|
Khabari
ya Mtume wa Allah - Rehema na
Amani zimshukie kutoka Makkah kuelekea
Madinah ziliugubika mji mzima wa Madinah. Wenyeji wa mji huu Answaar wakawa
waunguzwa na shauku ya kukutana na kumpokea mgeni huyu mtukufu, mwenye baraka anayehamia kwao.
Kila siku asubuhi walikuwa wakitoka kwenda kumngojea katika njia itokayo Makkah
ili wamlaki kwa shangwe, hoihoi na furaha. Waliendelea kumsubiri mpaka
waliposhindwa kuvumilia ukali na joto
la jua ndipo kurejea majumbani mwao. Hio ndilo lililokuwa zoezi la kila siku
mpaka siku ile Bwana Mtume alipofika Madinah kuanza ukurasa mpya wa
da’wah akizungukwa na watu wenye
nyoyo thabiti na imani isiyotetereka na walio tayari kumuhami hata kwa
gharama ya uhai wao.
Kundi
kubwa la wanasera na wataalamu wengi wa tarekh (historia) wanasema kwamba
Mtume wa Allah Rehema na Amanzi zimshukie alifika mjini Madinah siku ya Jumatatu, mwezi kumi na mbili, mfunguo
sita, katika mwaka wa kumi na tatu (13 wa utume). Hii inawafikiana na tarehe
20 ya mwezi Septemba mwaka mia sita ishirini na mbili (622) Miladia. Na
kwamba kabla hajaingia Madinah
alipiga kambi Qubah. Qubah ni kitongoji kilichopo umbali wa maili tatu (3)
kusini mwa mji wa Madinah. Hapo Qubah, Bwana Mtume alifikia nyumbani kwa
Bwana Kulthum Ibn Al-hidmi, mkubwa wa kabila la Baniy Amri Ibn Auf. Alikaa na
kupumzika kwa wenyeji wake hawa kwa siku kadhaa. Kazi ya mwanzo aliyoifanya
Mtume wa Allah hapo Qubah, ilikuwa ni ujenzi wa msikiti na msikiti huu ukawa
ndio msikiti wa kwanza kujengwa katika
Uislamu. Huu ndio msikiti anaoutaja Allah na kuusifia ndani ya Qur-ani
kwa kauli yake tukufu.
“………………MSIKITI
ULIOJENGWA JUU YA MSINGI WA KUMCHA ALLAH TANGU SIKU YA KWANZA (ya kufika
Mtume Madinah) UNASTAHIKI ZAIDI WEWE USIMAME HUMO. HUMO WAMO WATU WANAOPENDA
KUJITAKASA NA ALLAH ANAWAPENDA WAJITAKASAO: (9: 108)
Hii ndio kauli ya Mufasirina walio wengi kwamba msikiti uliokusudiwa hapa ni
Masjid Qubah. Bwana Mtume alishiriki katika ujenzi wa msikiti huu kwa mkono
wake katika ubebaji wa mawe na miamba. Alifanya kazi mpaka ikawa inaonekana athari ya uchovu.
Maswahaba kutokana na kuijua daraja ya Mtume wa Allah walimsihi apumzike na
awaachie wao kuifanya kazi hiyo peke yao, lakini Mtume hakupenda ila awe mmoja wao..
iii./KUSWALI
MADINAH NA IJUMAA YA KWANZA BAADA YA HIJRAH.
MJI
WA MADINAH WAZIZIMA KWA FURAHA YA KUJA KWA MTUME
Siku
aliyowasili Bwana Mtume Rehema na Amani zimshukie Madinah, ilikuwa ni siku ya
furaha kuu. Mji huo haukuwahi kushuhudia katika historia yake siku ya furaha,
shangwe, hoihoi, nderemo na vifijo kuliko siku hiyo ya watu walivaa nguzo zao
nzuri nzuri kana kwamba wanaisherehekea siku kuu. Wanawake nao hawakubakia
nyuma, walisimama nje ya nyumba zao wakimpungia Mtume mkono wa karibu. Watoto
nao wakalipuka kwa furaha wakipiga makelele ya Amekuja Mtume wa Alah…………..!
