|
Tumeona kwamba miongoni mwa wakazi wa Madinah yalikuwemo
makundi ya Mayahudi. Mayahudi hawa walikuwa si watu wa kupuuzwa hata kidogo,
kwani walikuwa na nguvu za kijeshi na kiuchumi, Bwana Mtume alilitambua vema
hili. Kwa upande wa kijeshi mayahudi walikuwa na ngome imara zilizouzunguka
miji yao huku ikilindwa na askari mahiri wenye zana bora na za kutosha.
Qur-ani Tukufu inazitaja ngome zao hizi na nguvu yao: “YEYE NDIYE ALIYEWATOA
WALIOKUFURU MIONGONI MWA WATU WA KITABU (Mayahudi wa Kibanin-Nadhwir) KATIKA
NYUMBA ZAO (huko Madinah); WAKATI WA UHAMISHO (wao) WA KWANZA. HAMKUDHANI YA
KUWA WATATOKA (kwa nguvu zao walizokuwa nazo Madinah) NAO WALIDHANI KUWA NGOME
ZAO ZITAWALINDA NA (kufikwa na amri ya) ALLAH, LAKINI ALLAH ALIWAJIA KWA
MAHALA WASIPOPATAZAMIA, NA AKATIA WOGA KATIKA NYOYO ZAO (wasiweze kupigana na
waislamu walipokuja kupigana nao)…” [59:2]
Kwa nyanja ya uchumi mayahudi walimiliki mashamba makubwa
na asilimia kubwa ya biashara.Mayahudi wa Baniy Qayunqaa waliishi katika
kitovu cha mji wa Madinah wakijishughulisha na kazi ya usonara. Kadhalika
walimiliki soko kuu mjini Madinah.
Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie- aliiona hatari
hii ya ndani inayoukabili Uislamu. Akaamua kutumia siasa ya ujirani mwema na
amani ili apate amani ya ndani, itakayomsaidia kupambana na adui wa nje. Mtume
akaanzisha mazungumzo ya amani baina yake na mayahudi, akajitahidi sana
kutumia lugha ya kirafiki na maridhiano na kuustahamilia ufedhuli na ujeuri
wao. Akajikurubisha sana kwao kwa kushirikiana nao katika baadhi ya matukufu
ya dini yao ambayo hayakhalifiani na Uislamu. Akajumuika nao katika swaumu ya
Ashuraa waliyokuwa wakiiadhimisha kila mwaka. Swahaba wa Mtume, Ibn
Abbas-Allah amuwiye radhi-anatuambia kuhusiana na swaumu hii ambayo asili
(chimbuko) yake ni mayahudi anasema: “Mtume wa Allah-Rehema na Amani
zimshukie-alipofika Madinah aliwakuta mayahudi wakifunga siku ya Ashura(mwezi
10 Muharram). Mtume akawauliza: Ni siku gani hii muifungayo? Wakamjibu: Hii ni
siku tukufu, ni siku ambayo Allah alimuokoa Musa na watu wake na kumgharikisha
Fir-aun na jeshi lake. Musa aliifunga siku hii kwa kumshukuru Allah, na sisi
ndio tunaifunga (kuadhimisha tukio hilo). Mtume wa Allah-Rehema na Amani
zimshukie-akasema: Sisi tuna haki zaidi (ya kumfuata Musa) kuliko nyinyi,
Mtume akaifunga (siku hiyo) na akawaamrisha maswahaba wake kuifunga”.
Bukhaariy & Muslim.
Kadhalika wakati wa swala Bwana Mtume alielekea
Baytil-Maqdis (Jerusalem) kama walivyokuwa wakielekea wao. Akaheshimu uhuru
wao wa kuabudu kwa mujibu wa taratibu na sheria za dini yao. Akaheshimu haki
yao ya kuishi na kumiliki mali. Akawafungulia wazi mlango wa ushirikiano
katika kuuhami mji wao wa Madinah dhidi ya maadui wa nje. Bwana Mtume-Rehema
na Amani zimshukie-aliyafanya yote haya kwa lengo la kujenga mazingira ya
uhusiano bora na hali ya kuaminiana ili amani itawale Madinah.
Lakini wapi, mayahudi ni mayahudi tu hata ukiwafanyia
nini! Juhudi hizi za Bwana Mtume zikawa kama mavumbi yapeperushwayo na upepo
na mayahudi wakaziona kama ni njia ya Bwana Mtume kutaka kujipendekeza kwao.
