|
Tumeeleza katika somo lililopita kwamba baba yake Bwana Mtume ni Mzee Abdallah Bin
Abdul-Mutwalib na mama yake ni Bi Aaminah Bint Wahab. Bwana Abdallah alikuwa ni miongoni
mwa vijana bora wa mji wa Makkah na alikuwa mzuri wa umbo na tabia njema. Bi Aaminah
alitokana na kabila tukufu na alikuwa ni miongoni mwa mabinti wa makkah waliosifika kwa
tabia njema na alijaaliwa na umbo na sura nzuri.
Baada ya Bwana Abdallah kumuoa Bi. Aaminah alisafiri pamoja na mkewe kuelekea
Shaamu kwa ajili ya biashara,Wakati anarudi Makkah akitokea Shaamu alishikwa na maradhi
njiani, akaamua kwenda kujitibia Madinah ambako maradhi yalimzidia akafa na kuzikwa hapo
hapo Madinah.
Baada ya mazishi mkewe alirudi Makkah hali ya kuwa ana huzuni ya kumpoteza mumewe
mpenzi na wakati huo Bin. Aaminah alikuwa na mimba ya Bwana Mtume
Ama kisa cha kuchinjwa Bwana Abdallaha baba yake Mtume kilikuwa kama ifuatavyo:-
Bwana Abdallah alikuwa akipendwa sana na baba yake kuliko nduguze wengine.
Ikatokezea kukauka chem chem ya maji ya ZamZam nyakati za Hijjah ndipo Mzee Abdul-
Mutwalib akaweka nadhiri ya kumchinja mmojawapo wa wanawe kwa ajili ya kujikurubisha kwa
Mola wake maji yatakapozidi/yatakapoongezeka. Maji yalipoongezeka ndipo ikamlazimu Bwana
Abdallah kuitekeleza nadhiri aliyoiweka ya kumchinja mmojawapo wa wanawe. Sasa achinjwe
nani? Ikabidi ipigwe kura, na kila mara ikawa inamuangukia Bwana Abdallah baba yake Mtume.
Kwa kuwa mtoto huyu ndiye aliyekuwa kipenzi cha baba yake bali watu wote ndipo
kiongozi mmoja wa dini akamshauri Mzee Abdul-Mutwalib apige kura baina ya mwanawe Abdallah
na idadi fulani ya ngamia. Kila mara kura itakapo muangukia Abdallah iliongezwa idadi ya
ngamia mpaka kura iwaangukie ngamia. Idadi ya ngamia ilipofika ngamia mia ndipo kura
ikawaangukia ngamia wale, Mzee Abdul-Mutwalib akawachinja ngamia wale kwa ajili ya
kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu na kwa kitendo hicho ikawa Bwana Abdallah ameokoka na
kuchinjwa na ngamia wale wakawa ndio fidia yake. Kisa hiki kinatukumbusha kisa kikongwe
kilichojaa mafunzo mengi cha kutaka kuchinjwa Nabii Ismail Bin Ibrahim Amani ya
Allah iwashukie wakati Nabii Ibrahim alipooteshwa usingizini amchinje mwanawe Ismail. Kwa
kuwa ndoto za mitume huwa ni wahyi kwa Mwenyezi Mungu, Nabii ibrahim akaanza kuchukua
hatua za kuitekeleza amri ya Mola wake, akamlaza mwanawe ili amchinje ndipo Mola mwingi wa
huruma akamkomboa mja wake Ismail kwa kumleta kondoo wa peponi achinjwe badala ya Ismail
kama tunavyosoma ndani ya Qur-ani.
Imepokelewa hadithi kutoka kwa Bwana Mtume akisema: "Mimi ni mtoto wa
wachinjwa wawili " Nao ni Babu Nabii Ismail, huyu ndiyo mchinjwa wa kwanza na wa pili
ni baba yake Mzee Abdallah.
