|
SOMO LA KWANZA
I/. RUHUSA YA KUPIGANA.
UISLAMU HAURUHUSU VITA
ILA KWA AJILI TU YA KULINDA NA KUTETEA IMANI.
Mtume wa Allah-Rehema na
Amani zimshukie-aliendelea kulingania dini kwa nguvu za hoja na kubashiri na
kukhofisha katika mji wa Makkah, kwa kipindi kisichopungua miaka kumi na tatu.
Katika kazi yake hii, Makurayshi walimpinga vikali kabisa na kumfanyia kila
aina ya maudhi na madhila. Pamoja na maudhi yote hayo, bado Bwana Mtume na
maswahaba wake waliendelea kustahamili na kusubiri bila ya kujibu. Walifanya
hivyo wakiamini kuwa wanaitii amri ya Mola wao: “BASI SUBIRI KAMA
WALIVYOSUBIRI WALE MITUME WENYE USTAHAMILIVU(kama Nabii Nuhu, Ibrahimu, Musa
na Isa)WALA USIWAHIMIZIE (adhabu)…” [46:35]
Makurayshi hawakutosheka
na maudhi tu bali wakifikia hatua ya kupanga njama za kumuua Mtume na
kuwafyagilia mbali maswahaba wake. Ni njama hizi ndizo zilizomlazimisha Bwana
Mtume kuukimbia mji wa Makkah na ilhali anaupenda na kwenda kuishi uhamishoni
Madinah. Makurayshi bado hawakuridhika na kutoka kwa Mtume Makkah na kuhamia
Madinah, wakazielekeza nguvu zao za uadui huko huko Madinah.
Kwa hatua hii sasa ikawa
hapana budi tena Uislamu utetewe, ulindwe na kuhamiwa dhidi ya kila
aliyejitokeza kama adui. Ni lazima sasa ziwepo hatua na juhudi za makusudi za
kulinda heshima, uhuru, amani na utulivu wa waislamu. Waislamu wakiwa na haki
na uhuru wa kuabudu kwa mujibu wa dini yao bila ya kuingiliwa au kubughudhiwa
na mtu ye yote, hapo tena Mtume aseme: “…HUU NI UKWELI ULIOTOKA KWA MOLA
WENU, BASI NA ANAYETAKA NA AAMINI NA ANAYETAKA NA AKUFURU…” [18:29]
Kwani: “HAKUNA
KULAZIMISHWA (mtu kuingia)KATIKA DINI. UONGOFU UMEKWISHA PAMBANUKA NA
UPOTOFU…” [2:256]
Ni kwa ajili tu ya
kulinda imani na uhuru wao wa kuabudu ndio Allah akawapa sasa idhini ya
kupigana. Wapigane tu kwa ajili ya kujitetea wao wenyewe na itikadi yao. Hapa
sasa ndio zikaanza kushuka aya za jihadi zikiwa na mipaka maalumu.
Waumini wapigane na wale
tu wanaowapiga: “NA PIGANENI KATIKA NJIA YA ALLAH NA WALE WANAOKUPIGENI,
WALA MSIPINDUKE MIPAKA (mkawapiga wasiokupigeni) KWANI ALLAH HAWAPENDI WARUKAO
MIPAKA”. [2:190]
Waumini wapigane na wale
tu waliowatoa (waliowafukuza) makwao: “NA WAUWENI (hao wanaokupigeni bure)
PO POTE MUWAKUTAPO, NA MUWATOE PO POTE WALIPOKUTOENI KWANI KUWAHARIBU WATU NA
DINI YAO NI KUBAYA ZAIDI KULIKO KUUA. WALA MSIPIGANE NAO KARIBU NA MSIKITI
MTAKATIFU (wa Makkah) MPAKA WAKUPIGENI HUKO. WAKIKUPEGENI (huko) BASI NANYI
PIA WAPIGENI. NAMNA HIVI NDIVYO YALIVYO MALIPO YA MAKAFIRI”. [2:191]
Waumini wapigane tu na
wale ambao wanakuwa ni pingamizi na kikwazo cha kuueneza Uislamu: “NA
PIGANENI NAO MPAKA KUSIWE NA MATESO (fitna, wao kuwatesa waislamu bure) NA
DINI IWE KWA AJILI YA ALLAH TU. NA KAMA WAKIACHA BASI USIWEKO UADUI ILA KWA
MADHALIMU”. [2:193]
Waumini wenye nguvu
wapigane kwa ajili ya kuwatetea waumini wenzao wanyonge wanaoteswa na
makafiri: “NA MNA NINI HAMPIGANI KATIKA NJIA YA ALLAH NA (katika kuwaokoa)
WALE WALIO DHAIFU (wanyonge) KATIKA WANAUME NA WANAWAKE NA WATOTO AMBAO
HUSEMA: MOLA WETU! TUTOE KATIKA MJI HUU AMBAO WATU WAKE NI MADHALIMU, NA
TUJAALIE TUWE NA MLINZI ANAYETOKA KWAKO, NA TUJAALIE TUWE NA WA KUTUNUSURU
ANAYETOKA KWAKO”. [4:75]
Waumini wapigane katika
njia ya Allah tu: “WALE WALIOAMINI WANAPIGANA KATIKA NJIA YA ALLAH, LAKINI
WALIOKUFURU WANAPIGANA KATIKA NJIA YA SHETANI. HAKIKA HILA ZA SHETANI NI
DHAIFU”. [4:76]
Waumini wapigane na wale
wavunjao ahadi ya mkataba wa amani baada ya kuwatahadharisha natija ya kuvunja
ahadi: “NA KAMA UKIOGOPA KHIYANA KWA WATU (mliofanya nao ahadi) BASI WATUPIE
(ahadi yao) KWA USAWA, HAKIKA ALLAH HAWAPENDI MAKHAINI”. [8:58]
Haya ndiyo malengo na
ndio maeneo ambayo yanampa idhini na uhalali muislamu wa kuingia vitani kwa
mali na nafsi yake. Muislamu hapigani na ye yote ila tu pale itakapopatikana
mojawapo ya sababu hizi.
