|
Msafara alioutokea Bwana Mtume-Rehema na Amani
zimshukie-katika shambulio (Ghaz-wah) la Ushayrah, ulikuwa ndio msafara mkubwa
na wenye mali nyingi sana kuliko misafara yote iliyotangulia. Khabari
zikamfikia Bwana Mtume kwamba tayari msafara huo umeshaondoka Shamu na huko
njiani kurudi Makkah. Mtume akautokea na kuwaambia maswahaba wake: “Huo
msafara wa makurayshi (unakuja) na ndani yake mna mali zenu (mlizoziacha
Makkah), haya utokeeni huenda Allah akaufanya ngawira kwenu”.
Mtume aliupania sana msafara huu usimponyoke wakati wa kurudi
kwake Makkah, kama ilivyojitokeza wakati wa kwenda na huko nyuma kwa misafara
mingine kama hiyo. Mtume akaukusanyia msafara huo kila aliye mwepesi; asiye na
udhuru. Na akamuamrisha kila aliyekuwa na kipando (mnyama) atoke pamoja naye.
Watu wakaharakisha kutoka bila ya kuwa na maandalizi yo yote ya vita kwa
kudhania ni suala la msafara tu. Na kwa kudhania kuwa Mtume wa Allah
hatolazimika kupigana vita kama ilivyokuwa ikitokea mara kwa mara huko nyuma.
Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-alitoka kuuzengea
msafara huu siku ya Jumamosi, mwezi kumi na mbili Ramadhani/02 A.H. (Januari
624). Alitoka na idadi ya Muhajirina na Answari ipatayo mia tatu na kumi na
kitu. Kabla ya kutoka alikuwa tayari amekwisha watuma Twalhah Ibn Abdillah na
Sa’ad Ibn Zayd kupeleleza khabari za msafara ule. Lakini ikasadifu Mtume
kutoka na maswahaba wake kabla ya kurejea kwa wapelelezi wake na kumletea
taarifa ya upelelezi wao. Mtume alifanya hivyo kutokana na pupa aliyokuwa nayo
ili msafara usimponyoke na kama tahadhari isije ikawa wapelelezi wake
wamefikwa na la kufikwa.
BWANA MTUME ALIKAGUA JESHI LAKE NA KUWAREJESHA MADINAH WALE
WOTE WALIOTHIBITIKA KUWA BADO NI WADOGO (SIO WATU WAZIMA).
Mtume-Rehema na Amani zimshukie-akashika njia, akaenda zake
mpaka akafika sehemu iitwayo “Buyuut-Suq-yaa”. Hili ni eneo lenye maji
matamu (yasiyo na chumvi), umbali wa maili moja kutoka mji wa Madinah. Bwana
Mtume akapiga kambi hapo siku ya Jumapili, kisha ndipo lilipoanza zoezi la
kulikagua jeshi lake. Akampa amri ya kurejea Madinah kila aliyemuona kuwa ni
mdogo na hawezi kubeba silaha pindipo vita vitauma. Wakawa miongoni mwa
waliopewa amri ya kurudi ni mabwana Abdullah Ibn Umar, Raafii Ibn Khadiyji,
Al-Baraai Ibn Aazib, Usaid Ibn Hudhwayr, Zayd Ibn Al-Arqam na Zayd Ibn Thabit.
Mtume pia alimkagua Umeir Ibn Abiy Waqaaswi na kumuona kuwa bado ni mtoto
asiyeruhusiwa kushiriki vitani. Umeir akalia sana baada ya kutakiwa arejee,
Mtume kuona hivyo ikabidi amruhusu kujiunga na jeshi na kusonga mbele.
Al-Waaqidiy amepokea kutoka kwa Sa’ad Ibn Abiy
Waqaaswi-kwamba yeye mwenyewe amesema: Nilimuona ndugu yangu Umeir Ibn Abiy
Waqaaswi kabla hatujakaguliwa na Mtume wa Allah-Rehema na Amani
zimshukie-akijifichaficha. Nikamuuliza : Una nini ewe ndugu yangu? Akanijibu:
Mimi ninachelea Bwana Mtume asije kuniona mdogo na kuniamuru kurudi na ilhali
mimi ninapenda kutoka, huenda Allah akaniruzuku shahada (kufa shahidi).
Akasema: (Sa’ad): Akakaguliwa na Bwana Mtume akamuona kuwa bado ni mdogo,
akamwambia: “Rudi”. Umeir akalia ndipo Bwana Mtume akamruhusu. Akasema
(Al-Waaqidiy): Sa’ad akawa akisema: Nilikuwa nikimbebea kamba (upachikio) za
upanga wake. Akauawa shahidi (kama alivyotamani) katika vita vya Badri akiwa
na umri wa miaka kumi na sita tu.