Mtume wa Allah……………! Wajakazi na
vigori wakawa wanaimba na kupiga madufu na wahabeshi wakicheza na mikuki yao,
yote hayo yakiwa ni katika kumlaki na kumpokea Mtume wa Allah - Rehema na
Amani zimshukie Imekuja riwaya katika sahihi Muslim na Bukhariy kutoka kwa
Abuu Bakri amesema: Tulipofika Madinah, watu walitoka majumbani na majiani
(kutulaki), vijana na watumishi wakisema: Allaahu Akbari, amekuja Mtume wa
Allah……..! Allaahu………! Akbar, Amekuja Muhammad! Allaahu Akbar, amekuja
Muhammad………..Allaahu Akbar, amekuja Mtume wa Allah……..”
Kadhalika
imepokelewa kutoka kwa Bi Aysha - Allah amuwiye radhi - amesema Mtume wa
Allah - Rehema na Amani zimshukie - alipowasili Madinah, wanawake, vijana wa
kiume na wa kike wakaanza kuimba:
TALA-‘AL-BADRU
ALAYNAA MIN
THANIYYATILWADAA’I
WAJABA-SHHUKRU
ALAYNAA MAA DA’AA LILLAHI DAA’I
AYYUHAL-MAB’UUTHU
FIINA JI-TA BIL-AMRIL-MUTAA’I
Tafsiri:
Umetuchomozea
mwezi sisi* kutoka njia ya upande wa Wadaa inapasa shukrani juu yetu* Muda wa kulingania kwa Allah mlinganiaji Ewe
uliyetumwa wee katika sisi* Umeleta jambo kuliokuwa wajibu kulifuata.
Mchana
ulipopanda (mchana wa saa sita), Mtume wa Allah - Rehema na Amani zimshukie -
alimpanda farasi wake, huku waislamu wakiwa wamemzunguka, wengine wakitembea
kwa miguu na wengine wamepanda
wanyama wakiwa na mapanga yao. Kutokana na pupa yao katika kumuheshimu
na kumtukuza Mtume wa Allah walisongamana kugomea hatamu za ngamia wa Mtume
ili kutabaruku na Mtume. Hiyoo Mtume anaelekea upande wa Madinah, kila
alipoitia nyumba mojawapo miongoni mwa nyumba za Answaar walikuja mbele yake
na kumwambia: “Njoo ewe Mtume wa Allah kwenye nguvu, ulinzi na utajiri!” Nae
Bwana Mtume akitabasamu kuonyesha shukrani na akiwaombea dua njema, halafu
akasema huku akimuashiria ngamia wake: “Muacheni njia, kwani yeye
ameamrishwa.
KHUTBA
YA KWANZA YA MTUME - MADINAH
Bwana
Mtume Rehema na Amani zimshukie
alipofika kwenye makazi ya ukoo wa Bariy Saalim Ibn Auf, ulimdiriki
hapo swala ya Ijumaa. Akaiswali swala hiyo katika uwanda wao pamoja na
waislamu aliokuwa nao. Ijumaa hii ndio iliyofanya ukurasa wa swla za ijumaa
katika Uislamu, yaani ndio iliyokuwa Ijumaa ya kwanza kuswaliwa. Mtume
alisimama, akamuhimidi Allah na Kumsifia kwa sifa zilizo laiki yake na
khutbah yake ya mwanzo ikawa: “Ama baad, enyi watu! Zitangulizenieni (wema)
nafsi zenu. Jueni, wallah! Mmoja wenu atafikiwa ghafla na mauti na awaache
mbuzi (mifugo) wake bila ya mchungaji. Mola wake amwambie akiwa hana
mkalimani wala bawabu wa kumzuia. Je, hakukujia mjumbe wangu na kukufikishia
ujumbe wangu na nikakupa mali na kukufadhili kwa fadhila nyingi? Basi leo
umeitangulizia nini nafsi yako? Basi na aangalie kuliani na kushotoni asione
chochote. Halafu aangalie mbele yake na hataona ila Jahanam. Basi atakayeweza
kuukinga uso wake kutokana na moto kwa kutoa japo nusu ya tende na afanye
hivyo. Na asiyepata (hata hicho kidogo cha kutoa) basi na atoe neno zuri,
kwani hulipwa kwa neno hilo mfano wake mara kumi mpaka mia saba maradufu.
