|
Baada
ya safari ya Twaif, Bwana Mtume
- Rehema na Amani zimshukie - alirejea Makkah na kuuwahi msimu wa Hijja.
Makabila mbalimbali ya waarabu kutoka pande mbalimbali huja Makkah katika
msimu huu kutekeleza ibada ya hijja na kutekeleza nadhiri zao kwa miungu
masanamu sambamba na dhabihu zao (sadaka za kutekeleza) Ilikuwa ni ada ya
waarabu wanapofika Makkah katika msimu huu wa hijjah, kuitumia vema fursa ya
miezi mitukufu ya Hijjah kwa kufanya
biashara katika masoko ya Makkah. Masoko
mashuhuri yalikuwa ni matatu, ambayo ni ukaadhwi, Majannah na Dhul
- Majaaz.
Waarabu
walikuwa wakianza na soko la ukaadhwi
katika mwezi wa Dhul-qa'adah (mfunguo pili) wakikaa hapo siku kumi. Kisha
huelekea katika soko la Majannah ambako pia hufanya biashara kwa siku kumi.
Halafu wakiuona mwezi muandamo wa Dhul-hijjah (mfunguo tatu) hao hushika
njia na kuelekea katika soko la Dhul-Majaaz na soko
hili ndilo lililokuwa karibu zaidi na Makkah. Hufanya biashara hapo
kwa siku nane tu, kisha huelekea
arafu kutekeleza ibada ya Hijjah.
Baada
ya kupita muongo mmoja wa da'awah, yaani ile miaka kumi ambamo Bwana Mtume
alikuwa akiwalingania jamaa zake uislamu kwa njia ya
upole na ulaini. Aliazimia sasa kubadili mtindo/mbinu ya da'awah,
kwa kuzielekeza nguvu zake katika masoko
haya ya msimu ambako
huko angekutana na watu kutoka sehemu mbalimbali na kuwafikishia
ujumbe wa Allah. Makurayshi baada ya kuijua azma hii ya Mtume,
wakapanga njama za pamoja ili kuitia doa da'awah hii na hatimaye kuibomoa
kabisa, mbele ya kadamnasi ya makabila haya. Mwanasira mkubwa; Ibn Is-haaq
- Allah amrehemu - anaelezea katika kulisimulia hili - "kwamba kundi
la makurayshi lilimkusanyikia Al - waleed Ibn Al - Mughiyrah, huyu alikuwa
ni mtu mzima wao nae alikuwa amefika kwenye msimu. Akawaambia enyi
Makurayshi, msimu ndio ushafika tayari na ujumbe (makundi) wa waarabu
utakujieni. Watu hawa wameshalisikia
suala la ndugu yenu
huyu (Muhammad na dini yake). Sasa kongamaneni kwa rai moja tu (juu ya
hili) na wala msitofautiane ikawa hawa wanakadhibisha wale na kujibizana wenyewe kwa wenyewe. Wakasema; Ewe Baba Abdi
Shamshi sema wewe, tuambie wewe tuseme nini. Akawajibu; semeni nyinyi,
mimi nitakusikilizeni wakasema; basi tuseme yeye kuhani. Akawaambia;
Wallah! Hapana yeye si kuhani.
Tumewaona Makuhani hawako kama yeye. Wakasema; basi tuseme ni mwendawazimu.
Akawaambia; yeye si mwendawazimu, tumekwishauo na kuujua
wazimu, yeye hana wazimu. Wakasema basi tuseme ni mshairi.
Akawaambia; yeye si mshairi, sisi tunaujua ushairi na fani zake zote,
maneno ayasemayo si ushairi hata kidogo. Wakasema; basi tuseme
ni mchawi. Akawaambia; Wallah ! kwa hakika maneno yake ni matamu
sana yenye kuvutia. Hamtosema
lolote kati ya yote haya mliyoyataja ila itajulikana kuwa ni uongo. Kauli
ya karibu zaidi semeni; yeye ni mchawi, ameleta maneno ambayo yenyewe ni
uchawi, humtenganisha kwa maneno hayo mtu na mwanawe, na baina ya mtu na
mkewe na baina ya mtu na ndugu zake! wakatawanyika na kauli hii, wakawa
wanawangojea watu majiani wanapokuja msimuni, hawapitii mtu yeyote ila
humtahadharisha juu ya Mtume na kumuelezea khabari zake".
Tusome
na tuwaidhike tukitaka; (BASI
NDIVYO HIVI HIVI, HAKUNA MTUME YEYOTE ALIYEWAJIA WALE WA KABLA YAO (hawa
Makurayshi) ILA WALISEMA; "HUYU NI MCHAWI AU MWENDAWAZIMU" JE!
