|
II/. VIKOSI VYA KIJASUSI VYATUMWA KUCHUNGUZA NYENDO ZA ADUI.
Wanasira na wanatarekh (wanazuoni wa fani za Sira naTarekh)
wana istilahi (terminologies) wanazozitumia wanapoandika habari zihusianazo na
vikosi vya vita vya Mtume. Hutumia neno “sariyah” kumaanisha kikosi cha
vita ambacho mtume hakuwemo. Na kile kikosi alichoshiriki Mtume hukiita
“ghaz-wah”, hata kama hayakutokea mapambano. Vita/mapambano hayakuwa ndio
lengo la vikosi hivi, hili linathibitika kutokana na idadi ndogo iliyounda
vikosi hivi. Idadi hii ndogo haikutosha kuvipa vikosi hivi uwezo wa kuanzisha
mapambano. Kwa hivyo basi itakudhihirikia kuwa lengo khasa la kutumwa vikosi
hivi, ilikuwa ni kuchunguza nyendo na harakati za adui. Wakati mwingine
yakitokea mapambano mepesi yaliyohusisha urushianaji wa mishale, pale vikosi
hivi vinapokutana na adui ana kwa ana. Waumini waliyatumia mapambano hayo
kumtia khofu adui yao na kumfanya awe na hisia kwamba waislamu wana nguvu na
uwezo wa kukabiliana nae.
Tafiti zilizofanywa na wanasira na wanatarekh zinaonyesha kuwa
kimsingi lengo la kuundwa na kutumwa kwa vikosi hivi lilikuwa:-
Kuunda nguvu za kijeshi zitakazokuwa zikizunguka baina ya
Madinah na Makkah. Kwa lengo la kuhakikisha kuwa mji wa Madinah hauvamiwi na
kushambuliwa ghafla.
Kuwakaribia Makurayshi kwa mashambulizi mepesi ya ghafla
yatakayokata mawasiliano baina ya Makkah na Shamu. Kukatika kwa mawasiliano
baina ya pande mbili hizi hakutamaanisha kingine zaidi ya kudhoofika nguvu za
Makurayshi za kiuchumi na kijeshi.
Vikosi hivi viliwafanya Makurayshi kuwa katika hali ya
tahadhari kila mara na hivyo kuwaondoshea hali ya utulivu na amani. Ikawa sasa
wanatumia gharama maradufu katika kuhakikisha usalama wa misafara yao ya
kibiashara. Kwa kuchelea kuwa isije kuangukia mikononi mwa waislamu na
kuwaongezea nguvu. Kwa ujumla utumaji wa vikosi hivi ulikuwa na msaada mkubwa
sana kwa upande wa waislamu. Vikosi hivi vilichangia kwa kiasi kikubwa kuwatia
khofu maadui na kuwafanya wafikirie mara mbili mbili kabla ya kuamua kuchukua
hatua yo yote dhidi ya waislamu. Kwa upande mwingine viliwasaidia waislamu
kujua nyendo na mikakati ya baadae ya maadui. Mapatano ya kusaidiana (league)
baina ya waislamu na makabila ya Kiarabu. Yaliyokuwa yakiishi katika jangwa
lililo baina ya Makkah na Madinah, ni moja ya matunda ya vikosi hivi. Viongozi
wa makabila haya walichukua dhima na ahadi ya kushirikiana na waislamu pindipo
watakaposhambuliwa. Na kwamba makabila haya hayatajiunga na Makurayshi au adui
mwingine wa waislamu na kuwa pamoja nae dhidi ya waislamu.
MAKURAYSHI WAJARIBU KUTUMIA FURSA YA KOSA LILILOFANYWA NA
WAISLAMU.
Cheche zilizowasha moto mkali baina ya pande mbili
hizi;waislamu na makurayshi, ni ile “sariyah” ya Abdullah Ibn Jahshi.
Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-alimtuma Abdullah kuongoza kundi la
Muhajirina wasiopungua wanane, wakapeleleze khabari za Makurayshi. Mtume
akamuandikia barua na akamuamrisha asiifungue ila baada ya kwenda mwendo wa
siku mbili. Akishaifungua na kuisoma baada ya siku mbili hizo, atekeleze
maagizo yaliyomo na wala asimlazimishe ye yote katika watu aliopewa
kuwaongoza. Abdullah alipokwenda nao mwendo wa siku mbili, akaifungua ile
barua aliyopewa na Mtume, tahamaki akakuta imeandikwa: “Utakapoisoma barua
yangu hii, endelea kwenda mpaka ufike mahala paitwapo {Nakhlah} baina ya
Makkah na Twaif. Hapo wangojelee Makurayshi na utuletee khabara zao”.