Moto wa hasadi ya kuhama utume kutoka kwao na kwenda kwa waarabu ulikuwa
ukiwaka nyoyoni mwao. Mbele yao kulikuwa hakuna maji ya kuuzima moto huo ila
ni kwa waislamu kurejea ukafirini baada ya kupata neema ya Imani (Uislamu).
Likawa lengo lao na lengo la mushrikina ni moja; kuutokomeza Uislamu, Allah
anawataja mayahudi na wenzao mushrikina: “HAWAPENDI WALIOKUFURU MIONGONI MWA
WATU WALIOPEWA KITABU (nao ni mayahudi na manaswara) WALA WASHIRIKINA,
MTEREMSHIWE KHERI KUTOKA KWA MOLA WENU. NA ALLAH HUMTEREMSHIA REHEMA ZAKE
AMTAKAYE NA ALLAH NI MWENYE FADHILA KUBWA KABISA”. [2:105]
“HAWATAKUWA RADHI JUU YAKO MAYAHUDI WALA MANASWARA
MPAKA UFUATE MILA YAO…” [2:120]
Moto huu wa hasadi na uadui ukazidi kuwaka pale walipoona
nguvu ya Mtume inarudufika na dini yake kudhihiri na kuenea. Hapo sasa
wakashindwa tena kujimiliki na kuidhibiti chuki na uadui waliouficha nyoyoni
mwao. Wakaianika wazi hasadi yao dhidi ya Mtume na Uislamu, wakaanza kumfanyia
vitimbi namna kwa namna. Mtume akaamua kuchukua juhudi za mwisho ili
kuhakikisha kuwa kuna maridhiano na hali ya maelewano baina yao. Akaandikiana
nao mkataba wa amani ambao ulilenga:
q
Kuacha vita na uadui baina yao.
q
Kuacha kushirikiana na maadui wa pande mbili hizo dhidi ya
upande mmoja.
q
Kupigana bega kwa bega na ye yote atakayeishambulia Madinah.
q
Kila mmoja aabadu kwa mujibu wa imani yake bila ya kubughudhiwa.
Haya ndiyo yaliyokuwemo ndani ya mkataba huu wa amani
baina ya Mtume na mayahudi wasio na ahadi. Je, mayahudi waliuheshimu mkataba
huu? Endelea kufuatana nasi katika mfululizo wa darasa hizi ili upate jawabu
kaafi ya swali hili.
WANAFIKI WALIDHIHIRISHA UISLAMU NA KUFICHA UADUI WAO.
Wanafiki ni wale ambao husema wameamini kwa vinywa vyao
na ilhali nyoyo zao zimebakia katika ukafiri. Hawa huswali kama wanavyoswali
waislamu, hufunga kama wanavyofunga waislamu. Hushirikiana pamoja na waislamu
katika matukufu ya kidini, wao katika sura ya nje ni waislamu safi tena
wakereketwa. Lakini batini yao imeficha chuki na uadui dhidi ya Uislamu na
waislamu. Hii ndio Qur-ani Tukufu na sura ya wanafiki: “NA KATIKA WATU WAKO
(wanafiki) WASEMAO: TUMEMUAMINI ALLAH NA SIKU YA MWISHO, NA HALI YA KUWA WAO
SI WENYE KUAMINI.WANATAFUTA KUMDANGANYA ALLAH NA WALE WALIOAMINI, LAKINI
HAWADANGANYI ILA NAFSI ZAO, NAO HAWATAMBUI. NYOYONI MWAO MNA MARADHI, NA ALLAH
AMEWAZIDISHIA MARADHI. BASI WATAKUWA NA ADHABU IUMIZAYO KWA SABABU YA KULE
KUSEMA KWAO UWONGO”. [2:8-10]
Hili ni kundi hatari sana ni mithili ya chui aliyejivisha
ngozi ya mwanakondoo ndani ya kundi la wanakondoo. Hatari yao inatokana na
kule kujichanganya kwao na waislamu wakajipamba na mapambo na matendo ya
dhahiri ya Uislamu, kiasi cha kushindwa kuwatambua wawapo pamoja na waumini.
