|
Wakimbizi
wa haki “Muhajirina” walipofika Madinah kwa mara ya kwanza, walisumbuliwa na
hali ya hewa ya uhamishoni. Hali hii ya hewa iliyotofautiana kwa kiasi
kikubwa na hali ya hewa ya kwao ilipelekea wengi wao kupatwa na homa za mara
kwa mara. Homa hizi zilisbabisha kuathirika na kutetereka kwa afya zao ambako
kuliwaathiri kisaikolojia pia. Wakaanza kuukumbuka mji wao waliozaliwa na
kuishi hapo na kuizoea hali yake ya hewa na maisha yake. Fikra na kumbukizi
hizi ziikawatumbukiza katika dimbwi la utungaji na uimbaji wa mashairi ya kuusifia
mji wao waliolazimika kuuhama kwa ajili tu ya Imani yao. Walifanya hivi kwa
lengo la kujiliwaza kutokana na maisha haya ya ugenini waliyomo na hali hii
ya hewa inayowasumbua. Hali ilipozidi na kuwafanya Muhajirina hawa kusindwa
kustahamili, walimwendea Bwana Mtume kumshitakia hali yao hiyo. Nae Mtume wa
Allah Rehema na Amani zimshukie akawa hana la kufanya ila kumuelekea Mola
wake, akaomba: “Ewe Mola wa haki wee! Tupendezeshee sisi Madinah kama
ulivyotupendezeshea Makkah na zaidi. Na utubarikie katika vibaba na pishi
zake, na uyahamishie maradhi yake juhfah.” Mwenyezi Mungu Mtukufu akajibu dua
ya Mtume wake, hali ya hewa ya Madinah ikawa nzuri na waislamu wakaupenda mno
mji wa Madinah na wakaishi humo kwa amani na furaha.
iii/. UJENZI WA MSIKITI WA MTUME.
Mahala
alipokita magoti ngamia wa Mtume wakati anaingia mjini Madinah palikuwa ni
uwanja unaomilikiwa na vijana wawili yatima. Uwanja huu ndio aliouchagua
Mtume wa Allah Rehema na Amani zimshukie kuwa ndio mahala pa kuujenga
misikiti wake. Mahala hapa lilikuwa ndio chaguyo la Mtume kutokana na ilhamu
ya Mola wake. Mahala hapa palikuwa ni uwanja mpana uliokuwa ukitumika kama
maanikio/makaushio ya tende baada ya kuvunwa. Katika uwanja huu kulikuwepo na
baadhi yta miti ya mitende na miti mingine. Pia yalikuwepo baadhi ya makaburi
ya zamani ya mushrikina yaliyokuwa hayatumiki tena na mashimo machache
yaliyokuwa madimbwi ya maji. Mtume aliumiliki uwanja huu kwa kuununua kwa
wamiliki wake wa mwanzo ambao walikuwa ni vijana wale yatima, japokuwa wao
walikuwa radhi kumpa bura, lakini yeye hakuridhia ila kuununua. Baada ya
kuumiliki uwanja ule kihalali, ndipo shughuli nzima ya Ujenzi wa msikiti
ilipoanza. Mtume akaamrisha miti yote iliyokuwepo ikatwe, makaburi yote
yafukulwe na mifupa itakayotolewa ikazikwe sehemu nyingine na mashimo yote ya
maji yafukiwe na ardhi isawazishwe. Baada ya kutekelezwa yote haya ndipo
Mtume akaianza kazi ya Ujenzi wa msikiti wake. Huu ulikuwa ni msikiti wa
kawaida kabisa, haukuwa na sura ya misikiti yetu ya leo. Kimo chake kilikuwa
ni dhiraa 35 na upana dhiraa 30. ukuta uliolizunguka jingo urefu wake
haukuzidi kimo cha mtu mzima wastani wa kimo kusimama na kunyoosha mkono.
Msingi wake ulikuwa ni wa mawe, kuta zake ziliundwa na matofali ya udongo.
Msikiti ulikuwa na milango mitatu, mmoja upande wa mashariki na mwingine
upande wa magharibi na ule uliokuwa nyuma upande wa kusini. Katika upande huu
wa nyuma kulishushwa kipaa cha makuti ya mitende kikiegemea magogo ya
mitende. Sehemu hii ya msikiti ilijulikana kama “Swufah” ndipo palipokuwa makazi
ya maswahaba mafakiri, wakitunzwa na kuhudumiwa na mwenyewe Bwana Mtume. Wale
wote waliokuwa wakiishi mahala hapa walijulikana kama “Ahlus swufah” na
miongoni mwao akiwa ni mpokezi mkubwa wa hadithi Bwana Abuu Hurayrah Allah
awawiye radhi wote. Ama sehemu nuyinine ya msikiti ukiiondoa hii iliwachwa
wazi bila ya kuezekwa. Sakafu ya msikiti ikabakia kuwa ni ardhi kama ilivyo
bila ya kuitandikwa cho chote. Sakafu ailibakia hivyo hivyo mpaka
iliponyeesha mvua usiku mmoja, ardhi ikawa imelowa na kuwa tope. Hapo ndipo
ikawa kila ajae anafuangasha vijikokoto kadhaa katika nguo yake, akavitandika
na kuswali juu yake. Mtume rehema na Amani zimshukie alipomaliza kuswali
akasema “Eeh, uzuri ulioje wa busati/tandiko hilo!”
