah! Maneno haya uliyoyatamka hayasemwi kabisa na watu wa mji huu
(wakati wa kula)". Bwana Mtume akamuuliza. Wewe ni mtu wa wapi? Adaasi
akajibu. Mimi ni mnasara wa niynawaa. Mtume akamwambia "unaotoka katika
mji wa yule mtu mwema Yuunus Ibn mattaa? Adaasi akamuuliza Mtume: Umemjuaje Yuunus
Ibn Mattaa. Wallah! Nilitoka niynawaa kukiwa hakuna hata watu kumi wanaomjua mtoto wa
Matta (Yuunus). Mtume akamjibu huyo ni ndugu yangu, yeye alikuwa Mtume na mimi ni
Mtume. Kusikia hivyo Adaasi akamvamia Mutme na kuanza kumbusu kichwani, mikononi na
miguuni. Wakati hayo yote yakitendeka, wamiliki wa bustani walikuwa wakiangalia, mmoja wao
akamwambia nduguye. Wallah! Amekwishatuharibia kijana wetu. Adaasi aliporejea
wakamwambia. Ole wako ewe Adaasi! Kwa nini unakibusu kichwa, mikono na miguu ya mtu
yule? Adaasi akawajibu. Wallah! hakuna katika ardhi mtu bora kuliko huyu!
Amenieleza jambo asilolijua ye yote ila Mtume (Mtu) wakazidi kumwambia Ole wako ewe
Adaasi! Angalia asije akakutoa katika dini yako kwani dini yako ni bora kuliko dini
yake". Wapokezi wa riwaya hii wanasema kuwa Adaasi alisilimu na kwamba anahesabiwa
kuwa ni miongoni mwa maswahaba wa Bwana Mtume
Naam, siku ile ilikuwa ni siku ngumu mno katika historia ya maisha ya
Mtume kutokana na yaliyomsibu kutoka kwa watu hawa wa kabila la Thaqiyfu. Akiwa katika
hali ya kulitafakari hili alijiwa na malaika Jibril Amani imshukie na kumwambia hakika
Mwenyezi Mungu ameniamrisha nikutii kwa ulitakalo nikufanyie kwa watu hawa kutokana na
waliyokutendea. Mtume akamjibu kwa kusema; Ewe Mola wangu waongoze watu wangu kwani
wao hawajui. Jibril akasema, Amesema kweli aliyekuita mpole mwenye huruma. Mtume
alipokuwa njiani kurudi Makkah, akafika sehemu moja inayoitwa Nakhlah usiku,
akawa anaswali na kusoma Qur-ani. Hapo ndipo likampitia kundi la majini wakavutwa na
Qur-ani aliyokuwa akusoma Mtume, wakakaa kimya kusikiliza kisha wakarejea kwa ndugu zao
kuwaelezea habari za Mtume hebu tuipe fursa Qur-ani tu isimulie hali ilivyokuwa "NA
(wakumbushe) TULIPOKULETEA KUNDI LA MAJINI (kuja kwako) KUSIKILIZA QUR-ANI BASI
WALIPOIHUDHURIA WALISEMA (kuambiana) NYAMAZENI (msikilizeni maneno ya Mwenyezi
Mungu), NA ILIPOKWEISHA (Somwa) WALIRUDI KWA JAMAA ZAO WAKIWAONYA WAKASEMA.
ENYI WATU WETU! HAKIKA TUMESIKIA KITABU KILICHOTEREMSHWA BAADA YA MUSA,
KINACHOSADIKISHA YALIYOKUWA KABLA YAKE NA KINACHOONGOA KATIKA HAKI NA KATIKA NJIA
ILIYONYOOKA. ENYI WATU WETU! MUITIKIENI MLINGANI (muitaji) WA ALLAH NA MUMUAMINI,
ATAKUSAMEHENI (Allah) MADHAMBI YENU NA ATAKUKINGENI NA ADHABU IUMIZAYO NA WASIOMUITIKIA
MLINGANI WA ALLAH, BASI WAO HAWATAMSHINDA (asiwapate) HAPA KATIKA ARDHI, WALA HAWATAKUWA
NA WALINZI MBELE YAKE. HAO WAMO KATIKA UPOTOFU ULIO DHAHIRI" (46:29 32)
Bwana Mtume Rehema na Amani zimshukie akakaa pale Nakhlah siku tatu
akipanga mikakati ya namna ya kuingia tena Makkah baada ya habari zake za Twaifu kufika
huko. Mtume alipotaka kuingia Makkah akazuiliwa mpaka alipopata dhamana ya Mutw-im Ibn
Adiyyi. Mtume akaingia tena Makkah kuendelea na kazi yake ngumu chini ya udhamini wa Bwana
huyu.
|