Makala
Uislamu-Utangulizi
Fiqhi na Sheria 
Akhlaaq-Tabia
Sira ya Mtume
Nasaha za dini
Maswali na Majibu
Uliza Suala la dini
Jiunge na Mtandao !!!

 

SIRA YA MTUME (SAW)  

"BILA SHAKA MNAO MFANO MWEMA KWA MTUME WA MWENYEZI MUNGU…"Al-qur-an (33:21)

IV) AHLUL BAYT WAHAMIA MADINA

Faida

Amesema Ibn Sa’ad - Allah amrehemu: “Mtume wa Allah alimtuma huru wake Zayd Ibn Haarithah na Abuu Raafii kwenda mjini Makkah kuwahamisha Ahli zake na akawapa ngamia wawili na Dir-ham mia tano (500) ziwasaidie safarini. (Wakarudi Madinah) na kumletea Fatma na Umuu kulthuum binti za Mtume wa Allah, na Bi. Saudah Bint Zum-ah mkewe (mtume). Ama Bi Rukia (Bint mwingine wa Mtume) yeye alikwa amekwisha hama zamani pamoja na mumewe: Uthman Ibn Affaan. Bi Zainab (bint ya Mtume )nae alizuiliwa na mumewe Abul-aaswi Ibn Ar-rabii kuondoka. Zayd Ibn Haarithah akamchukua mkewe, Umuu Ayman pamoja na mwanawe Usaamah. Abadallah Ibn Abuu Bakri ndiye aliyeondoka na watu hawa pamoja na familia ya Abuu Bakri akiwemo pia Bi. Aysha kuja Madinah. Akafikia nao katika nyuma ya Bwana haarithah Ibn An-numaan” Baada ya Ahulu Bayt na Mtume kuhama Madinah wakitokea Makkah ambako usalama wao ulikuwa hatarini. Mtume - Rehema na Amani zimshukie - aliendelea na shughuli yake aliyokuwa ameianza akiwa kama Mtume wa Allah na kiongozi wa mji huo wa madinah. Aliendelea kuratibu masuala yake na ya jamii ya maswahaba wake ili kuasisi jamii njema itakayopigiwa mfano kwa kila jambo jema. Jamii itakayojengwa katika misingi ya upendo, udugu, uadilifu, usawa, kusaidiana na kujitoa muhanga kwa jaili ya manufaa ya umma. Hii ndio misingi na nguzo imara za jamii njema iliyowekwa na mfumo sahihi wa maisha, uislamu ili jamii ya wanadamu mahala popote ilipo na zama zozote iwazo  iweze  kuishi ikiwa kama ndugu moja yenye kusaidiana ikitawaliwa na mshikamano wa kidungu na kufunikwa na wingu la amani na salama. Hii ndio iliyokuwa sera na siasa aliyoitumia Mtume wa Allah- Rehema na Amani zimshukie ili kuhakikisha kuwa anaasisi jamii njema, yenye utu kamili: ‘NA SHIKAMANANENI KWA KAMBA (dini) YA ALLAH NYOTE, WALA MSIACHANE. NA KUMBUKENI NEEMA YA ALLAH ILIYO JUU YENU., (zamani) MLIKUWA MAADUI, NAYE AKAZIUNGANISHA NYOYO ZENU, HIVYO, KWA NEEMA YAKE, MKAWA NDUGU………………………..(3: 103).

 

SOMO LA TATU

i.  ATHARI ZA HIJRAH KWA WATU WA MADINAH.

MADINAH YAANZA UKURASA MPYA WA MAISHA, MAISHA YA AMANI NA UTULIVU BADALA YA MAISHA YA VITA NA UADUI.