SOMO LA NNE
i/ KUZALIWA KWA BWANA MTUME
Bwana Mtume Allah amshushie rehma na amani alizaliwa katika mji wa
Makkah, siku ya Jumatatu mwezi wa mfungo sita, mwaka wa tembo sawa na tarehe 20 ya mwezi
April mwaka 571 Miyladia (tangu kuzaliwa Nabii Issa). Bwana Mtume alizaliwa hali ya
kuwa ni yatima kwani baba yake alikufa akimuacha mkewe ana mimba ya Mtume. Mama yake
alipojifungua tu alimpeleka mjumbe kwa babu yake Mtume Mzee Abdul -Mutwalib kumpa khabari
njema za kuzaliwa mjukuu wake. Mzee Abdul Mutwalib akafurahikia sana mjukuu wake
akamchukua na kumzungusha katika Al-Kaaba na akamuita Muhammad.
Tumesema Bwana Mtume amezaliwa mwaka wa tembo. Qur-ani Tukufu imeuzungumza mwaka
huu katika sura maalum iliyoitwa kwa jina la Suuratul Fiyl (Sura ya tembo) kisa cha
mwaka wa tembo kinaanzia pale Abraha mfalme wa Habashah na Yaman alipowaona Waarabu
wakihiji Makkah na ibada hii ya Hijjah ikaufanya mji wa Makkah kuwa ni kitovu cha biashara
. Mfalme Abraha akadhamiria kuihamisha ibada hii ya Hijjah kutoka Makkah na kuipeleka
katika milki ya himaya yake ya Yaman. Ili kuutekeleza mkakati wake huu akajenga kanisa
kubwa sana na kulipamba kwa mapambo ya fakhari ili watu wavutike na kuja kufanya ibada ya
Hijjah hapo. Baada ya ujenzi huo, akawaamrisha watu waje kuhiji hapo, amri hii ikawa nzito
kwa Waarabu kuitekeleza na hawakuiridhia. Ili kuonyesha chuki yao dhidi ya amri hii
alitoka mtu mmoja wa kabila ya kinaanah akaja kufanya haja kubwa ndani ya kanisa lile.
Kitendo hiki cha kulichafua kanisa kilimkasirisha sana Mfalme Abraha, hasa baada ya
kugundua kwamba mhusika wa kitendo hicho ni mtu kutokea pande za Makkah. Akaandaa jeshi
kubwa lililokuwa limesheheni tembo wengi ili kwenda kuivunja Al-kaaba na yeye mwenyewe
alikuwa amempanda tembo mkubwa sana kuliko wote. Waarabu wa Makkah waliogofya sana na
jeshi lile. Jeshi la Abraha lilipofika katika viunga vya mji wa Makkah likawakuta ngamia,
kondoo na mbuzi wa watu wa Makkah na wengine walikuwa ni milki ya babu yake Mtume Mzee
Abdul-Mutwalib, Abraha awachukua wanyama wale wote. Mzee Abdul-Mutwalib kiongozi wa kabila
la Kikurayshi, mtumishi wa Al-Kaab na mtawala wa Makkah akamuendea Abraha na kumtaka
amrejeshee wanyama wake aliowachukua Abraha akamshangaa sana Mzee Abdul Mutwalib
akamwambia:
"Mimi nilitazamia umekuja kuniomba nisiivunje Al-Kaab, kumbe umekuja kunitaka
nikurudishie wanyama wako!" Mzee Abdul Mutwalib akamjibu: "Mimi wa kwangu
ni hawa wanyama, ama hii nyumba yupo mwenyewe atayeihami".
Kisha Mwenyezi Mungu Mtukufu alishushia jeshi la Abraha jeshi la ndege
wanaolidondoshea jeshi la Abraha mawe kutoka motoni. Jiwe likimpata mtu anasagikasagika
yeye na tembo wake na kuwa kama majani yaliyoliwa na wadudu kama tunavyosoma ndani ya
Qur-ani. Tokea hapo Waarabu wakawa wanaitaja kalenda yao kwakuinasibisha na tukio hili
kubwa na hii ndio maana tunasema Bwana Mtume alizaliwa mwaka wa tembo.
|