VITA KATIKA UISLAMU SIO
NJIA YA KUWALAZIMISHA WATU KUINGIA KATIKA DINI HII BILA YA RIDHAA YAO.
Msingi mkuu wa vita
katika Uislamu ni: “…NA WANAOKUSHAMBULIENI NANYI PIA WASHAMBULIENI KWA
KADRI WALIVYOKUSHAMBULIENI. NA MUOGOPENI ALLAH (msiongeze kuliko
walivyokufanyieni)…” [2:194]
Ye yote atakayewafanyia
uadui waislamu, akawapiga vita, waislamu nao wana haki ya kujibu mashambulizi
hayo. Ye yote atakayewafukuza na kuwatoa waislamu katika makazi yao, waislamu
nao wanapewa idhini ya kutetea na kulinda haki yao ya kuishi po pote katika
ardhi ya Mola wao. Ye yote atakayewafitini na kuwazuilia waislamu na dini yao,
basi atambue kwamba waislamu wanaambiwa na Mola wao: “…KUWAHARIBU WATU
(kuwazuilia watu) NA DINI YAO NI KUBAYA ZAIDI KULIKO KUWAUA…” Kwa msingi
huu awe na yakini kuwa waislamu wa kweli hawataweza kukaa kimya na kuangalia
macho tu mtu aichezee dini yao na kuwazuia kuufikisha ujumbe wa Mola wao, hili
ni muhali halitokuwa kamwe. Kutokana na maelezo haya utaoana kuwa lengo la
vita katika Uislamu ni kwa ajili ya:-
Kutokutoa nafasi ya
kuzuiliwa waislamu na dini yao.
Kutokufukuzwa waislamu
katika miji yao kwa sababu tu ya imani yao.
Kutokuvunjwa heshima na
utukufu wa dini ya Allah.
Kuwepo uhuru na haki ya
kuabudu bila ya kubughudhiwa na ye yote.
Kutokumzuia mtu kuingia
katika Uislamu kwa radhi yake.
Ilimradi vita katika
Uislamu viwe ni kwa ajili ya kuilinda na kuitetea dini ya Allah na neno lake
liwe juu na kushinda: “YEYE NDIYE ALIYEMTUMA MTUME WAKE KWA UONGOFU NA DINI
ILIYO YA HAKI ILI AISHINDISHE JUU YA DINI ZOTE…” [48:28]
Na inatakiwa taq-wa
(kumcha Allah) ndio iwe nembo na alama ya waumini katika hali zao zote:
“…NA MUOGOPENI ALLAH (msiongeze kuliko walivyokufanyieni) NA JUENI KWAMBA
ALLAH YU PAMOJA NA WANAOMUOGOPA”. [2:194]
Na vita vinatakiwa
vikome mara moja pale tu linapokomeleka lengo la vita hivyo: “…NA KAMA
WAKIACHA (kuwatesa bure) BASI USIWEKO UADUI ILA KWA MADHALIMU”. [2:193]
Tena waislamu wanatakiwa
wapupie zaidi mazungumzo ya amani ikiwa adui yao ataonyesha nia ya kuwa na
mazungumzo yenye kulenga kuleta amani baina ya pande mbili hizi hasimu: “NA
KAMA (hao maadui) WAKIELEKEA KATIKA AMANI,NAWE PIA IELEKEE NA MTEGEMEE ALLAH.
HAKIKA YEYE NDIYE ASIKIAYE (na) AJUAYE. NA KAMA WAKITAKA KUKUKHADAA BASI ALLAH
ATAKUTOSHELEZA…” [8:61-62]
Kwa mantiki hii basi,
utaona vita katika Uislamu haviko kwa ajili ya kuwalazimisha watu kuingia
katika Uislamu bila ya ridhaa zao. Wala si kwa ajili ya kupata ngawira na
manufaa vitani, si kwa lengo la kukalia ardhi na mali ya watu kwa mabavu. Si
kwa madhumuni ya kuwafanya watu watumwa, wala si kwa makusudi ya utawala,
wala….wala……Bali vita katika Uislamu; mfumo sahihi wa maisha ni kwa
ajili tu ya kulinda uhuru wa itikadi na kuhifadhi na kutetea heshima ya
waumini. Waumini wasiteswe na kudharauliwa kwa sababu tu ya imani yao.
