|
Wakati
wa swala ulipowadia alilingana mlinganiwa Mtume wa Allah – rehema na
Amani zimshukie – akawaita watu kuja kuswali kwa kusema “Asswalaatu
Jaamiah,” basi watu wakakusanyika kwa ajili ya swala. Kadhalika historia
imetusajilia kauli pinzani inayopingana na hii ya mwanzo. Kauli hii
iliyomo katika vitabu vya histora inasema watu walikuwa wanakusanyika kwa
ajili ya swala bila ya wito wowote ule. Mtume wa Allah Rehema na Amani
zimshukie lilimshughulisha
sana suala la adhana. Alifikiria ni jinsi gani ataratibu namna ya
kuwajulisha watu kuwa wakati wa swala umeingia na hivyo wanawajibika
kukusanyika kwa ajili ya kuitekeleza ibada ya swala. Mtume akaitisha
mkutano wa hadhara na kuwataka kushauri maswahaba katika suala hili.
Maswahaba wakaitumia fursa hii vema kwa kuchangia fikra mbalimbali. Baadhi
ya maswahba wakashauri itumike kengele, igongwe kila unapoingia wakati wa
swala kama wanavyofanya Manaswara. Bwana Mtume hakuiafiki rai hii kwa
sababu kufanya hivyo itakuwa ni kushabihiana na kuwaiga Manaswara. Kundi
jingine likasema tupulize
tarumbeta kama wafanyavyo Mayahudi, rai hii pia ikakataliwa na Mtume kwa
hoja ile ile ya kushabihiana
na Mayahudi. Maswahaba wakaendelea kuchangia fikra na mawazo na kusema
tupige ngoma, mtu akisikia mlio wa ngoma hiyo atajua kuwa wakati wa swala
umeingia Bwana Mtume hakuikubali rai hii kwa kuwa huo ulikuwa ni utaratibu
uliokuwa ukitumiwa na warumi. Wengine wakashauri uwashwe moto mkubwa
utakaopanda juu angani na kuonekana na kila lmmoja kama wafanyavyo Majusi.
Mtume akaona si busara kutumia njia hii, kwa kigezo kuwa ni njia ya hatari
na pia ni kuutukuza moto unaoabudiwa na Majusi. Rai nyingine iliyotolewa
ilikuwa ni kusimikwa bendera
mahala pa muinuko itakapoonekana na kila mtu, na hivyo kumfahamisha kila
aionaye kuwa wakati wa swala umeingia. Rai hii pia ilikumbana na upinzani
wa wajumbe kwa hoja kuwa bendera itaonekana tu na yule
aliye nacho, aliyelala haitamsadia. Kwa ujumla Mtume wa Allah
Rehema na Amani zimshukie hakukubaliana na fikra na rai zote hizi, kwa
sababu zote zilikuwa tayari zinatumika na watu wa dini nyingine kuitana
katika ibada zao potofu. Mtume hakupenda kushabiahiana na watu hawa wanaofuata dini (mifumo) potofu,
alipenda Uislamu uwe na utaratibu wa pekee wa kuitana na kukusanyana kwa
ajili ya swala. Mkutano huu
wa hadhara ukamalizika bila ya kupatikana muafaka wowote juu ya suala la
wito wa swala. Wajumbe wakatawanyika kurudi majumbani mwao huku wakiamini
kuwa bado wana jukumu la kutafakari mpaka waweze kupata utaratibu muafaka
wa wote wa swala utakaoridhiwa na Mtume wa Allah Ibn Is-haaq – Allah
amurehemu anasema: “Baina ya wato kuwa katika hali hiyo (ya kutafakari),
mara tahamaki hivi Abullah Ibn Zayd Ibn Tha’alabah – Al- answaariy
akaona (akaota) usingizini wito wa swala. Akamuendea mbio Mtume wa Allah-
Rehema na Amani zimshukie – Akamwambia, “Ewe Mtume wa Allah, hakika
imenitokea pepesi usiku wa leo. Amenipitia mtu mmoja aliyevaa nguo za
kijani akiwa na kengele mkononi mwake, nikamwambia: Ewe mja wa Allah,
unaniuza kengele hiyo? Akaniuliza: Unaitaka kwa ajili ya nini? Nikamjibu:
Tuitumie kuwaita watu katika swala. Akaniambia: Je, nikufahamisha namna
bora zaidi kuliko hiyo (unayotaka kuitumia)? Nikamuuliza: Ni ipi hiyo?
