|
Msimu
uliofuatia wa Hijjah, Uislamu ulikuwa tayari umeenea kwa kiasi kikubwa
katika mji wa Yahrib (Madinah). Katika kundi kubwa la Mahujaji kutoka
Yathrib lililowajumuisha pamoja waislamu na mushrikina, walikuwemo
waislamu sabini na tatu, miongoni mwao wakiwemo wanawake wawili. Mtume
Rehema na Amani zimshukie akapanga kukutana na ujumbe huu kutoka Yathrib
“Aqabah” usiku. Akawaagiza kutokufanya harakati zozote zitakazowafanya
mushrikina waliokuja nao kuhisi kitu. wasije kama kundi, bali mtu mmoja
mmoja au wawili wawili na waje baada ya kupita theluthi ya kwanza ya usiku
yaani baada ya saa nne usiku na kwamba wasimsubiri asiyepo na wala
wasimuashe aliyelala.
Swahaba
Kaa’abu Ibn Maalik Allah amuwiye radhi, analisimulia tuko hili zima la
maagano ya pili ya “Aqabah”, anasema: --- Kisha tukatoka kwenda kuhiji
na tukaagana na Mtume wa Allah Rehema na Amani zimshukie kukutana
“Aqabah” katika masiku ya kuanika nyama {Ayyaamut tashriyq}.
Tulipomaliza kuhiji, na ukawa uwewadia ule usiku wa maagano yetu na Mtume
wa Allah. Akaendela kusema: Usiku ule tukalala pamoja na jamaa zetu katika
makambi yetu mpaka ilipopita theluthi ya usiku. Tukatoka makambini mwetu
kwenda katika maagano yetu na Mtume wa Allah Rehema na Amani zimshukie.
Tukatoka kwa uficho mkubwa mpaka tukakutana na Mtume pale “Aqabah”
nasi tukiwa watu sabini na tatu pamoja na wanawake wawili. Akaendelea
kusema: Tukakusanyika pale tukimngojea Mtume wa Allah Rehema na Amani
zimshukie mpaka alipotujia akiwa pamoja na ami yake Abbaas Ibn Abdul
Mutwallib. Wakati huo alikuwa bado hajasilimu, ila alipendelea tu
kuhudhuria suala la mwana wa nduguye. Mtume alipokaa, mzungumzaji wa
mwanzo akawa ni Abbaas, akasema: “Enyi kusanyiko la Khazraji, bila shaka
mnatambua Muhammad alivyo kwetu. Sisi tumemkinga na madhara ya ndugu zetu
wenye msimamo kama wetu kwake. Kwa hiyo yeye anaishi katika utukufu wa
jamaa/ndugu zake na ulinzi katika nchi yake. Nae ameyakataa yote hayo na
kutaka kujumuika na kujiunga nanyi. Sasa iwapo nyinyi mnaona mnaweza
kumtekelezea mnayomuitia na mtamlinda dhidi ya wapinzani wake, basi hilo
ni jukumu lenu mnalibeba. Na ikiwa nyinyi mnaona mtamsaliti na kuacha
kumnusuru baada ya kwenda nae huko kwenu, basi muacheni kuanzia sasa
hivi”. Baraau Ibn Al-ma’aruwr (akasimama) na kusema: “Hakika sisi,
wallah! Lau lingekuwemo mioyoni mwetu tusilolitamka basi tungelilisema tu,
sisi tunachotaka ni ukweli na utekelezaji ahadi na kumwaga damu zetu kwa
ajili ya Mtume wa Allah Rehema na Amani zimshukie sema tu ewe Mtume wa
Allah, shurutiza ulitakalo kwa nafsi yako na kwa ajili ya Mola wako, nasi
tutakupa ahadi ya utii.”
Mtume
wa Allah Rehema na Amani zimshukie akazumgumza kwanza akawaraghibishia
uislamu, halafu ndipo akasema: “Nipeni ahadi kuwa mtanisikiliza na
kunitii na mtaamrisha mema na kukataza maovu. Mtailingania dini ya Allah
bila kuogopa lawama ya anayewalaumu na kwamba mtaninusuru na kunilinda
nitakapokuja kwenu, kama mnavyojilinda wenyewe, wake zenu na wana wenu,
nanyi mtapata pepo.” Akaendelea
kusema: Baraau Ibn Al-ma’aruwr akaushika mkono wake (Mtume) na kusema:
“Naam, ninamuapia yule aliyekutuma kwa haki, fanya maagano nasi, wallah
sisi ni wana wa vita na watu wa silaha, haya tumeyarithi kizazi hadi
kizazi.
Akaendela
kusema: Abul-haytham Ibn Tayihaan akamkata kauli Baraau, akasema: Ewe
Mtume wa Allah, hakika sisi tuna ahadi/mkataba na mayahudi, nasi
tunaivunja kwa ajili yako. Sasa isije ikawa huku sisi tumevunja ahadi,
nawe Allah akakupa ushindi, ukarejea kwenu na kutuacha! Akasema: Mtume wa
Allah Rehema na Amani zimshukie akatabasamu na kusema: “Bali damu kwa
damu! Mimi ni katika nyinyi nanyi ni katika mimi, nitapigana na
mnayepigana nae na nitampa amani mtakayempa amani.”