Mtume
Rehema na amani zimshukie alishirikiana bega kwa bega na maswahaba wake
katika shughuli nzima ya ujenzi wa msikiti huu. Alikuwa akibeba mawe na
matofali mpaka kifua chake kikatapakaa vumbi. Jambo hili likazidi
kuwashajiisha maswahaba kufanya kazi kwa nguvu zao zote, huku wakijikuta
wakiimba ubeti huu wa shairi:
Na iwapo tutakaa na il-hali Mtume
afanya kazi,
Hicho kwetu ni kitendo cha upotevu.
Pamoja
na kuwa maswahaba walimsihi sana Bwana Mtume awaachie wao wamtoshee katika
kazi hiyo, lakini yeye hakuona raha ila awe mmoja wao. Akifanya kazi sawa na
wao na akiimba kama waimbavyo. Mmoja wa maswahaba wake akakutana nae akiwa
amebeba jiwe thaqili (zito), akamwambia: Nipe mimi ewe Mtume wa Allah.
Akikusudia kumsaidia, Mtume akamwambaia: “Nenda kachuke jingine, wewe sio
fakiri zaidi kwa Allaha kuliko mimi.” Watu wote, waliifanya kazi hii kwa
ukunjufu wa nyoyo na vifua, huku wakiimba beti mbalimbali za mashairi
kuashiria furaha yao kwa kazi hii tukufu ambayo waliijua vema thamani na kima
chake. Miongoni mwa beti zilizoimbwa ni huu.
Ewe Mola hapana kheri kama kheri ya
akhera,
Basi warehemu Answaari na
Muhajirina.
Ujenzi
ulipokamilika, Mtume akaufanya msikiti kuwa ni:-
· Kituo cha mikutano, akikutana humo na maswahaba kujadili na
hatimaye kutoa maamuzi ya pamoja juu ya masuala mbalimbali.
· Jengo la ibada, akiwaongoza kaswahaba katika ibada mama; swala na
kutoa humo khutuba za Ijumaa na za kadhia mbalimbali zilizokuwa zikijitokeza.
· Chuo/shule ya kutoa taaluma ya dini. Akiwafundisha humo maswahaba
masuala yote yahusianayo na dini yao kama mfumo mzima wa maisha.
· Mahakama, Akitoa humo hukumu mbalimbali kwa kesi zilizoletwa
mbele yake.
· Kituo cha misaada, akiwalea na kuwahudumia humo maswahaba
masikini.
· Idhaa, habari yo yote
iliyowahusu waislamu ahitangaza humo kwa sababu msikiti ndio uliokuwa
mahala pekee panapoweza kuwakusanya watu wote kwa wakati mmoja kwa hivyo
kuwezesha ujumbe kufika kwa walengwa kwa haraka na wepesi.
· Kambi ya jeshi, maandalizi yote ya jeshi la kiislamu, jeshi la
haki lililoligania dhidi ya batili aliyafanya humo.
· Huo ndio ulikuwa msikiti wa Mtume na hizo ni baadhi tu ya kazi
ngingi zilizofanywa na msikiti huo kama kituo cha kijamii
Mtume
Rehema na Amani zimshukie alipokuwa akiwahutubia maswahaba ndani ya msikiti
wake huu alikhutubu akiwa ameswimama akijiegemeza kwenye kigogogo cha mtende
Mtume aliendelea kukhutubu katika hali hiyo mpaka alipokuwa na umri mkubwa na
hivyo kushindwa kusimama muda mrefu. Hapo ndipo maswahaba wakamtengeneea
mimbari nyepesi ya mbao na ya kawaida kabisa isiyo na mapambo ya aina yo yot
ile. Mimbari hii ilikuwa na vidato viwili na sehemu ya kuakalia ambapo Mtume
alikaa mpaka anapotaka kuanza kukhutubu ndipo husimama chini ya vile vidato
viwili na akaanza kukhutubu. Msikiti huu haukuwa na taa zinazonurisha wakati
wa usiku, giza linaposhitadi walikuwa wakileta kuni na kuwasha moto ambao
uliwaangazia mpaka wakamaliza swala yao. Waliendelea na hali hii ya kuswali
kisa bila ya taa mpaka pale alipowajia Bwana Tamiym Addaariy akitokea shamu.
Huyu ndiye mtu wa kwanza aliyewasha taa na kuzitundika katika nguzo za vigogo
vya mitende zilizokuwemo msikitini humo. Kitendo hiki kilimfurahisha sana
Mtume wa Allah Rehema na Amani zimshukie, na akamwambia “Umeutia nuru msikiti
wetu, Allah akunawirishia nawe.”
Msikiti
huu uliendela kubakia na hali yake hii bila ya mabadiliko yoyote zaidi ya
kupanuliwa kidogo tu. Mtume aliufanya upanuzi huu kutokana na ongezeka kwa
idadi ya waislamu Madinah na msikiti kushindwa kukidhi haja. Upanuzi huu
ulifanyika katika mwaka wa saba wa Hijrah.
Makazi
ya Mtume.
Baada
ya Ujenzi wa msikiti kukamilika ndipo Bwana Mtume akaanza ujenzi wa makazi
yake akaanza kwa kujenga vyumba viwili pembezoni mwa msikiti, kimoja kikiwa
ni cha mkewe Bi Saudah Bint Zam-ah na kingine kilikuwa ni cha Bi Aysha Bint
Abuu Bakri. Mtume akaendelea kuyaongeza makazi yake kidogo kidogo kila
alipooa mke mwingine mpaka idadi ya vyumba vyake ikafikia tisa sawa na idadi
ya wake hao, Allah awawiye radhi wote. Baadhi ya vyumba hivi vilikuwa upande
wa kusini mwa msikiti na vingine upande ule wa mashariki. Makazi haya ya
Bwana Mtume yalikuwa katika hali ya kawaida kabisa inayolingana na maisha ya
watu wa tabaka la chini.
|