|
i./ BWANA MTUME ATOKA MAFICHONI NA KUANZA SAFARI YA
MADINAH.
Makurayshi walipokata tamaa ya kumtia mbaroni Mtume wa
Allah na kuamini kwamba tayari atakuwa nje ya mipaka ya himaya yao. Hapo
ndipo Bwana Mtume – Rehema na Amani zimshukie – alipoitumia fursa hiyo kutoka
pangoni mle, tayari kwa safari ya kuelekea Madinah. Lilikuwa ni jambo
lisiloingia katika dhihni na fikra za
makurayshi kwamba Mtume anaweza kuwaponyoka
bila ya kumkamata. Baada ya kukaa pangoni thauri kwa muda usiopungua siku
tatu, ndipo alipokuja yule mtaalamu wa njia waliyemkodi. Akaja na wale ngamia
wawili aliopewa na Abuu Bakri – Allah amuwiye radhi – kwa ajili ya safari yao
hiyo na ngamia mwingine kwa ajili yake yeye. Bila ya kupoteza muda, wote
watatu, Bwana Mtume, swahibu yake na mtaalamu wa njia, wakaanza kujiandaa kwa
ajili ya safari ndefu iliyosheheni hatari njia nzima.
Ibn Is-haaq – Allah amrehemu –
anasimulia: “Abuu
Bakri- Allah amuwiye radhi – alivisogeza vipando viwili vile kwa Mtume wa
Allah – Rehema na Amani zimshukie – akampa yule aliye bora na kumwambia
“Panda, nakufidia baba na mama
yangu!” Mtume akasema: “Mimi siwezi
kumpanda ngamia asiye wangu” Akasema (Abuu Bakri) Huyo ni wako ewe Mtume wa
Allah (Mtume) akasema” Hapana, niambie umemnunua kwa thamani gani?” Akajibu
“Kiasi kadha wa kadha” (Mtume) akasema: “ Nimekubali kumchukua kwa thamani
hiyo: (Abuu Bakri) aksema, “Huyo ni wako tu ewe Mtume wa Allah”) Wakapanda na
kuanza safari………………..
Bi Asmaa bint Abuu Bakri – Allah amuwiye radhi
yeye na babiye – alikuwa amewaletea chakula maalum cha safari na kukihifadhi katika chombo kinachoweza
kuchukulika kiurahisi safarini.
Mtume
autupia mji wa Makkah jicho la kwaheri .
Msafara huu wa Mtume ukaanza safari kwa jina la
Allah wakati giza lilipochukua nafasi ya nuru ya mchana na mwezi kutawala
mahala pa jua. Msafara huu ulikuwa ni mwanzoni mwa mwezi wa mfunguo sita.
Msafara ulipoielekea njia ya Madinah tayari kuondoka, Mtume – Rehema na Amani
zimshukie – akageuka nyuma na kuutazama mji wa Makkah mtazamo wa kwaheri kwa
kitambo, kisha akasema, “Wallah! Hakika mimi ninatoka ndani yako na il-hali
ninajua kwamba wewe (Makkah) ndiwe kipenzi cha ardhi ya Allah mbele ya Allah
na tukufu yake. Lau si watu wako (wakazi wako) kunitoa ndani yako (kwa nguvu)
nisingelitoka.
Hii ni kwaheri iliyosheheni na kujaa uzalendo na
mapenzi ya kweli kwa mji huu mtukufu ulio kipenzi cha Allah na Mtume wake.
Kwa heri inayoashiria majonzi na masikitiko ya Mtume wa Allah juu ya
kutengana na mji wake huu aliuzoea na kuupenda.
Mtaalamu wa
njia awapitisha njia yenye usalama zaidi.
Msafara ulipoondoka, yule mtaalamu wa njia
akautumia ujuzi na uzoefu wake kuwapitisha katika njia yenye usalama na amani na akijiepusha kupita njia
aliyohisi kuwa inaweza kuwa ni hatari kwao. Hawakupita katika njia iliyokuwa
ikitumika na watu wote inayoelekea nyanda za juu kaskazini. Bali wao
waliifuata ile njia isiyozoeleka ya nyanda za chini kusini ipitayo chini ya
Makkah kuelekea upande wa Yemen. Kisha wakaelekea Mashariki upande wa Pwani
ya Ithamah, wakaenda mpaka walipoukaribia ukanda wa mwambao wa bahari (Red
Sea) wakaelekea kaskazini wakiiacha njia iliyozoeleka. Ramani ifuatayo itakusaidia kuona jia alimopitia
msafara tokea Makkah mpaka Madinah.
Wakaendelea na msafaa wao usiku kucha na nusu ya
mchana, wakapumzika kutokana na uchovu chini ya mwamba.
Makurayshi watangaza zawadi nono kwa yeyote
atakayemkata Bwana Mtume na kuwaletea akiwa hai au amekufa.