Akasema baada ya kusoma: “Usikivu na utii”, na akawaambia wale wenzake
yale yaliyoandikwa ndani ya barua ile ya Mtume. Na akazidi kuwaambia Mtume wa
Allah-Rehema na Amani zimshukie-amenikataza kumlazimisha ye yote miongoni
mwenu. Basi anayetaka kufa shahidi pamoja nami na anifuate na asiyetaka na
ashike njia arudi. Ama mimi ninasonga mbele kuitekeleza amri ya Mtume wa
Allah. Akasonga mbele na wakasonga pamoja nae wote aliokuwa nao, hakuna hata
mmoja aliyerejea nyuma. Isipokuwa mabwana Sa’ad Ibn Abiy Waqaasw na Utbah
Ibn Ghaz-waan ndio walibakia nyuma kwa ajili ya kumtafuta ngamia wao
aliyepotea, ambaye walikuwa wakimpanda kwa zamu. Abdullah na wenzake wengine
wakaendelea na safari mpaka wakafika “Nakhlah”, kama walivyoamrishwa na
Bwana Mtume. Hapo wakasadifu kukutana na msafara wa Makurayshi ukija kutokea
pande za Twaif, ukiwa na shehena ya zabibu, ngozi na bidhaa nyingine. Msafara
huu ulikuwa unaongozwa na watu wanne tu, ambao ni; Abdullah Ibn Al-hadhwramiy,
Uthman Ibn Al-Mughiyrah na Naufal na Al-Hakam Ibn Al-Kaisaan. Kukutana kwa
makundi mawili haya kulikuwa ni katika siku ya mwisho ya mwezi wa Rajab.
Abdullah akashauriana na wenzake wachukue hatua gani kuhusiana na msafara ule
wa Makurayshi. Wakaambizana baada ya mashauriano mafupi: Wallah! Lau mkiwaacha
waende zao usiku huu wa leo, wataingia Haram (Makkah) na wataitumia mali hii
dhidi yenu. Na mkipigana nao mtakuwa mmepigana katika mwezi mtukufu, ambao ni
haramu kupigana. Wakasita na wakaogopa kuwasogelea, wakiwa katika hali hiyo ya
kusita na kutaka kuwasogelea, ndipo wakashajiishana na kutiana mori.
Wakauvamia msafara ule na kuushambulia, katika purukushani hizo wakamuua
Abdullah Ibn Al-Hadhwramiy; mmoja wa walinzi wa msafara ule. Na kuwateka
wengine wawili na mmoja akafanikiwa kukimbia. Bwana Abdulah na wenzake
wakarejea Madinah na ngawira yao ile ya msafara na mateka wawili. Walipofika
kwa Mtume na kumuhadithia mambo yalivyokuwa, Mtume alighadhibika na kusema:
“Mimi sikuwaamrisha kupigana katika mwezi mtukufu”. Akakataa kupokea
ngawira ile, Abdullah na wenzake wakahemewa wasijue la kufanya. Wakajutia
kitendo chao kile na wakayakinisha kuwa wameangamia na waislamu wenzao wakawa
wanawalaumu kutokana na kitendo walichokifanya.
Makurayshi kwa upande wao wakakichukulia kitendo kile cha
Abdullah na wenzake kuwa ni fursa muafaka ya kuwachochea waarabu kupigana na
Mtume. Wakaanza kueneza khabari miongoni mwa waarabu kwamba Muhammad na
maswahaba wake wamevunja utukufu na heshima ya mwezi mtukufu. Khabari za tukio
hili ziliwafadhaisha sana watu mpaka wakafikia kujiuliza kwa mshangao: Hivi
vita hupiganwa katika mwezi mtukufu, tena iwe hivyo kwa Muhammad ambaye yeye
ndiye anadai kumtii Allah na anailingania dini ya haki?!
Waislamu Madinah waliposikia tuhuma hizo nzito dhidi ya wenzao na dini yao
khasa, walianza kuchukua hatua za kujibu shutuma hizo na kuwatetea wenzao.
Wakisema kuwa yote yaliyofanyika hayakufanyika ndani ya mwezi mtukufu wa
Rajab, bali yamefanyika ndani ya mwezi wa Shaabani. Kwa kweli tukio hili
liliwafurahisha mno maadui wa Uislamu. Mayahudi nao hawakubakia nyuma katika
kulifurahia hili. Kutokana na tukio hili, wao waliamini kuwa sasa ni lazima
vita itokee baina ya waislamu na makurayshi, bali na waarabu wote. Kwa sababu
ya kuvunjwa heshima/utukufu wa mwezi mtukufu na waislamu. Kisha wao kama
kunguru wakae pembeni wakitazama ugomvi wa panzi. Kwa ujumla hali ya hewa ya
kisiasa ilichafuka sana baina ya waislamu kwa upande mmoja na makurayshi na
pamoja na makabila mengine ya kiarabu kwa upande mwingine. Na yakasemwa mengi
kuhusiana na kadhia hii.
|