Akaniambia sema:
ALLAHU
AKBAR ALLAHU AKBAR ALLAHU AKBAR ALLAHU AKBAR,
ASH-HADU
AN LAAILAHA ILLA-LLAH, ASH-HADU AN LAAILAHA ILLA-LLAH,
ASH-HADU
ANNA MUHAMMADAN RASULULULLAH, ASH-HADU ANNA MUHAMMADAN RASULULULLAH
HAYYA
ALALSWALAAH, HAYYA ALALSWALAAH
HAYYAH
ALALFALAAH, HAYYAH ALALFALAAH
ALLAHU
AKBAR ALLAHU AKBAR
LAA
ILAHA ILLALLAH
Alipomueleza
Mtume pepesi hiyo iliyomtokea, Mtume – Rehema na Amani zimshukie –
akasema, “Hakika bila ya shaka hiyo ni ndoto ya haki (kweli) pindipo
atakapo Allah, inuka pamoja na Bilali ukamfundisha aadhini kwa kutumia
maneno hayo kwani yeye ndiye mwenye sauti kali yenye kwenda mbali zaidi
kuliko wewe. Bilali aliyotoa adhana kama alivyofundishwa kwa amri ya
Mtume, Sayyidna Umar Ibn Khatwaab akaisikia adhana hiyo akiwa nyumbani
kwake. Akatoka kumuendea Mtume wa Allah huku akipita na kuburura nguo yake
kutokana na haraka aliyokuwa nayo, akamwambia Mtume: Ewe Mtume wa Allah,
ninamuapia yule ambaye aliyekupeleka kwa haki nimeona usingizini mithili
ya maneno haya aliyoyaona! Mtume wa Allah – Rehema na Amani zimshukie
akasema: “Himda zote njema zinamstahikia Allah kwa hilo”
Hii
ndio adhana na hivyo ndivyo ilivyoanza katika mwaka wa kwanza wa Hijrah.
Ibn Saad – Allah amrehemu – anasema: Wito wa ASSWALATU JAAMIA uliokuwa
ikitumika kabla ya adhana hii iliyoidhinishwa na kupitishwa na Bwana Mtume
uliendelea kutumiwa. Ulitumika katika hali ya dharura kila ilipojitokeza
kama vile vita. Waislamu waliitwa kwa wito huu, wakakusanyika kuja
kusikiliza kulikoni hata. Kama si wakati wa swala. Kumbukumbu sahihi za
kihistoria zinaonyesha kwamba kulikuwa na waadhini wawili katika mji wa
Madinah zama za uhai wa Bwana Mtume. Muadhini mkuu akiwa ni Sayyidna
Bilali na msaidizi wake alikuwa ni Abdullah Ibn Umuu Maktum. Bilali
alikuwa akisema kaitka adhana ya Sub-hi baada ya HAYYA ALALFALAAH maneno
haya ASSALAATU KHAYRUN MINANNAWM. Bwana Mtume akamsikia akiyasema maneno
hayo, akayakubali na hivyo yakaendelea kutumika hadi hii leo. Mtume wa
Allah Rehema na Amani zimshukie aliamrisha paadhiniwe adhana mbili katika
alfajiri ya mwezi wa Ramadhani. Adhana ya kwanza ililenga kuwaamsha
waliolala kwa ajili ya kula daku, ama ile ya pili ndio ilikuwa adhana kwa
ajili ya swala.
|