Makurayshi waliposhindwa kumpata Bwana Mtume wao
wenyewe baada ya juhudi za makusudi, wakaamua kutafuta msaada kutoka kwa
wakazi wa vitongoji vilivyo nje ya
mji Makkah. Ili kuwahamasisha
kujituma na kuifanya kazi hiyo haraka iwezekenavyo, wakaweka kivutio/Motisha. Wakatangaza zawadi nono
ya ngamia mia moja kwa yeyote yule atakayewaletea Mtume, hasimu wao mkuu
akiwa hai (mateka) au amekufa (maiti).
Ngamia mia moja ilikuwa ni dau kubwa mno kuwahi
kutolewa katika historia ya Waarabu. Dau hili likawavutia na kuwashawishi
wengi miongoni mwa watu wa vitongoji
kuingia katika wimbi la kumsaka Mtume wa Allah kwa tamaa ya kupata zawadi hii
nono. Kupata ngamia mia moja katika fikra zao hakukumaanisha kingine zaidi ya
kuupiga teke umaskini. Miongoni mwa walowania na kupania kupata zawadi hii
nono alikuwa ni Suraaqah Ibn Maalik. Huyu ni mtu wa kabila lililokuwa
likijulikana kama Bariy Mudlaj, hawa ni wakazi na wenyeji wa kitongoji
kilichojulikana kama Qudayd (Fudhayd). Kitongoji hiki kilipakana na pwani ya
“Raabigh” Kabla ya kutangazwa kwa zawadi hii nono, tayari Suraaqah alikuwa
amepata khabari kwamba kuna watu watatu wameonekena wakipita katika pwani
yao. Aliposikia tangazo lile akawa hana
sababu ya kuamini kwamba hao walionekana ndio hao watafutwao: bila
shaka huyo atakuwa ni Muhammad na
Wafuasi wake. Tamaa ya zawadi ile nono ikamtambaa mwili mzima na
kumshajiisha kuingia msakoni. Akaanza
kufuata mbiombio nayo zilizoachwa nyuma na Mtume na wenzake, akiwa na imani
kuwa atakuta tu njiani.
Hebu na tumpe nafasi Imam Bukhaairy- Allah
amrehemu – atupokelee hadithi kutoka kwa Ibn Shihaab ikielezea aliyoyasimulia
Suraaqah mwenyewe yale yaliyomkuta
katika msako wake huo, anasema (Suraaqah) “Walitujia wajumbe wa makafiri wa
kikurayshi, wakaweka dau kubwa kwa yoyote yule atakayemkamata mateka au
kumuua Mtume wa Allah na Abuu Bakri. Wakati nilipokuwa nimekaa katika mojawapo ya baraza za kaumu yangu, mara ghafla akaja mtu mmoja wa kabila letu akatusimamia huku sisi
tukiwa tumekaa. Akasema. Ewe Suraaqah hakika mimi nimeona muda mchache tu
uliopita kiwingu cheusi (watu kwa mbali) ufukweni. Ninadhani huyo atakuwa ni
Muhammad na wenziwe tu. Suraaqah akasema: Nikatambua kwamba hao aliowaona
ndio wenyewe khasa, nikamwambia: Hao sio wao, lakini wewe umemuona fulani na
fulani ambao wameondoka hapa hapa mbele ya macho yetu. Kisha nikakaa kitambo
kidogo katika baraza ile, halafu nikainuka nikaenda nikamuamuru mjakazi wangu
atoke na farasi wangu mpaka nyuma ya kilima anisubiri hapo. Nikautwaa mkuki
wangu na kutoka nao kwa kupitia nyuma ya nyumba yangu. Nikaenda mpaka kule
alikokuweko farasi wangu akinisubiri nikampanda. Nikamuendesha shoti mpaka nikawakaribia,
farasi wangu akanipiga mweleka na
kunibwaga chini pwaa! Nikainuka na
kuupeleka haraka mkono wangu kwenye mkoba wangu wa mishale, nikatoa mishare
ya kupigia ramli. Nikapiga bao
(ramli) kwa mishare hiyo. Ukatoka mshare niuchukiano, nikaipuuzia mbali ramli
ile, nikampanda tena farasi wangu Farasi wangu akaenda, mbio mpaka
nikawakaribia tena kwa mara ya pili. Nikawa namsikia Mtume wa Allah akisoma
(Qur-an) bila ya kugeuka nyuma na Abuu Bakri akigeuka mara kwa mara. Hapo
ndipo ilipozama mchangani miguu ya farasi wangu mpaka kufikia magotini.