WAMEUSIANA KWA (jambo) HILI? (La, hawakuusiana chochote) LAKINI (wote) WAO
NI WATU WAOVU) (51: 52 - 53)
Makurayshi
wakawa wanamfuata Bwana Mtume Rehema na Amani zimshukie - kila alipokwenda
kila alipoliendea kabila miongoni mwa makabila yaliyofika msimuni
kulifikishia ujumbe wa Allah, huja Mkurayshi mmoja akasimama mbele yake na
kuwatahadharisha dhidi ya uchawi na vitimbi (hila) za Muhammad, kama
walivyoona wao. Mara nyingine wakimtuhumu kuwa ana wazimu, wakati mwingine
wakisema ni muongo mzandiki na pengine huibuka na kusema, kuwa ni mchawi
kwa kuwa Makurayshi walikuwa na hadhi na wakikubalika mbele ya waarabu
wote, maneno yao haya yalipokewa kwa uzito mkubwa na wageni wao hawa na
kuathiri kwa kiasi kikubwa kazi ya Mtume. Miongoni mwa athari zilizoletwa
na uzushi huu wa Makurayshi ni watu kumpuuza Mtume na alichokisema na
kukataa kuitikia haki iliyo wazi. Lakini yote haya, hayakumzuia Bwana
Mtume kuendelea kuyafuata makabila na kuyafikishia ujumbe bila kujali
upinzani wa Makurayshi. Mtume alifanya hivyo huku akiamini kuwa haki
itashinda tu hata kama itachukua muda mrefu na kwamba nusra ipamoja na
subira, faraja imo ndani ya shida/matatizo na wepesi umo ndani ya uzito.
Msimu
huu ukapita bila ya mafanikio yoyote Msimu uliofuatia, lilifika Makkah
kundi la kabila la Khazraji. Kundi hili likamsikia Mtume akiufikisha
ujumbe kwa makabila, wakaziona alama na dalili za ukweli katika yale
aliyokuwa akiyasema. Wakaambizana; "Wallah! Huyu ndiye Mtume ambaye
Mayahudi walikuwa wakikutisheni nae, basi wasikutangulieni kumuamini".
Mtume alipowafikishia ujumbe tu, mara moja wakamuamini na kumsadiki na
wakataraji kuwa Mwenyezi Mungu ataleta suluhu baina yao kwa sababu ya
Mtume huyu, wakamwambia Mtume; "Hakika sisi tumeiacha kaumu yetu,
hakuna kaumu yenye uadui na shari baina yao kuliko kaumu yetu, huenda,
Mwenyezi Mungu akawaunganisha kwa ajili yako. Tutawaendea na kuwafikishia
ujumbe wako na kuwaelezea juu ya dini hii tuliyoifuata. Ikiwa Mwenyezi
Mungu atakukusanyia watu hawa, basi hapatakuwa na mtu mtukufu kuliko wewe.
Wakaagana na Mtume kukutana nae msimu wa mwaka ujao. Kisha wakaondoka
kurudi kwao Madinah wakiwa wamemsadiki na kumuamini Mtume. Walipofika kwao
Madinah, walieleza jamaa zao habari za Mtume na kuwalingania Uislamu mpaka
habari hizi zikaenea mji wote wa Madinah. Hapakuwa na nyumba yoyote ya
Maanswaari ila Mtume alitajwa humo. Huu ndio mwanzo wa kuingia Uislamu
Madinah wakati huo mji ulikuwa ukiitwa "Yathribu" Darsa/somo
hili halitakamilika ikiwa hatukuwataja na
kuwakumbuka vema watu
hawa na mwanzo kutoka
Yathribu walioupokea kwa mikono miwili ujumbe wa Mtume wakamuamini na kuwa
mabalozi wema wa Uislamu huko kwao Yathribu "Madinah".
Kumbukumbu za kihistoria zinaonyesha kuwa watu hawa walipata sita na wote
ni wa kabila la Khazraji. Watu hao ni:-
1.As'ad Ibn Zaraarah, na
2.Auf Ibn Al- Haarith. Wote hawa ni wa ukoo wa Najjar.
3.Raafii Ibn Maalik wa ukoo wa Zariyq
4.Qutwbah Ibn Aamir wa ukoo wa Salamah.
5.Uqbah Ibn Aamir wa ukoo wa Hiraam na
6.Jaabir Ibn Abdillah wa ukoo wa Ubayd Ibn Adiyyi - Allah awawiye
radhi wote
|