|
Tumeeleza huko nyuma kwamba yalipatikana makabila mengi ya kiarabu kutokana na
kizazi cha Nabii Ismail. Kila kabila liliundwa kutokana na kaya/familia kadhaaa
zilizojiunga pamoja. Kila kabila liliongozwa na kiongozi aliyekuwa mtu mzima
anayeheshimika, kukubalika na kutiiwa na wote. Ukabila ulikuwa ndio sera ya kila kabila,
na kila kabila lilikuwa tayari kuilinda sera yake hiyo ya ukabila dhidi ya uadui wa wote
ule kutoka makabila mengine kwa gharama yoyote ile. Msimamo huu na sera hii ya ukabila
ilisababisha mizozo, ugomvi na mapigano ya mara kwa mara baina ya makabila haya. Kugombea
vyanzo vya maji, machungo na kujifakharisha kwa nasabu pia vilichochea kwa kiasi kikubwa
mizozo na mapigano.
Kama ambavyo watu hutofautiana katika vyeo/hadhi, kazi na hali za kimaisha,
Waarabu pia waligawanyika katika matabaka yafuatayo:-
- Mabwana/Viongozi: hawa ndio waliokuwa na mamlaka juu ya wengine na hatamu za
uongozi zilikuwa chini yao.
- Makuhani: hawa walikuwa ndio viongozi wa kidini wakiyatawalia mambo yote yanayohusu
dini ikiwa ni pamoja na ibada, sherehe za kidini na mengineyo.
- Wafanyabiashara: hawa walijishughulisha na usambaji na uuzaji wa bidhaa mbalimbali
ndani na nje ya maeneo yao.
- Wachungaji: hawa ndio waliokuwa wakijishughulisha na uchungaji wa wanyama na kazi
ya kilimo kwa kiasi fulani.
Ama kwa upande wa kitabia,Waarabu za jahilia kama walivyo watu wa zama hizi
walikuwa na tabia nzuri na nyingine mbaya. Miongoni mwa tabia njema walizokuwa nazo ni
kama vile ukarimu, murua, ushujaa na utekelezaji wa ahadi. Tabia mbaya zilizoitawala jamii
ile ni pamoja na ulevi, uchezaji wa kamari, ulaji riba na kuwazika watoto wa kike wakiwa
hai kama ilivyoelezwa na Qur-ani:
"NA MTOTO MWANAMKE ALIYEZIKWA HALI YAKUWA YU HAI ATAKAPOULIZWA. KWA MAKOSA GANI
ALIUAWA. (81:8-9)
SOMO LA TATU
i/NASABU YA MTUME KUUMENI KWAKE
Nasabu ya Bwana Mtume Allah amrehemu na kumshushia amani kwa upande
wa baba yake ni kama ifuatavyo:-
Yeye ni Muhammad Bin Abdillah Bin Abdil Mutwalib Bin Haashim Bin Abdi Manaf
Bin Qusway Bin Kilaab Bin Murrah Bin Kaab Bin Luayyi Bin Ghaalib Bin Fihr Bin Maalik Bin
Nadhr Bin Kinaanah Bin Khuzaymah Bin Mudrikata Bin Ilyaas Bin Mudhwar Bin Nizaar Bin Maad
Bin Adnaan. Huu Adnaan ni katika kizazi cha Nabii Ismail Bin Ibrahim Amani iwe juu
yao.
ii/NASABU YA MTUME KUKENI KWAKE
Nasabu yake Bwana Mtume Allah amrehemu na kumshushia amani kwa
upande wa mama yake:-
Yeye ni Muhammad Bin Aaminah Bint Wahab Bin Abdi Manaf Bin Zuhrah Bin Hakiym. Huyu
Mzee Hakiym ndiye Kilaab ambaye ni babu wa tano wa Mtume kwa upande wa baba yake.
Tumekwishaeleza huko nyuma kwamba huyu Mzee Qusway ambaye ni babu wa nne katika
mlolongo wa babu zake Mtume ndiye aliyeweka mpango wa mji wa Makkah na akawaunganisha
pamoja Waarabu kwa kuondosha ukabila.
Baada ya kifo cha Mzee Qusway, hatamu za uongozi wa mji wa Makkah zilishikwa na
babu wa pili wa Mtume Mzee Haashim. Huyu alikuwa tajiri na ndiye aliyeasisi mfumo wa
biashara za Kusi na kaskazi kama ulivyoelezwa na Qur-ani:-
"ILI KUWAFANYA MAKURESHI WAENDELEE. WAENDELEE NA SAFARI ZAO ZA WAKATI WA KUSI
(kwenda yaman) NA WAKATI WA KASKAZI (kwenda Shamu, ndio maana tukajaalia jeshi la ndovu
kushindwa) (102:1-2)
Pia Mzee huyu ndiye aliyesimamia usambazaji wa maji na chakula kwa wageni wote
wanaokuja kufanya ibada katika Al-kaaba na hili linaashiria ukarimu walikuwa nao Waarabu.
Naye ndiye mtu wa mwanzo aliyeanzisha uokaji na usambaji wa mikate katika mji wa Makkah na
hili linaonyesha ni jinsi gani alivyowajibika kwa jamii iliyompa dhamana ya uongozi.
Mwenyezi Mungu aliitakasa nasabu ya Mtume kutokana na uchafu wa kijahilia. Mababa
zake wote walikuwa ni watu watukufu na viongozi kama ambavyo mamama zake pia walikuwa ni
wanawake waungwana,watakasifu wasio na uchafu wowote.
Lifuatalo ni jedwali na kielelezo kinachoonyesha nasabu ya Mtume kuanzia kwa babu
wake wa nne Mzee Qusway. Jedwali hili litatusaidia kuelewa koo za Maqureshi huko mbele.
|