Nikaruka kutoka juu yake, nikamkemea akainuka, kabla hajamaliza kuitoa mikono
yake likatimka vumbi liloenea angani mithili ya moshi. Nikapiga ramli tena na
bado ukatoka ule ule mshare niuchukiao. Mpaka hapo sikuwa na hila tena ila
kuwatolea mwito wa amani, wakasimama, wakasimama. Nikampanda farasi wangu
mpaka nikawafikia. Kutokana na yote yaliyonisibu, ikanipitia moyoni kuwa ibla
ya shaka jambo hili la Mtume wa Allah – Rehema na Amani zimshukie litadhihiri
tu. Nikamwambia hakika ndugu zako wamekuwekea dau na nikawaeleza khabari za
namna watafutwavyo, nikawapa pamba (chakula cha safari). Hawakunikatalia wala
kuniomba ila waliniambia: Wapoteze watu nasi (usiwaambie njia tupitayo).
Nikamuomba aniandikie hati/mkataba wa amani, akamuamrisha Aamir Ibn Fuhayrah
aniandikie katika kipande cha ngozi. Kisha Mtume wa Allah, huyoo akaenda
zake”.
Ummu Maabad
Msafara ukaendelea katika hali ya machovu makubwa katikati ya vumbi la jangwani,
ukistahamili joto liunguzalo. Kila walipochoka, basi walipiga kambi kupumzika
katika vitongoji, vya njiani. Wakawatafuta wenyeji ili pengine wanaweza kupata maji au chakula. Wakaenda
katika hali hiyo mpaka wakapita kwa Umuu Ma’abad, mwanamke karimu wa kabila
la Khuzaah. Alikuwa amekaa mbele ya khema lake, akiipa misafara ipitayo hapo
maji na chakula. Walipofika hapo Mtume akamuomba awauzie tende au nyama,
lakini hawakuambulia kitu chochote. Akawajibu huku akionyesha masikitiko
yake. “Wallah, lau tungelikuwa na chochote cha kukuandalieni, msingelikuwa na
haja ya kuomba au kutoa thamani” Na huo ulikuwa ni mwaka wa ukame.
Amesema Ibn Sa’ad – Allah amrehemu – akipokea
riwaya kutoka kwa Abuu Ma’abad (mumewe Ummu Ma’abada) “Mtume wa Allah –
Rehema na Amani zimshukie
akamuangalia mbuzi aliyekuwepo pembeni mwa Khema, akasema
(akauliza) Huyu ni mbuzi gani ewe
Ummu Ma’abad?) Akajibu: “Mbuzi huyu ameshindwa kwenda machungani (Malishoni)
pamoja na wenziwe kutokana na udhaifu (Mtume) akauliza (tena) “Je, anayo (anatoa)
maziwa?” Akajibu: “yeye ni dhaifu mno haiwezi kutoa maziwa “ (Mtume) akasema:
“Je, unanipa idhini ya kumkama (Maziwa)?” Akajibu (Ummu Ma’abad): “ Naam,
ikiwa unaona kuwa anakamika!” Mtume- Rehema na Amani zimshukie – akamuitisha
mbuzi yule, akampapasa akaomba: “ Ewe Mola wa haki wee! Mbarikie (mama huyu)
kwa mbuzi wake huyu! “(Anaendelea kusema Ibn Sa’ad): mbuzi yule akaitanua
miguu yake na chuchu zake zikajaa maziwa tele. Mtume akaagiza kiletwe chombo
kikubwa kiwezacho kuwashibisha watu wote. Akakama maziwa tele ndani yake,
akampa mama yule akanywa mpaka akatosheka, kisha akawapa wenziwe mpaka
wakatosheka. Halafu yeye Mtume ndie akawa wa mwisho kunywa maziwa na akasema:
“Mnyweshaji watu ndie huwa wa mwisho kunywa” Kisha akamkama tena mara ya
pili, akamuachia mama yule maziwa yale, hao washika njia na kuondoka.
Haukupita muda mrefu mumewe Abuu Ma’abad akarudi akiwaswaga mbuzi na kondoo
wakondefu. Alipoyaona maziwa yale tele alistaajabu na akauliza. Mmeyapata
wapi maziwa haya na il-hali mbuzi hawakuwepo hapa nyumbani? Akajibu (Ummu
Ma’abad) Wallah hapana, ila hakika ya hjali ametupitia mtu mwenye baraka,
mazungumzo yake yalikuwa hivi na hivi. Akasema: Wallah, mimi namdhania huyo
ndie mtu (jamaa) wa Makurayshi wanayemtafuta. Ewe Umuu Ma’abad hebu nisifie
hivyo……………………”
Ummu Ma’abad akaanza kumsifia mumewe namna Mtume
alivyo, umbile lake, tabia zake, uzungumzaji wake, haiba yake na
…………na……………Akasema (Abuu Ma’abad): “ Wallah, huyo ndiye mtu wa Makurayshi
tuliyetajiwa khabari zake! Lau ningemkuta ewe Ummu Ma’abad, ningetaka
kufuatana nae, na nikipata upenyo nitamfuata, nitamfuata tu!”
|