Ama itikadi kwa maana ya
imani, kimaumbile ni kitu kisichokubali kulazimishwa na kupandikizwa kwa
nguvu. Wala huwezi kuilazimisha itikadi katika nafsi ya mwanadamu hata kwa
mtutu wa bunduki. Hiyo haitakuwa kamwe itikadi ya moyo bali itikadi ya mwili,
yaani sura tu ya itikadi na si dhati ya itikadi. Itikadi halisi na ya kweli ni
ile fikra/jambo linalokubaliwa na kuridhiwa na moyo kwa njia ya khiyari bila
ya kulazimishwa. Na hakutoshi tu kukubaliwa na moyo bali ni lazima pia akili
ishirikishwe na ilikubali jambo/fikra hiyo kwa nguvu za hoja. Kwa hivyo
matumizi ya nguvu siku zote si njia sahihi ya kupandikiza itikadi katika nyoyo
za watu. Hili Allah Mtukufu amelibainisha bayana katika kitabu chake kitukufu,
haya na tuukiri na kuukubali ukweli huu: “HAKUNA KULAZIMISHWA (mtu kuingia)
KATIKA DINI…” [2:256]
Akasema tena: “KWA
HAKIKA HII (Qur-ani) NI MAWAIDHA, BASI ANAYETAKA ATAJIFANYIA NJIA (nzuri ya
kwenda) KWA MOLA WAKE”. [73:19]
Akaendelea kusema: “NA
SEMA: HUU NI UKWELI ULIOTOKA KWA MOLA WENU, BASI ANYETAKA NA AAMINI NA
NAYETAKA NA AKUFURU…” [18:29]
Tena Allah Taala
akamuwekea Mtume wake mipaka katika kazi yake hiyo: “…SI JUU YAKO ILA
KUFIKISHA TU…” [42:48]
Akazidi kumwambia:
“HUKUWA WEWE ILA NI MUONYAJI TU”. [35:23]
Kadhalika
akamtahadharisha kufanya matumizi ya nguvu kuwa ndio njia/chombo cha kuwafanya
watu waamini, akamwambia: “BASI KUMBUSHA, HAKIKA WEWE NI MKUMBUSHAJI (tu).
WEWE SI MWENYE KUWATENZA NGUVU”. [88:21-22]
“NA KAMA ANGALITAKA
MOLA WAKO (kuwalazimisha kwa nguvu kuamini) BILA SHAKA WANGALIAMINI WOTE
WALIOMO AKTIKA ARDHI (hasibakie hata mmoja. Lakini Allah hataki kuwalazimisha
watu kwa nguvu) BASI JE, WEWE UTAWASHURUTISHA WATU KWA NGUVU HATA WAWE
WAUMINI? NA HAKUNA MTU ANAYEWEZA KUAMINI ISIPOKUWA KWA IDHINI YA ALLAH…”
[10:99-100]
Zaidi ya yote haya Allah
Taala alimlaumu Mtume wake kutokana na huzuni aliyokuwa nayo kutokana na
kutoamini kwa watu wake: “HUWENDA (wewe Nabii Muhammad) UTAANGAMIZA NAFSI
YAKO KWA SABABU HAWAWI WAISLAMU”. [26:3]
Aya zote hizi ni
ushahidi wa wazi kabisa kwamba matumizi ya nguvu hayakuwa na wala hayatakuwa
ndio chombo/njia ya kuwafanya watu waukiri na kuukubali Uislamu. Hakika
matumizi ya nguvu hayakuwa ila ni kwa ajili ya kupambana na wale watumiao
nguvu katika kuupinga na kuuzuia Uislamu. Ndio ikawa jino kwa jino ili kuwatia
adabu maadui hawa na kujilinda na shari lao.
Itikadi/imani ndio kitu
kitukufu kabisa anachokimiliki mwanadamu, kwa sababu ndio kitu pekee
kinachomtofautisha mwanadamu na hayawani wengine. Kwa mantiki hii kuichezea
imani/itikadi ya mtu ni kuuchezea utu wake. Uislamu kwa kuutambua umuhimu na
thamani ya imani, ukafanya kuizuia/kuishambulia imani ni kosa/hatia/jinai
kubwa zaidi kuliko jinai ya kutoa uhai wa mtu. Kwa kulizingatia hili ndio
ikawa: “…KUWAZUILIA WATU NA DINI YAO NI KUBAYA ZAIDI KULIKO KUWAUA…”
[2:191]
Na ikawa waumini
kuilinda, kuitetea na kuihami itikadi/imani yao ni jambo lisiloepukika na ni
dharura isiyokimbilika.
|