|
Khabari za Mtume
kuuvizia msafara wa Makurayshi utokao Shamu kurejea Makkah kupitia Madinah
zilivuja na kumfikia Abuu Sufyaan; kiongozi wa msafara ule. Bila kuchelewa
Abuu Sufyaan akamtuma mjumbe kwenda mjini Makkah kuwapasha Makurayshi khabari
ile na kuwaelezea juu ya uwezekano wa kupoteza mali yao, ikiwa hawatachukua
hatua za tahadhari kwa haraka. Akamuagiza mjumbe wake kutumia kila njia
iwezekanayo kuhakikisha kuwa anawahamasisha watu kutoka kuja kuuhami msafara
dhidi ya Mtume na maswahaba wake. Mjumbe huyu aliutambua umuhimu wa dhima
aliyoibeba, akaandaa mazingira yatakayomsaidia kufikisha haraka ujumbe wa Abuu
Sufyaan kwa watu wa Makkah. Alipokaribia kufika mjini Makkah akamkata sikio
ngamia wake, akaitupa sogi yake na kuichana kanzu yake na akaanza kupaaza
sauti jangwani, akisema: “Enyi kusanyiko la Makurayshi, msafara msafara!
Mali zenu pamoja na Abuu Sufyaan, Muhammad amezitokea na maswahaba wake,
sidhani kama mtaudiriki (kabla Muhammad hajautia mkononi)! Msaada msaada!”
Naam, kutokana na
mazingira haya yaliyoandaliwa barabara, haraka Makurayshi wakakiitikia kilio
kile cha msaada, mori ukawapanda wakasema: Hivi huyu Muhammad na maswahaba
wake wanadhania msafara huu ni kama ule wa Ibn Al-Hadhwramiy (waliouteka)?
Sivyo hivyo, Wallah atatutambua, tena atatambua kwamba sivyo hivyo! Makurayshi
wakatoka haraka tayari kuuhami msafara wao kwa gharama yo yote ile iwayo.
Mwenye uwezo akamsaidia asiye na uwezo ili naye atoke na ambaye hakuweza
kutoka mwenyewe basi alimtafuta mtu wa kutoka badala yake. Wanazuoni wa sira
na tarekh wanasema: Kwamba Umayyah Ibn Khalaf alitaka kubakia nyuma, asitoke.
Uqbah Ibn Abiy Muaitw akamuendea akiwa na chetezo na bukhuri
(ubani/uvumba/udi). Akaviweka mbele yake naye akiwa amekaa katika baraza ya
jamaa zake (Makurayshi wenziwe), akamwambia: “Jifukize ewe Abuu Aliy, kwani
hakika si vinginevyo wewe ni katika wanawake (wasioweza kutoka)”. Umayyah
akahisi soni na kuona haya, pale pale akainuka ili kuwaonyesha kwamba yeye sio
mwanamke. Akaenda kujiandaa na akatoka pamoja na watu wengine kwenda kuuhami
msafara wao.
ABUU SUFYAAN ATOROKA
NA MSAFARA:
Abuu Sufyaan akauongoza
msafara ule huku akipeleleza khabari za Mtume na maswahaba wake njiani.
Akaenda mpaka alipokaribia Badri akauacha nyuma msafara kwa tahadhari. Akaenda
mbele peke yake mpaka akafika sehemu ya maji pale Badri. Hapo akawauliza watu
khabari za waislamu, akafahamu kutokana na maelezo aliyoyapata kwamba kuna
wapanda ngamia wawili walipiga kambi huko kilimani. Walipita pale kuchota na
kunywa maji kwa muda, kisha wakashika njia na kuondoka zao. Abuu Sufyaan
akaenda mpaka katika kile kilima alichoelezwa, akachunguza pale walipokita
ngamia wawili wale. Akachukua kinyesi chao akakisukasuka mkononi mwake,
akagundua kina athari ya tende. Akatambua kwamba wapanda ngamia wawili hao
aliolezwa wanatokea Madinah. Akasema: “Wallah! Hiki ni chakula cha wanyama
wa Yathrib (Madinah) na hapana shaka hawa ni majasusi wa Muhammad wamekuja
kupeleleza khabari zetu”. Akarejea haraka pale alipouacha msafara na
kuuelekeza kubadili muelekeo wa Badri na badala yake uelekee mwambao wa bahari
ukiiacha Badri kushotoni kwake. Kwa hila na mbinu hii Abuu Sufyaan akaweza
kuutorosha msafara na hivyo kuziokoa mali za Makurayshi zisiingie mikononi mwa
Mtume.