Mji wa Madinah (Yathrib) ulikuwa ukikaliwa na watu wenye asili tofauti waliosheheni chuki za ukabila, wenye itikadi tofauti, kila kundi likijiona bora kuliko jingine. Kila kundi likitumia nguvu na rasilimali zote kuhakikisha kuwa linakuwa bwana na mtawala wa makundi mengine. Mayahudi “Ahlul-Kitaab” walikuwa ni sehemu ya jamii ya wakazi wa Madinah. Jamii ya mayahudi wa madinah iliundwa na makabila matatu, Baniy Nadhwiyr, Baniy Quraydhwah na Baniy Qayunqaa, kila kabila likiwa  limegawanyika katika koo kadhaa. Hawa ndio waliokuwa wakitawala kwa miongo kadhaa uchumi wa mji wa Madinah. Walishika hatamu katika nyanja za kilimo na biashara. Jamii nyingine ya wakazi wa Madinah, ilikuwa ni jamii ya Waarabu washirikina iliyoundwa na makabila mawili makuu, Ausi na Khazraj ambayo pia yalikuwa yanaundwa na koo kadhaa. Historia inaonyesha kwamba waarabu hawa walifika madinah mwishoni mwa karne ya nne (4) ya Miladia (4th C A.D) wakitokea nchini Yemen. Kwa kiasi kikubwa ustadi wa kilimo waliokuwa nao Mayahudi walijifunza kutoka kwa waarabu hawa. Makundi haya mawili, Mayahudi na Waarabu hayakuwa na mafungamano mazuri baina yao. Bali ndani ya makundi haya pia hakukuwepo masikilizano na maelewano baina ya wenyewe kwa wenyewe. Waarabu waligawika katika makundi pinzani kama ilivyokuwa kwa upande wa Mayahudi pia. Moto wa uadui na chuki baina ya kundi na kundi ulikuwa ukiwaka mara kwa mara katika mji wa Madinah. Ushindani na ugombeaji wa maslahi ndio uliokuwa kwa kiasi kikubwa mafuta na kuni za moto huu uliokuwa ukiziangamiza na kuzivuna roho za wakazi wa Madinah. Ausi na Khazraj walipofikishwa bidhaa adimu, ghali, yenye faida kubwa, yaani ujumbe wa Uislamu, dini pekee iliyoridhiwa na Allah kwa wanadamu wote “……………….NA NIMEKUPENDELEENI (nimekuridhieni) UISLAMU UWE DINI YENU…………….” 5: 3

“BILA SHAKA DINI (ya haki )MBELE YA ALLAH NI UISLAMU………” (3: 19)

wakakubali kuinunua bidhaa hii  kwa thamani ya mali na nafsi zao: “ALLAH AMENUNUA KWA WAUMINI NAFSI ZAO NA MALI ZAO( wote nafsi na mali zao katika kupigania dini hii) ILI NA YEYE AWAPE PEPO. WANAPIGANA KATIKA NJIA YA ALLAH, WANAUA NA WANAUAWA …………..” (9: 111)

wakasilimu na kuwa waislamu wa kweli, wanyenyekevu na watiifu kwa Allah na Mtume wake, wakiliitikia agizo la Mola Wao. :” ENYI MLIOAMINI! MTIINI ALLAH NA MTUME WAKE NA WENYE MAMLAKA JUU YENU, WALIO  KATIKA NYIE (waislamu wenzenu)………….” (4: 59)

hawa kwa pamoja wakaunda kundi lenye nguvu itokanayo na imani ya kweli, kundi la Answaar alilolitaja Allah ndani ya kitabu chake kitukufu: “ ………….NA WALE WALIOWAPA (Muhajiri) MAHALA PA KUKAA ( nao ni Answaar) NA WAKAINUSURU (dini ya Allah, ) HAO NDIO MARAFIKI, WAO KWA WAO……………” (8: 72).

Kundi hili likazidi kuimarika zaidi pale ndugu zao Muhajirina waislamu makurayshi walipojiunga nao kama wakimbizi wa Imani kutoka Makkah. Hawa ndio wanaotarajwa na kauli ya Allah: “ HAKIKA WALE WALIOAMINI NA WAKAHAMA NA WAKAPIGANIA DINI YA ALLAH KWA MALI ZAO NA NAFSI ZAO…………..’ (8: 72).

