|
SOMO
LA KWANZA
I/
HIJRAH YA MADINAH/WAISLAMU WAHAMIA MADINAH
Makurayshi
walihisi khatari inayowanyemelea ikiwa ni natija ya yale maagano ya pili
ya Aqabah. Katika maagano haya Answaar (wenyeji wa Madinah) waliagana na
Mtume wa Allah yeyote awaye atakayemzuia kuufikisha ujumbe wa Mola wake
kwa watu. Nae Mtume kwa upande wake akaahidi kushirikiana nao bega kwa
bega. Kwa hivyo Makurayshi wakatambua kuwa Bwana Mtume tayari sasa ana
himaya, ana watu walio tayari kwa lolote katika kuihami na kuitetea imani
yao: “ …………WATAIPIGANIA DINI YA ALLAH, WALA HAWATAOGOPA LAWAMA
YA ANAYEWALAUMU……..” (5:54) Miaka kumi na tatu, ya utume aliyokaa
Mtume Madinah, Makurayshi walifanikiwa kwa kiasi kikubwa kuidhibiti
da’awah ya Uislamu isitoke nje ya mipaka ya Makkah. Wakafanya juhudi za
makusudi kuhakikisha kuwa habari za Uislamu haigongi masikio ya waarabu
walio nje ya mipaka ya Makkah. Lakini Mwenyezi Mungu Mtukufu ambaye ndiye
aliyemtuma Mtume wake kwa uongofu na dini iliyo ya haki alitaka dini yake
ienee katika ardhi kinyume na matakwa yao. “WANATAKA KUIZIMA NURU YA
ALLAH KWA VINYWA VYAO, LAKINI ALLAH AMEKATAA ISIPOKUWA KUITIMIZA NURU YAKE,
IJAPOKUWA MAKAFIRI WANACHUKIA” (9:32).
Allah
akamuandalia Mtume wake kundi hili lenye imani thabiti, isiyoyumbishwa
wala kutetereshwa na chochote wala yeyote, kundi la watu wa Madinah. Kundi
hili likamuamini Mtume na kusadiki yote aliyokuja nayo yakiwa yamehodhi
uongofu na bayana ya kila kitu. Likamuahidi kumlinda kwa nafsi na mali na
wataipigania dini ya Allah kufa kupona”……..WANAPIGANA KATIKA NJIA YA
ALLAH, WANAUA NA WANAUAWA…….” (9:111).
Kadhalika
Makurayshi walitambua fika ujuzi, uhodari na ushujaa wa vita waliokuwa nao
Ausi na Khazraji. Nguvu yao itarudufika mara mbili zaidi Waislamu wa
makkah wakihamia kwao, hapo wote watakuwa mkono mmoja, sauti moja dhidi
yao. Pia Makurayshi walifikiri kuwa Mtume amewapangia maswahaba wake mkakati wa kuhamia Madina kwa ndugu zao wa imani ambao
“…..WANAWAPENDELEA KULIKO NAFSI ZAO INGAWA WENYEWE WANA HALI NDOGO……..”
(59:9)
Baada
ya kupewa idhini ya kuhama na Mtume, maswahaba walianza kuelekea Madina
kwa uficho mkubwa. Walikuwa wakiondoka mmoja mmoja au makundi ya watu
wachache. Walihama wao wenyewe na imani yao tu, huku wakiwaacha nyuma wake
zao, watoto na mali zao. Nae Mtume akabakia Makkah akisubiri amri na
idhini ya Mola wake ya kuhamia Madinah kuungana na maswahaba wake.
Makurayshi walipoona kwamba waislamu wanapenya kwa uficho wakifuatana
kwenda Madina, waliiona hatari ya uhamiaji huu. Wakafanya kila waliwezalo
kuuzuia uhamaji huu, lakini wapi, hawakuweza ila kuwazuia wanyonge tu.
Wanahistoria
wa kiislamu wamepokea riwaya nyingi zinazohusiana na hijrayh hii ya
masahaba wa Mtume na namna waliyojitolea muhanga. Miongoni mwa riwaya hizo,
wamepokea kwamba Bwana Swuhayb Ibn Sinaah
alipotaka kuhama,
makafiri wa Makkah walimwambia ulikuja kwetu ukiwa fakiri hohehahe, mtu
duni kabisa, ukachuma mali hapa kwetu mpaka ukafikuia hapo ulipo. Kisha
eti leo unataka uondoke wewe na mali hiyo! Wallah, hilo haliwezekani katu!
Swuhayb akwaambia: Mnaonaje, nikikuachieni mali yangu, mtaniacha niondoke?