BONDE LA BADRI.
Hebu turejee nyuma
kidogo ili tuweze kulijua vema eneo au mahala hapa panapoitwa “Badri”.
Badri hili ni bonde ambalo lilikuwa ni mahala pa msimu wa biashara wa makabila
mbali mbali ya Kiarabu kila mwaka. Hukutanika hapo na kufanya gulio kubwa
sana, ambapo bidhaa za kila aina zilipatikana. Badri hali kadhalika lilikuwa
ni eneo mashuhuri lenye maji katika njia ya Makkah-Madinah. Pia Badri ndio
ilikuwa stesheni ya kupumzikia misafara ielekeayo Shamu kutokea sehemu mbali
mbali. Kutoka hapo Badri mpaka Madinah kuna umbali wa kiasi cha kilometa
zipatazo mia moja na sitini. Mahala hapa ni eneo tambarare la mchanga lenye
vilima vyenye mteremko mkali upandae wa Kaskazini na Mashariki. Upande wa
Magharibi kuna eneo lenye mafungu ya mchanga na upande wa kusini kuna miamba
yenye mteremko usio mkali. Vimeenea vijito vya maji vinavyolikata bonde hili
kutokea upande wa mashariki kuelekea magharibi. Vijito hivi hujikata na kuwa
vijito vidogo vidogo vilivyoenea huku na huko na kuwa mithili ya visima vingi.
Wasafiri wapitao hapo huvijengea kuta visima hivi na kuvifanya kuwa mithili ya
mahodhi (basin) makubwa ya kuhifadhia maji. Mpaka hapa tunataraji maelezo haya
yatakuwa yamekupa taswira ya Badri kiasi cha kuelewa tunapoitaja Badri
tunaongelea mahala pa namna gani.
MTUME ATAMBUA KUTOKA
KWA MAKURAYSHI NA ANAWATAKA USHAURI MASWAHABA WAKE WAFANYE NINI ILI
KUKABILIANA NA HALI HIYO.
Mtume wa Allah-Rehema na
Amani zimshukie-alisonga mbele na maswahaba wake mpaka wakafika katika bonde
liitwalo “Dhafiraan”. Hapo ndipo zilipomfikia khabari kwamba Makurayshi
wametoka wote kwa ujumla wao kuja kuuhami msafara wao. Pia wakamjia wale
wajumbe wake wawili aliowatuma kule “Buyuut-Suq-yaa”, wakamueleza khabari
za upelelezi wao kuhusiana na msafara ule wa Makurayshi. Baada ya kupokea
taarifa zote mbili; taarifa ya kutoka kwa Makurayshi na ile ya upelelezi.
Bwana Mtume aliwakusanya maswahaba wake na kuwapasha khabari zile na kuwataka
ushauri wafanye nini katika kukabiliana na kundi hilo kubwa la Makurayshi
linalowajia. Likawepo kundi miongoni mwao ambalo halikupenda kukabiliana na
Makurayshi kivita bila ya kuwa na maandalizi ya kutosha ya vita. Wakasema wao
wametoka kwa ajili ya kuteka msafara na wala sio vita, wakamwambia Bwana
Mtume: “Kwa nini hukutuambia kuwa tunakuja vitani ili tupate kujiandaa!”
Mtume wa Allah hakuufurahia uoga huu wa maswahaba wake katika kukabiliana na
Makurayshi, akafikiria matokeo ya hali ile, akawakariria kauli yake:
“Mnalionaje suala la kupigana na watu hawa (Makurayshi)?” Wakamjibu:
“Wallah, hatuna uwezo (nguvu) wa kupigana na adui, sisi tuliukusudia
msafara”. Kusikia jawabu hilo, pale pale uso wa Mtume ukabadilika na
ikadhihiri ghadhabu yake usoni mwake. Hapo ndipo maswahaba wakadiriki khatari
inayowakabili ikiwa watayakhalifu matashi ya Mtume wa Allah. Likasimama kundi
moingoni mwao na kutoa wito wa vita, Abuu Bakri akainuka na kusema maneno ya
kuhamasisha. Umar naye akasimama na kuamsha ari na mori wa maswahaba, kisha
akasimama Miqdaad Ibn Amri akasema: “Ewe Mtume wa Allah, tekeleza
alilokuamrisha Allah na sisi tuko pamoja nawe. Wallah, hatusemi kukuambia wewe
kama Baniy Israili walivyomwambia (Mtume wao) Musa : “…NENDA WEWE NA MOLA
WAKO MKAPIGANE, SISI TUTAKAA HAPA (kungojea nini litakalokuwa)…” Lakini
sisi (tunasema) nenda wewe na Mola wako mkapigane na sisi ni wenye kupigana
pamoja nanyi. Tunaapa kwa yule aliyekutumiliza kwa haki lau ungeenda nasi
mpaka Barkil-Ghimaad (hii kwa wakati huo ndio ilionekana kuwa sehemu ya mbali
kabisa, inasemekana ilikuwa pande za Yemen), tungelivaa panga zetu pamoja nawe
mpaka tufike huko”. Bwana Mtume akamwambia Miqdaad umenena vema na
akamuombea dua njema.