Hili likawa ni kundi jipya kuzaliwa katika jamii  ya wakazi wa Madihan, kundi la waislamu. Kundi hili likaigeuza kabisa sura yakisiasa ya Madina. Madinah sasa ikawa ni ya makundi mawili, kundi la haki (waislamu) na kundi la batili (mayahudi - mushrikina). Kundi la haki likitazamwa na makafiri kama adui mkubwa. “HAKIKA UTAWAKUTA WALIO MAADUI ZAIDI KULIKO WATU(wengine) KWA WAISLAMU NI MAYAHUDI NA WALE MUSHRIKINA (Wasiokuwa na kitabu)…………..”  (5: 82)

Hivi ndivyo Mtume wa Allah - Rehema na Amani zimshukie alivyoukuta mji wa Madinah ukiwa na mchanganyiko wa makundi na itikadi tofauti za kishirikina. Makundi  ambayo hayafungamanishwi na nidhamu (utaratibu/mpango) moja ya maisha, hayana umoja wala mshikamano. Bwana Mtume akaiona hatari ya mchanganyiko huu wa imani potofu, chuki za kikabila na ugombeaji wa madaraka, hapa ndio pakawa mahala pa kuanzia. Mjumbe wa Allah akafanya kazi na juhudi kubwa katika kuibadilisha jamii hii kutoka katika mfumo mbaya na mbovu wa maisha kuipeleka katika mfumo shaihi wa maisha, wenye amani waliochaguliwa na Mola Muumba wao. Akapanga mikakati ya kuiunganisha jamii ile iliyogawanyika katika misingi ya ukabila na kuikusanya pamoja dini ya chuo kikuu cha utu. Akaasisi moyo wa kushirikiana na kusaidiana katika misingi ya udugu wa kiislamu ambao huwafanya waislamu kuwa ndugu moja: “ KWA HAKIKA WAISLAMU WOTE NI NDUGU………” (49: 10)

Udugu huu uliimarishwa zaidi na uhusiano alioujenga, uhusiano baina ya muislamu na Muumba wake, uhusiano baina ya muislamu na muislmau mwenziwe na uhusiano baina ya muislamu na asiye muislamu.`

 

a./. UHUSIANO BAINA YA MUISLAMU NA ALLAH.

Uhusiano  huu baina ya mja na Mola wake ulijengwa katika misingi ya kumuabudu yeye pekee bila ya kumshirikisha na chochote kiwacho.

“MWABUDUNI ALLAH WALA MSIMSHIRIKISHE NA CHOCHOTE…….” (4: 36) juu ya itikadi ya kuwa YEYE ALLAH ndiye Bwana Mlezi wa viumbe vyote: “SHUKRANI ZOTE ANASTAHIKI ALLAH, MOLA WA WALIMWENGU WOTE” (1:2)

“……………….BWANA MWENYE KUWALEA. MFALME WA WATU. MUABUDIWA WA WATU”  (114: 1-3)

waitakidi kwamba Allah ndiye muumba anayeruzuku, anayehuyisha na kufisha. Ni yeye pekee tu anayeweze kudhuru na kunufaisha na ni yeye pekee anayestahili kuabudiwa, kunyenyekewa na kuombwa msaada na wafanye amali zao zote kwa ajili ya kutaraji radhi zake tu.

 

b./. UHUSIANO BAINA YA MUISLAMU NA NDUGUYE MUISLAMU.

Msingi wa uhusiano huu ni udugu na kiimani  ambao Bwana Mtume aliufanya kuwa juu ya udugu wa nasabu/damu, akimtegemezea kauli ya Allah: KWA HAKIKA WAISLAMU WOTE NI NDUGU…………….’ Naye Mtume akaifasiri kauli hii ya Mola wake kwa kusema: “Muislamu ni ndugu ya Muislamu, hamdhulumu na wala hamsalimishi (kwa makafiri). Na atakayemsaidia nduguye naye atapata msaada wa Allah, na atakayemuondoshea muislamu  mwenziwe matatizo (shida), Allah atamuondoshea mtu huyo matatizo/shida miongoni, mwa matatizo ya siku ya kiyama. Na mwenye kumsitiri muislamu mwenziwe naye atasitiriwa na Allah siku ya Kiyama”Bukhaariy na Muslim.