Ka’ab
akasema: Mtume wa Allah Rehema na Amani zimshkie akasema: “Nipeni
miongoni mwenu wadhamini kumi na mbili ili wawe wachunga/wakubwa wa jamaa
zao.” Wakampa watu hao kumi na mbili, tisa kutoka katika kabila la
Khazraji na atatu kutoka Ausi. Mtume akawaambia wale wadhamini/wakubwa:
“Nyinyi ndio wakubwa wa jamaa zenu, kama walivyokuwa wafuasi wa Issa Ibn
Maryam, nami ni mkubwa kwa jamaa/watu wangu.” wakasema: Naam. Wakasema:
Kunjua mkono wako, Mtume akaukunjua nao wakampa ahadi ya utiifu. Kisha
Mtume akawaambia: “Rejeeni makambini mwenu”. Akaendela kusema:
Tukararejea makambini mwetu na kulala mpaka asubuhi. Kulipokucha wakatujia
viongozi wa Makurayshi, wakatuambia: “Enyi jamaa Makhazraji, imetufikia
khabari kwamba nyinyi mmemjia mwenzetu huyu {Muhammad} mumchukue na mmempa
ahadi ya utii kupigana nasi. Wallah! sisi tunachukia kupigana nanyi.
Akaendela kusema: Wakainuka jamaa zetu mushrikina wakaapa na kusema hakuna
jambo kama hilo na wala hatulijui! Akasema: Wakasadiki {Makurayshi} kwa
jinsi wanavyotujua, nasi tukawa tunaangaliana wenyewe kwa wenyewe”.
Haya
ndiyo maagano ya pili ya “Aqabah” yaliyotokea katika mwaka wa kumi na
tatu wa utume. Maagano haya yalikuwa na taathira kubwa katika historia
nzima ya da’awah ya Kiislamu. Maagano haya baina ya Mtume wa Allah
Rehema na Amani zimshukie na maanswari Allah awawiye radhi yalitia
matumaini mioyoni mwa waislamu wanyonge waliokuwa wakiteswa na kuadhibiwa
Makkah kwa sababu tu ya kumkubali Mwenyezi Mungu mmoja asiye na mshirika,
tusome: “NAO HAWAJAONA BAYA LOLOTE KWAO (Waislamu) ILA KUMUAMINI ALLAH
MSHINDI (na) MWENYE KUSIFIWA. “[85:8] wakawa na yakini kwamba nusura ya
Mwenyezi Mungu i karibu. Maagano haya yakawa ni faraja kwa upande wa
waislamu na pigo kubwa upande wa Makurayshi. Maagano haya yalikuwa ni
tukio lisilotazamiwa kabisa na makurayshi, kwani wao waliamini kwamba
wamshamdhibiti kabisa Bwana Mtume. Waliweka mikakati kuhakikisha kuwa
da’awah ya Mtume haivuki majabali ya Makkah na kutoka nje ili isije
ikawaathiri Waarabu wengine na Mtume akapata nguvu. Walipotambua kwamba
Ausi na Khazraji, wenyeji wa Madinah wamemfuata Mtume na wamempa ahadi ya
utii juu ya kumnusuru na kumlinda dhidi ya wapinzani wake, habari hii
ilizigonga nyoyo zao na kuwatetemesha, akili ikawatoka. Wakaanza
kuwatafuta Maansari na kuwasihi wayavunje maagano haya ambayo ni hatari
machini mwao, lakini wapi, hayawi hayawi hayo wayatakayo: “HAKI
IKASIMAMA NA YAKAHARIBIKA WALIYOKUWA WAKIYATENDA KWA HIVYO WALISHINDWA
HAPO NA WAKAWA WENYE KUDHALILIKA.” [7:118-119]
Kadhalika
maagano haya yakawa ni mpaka wa upambanuzi baina ya vipindi viwili vya
da’awah kipindi cha majaribio na mtihani, hiki ndicho kilichokuwa
kipindi cha kwanza, kipindi walichokipitia waislamu Makkah. Kipndi cha
uchache, unyonge na adhabu na mateso yasiyovumilika ila na mtu mwenye
imani ya kweli na yakini thabiti. Haya yote yalikuwa ni maandalizi ya
kuwaandaa kuwa mfano wa kupigwa juu ya imani ya kweli ambayo Mwenyezi
Mungu aliwataka waineze katika ardhi. Walipofaulu mtihani huu na kuonekana
ukweli na nguvu ya imani yao ndipo kikaja kipindi cha malipo na jazaa ya
subira na uvumilivu, Mwenyezi Mungu akawaokoa na adhabu hii. Akawaandalia
mji wa Madinah wahamie huko, na akawapa hawa ndugu wakweli (Maanswari),
waliowapa makazi na wakawanusuru. Wakagawana nao mali na majumba yao na
wakawapendelea zaidi kuliko wao wenyewe. Mwenyezi Mungu akawafungulia
milango ya rehema zake na akaibadilisha khofu yao kuwa amani, udhalili wao
kuwa utukufu. Mwenyezi Mungu mtukufu akawaneemesha kwa neema hizi,
kuhusiana na hili tunasoma: “ NA KUMBUKENI (Enyi waislamu) MLIPOKUWA
WACHACE, MKIONEKANA MADHAIFU (Wanyonge) KATIKA ARDHI, MKAWA MNAOGOPA WATU
WASIKUNYAKUENI, AKAKUPENI MAHALA PAZURI
PA KUKAA (napo ni hapa Madinah) NA AKAKUTIENI NGUVU KWA NUSURA YAKE NA
AKAKUPENI RIZIKI NZURI ILI MPATE KUSHUKURU.” [8:26]
|