Kisha Mtume wa
Allah-Rehema na Amani zimshukie-akasema: “Nipeni ushauri enyi watu”,
akiwalenga Maanswari, kwani wao ndio waliokuwa wengi. Na ikumbukwe kwamba
tayari walikuwa wamempa huko nyuma kabla ya kuhamia Madinah ahadi ya kumlinda
ndani ya miji yao. Ama nje ya miji yao ahadi hiyo hawakuitoa, kwa hivyo suala
hili linabakia kuwa katika khiari yao. Mtume alipokwisha kusema hivyo,
akasimama Sa’ad Ibn Muaadh na kusema: “Huenda unatukusudia sisi ewe Mtume
wa Allah?” Mtume akajibu: “Ndio khasa”. Sa’ad akasema: “Bila ya
shaka wewe umelitokea jambo fulani na Allah akakuondoshea jambo jingine. Basi
litazame hilo alilokuondoshea wewe Allah na ulitekeleze hilo. Hakika sisi
tumekuamini na kukusadiki wewe na tumeshuhudia kwamba uliyokuja nayo ni haki
(kweli). Na tumekupa ahadi zetu za usikivu na utii, labda ewe Mtume wa Allah
unachelea kuwa Maanswari wanaona kuwa hizo ni ahadi za kukunusuru ndani ya
miji yao tu (na sio nje yake). Mimi ndiye ninayewasemea na kuwajibia
Maanswari: Nenda ewe Mtume wa Allah ukutakapo, iunge kamba ya umtakaye na
ikate ya umtakaye, msalimishe umtakaye na mpige vita umtakaye. Twaa katika
mali zetu ukitakacho na utakachokichukua katika mali zetu chapendeza mno kwetu
kuliko utakachokiacha. Amri yo yote utakayoitoa sisi tutaamrika, endelea ewe
Mtume wa Allah na ulilolikusudia, sisi tu pamoja nawe. Tunaapa kwa yule
aliyekutumiliza kwa haki, lau ungelituonyesha bahari hii na ukaiingia, basi
nasi tungeliingia pamoja nawe na wala hasingebakia nyuma ye yote miongoni
mwetu. Hatuchukii wewe kutukutanisha na adui yetu kesho, sisi ni wastahamilivu
wa vita, wakweli wakati wa mapambano. Huenda Allah akakuonyesha kwetu yale
yatakayoyaburudisha macho (moyo) yako, songa mbele kwa baraka za Allah”.
Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akafurahi na kifua chake kikakunjuka
kwa kusikia maneno hayo yenye ukweli na utii ndani yake. Akasema: Enendeni kwa
baraka za Allah na ikupateni bishara njema. Hakika Allah ameniahidi mojawapo
ya mataifa (mapote) mawili, wallah kama kwamba mimi ninayaona maanguko ya watu
hao”. Lirejee tukio hili katika Qur-ani ukitaka: “(Atakunusuruni) KAMA
ALIVYOKUTOA MOLA WAKO KATIKA NYUMBA YAKO KWA HAKI, NA KUNDI MOJA LA WALIOAMINI
HALIPENDI (utoke). WAKABISHANA NAWE KATIKA ( lile jambo la) HAKI BAADA YA
KUBAINIKA (haki ile wanachukia kwenda huko vitani) KAMA KWAMBA WANASUKUMWA
KATIKA MAUTI NA HUKU WANAONA. NA (kumbukeni) ALLAH ALIPOKUAHIDINI MOJA KATIKA
MATAIFA MAWILI YA KWAMBA NI LENU. NANYI MKAPENDA MPATE LILE LISILO NA NGUVU,
NA ALLAH ANAPENDA KUTHUBUTISHA HAKI KWA MANENO YAKE NA (anapenda) KUIKATA
MIZIZI YA MAKAFIRI. ILI KUTHUBUTISHA HAKI NA KUIONDOA BATILI, HATA WAKICHUKIA
WATU WABAYA” [8:5-8]
|