 

Ni kutokana na msingi huu ndio Bwana Mtume Rehema na Amani zimshukie akaunga udugu baina ya Muhajirina (wakimbizi wa Imani) na Answaar (wasaidizi/watetezi wa imani). Kila muhajiri awa na nduguye wa imani Muanswaar. Muanswaar akagawana mali, nyumba na shamba na nduguye muhajiri nusu bin nusu. Undugu huu ukawafikisha mahala pa muanswaar kuwa tayari taliki mmoja wa wakeze ili aolewe na nduguye Muhajiri kama alivyofanya hivyo Sa’ad Ibn Rabii (Muanswaar) kwa nduguye Muhajir, Abdul-Rahman Ibn Auf. Answaar wakapiga mfano wa udugu uiso na mithili katika historia nzima ya mwanadamu, huu ndio udugu anaoutaja Allah ndani ya kitabu chake kitukufu. “ NA WALE WALIOFANYA MASKANI YAO HAPA (yaani madinah) NA WAKAUTAKASA UISLAMU (wao barabara) KABLA YA (kuja) HAO (Muhajiri huko Madinah) NA WAKAWAPENDA HAO WALIOHAMIA KWAO, WALA HAWAPATI, HAWAONI DHIKI NYOYONI MWAO KWA HAYO WALIYOPEWA (hao Muhajiri) NA WANAWAPENDELEA KULIKO NAFSI ZAO INGAWA WENYEWE WANA HALI NDOGO……………” 59:9)

Udugu huu ukakata kabisa mizizi ya ubaguzi na tofauti katika misingi ya ukabila, nasabu, rangi na utaifa. Hii ni aina pekee ya udugu katika historia ya jamii ya wanadamu.

 

c./. UHUSIANO BAINA YA MUISLAMU NA ASIYE MUISLAMU.

Mtume wa Allah Rehema na Amani zimshukie hakufanya kosa la kuitenga na kuibagua jamii ya wasiokuwa waislamu. Bali alihakikisha kuwa kunakuwepo mafungamano na uhusiano usio na madhara baina ya waislamu na wasio waislamu (Mayahudi). Uhusiano huu aliujenga katika misingi ya ubinadamu ambao   unamuunga na kumjumuisha pamoja bianamu na binadamu mwenzie. Mizani ya udugu huu ikawa ni kauli yake Mtume: “Wapendelee watu uyapendayo wewe”.Bukhaariy.

 

Hii ni kutokana na kutambua kwake Bwana Mtume kwamba watu pamoja na tofauti ya jinsia na itikadi zao, wanategemeana katika haja zao mbalimbali za kimaisha ya siku hata siku. Kwa hivyo ni lazima wawe pamoja, washirikiane na wasaidiane. Na hapana njia ya kusaidiana na kushirikiana ila chini ya njia ya mwavuli salama, amani na utulivu. Na amani na utulivu havitapatikana mpaka jamii ya wanadamu itawaliwe na hisia za udugu upendo na mafungamano ya kibinadamu. Chini ya hisia hizi kila mtu ataheshimu utu, hadhi na itikadi ya mwenziwe. Ili kuonyesha kuwa Mtume wa Allah anajali na kuthamini utu, heshima na imani ya watu wengine aliandikiana mkataba na Mayahudi. Mkataba huu uliwapa Mayahudi uhuru kamali wa kuabudu kwa mujibu wa itikadi yao. Waislamu na Mayahudi wawe kitu kimoja dhidi ya adui yeyote atakayeishambulia Madinah. Mtu yoyote, muislamu au muyahudi ana haki ya ama kuishi Madinah au kokote kule akutakako.


TUJIFUNZE NA TUKUBALI  kuwa: Uislamu ni dini inayokubali kuishi na kuchanganyika na watu wa dini nyingine maadam hawaupigi vita Uislamu. “ALLAH HAKUKUKATAZENI KUWAFANYIA IHSANI NA UADILIFU WALE AMBAO HAWAKUPIGANA NANYI KWA AJILI YA DINI WALA HAWAKUKUFUKUZENI KATIKA NCHI ZENU. HAKIKA ALLAH ANAWAPENDA WAFANYAO UADILIFU”  (6: 8).


Forum | Guestbook | Tuandikie |