Wakajibu: naam. Akasema: Basi mimi nimekupeni mali yangu yote. Anasema
mpokezi Ibn Is-haaq : Khabari ile ikamfikie Mtume wa Allah – Rehema na
Amani zimshukie – akawa akisema “amepata faida swuhayb! Amepata faida
swuhayb!”. Kuhusiana na kitendo hiki adhimu cha swahba wa Mtume, Bwana
Swuhayb ikashuka kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu “NA KUNA KATIKA WATU,
WAUZAO NAFSI ZAO KWA KUTAKA RADHI YA ALLAH, NA ALLAH NI MPOLE KWA WAJA
WAKE” (2:207).
Alipofika Madinah alipokelewa kwa shangwe na maswahaba wenzake huku
wakimpa bishara njema hiyo.
Ama
Sayyidna Umar-Allah amuwiye radhi– yeye hakuhama kwa uficho, bali
alitangaza wazi kuhama kwake kama alivyotangaza kusilimu kwaka.
Imepokelewa riwaya kutoka kwa Imam
Aliy. Ibn Twaalib – Allah amuwiye radhi – kwamba yeye amesema.
Muhajirina wote walihama kwa uficho isipokuwa umar tu peke yake. Yeye
alipotaka kuhama, alichukua upanga, upinde, mishale na shoka yake ndogo
aliyoivaa kiunoni. Akatoka akaenda kwenye Al–kaaba ambapo wazee wa kikurayshi walikuwa wamekaa,
akatufu mara saba. Kisha akaja Maqaamu Ibrahim kaswali rakaa mbili, halafu
akaziendea baraza zile za mabwana wakubwa wa Makkah moja baada ya nyingine
akiwaambia, Anayetaka mama yake ampoteze mwanae, au wanawe wawe yatima, au
mkewe awe mjane, basi na anifuate nyuma ya jangwa hili. Imam Aliy anasema.
Hakuna hata mmoja aliyethubutu kumfuata, nae akashika njia kuungana na
wenziwe Madinah.
Hivi
ndivyo Waislamu walivyouacha mji wao wa Makkah, mahala walipozaliwa,
kukulia na kupazoea. Hawakubeba chochote zaidi ya imani yao, wanakwenda
ugenini Madinah kuanza maisha upya. Waislamu wakamiminika Madinah mpaka
hawakusalia Makkah ila Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie Abuu Bakri,
Aliy na baadhi ya wanyonge ambao
Mwenyezi Mungu Mtukufu anawataja ndani ya Qur-ani Tukufu: “ISIPOKUWA
WALE WALIOKUWA MADHAIFU KWELI, KATIKA WANAUME NA WANAWAKE NA WATOTO WASIO
NA UWEZA WA HILA YOYOTE, WALA HAWAWEZI KUONGOZA NJIA (kwenda Madinah) BASI
HAO HUENDA ALLAH AKAWASAMEHE,. ALLAH NI MWINGI WA KUSAMEHE (na) MWINGI WA
KUGHUFURIA”. (4:-99) Hapo Madinah, Muhajirina hawa wakapokelewa na ndugu
zao wa Imani Answaar kwa mapenzi yaliyochanganyika na udugu kwa Imani ya
kweli. Wakawapa makazi, wakagawana nao mali na majumba yao na
wakawapendelea kuliko nafsi zao. Kuhusiana na udugu huu tunasoma.
“HAKIKA WALE WALIOAMINI NA WAKAHAMA NA WAKAIPIGANIA DINI YA ALLAH KWA
MALI ZAO NA NAFSI ZAO (nao ni wale Muhajiria – Waislamu wa Makkah) NA
WALE WALIOWAPA (Muhajirina) MAHALA PA KUKAA (Nao ni Answaar) NA
WAKAINUSURU (dini ya Allah) HAO NDIO MARAFIKI, WAO KWA WAO……….”
(8:72) Ama Mtume yeye aliendelea kubakia Makkah akisubiri idhini ya kuhama
kutoka kwa Mola wake. Sayyidna Abu Bakri kila alipotaka kuhama, Bwana
Mtume alimsubirisha na kumwambia. “Usiwe na haraka, huenda Allah akakupa
mtu wa kufuatana nae” Hapo
ndipo Abu Bakri alipotambua kwamba Bwana Mtume ana nia ya kuhama lakini tu
anaingojea ruhusa ya Mola wake. Akanunua vipando(wanyama) viwili akaviweka
nyumbani kwake tayari kwa safari ya Madinah, yeye na Mtume wa Allah.
|