Amani iwe juu yenu na juu ya Mtume wa Allah na Rehema na Baraka za Allah”
NGAMIA
AENDA MPAKA ANAKITA MAGOTI MAHALA PA KUJENGWA MSIKITI WA MTUME.
Baada
ya swala ile ya Ijumaa kumalizika, Mtume - Rehema na Amani zimshukie
akampanda ngamia kuendelea na safari yake ya kuingia mjini Madinha. Ngamia
akendelea kwenda huku Bwana Mtume akiwa ameziachia hatamu zake, mpaka akakita
magoti mahala pa kujengwa msikiti wa Mtume. Mahala hapo palikuwa ni uwanja wa
kuanikia tenda aliokuwa ukimilikiwa na vijana wawili mayatima wa ukoo wa
Baniy Najjaar. Uwanja huo ulikuwa ukielekeana na nyuma ya Abuu Ayyuub,
Khaalid Ibn Zayd Al-answaariy . Mtume akashuka kutoka juu ya ngamia akaomba
dua iliyomo ndani ya Qur-ani: “ MOLA WANGU! NITEREMSHIE MTEREMSHO WENYE
BARAKA MAANA WEWE NI MBORA WA WATEREMSHAJI” (23: 29)
Aliiomba
dua hii mara nne. Hii ni dua ambayo Allah alimfundisha Mtume Nuhu - Amani
imshukie aisome wakati wa kushuka
kutoka ndani ya Safina. Kisha ikamjia ile hali inayomjia wakati wa kuja
wahyi, walipomuondoka akasema: “Hapa ndipo patakapokuwa makazi, Inshaallah,
na akaamrisha ishushwe mizigo yake, kisha akauliza. Ni nyumba ipi ya jamaa
zetu (wenzetu) iliyo karibu? Abuu Ayyuub akajibu: “Mimi ewe Nabii wa Allah,
hii ndio nyumba yangu na huu hapa ndio mlango wangu” Mtume akamwambia:
“Haya nenda ukatauandalie mahala pa kupumzika” Akaenda kuandaa kisha akarudi
na kusema “ Ewe Mtume wa Allh, nimekwisha kukuandalia mahala pa kupumzikia,
haya inukeni kwa baraka za Allah mkapumzike.”
MTUME
AKAA KWA ABUU AYYUUB MPAKA ALIPOJENGA MSIKITI NA MASKANI YAKE.
Bwana
Mtume Rehema na Amani zimshukie akawa mgeni wa Bwana Abuu Ayyuub akaishi nae
mpaka alipojenga msikiti na makazi yake. Zawadi za aina kwa aina za vyakula
na vinywaji zikawa zikimiminika mfululizo kwa Mtume wa Allah wakati alipokuwa
nyumbani kwa Abuu Ayyuub. Zawadi ya kwanza aliyoletewa akiwa nyumbani hapo ni
sahani ya chakula iliyoletwa na Zayd Ibn Thaabit ikiwa na mkate uliochochevywa
kwa maziwa na samli, akampa Mtume huku akimwambia: “ Hii ni zawadi kutoka kwa
mama yangu” Mtume wa Allah Rehema na Amani zimshukie akapokea na kumuombe dua
akisema: “Allah akubariki wewe na mama yako” Akawaita maswahaba wake wakala
ilikuwa hauingii usiku ila mlangoni pa Mtume kuna watu watatu kwa uchache
waliobeba chakula. Mtume alikaa
nyumbani kwa Abuu Ayyuub kwa kipindi kisichopungua miezi saba na kisichozidi
mwaka mmoja, mpaka alipoujenga msikiti na maskani yake. Alikaa hapo pamoja na
swahaba wake Usaamah Ibn Zayd, inasemekana kwamba Imam Aliy Ibn Abiy Twaalib
pia alifikia hapo pamoja na Mtume ambaye alimkuta akiwa bado Qubah. Ama Bwana
Abuu Bakri yeye alifikia nyumbani kwake Bwana Khubayb Ibn Isaaf.
|