WALIKUWA WAKIPOKEZANA VIPANDO KUTOKANA NA UCHACHE WA
VIPANDO UKILINGANISHA NA IDADI YA WATU.
Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie- akaanua kambi hapo
“Buyuut-Suq-yaa”, akaondoka kusonga mbele kwa lengo la kutimiza azma yake.
Akiwa na askari wapiganaji (combatants) wapatao mia tatu na tano (305). Katika
hao walikuwemo Muhajirina wapatao sabini hivi na kiasi cha Answaari mia mbili
na arobaini hivi. Hawakuwa na farasi ila wawili tu na ngamia kama sabini tu.
Kutokana na uchache wa vipando walivyokuwa navyo ikawalazimu kupanda kwa zamu;
hawa wanapanda na wale wanatembea. Baada ya umbali fulani wale waliokuwa
wamepanda wanashuka na kuwapa fursa ya kupanda wenzao waliokuwa wakitembea.
Idadi ya watu iliwalazimisha kila watu wanne wapokezane kupanda ngamia mmoja.
Mmoja anapanda watatu waliobakia wanakwenda kwa miguu. Bwana Mtume naye
hakuiepa hali hii, naye ilimkumba. Akawa anapokezana kupanda na Aliy Ibn Abiy
Twaalib na Marthad Ibn Abiy Marthad. Hamzah Ibn Abdul Mutwalib (Ami yake
Mtume) yeye alipokezana na Zayd Ibn Haarithah, Abuu Kabshah na Anasah; hawa
walikuwa ni mahuru wa Bwana Mtume. Ama Abuu Bakri, Umar na Abdurahmaan Ibn
Auf, wao pia walishirikiana ngamia mmoja. Hivi ndivyo ilivyokuwa hali ya
kikosi hiki, kila watu wanne au watatu walipokezana kupanda na kutembea. Bwana
Mtume pamoja na kuwa kwake kiongozi aliyestahiki heshima zote, lakini
hakukubali wala kuona raha ila ashirikiane na askari (maswahaba) wake katika
raha na shida. Apande na kutembea inapofika zamu yake kama ilivyokuwa kwa watu
wengine wote. Ilipomalizika zamu yake ya kupanda alishuka, hapo wenzake
humwambia: Endelea kupanda ewe Mtume wa Allah. Nae akiwajibu kwa kusema:
“Nyinyi hamna nguvu ya kutembea kunishinda mimi na mimi si mkwasi wa ujira
kuliko nyinyi”.
Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-hakuwa amefunga bendera
ya vita alipotoka Madinah. Lakini tangu alipotoka “Buyuut-Suq-yaa”
alipokuwa amepiga kambi, aliwaweka watu wake katika hali ya utayarifu wa vita
ikiwa vitatokea. Mtume alifanya hivyo kutokana na uwezekano kuwa adui anaweza
kuwashtukiza ghafla nao wakiwa hawajajiandaa. Nao kila walivyosonga mbele
ndivyo walivyozidi kujitoma katika ardhi inayomilikiwa na mushrikina. Ni
kutokana na haya yote ndiyo Bwana Mtume akaanza kuwapanga watu wake kwa namna
ambayo watasalimika na shambulio la ghafla. Akamuweka mbele ya jeshi Qays Ibn
Abiy Swa’aswa’ah na nyuma akamuweka Zubeir Ibn Al-awwaam. Akaamuru kila
mtu ashike silaha yake tayari kwa lo lote litakalotokea. Akafunga bendera tatu
za vita; bendera nyeupe iliyobebwa na Musw’ab Ibn Umeir na bendera nyingine
mbili nyeusi. Moja alikuwa nayo Aliy Ibn Abiy Twaalib na nyingine alikuwa nayo
mtu mmoja katika Maanswari.
Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-aliwatanguliza mbele
yake majasusi wake wawili ili wampelelezee na kumletea khabari za adui. Hawa
hawakuwa wengine ila ni mabwana Basbas Ibn Amri na Adiy Ibn Abiy Zaghbaa.
Katika kuitekeleza amri ya Mtume, mabwana hawa walikwenda mpaka eneo la maji
la Badri. Hapo waliwakuta vijakazi wawili wakichota maji, wakafahamu kutokana
na mazungumzo yaliyokuwa yakijiri baina yao kwamba wao (vijakazi)
wanaungojelea ule msafara wa Makurayshi. Na kwamba msafara huo utafika mahala
hapo kesho yake. Haraka na bila kuchelewa wakarudi kwa Mtume na kumpasha
khabari ile.
|