Hili analithibitisha Allah ndani ya Qur-ani: “…NA KATIKA WENYEJI WA
MADINAH (pia kuna wengine wanafiki) WAMEBOBEA KATIKA UNAFIKI (hata) HUWAJUI
(kuwa ni wanafiki) SISI TUNAWAJUA. TUTAWAADHIBU MARA MBILI, KISHA WATARUDISHWA
KATIKA ADHABU KUBWA”. [9:101]
Kutokana na ukubwa wa hatari yao, Allah amewaandalia pia
adhabu kubwa na kali: “BILA SHAKA WANAFIKI WATAKUWA KATIKA TABAKA YA CHINI
KABISA KATIKA MOTO. HUTAMKUTA KWA AJILI YAO MSAIDIZI (yo yote)”. [4:145]
Kwa nini wanafiki walikuwa na chuki kwa Uislamu na
waislamu? Yalikuwepo makundi mengi ya wanafiki, lipo kundi lililoubughudhi
Uislamu kwa kuona kuwa Uislamu unalikosesha manufaa na maslahi yake kutokana
na sera ilizoleta. Lilikuwepo pia kundi lililouona Uislamu kama ni tishio na
hatari kuu dhidi ya dini yao. Yaani mfumo wao wa maisha unaofuata itikadi za
kishirikina. Pia lilikuwepo kundi lilouchukia na kuupiga Uislamu vita vya
ndani kwa ndani kutokana na kusikiliza propaganda za mayahudi, zilizolenga
kuupaka matope na kuutia dosari Uislamu. Kadhalika lilikuwepo kundi ambalo
lilikuwa na chuki binafsi, hili lilimuona Mtume na maswahaba wake kama ni
wahamiaji haramu waliokuja kuharibu mila na tamaduni zao. Hivyo ni lazima
watumie mbinu za makusudi kuhakikisha kuwa Mtume na maswahaba wanarudi kwao.
Makundi yote haya ya wanafiki yalikuwa yakitazamia ushindi wa Uislamu dhidi ya
mayahudi, washindani wao wakuu. Wanafiki walipoona Uislamu unazidi kupata
nguvu siku hata siku, wakajiingiza katika Uislamu ili wapate kichaka cha
kujificha na kuuhujumu Uislamu bila kujulikana. Wakafanikiwa kujipenyeza na
kuingia katika safu za waislamu na kupata fursa ya kujua siri za waislamu na
kuziuza kwa maadui. Kwa mtindo huu, wanafiki wakawa ni hatari zaidi kwa
waislamu kuliko mayahudi na mushrikina. Kundi hili la wanafiki liliongozwa na
Abdullah Ibn Ubayyi Ibn Saluul. Wataalamu wa mambo ya Sira na Tarekh
(historia) wanaeleza sababu iliyomsukuma mtu huyu kuuchukia Uislamu na kuamua
kuliongoza kundi hili pinzani, kundi hatari sana, wanasema: “Hakika Abdullah
Ibn Ubayyi Ibn Saluul ndiye aliyekuwa kiongozi wa wanafiki. Sababu
iliyompelekea kuufanyia uadui Uislamu ni kwamba wazalendo wa Madinah; Ausi na
Khazraji walitaka kumtawaza ufalme ( awe mfalme wao). Hili likipangwa
kutekelezwa na wakati huo huo ndio Mtume-Rehema na Amani zimshukie-akawasili
Madinah. Walipomuamini Mtume na kuisadiki da’awah yake, walilitupilia mbali
lile suala la kumtawaza Abdullah Ibn Ubayyi na wakauelekeza utii wao wote kwa
Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie. Jambo hili likaweka mfundo katika
nafsi ya Abdullah Ibn Ubayyi na akawa anamtazama Mtume wa Allah kwa jicho la
chuki. Chuki hii ikamsukuma kutokumuamini Mtume, akaendelea kubakia na imani
yake ya kishirikina mpaka pale waislamu walipopata ushindi mkubwa katika vita
vya Badri mnamo mwaka wa pili wa Hijrah. Alipoona Uislamu unazidi kupata
ushindi na kuenea kwa kasi ya kutisha, akawaambia wafuasi wake: “Hii sasa
ndio fursa”. Hapo ndipo walipojiingiza ndani ya Uislamu kwa lengo la
kuuhujumu kwa ndani na bila ya kujulikana upesi.
|